Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa


Rais Trump anasema mateka waliosalia ambao wanaaminika kuwa hai wataachiwa kufikia Jumatatu au Jumanne.
Na:Cantona Joseph|RFA
Israel yaidhinisha mpango wa Trump wa usitishaji mapigano Gaza na kuachiliwa kwa mateka

Serikali ya Israel imethibitisha rasmi kuidhinisha mpango wa kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza pamoja na mpango wa kuwaachilia mateka, kwa mujibu wa taarifa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu.
“Serikali imeidhinisha mfumo wa kuwaachilia mateka wote walio hai na waliopoteza maisha,” imesema taarifa hiyo. Hata hivyo msemaji wa serikali ya Israel amesema kwamba Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) litajipanga upya katika mstari mpya mara baada ya kuanza kwa usitishaji mapigano, hatua itakayowaacha wakidhibiti takribani asilimia 53 ya Ukanda wa Gaza.
Hatua hiyo hata hivyo imewakera wakosoaji wa mpango huo, akiwemo mjumbe mmoja wa siasa kali za mrengo wa kulia ambaye aliishutumu Marekani kwa “kufikia amani na Hitler”.
Hatua hii inafungua njia kwa usitishaji mapigano kuanza kutekelezwa. Pia na mwanzo wa mfululizo wa hatua zingine ambazo zitawezesha kuachiliwa kwa mateka katika siku chache zijazo.
Hamas sasa inatarajiwa kuanza kuhamisha mateka, na inatayarisha miili ya mateka ambao wamekufa. Hamas pia inatafuta miili ya baadhi ya mateka hao, ambayo imefukiwa chini ya vifusi.
Huku hayo yakijiri Israel inajiandaa kuachiliwa kwa wafungwa wa Kipalestina ambao kuachiliwa kwao kumekumbwa na utata mkubwa.
Umoja wa Mataifa unatarajiwa kutoa msururu wa misaada ya kiutu kama sehemu ya awamu ya kwanza ya mpango wa Trump wa kusitisha mapigano.
Mpango huo umeidhinishwa – hiki ndicho kitakachofanyika katika siku zijazo
Hatua ya Israel kutia saini m[ango wa kusitisha mapigano huko Gaza inatoa nafasi ya utekelezaji wa masuala kadhaa – katika kipindi cha muda mfupi na mrefu.
Haya hapa ni mambo manne ambayo yanatarajiwa kufanyika mara moja baada ya makubaliano kukamilika:
1. Kusitishwa kwa mapigano huko Gaza
Baada ya makubaliano hayo kuidhinishwa rasmi na baraza la mawaziri la Israel, usitishaji mapigano unatarajiwa kuanza kutekelezwa.
Ripoti katika vyombo vya habari vya Israel zinaonyesha kuwa hili litafanyika mara moja, msemaji wa ofisi ya waziri mkuu amesema hatua hiyo itaanza kutekelezwa ndani ya saa 24 baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri.
2. Wanajeshi wa Israel wataondoka
Jeshi la Israel litajiondoa vitani lakini itaendelea kudhibiti takriban 53% ya Ukanda huo, msemaji huyo alisema. Kulingana na ramani iliyosambazwa na Ikulu ya White House wiki iliyopita, hii ni hatua ya kwanza kati ya hatua tatu za kujiondoa kwa Israel.
3. Kubadilishana mateka na miili ya waliofariki
Baada ya hayo, Hamas inatarajiwa mkuwaachilia mateka wote 20 wanaoaminika kuwa hai ndani ya muda wa saa 72. Hatua hiyo pia itajumuisha kurejeshwa kwa miili ya mateka 28 waliofariki, ingawa haijabainika hilo litachukuwa muda gani.
Israel itawaachilia wafungwa 250 wa Kipalestina wanaotumikia vifungo vya maisha katika jela za Israel na wafungwa 1,700 kutoka Gaza, chanzo kimoja cha Wapalestina kiliiambia BBC.
Israel pia itarudisha miili 15 ya watu wa Gaza kwa mabaki ya kila mateka wa Israel, kulingana na mpango wa Trump.
4. Msaada kuiingia Gaza
Mamia ya malori yaliyobeba misaada pia yataanza kuingia Gaza, ambako njaa ilithibitishwa na wataalam wanaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa mwezi Agosti.
Simu janja na skrini ni chanzo cha janga la kutengana katika familia – Binti mfalme wa Wales

Binti mfalme wa Wales, Catherine Middleton, ameonya kwamba matumizi kupita kiasi ya simu janja na skrini za kompyuta yamesababisha kile alichokiita “janga la kutengana” ambalo linavuruga maisha ya kifamilia.
Kupitia tahariri aliyoiandika kwa ushirikiano na Profesa Robert Waldinger kutoka Chuo Kikuu cha Tiba cha Harvard, Catherine anasema kuwa, “Ingawa vifaa vya kidijitali vinaahidi kutuweka karibu, mara nyingi hufanya kinyume chake.”
Anabainisha kuwa simu janja na vifaa vingine vya teknolojia vimegeuka kuwa “mashine za kutuvuruga kila mara,” vinavyotatiza umakini wetu na kuharibu muda wa thamani unaotumika pamoja kama familia.
“Tupo kimwili lakini kiakili hatupo hatuwezi kushiriki kikamilifu na wale walioko mbele yetu,” ameandika Catherine katika insha hiyo, ambayo ni sehemu ya kampeni yake ya kuhamasisha uelewa kuhusu umuhimu wa malezi katika miaka ya awali ya mtoto.
Kwa mujibu wa tafiti, binti wa kifalme wa Wales anasisitiza kuwa mahusiano ya karibu, yenye afya na joto ndani ya familia huleta manufaa ya maisha ya muda mrefu kimwili na kiakili.
Hata hivyo, anatahadharisha kwamba mwenendo wa sasa wa kijamii unakwenda kinyume, huku watu wengi wakiishi katika hali ya upweke na kutengwa, na familia zikishindwa kupeana umakini wa kutosha.
“Tunaposhika simu wakati wa mazungumzo, kuburuta mitandao ya kijamii wakati wa chakula cha familia, au kujibu barua pepe huku tukicheza na watoto wetu hatupotezi tu umakini, bali pia tunapunguza upendo wa msingi unaohitajika katika mahusiano ya kibinadamu,” ameandika.
Ameeleza kuwa tatizo hili ni kubwa zaidi kwa watoto wa kizazi cha sasa ambao wanakua katika “mazingira yaliyojaa teknolojia ya kidijitali.”
Hali hii, anasema, inaweza kudhoofisha uwezo wao wa kuendeleza uhusiano wa karibu, kuwasiliana kwa ufanisi na kustawi kihisia.
Mwaka 2021, Catherine alianzisha Royal Foundation Centre for Early Childhood, taasisi inayolenga kuongeza uelewa na kuchochea tafiti kuhusu umuhimu wa miaka ya awali katika maisha ya mtoto.
Lengo ni kuhakikisha kwamba watoto wanapokea malezi bora ambayo yatawasaidia kustawi kwa afya bora kimwili, kiakili na kijamii kwa maisha yao yote.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.