Siasa Kimataifa

Na Cantona Joseph June 26, 2026 02:20 (EAT)

Ripoti ya Reuters Digital News 2026, iliyowasilishwa katika kongamano la Global Media Forum la DW mjini Bonn, inaonyesha mitandao ya kijamii na majukwaa ya video sasa ndiyo chanzo kikuu cha habari kwa watu wengi dunianiPicha: Björn Kietzmann/DW

Vijana wengi duniani wanazidi kujitenga na habari za kawaida, lakini Ripoti ya Reuters Digital News inaonyesha bado kuna matumaini. Wataalamu wanasema uandishi wa habari unaendelea kuwa muhimu kwa jamii.

Jinsi watu wanavyopata habari katika zama za kidijitali inaendelea kubadilika kwa kasi. Ripoti ya Reuters Digital News 2026, iliyowasilishwa katika kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari – Global Media Forum la DW mjini Bonn, inaonyesha kuwa mitandao ya kijamii na majukwaa ya video sasa ndiyo chanzo kikuu cha habari kwa watu wengi duniani, huku televisheni na tovuti za vyombo vya habari zikizidi kupoteza ushawishi.

Mwandishi mkuu wa ripoti hiyo, Jim Egan wa Taasisi ya Reuters katika Chuo Kikuu cha Oxford, amesema matokeo ya mwaka huu yanatia wasiwasi kwa sababu yanaonyesha mabadiliko makubwa katika namna watu wanavyotumia habari.

Kwa mara ya kwanza, watu wengi zaidi duniani wanasema wanapata habari kupitia mitandao ya kijamii na majukwaa ya video kuliko kupitia televisheni au programu na tovuti za vyombo vya habari. Hata hivyo, Egan anasema hali hiyo haitokani na ongezeko kubwa la matumizi ya mitandao ya kijamii bali na kupungua kwa matumizi ya vyanzo vya habari vya jadi.

Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari – Global Media Forum la DW limefanyika mjini BonnPicha: Björn Kietzmann/DW

Mabadiliko hayo yanaonekana zaidi kwa vijana. NchiniMarekani, zaidi ya theluthi moja ya watu wenye umri chini ya miaka 25 wanasema hawajawahi kuwa watumiaji wa kawaida wa habari za televisheni au tovuti za habari. Kwa maneno mengine, vijana wengi hawaachi kufuatilia habari za jadi; hawajaanza kabisa kuzitumia.

Mitandao inaongoza, lakini uaminifu ni mdogo

Licha ya umaarufu wake, mitandao ya kijamii inaendelea kukabiliwa na tatizo la uaminifu. Ripoti hiyo inaonyesha kuwa watu wengi wanazidi kutegemea majukwaa ambayo kwa ujumla wanayaamini kwa kiwango kidogo zaidi.

Egan anasema kuna hali ya ukinzani ambapo watumiaji wanahamia katika majukwaa wanayoyaamini kwa kiwango kidogo kuliko vyombo vya habari vya kawaida. Hali hiyo imeibua maswali kuhusu ubora wa taarifa na uwezekano wa kusambaa kwa habari potofu.

Wakati huo huo, matumizi ya video yanaendelea kuongezeka kwa kasi. Takribani robo tatu ya washiriki wa utafiti huo walisema hutazama video za habari kila wiki, hasa kupitia YouTube, TikTok na Instagram.

Matumizi ya video yanaendelea kuongezeka kwa kasi. Watu wengi wanasemekana kuangalia video za habari kila wiki, hasa kupitia YouTube, TikTok na InstagramPicha: Hollie Adams/REUTERS

Hata hivyo, vyombo vya habari vyenye majukwaa yao ya video havijanufaika sana na mwelekeo huo. Ripoti inaonyesha kuwa watazamaji wengi wanapendelea kutumia video kupitia mitandao ya kijamii kuliko kupitia tovuti za vyombo vya habari.

Vijana hawapendi video fupi pekee

Ripoti hiyo pia imekanusha dhana kwamba vijana wanapenda tu video fupi za sekunde chache. Takribani asilimia 20 ya watumiaji wa YouTube walisema hutazama video za zaidi ya dakika 20, huku idadi kama hiyo ikifuatilia matangazo ya habari ya moja kwa moja.

Kwa mujibu wa Egan, vijana wengi hawaridhiki na video fupi pekee bali pia wanapenda maudhui marefu yanayotoa maelezo ya kina.

Aidha, matumizi ya televisheni kama kifaa cha kutazamia habari kupitia majukwaa ya kidijitali yanaongezeka tena. Takribani robo ya washiriki wa utafiti huo duniani walisema hutazama habari za YouTube na majukwaa mengine kupitia runinga zao majumbani.

Katika baadhi ya nchi za Afrika, matumizi ya YouTube kama chanzo cha habari ni makubwa zaidi. Nchini Kenya, kwa mfano, asilimia 66 ya washiriki wa utafiti huo walisema hupata habari kupitia YouTube.

Matumizi ya Akili Mnemba imeongezeka kama chanzo cha habariPicha: Omar Marques/SOPA Images/ZUMA/picture alliance

Akili Mnemba yaanza kutumika kwa habari

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuongezeka kwa matumizi ya Akili Mnemba kama chanzo cha habari. Asilimia 10 ya washiriki duniani sasa wanasema hutumia programu za mazungumzo zinazotumia Akili Mnemba kupata habari, ikilinganishwa na asilimia saba mwaka uliopita.

Egan anasema ukuaji huo ni wa haraka, lakini bado si wa kiwango cha kulipuka. Anaongeza kuwa changamoto kubwa kwa sasa ni suala la uaminifu, kwa kuwa watumiaji wengi bado hawana imani kubwa na taarifa zinazotolewa na mifumo hiyo.

Kwa upande mwingine, watengenezaji wa maudhui na wanaojulikana kama “news influencers” wanaendelea kupata nafasi katika mazingira ya habari. Hata hivyo, ripoti inaonyesha kuwa kwa watu wengi hawawezi kuchukua nafasi ya vyombo vya habari vya kawaida. Ni asilimia 10 pekee ya washiriki waliodai kuwa mahitaji yao yote ya habari yanatimizwa kupitia watu hao.

Imani kwa habari inaendelea kushuka

Moja ya matokeo yanayotia wasiwasi zaidi ni kuendelea kupungua kwa imani kwa habari. Katika nchi 29 kati ya 48 zilizoshiriki utafiti huo, kiwango cha imani kwa habari kilishuka kwa angalau alama tatu ndani ya mwaka mmoja.

Takribani asilimia 20 ya watumiaji wa YouTube hutazama video za zaidi ya dakika 20, huku idadi kama hiyo ikifuatilia matangazo ya habari ya moja kwa moja.Picha: Florian Görner/DW

Kwa sasa ni asilimia 37 tu ya washiriki duniani wanaosema wanaamini habari mara nyingi, ikilinganishwa na asilimia 40 mwaka uliopita.

Licha ya changamoto hizo zote, Egan anasisitiza kwamba uandishi wa habari bado una umuhimu mkubwa katika jamii. Anasema katika kipindi cha ongezeko la sintofahamu, migogoro na taarifa zisizo sahihi, watu wengi bado wanahitaji habari za kuaminika zinazowasaidia kuelewa ulimwengu unaowazunguka.

Utafiti wa Reuters Digital News Report 2026 ulihusisha takribani watu 100,000 katika nchi 48 duniani. Taasisi ya Reuters ya Chuo Kikuu cha Oxford ndiyo inayoratibu utafiti huo kila mwaka ili kufuatilia mabadiliko ya matumizi ya habari katika enzi ya kidijitali.

CantonaDigital
CantonaDigital

Listen Live Radio Fortune Africa
Ukweli Na Burudani.

-Be ready to be Impacted, Inspired & Empowered.

-Keep watching our Channels

Cantona Cast Television,

Fortune Television Network (FTN)

Donation
Paypal https://www.paypal.com/donate/?hosted_button_id=6EKXMLNW8W6A2&fbclid=IwY2xjawQxeChleHRuA2FlbQIxMABicmlkETFRdkNBRndpclRDQTB5bXZZc3J0YwZhcHBfaWQQMjIyMDM5MTc4ODIwMDg5MgABHq960uGsyU3ABRIBc2h-iXGhHATvuEqe55gFsQ-rDb0fT-Z7SIQ3TV8LnkpD_aem_ybU2SvBlvyqrVsS9NAczRw

An attitude determines an altitude.

All Rights Reserved © Cantona Group PLC||2025

5,520 posts
0 followers

Fediverse Followers


Discover more from cantona.digital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a Reply

Trending

Discover more from cantona.digital

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading

Discover more from cantona.digital

Subscribe now to keep reading and get access to the full archive.

Continue reading