Serikali ya Kenya yalaani kitendo cha aibu cha kumrushia rais kiatu

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Rais William Ruto amekuwa akihutubia umati wa watu katika ziara yake magharibi mwa Kenya

Serikali ya Kenya imeelezea tukio la kurushiwa kiatu kwa Rais William Ruto kama la “aibu” na lisilokubalika, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Jumapili.

Video zilizosambaa katika mitandao ya kijamii zinaonyesha kiatu kikimgonga rais kwenye mkono wa kushoto alipokuwa ameuinua juu akizungumza.

Msemaji wa serikali, Isaac Mwaura, alilaani tukio hilo na kuitaka mamlaka husika kuwakamata waliohusika.

“Je, nini kingetokea kama sote tungeamua kurushiana viatu? Ni maadili gani tunayowafundisha watoto wetu?” alihoji kupitia chapisho lake katika mtandao wa X, akisisitiza umuhimu wa kuheshimu taasisi ya urais.

Vyombo vya habari nchini Kenya vimeripoti kuwa watu watatu wamekamatwa wakihusishwa na tukio hilo, ingawa polisi bado hawajathibitisha rasmi. Wabunge kadhaa pia wamekosoa tukio hilo la kurusha kiatu, wakilitaja kama dosari kubwa ya kiusalama.

Dennis Itumbi, afisa waandamizi katika ofisi ya rais, alilitaja tukio hilo kama “tukio ambalo lisingeweza kudhibitika,” akidokeza kuwa huenda lilikuwa la bahati mbaya.

Kupitia Facebook, alichapisha video nyingine kutoka pembe tofauti, akisema ilimuonyesha mtu mmoja akiinua kiatu kwa utani, akidanganya kuwa ni kamera, na mtu mwingine akikipiga kwa hasira kwa kuwa kilikuwa kimezuia mtazamo wake.

“Kwa bahati mbaya, kilirushwa mbele… moja kwa moja hadi kwa rais,” alisema.

Rais Ruto alikuwa akihutubia umati katika hafla ya umma katika kaunti ya Migori, magharibi mwa Kenya, akiwa katika ziara ya siku tatu kuzindua na kufungua miradi ya maendeleo katika eneo hilo.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a Reply