Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mlinzi mkuu wa Bobi Wine, Edward Sebuufu almaarufu Eddie Mutwe,amefunguliwa mashtaka ya uhalifu wa kutumia silaha,kwa mujibu wa wakili wake.
Hata hivyo haijafafanuliwa zaidi kuhusu uhalifu huo.
Eddy ambaye haikufahamika alipokuwa kwa siku kadhaa, alipatikana ametupwa katika Mahakama Kuu ya mji wa Masaka, kusini mwa Uganda, umbali wa takribani kilomita 130 kutoka mji mkuu Kampala.
Wakili wa Eddie Mutwe alisema mteja wake aliteswa.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu kwa muda mrefu yamekuwa yakishutumu mamlaka nchini Uganda kwa kukandamiza upinzani hasa wakati wa kuelekea uchaguzi.
Maafisa wa usalama nchini Uganda walijaribu kuzuia vyombo vya habari kumwona Eddi Mutwe alipokuwa akifikishwa mahakamani.
Lakini video zilionyesha mlinzi wa Bobi Wine akiwa hana viatu, na hawezi kutembea.
Wakili wake anasema mteja wake alipigwa mwili mzima kwa ‘shoti’ ya umeme akiwa chini ya ulinzi wa jeshi.
Kupitia chapisho la mitandao ya kijamii, kiongozi wa upinzani Bobi Wine alisema kuwa mlinzi wake amepigwa na kuteswa vibaya.
Eddie Mutwe ni mlinzi mkuu wa Bobi Wine—msanii wa muziki aliyegeukia siasa na kuwa mpinzani mkubwa wa rais wa muda mrefu nchini Uganda, Yoweri Museveni.
Inaripotiwa kuwa Edward Sebuufu alitekwa Aprili 27 na watu wasiojulikana waliovaa sare za kiraia na za kijeshi, katika mji wa Kiwango katikati mwa Uganda, jambo lililosababisha ghadhabu na hofu kubwa miongoni mwa wananchi.
Baada ya kutoweka kwake, Mkuu wa majeshi ya Uganda na kijana wa Rais Museveni, Muhoozi Kainerugaba, alidai kupitia mitandao ya kijamii kuwa alikuwa akimshikilia kwenye handaki lake.
Aidha, alitoa vitisho vya kutumia nguvu dhidi yake, jambo lililoibua taharuki zaidi.
Wanaharakati mbalimbali wa haki za binadamu wamelaani kushikiliwa kwa Sebuufu na jeshi, huku Tume ya Haki za Binadamu ya Uganda nayo ikitoa wito wa kuachiliwa kwake mara moja.
Wakati huohuo, mashirika ya kijamii yameonya kuwa kukamatwa kwake ni sehemu ya kampeni ya kimfumo ya kuwakandamiza wapinzani na kuzima sauti za upinzani kuelekea uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika mwaka ujao.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.