Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Eldoret, Kenya – Waendesha baiskeli wawili wa Uganda Charles Kagimu na Paul Lomuria walisherehekea siku kuu ya uhuru nchini Uganda kwa kishindo kufuatia ushindi wao katika mashindano ya Afrika ya kuendesha baiskeli za barabarani (CAC) mjini Eldoret, kaunti ya Uasin Gisu nchini Kenya.

Siku ya Uhuru nchini Uganda ni sikukuu ya kitaifa inayoadhimishwa Oktoba 9 kila mwaka. Inaadhimisha uhuru wa Uganda kutoka kwa Uingereza mnamo 1962.
Waganda walisherehekea kwa kusherehekea miaka 62 kwa furaha huku bendera yao ya taifa ikipandishwa mara mbili jukwaani kwenye kitengo cha wanaume mahiri na chini ya miaka 23 katika hafla ya majaribio ya wakati, shindano la mwisho la siku ya kwanza ya mashindano huko Eldoret.
Ili kuonyesha maudhui haya X (Twitter) maudhui, unahitaji kuidhinisha kipimo cha hadhira na vidakuzi vya matangazo.KubaliDhibiti chaguo langu
Charles Kagimu anahusisha baadhi ya mafanikio yake katika mashindano ya baiskeli ya Afrika mwaka 2024 na ari ya siku ya uhuru wa Uganda. Matukio kama siku ya uhuru yanaweza kuwatia moyo wanariadha kwa kukuza fahari na motisha ya kitaifa.
Kagimu aliyezaliwa mwaka wa 1998, alishinda taji la wachezaji mahiri baada ya kutinga kilomita 33.8 kwa muda wa dakika 44:10.050 akisema kwamba hakushinda tu kwa ajili ya nchi yake bali Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa ujumla.
“Siku ya uhuru ni siku muhimu sana haswa kwa nchi za Afrika. Nilitaka nishinde sababu ni siku kubwa nyumbani na hio ilinipa nguvu zaidi kando na mazoezi na matayarisho mazuri,” alisisitiza Kagimu baada ya kuvalishwa jezi nyeupe jukwaani.
Kagimu, 26, amehifadhi taji lake la Afrika kwenye kitengo cha majaribio ya muda ‘Time Trials’ aliloshinda mwaka jana nchini Ghana.

Kagimu alitua nchini Kenya akiwa na umri wa miaka 17 na amekuwa akifanya mazoezi katika bonde la ufa – Kaptagat na Iten. Kenya ni nchi ambayo Kagimu anaita “nyumbani”
Downes Brown kutoka Afrika Kusini alimaliza wa pili – 41:19.311 huku Abraoui Adil kutoka Morocco akikamilisha jukwaa kwa muda wa – 42:50.978
Lomuria aliongoza mwenzake wa Uganda Lawrence Lorot kumaliza nafasi mbili za kwanza katika jukwaa la vijana chini ya miaka 23 katika shindano la majaribio ya muda.

Mnyarwanda Moise Mugisha alimaliza wa tano kwenye kitengo cha wachezaji mahiri, wakenya Kamau Joseph na David Kinjah wakichukua nafasi ya nane na 11 mtawalia, Abdu-Noor Lubega wa Uganda alimaliza wa 12, Boniphase Ngwata na Sharif Hassan kutoka Tanzania wakichukua nafasi ya 13 na 16 mtawalia.
“Mashindano yako vizuri, maandalizi mazuri, barabara ziko vizuri. Mashindano haya yako bora zaidi kuliko yale ya awali,” alieleza Boniphase Ngwata.
Hii ikiwa ni mara ya kwanza Kenya kuwa mwenyeji wa mashindano haya makubwa barani Afrika, mashabiki walijitokeza kwa wingi katika barabara zote za Eldoret kuanzia mapema saa moja asubuhi kabla ya shindano la kwanza kuanza.
Ili kuonyesha maudhui haya X (Twitter) maudhui, unahitaji kuidhinisha kipimo cha hadhira na vidakuzi vya matangazo.KubaliDhibiti chaguo langu
Shabiki mmoja aliniambia “amefurahia sana kuona Olimpiki ya baiskeli nchini Kenya” huku mwingine akidai “amefurahia kiasi cha kutamani kuwa mwendesha baiskeli.”
Changamoto ya wenyeji
Siku ya ufunguzi wa mashindano ilikuwa yenye changamoto kubwa kwa wenyeji Kenya.
Katika mbio za wanawake mahiri, mwendeshaji wa muda mrefu Tabu Masiga Kendra alishika nafasi ya sita mbele ya nahodha wa timu Nancy Akinyi, aliyemaliza wa saba. Wote wawili wanatazamiwa kuongoza Kenya katika mchuano mseto hapo kesho.
“Ilikuwa siku ngumu ya ufunguzi, lakini tunatarajia kufanya vyema kesho.”
“Wengi wetu tulipambana na wakati kwa sababu tunashindana kwa kiwango hiki kwa mara ya kwanza lakini tunapaswa kuwa sawa kwani mashindano yanaendelea.”

Mwendesha baiskeli mkongwe David Kinjah alielezea kufurahishwa kwake kuona hafla hiyo ya kifahari ikiandaliwa nchini Kenya kwa mara ya kwanza.
“Tunafuraha kubwa kuwa na mchuano wa ufunguzi wa ukubwa huu katika nchi yetu.”
“Tunatumai ni mwanzo wa mambo mazuri zaidi katika nchi yetu kwenye uendeshaji baiskeli.”
Katika mbio za vijana wanaume, Keven Teklemariam wa Eritrea alitawala mwendo wa kilomita 22.5 kwa muda wa 14:18.8, akifuatwa kwa karibu na Alexander Erasmus wa Afrika Kusini. Billy Mbolo Mangwana wa Kenya alimaliza wa 14.
Chepkemboi Sherry wa Kenya alishika nafasi ya tisa katika kitengo cha vijana wanawake, shindano ambalo Darwish Benbella kutoka Misri aliibuka mshindi kwa muda wa dakika 17:06.47, Kiros Tsige wa Ethiopia na Botha Megan wa Afrika Kusini wakikamilisha jukwaa kwa nafasi mbili za kwanza.
Siku ya pili ya mashindano itahusisha umma kushindana kwa kutumia baiskeli zao za aina yoyote asubuhi kabla ya mashindano ya mseto kuanza mchana.
All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.