Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na : Cantona Joseph|RFA

Mwanaume mmoja ameteketea kwa moto katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Melbourne baada ya ‘power bank’ ya lithiamu iliyokuwa mfukoni mwake kulipuka, jambo lililosababisha majeraha ya kuchoma mguu na vidole.
Mwanaume huyo, mwenye umri wa takriban miaka 50, alikuwa katika ukumbi wa wageni wa Qantas asubuhi ya Alhamisi Novemba 6, 2025 wakati power bank hiyo ilipo lipuka moto, ikijaza eneo hilo la kifahari na moshi, na kusababisha watu takriban 150 kuhamishwa haraka.
Wafanyakazi walimsaidia na huduma za dharura kabla ya wahudumu wa afya kumtibu.
Baadaye alipelekwa hospitalini akiwa katika na afueni na kisha akaruhisiwa kwenda nyumbani.
Shuhuda wa tukio hilo amesema aliona “asidi ya betri ikirushwa kila mahali,” kulingana na gazeti la The Age.
Msemaji wa Qantas alisema ukumbi huo ulisafishwa na kufunguliwa tena baada ya saa mbili.
Qantas kwa sasa inakagua sera yake kuhusu abiria kubeba aina yoyote ya betri za lithiamu, ikiwemo power banks, na inatarajiwa kutoa mwongozo mpya hivi karibuni.
Ndege nyingi sasa zinashauri abiria kubeba power banks karibu nao, ama kwenye mfuko wa kiti au begi chini ya kiti, na si kwenye kabati la mizigo ya juu.
Mnamo Julai, moto ulizuka kwenye ndege ya Virgin Australia kutoka Sydney hadi Hobart, ukichochewa na power bank iliyokuwa kwenye kabati la mizigo ya juu.
Power bank ya kubebeka pia inashutumiwa kuwa chanzo cha moto ulioungua na kuharibu ndege ya abiria nchini Korea Kusini Januari mwaka huu.
Ndege kadhaa za kimataifa kama Emirates, Cathay Pacific, China Airlines, Korean Air, na Singapore Airlines zimepiga marufuku kutumia power banks na kuzi-chaji wakati wa ndege.
Pia kuna vikwazo vya idadi ya betri zinazoweza kubebwa kulingana na uwezo wake; baadhi ya ndege zinaruhusu power banks mbili tu zenye uwezo kati ya 100Wh hadi 160Wh.
IGP na wenzake watano waitwa mahakamani kwa kesi ya John Heche

Mahakama Kuu Dar es Salaam imetoa hati ya wito kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Camillus Wambura na wenzake watano kufika mahakamani, kufuatia ombi la mawakili wa CHADEMA wanaotaka Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, afikishwe mahakamani au aachiwe kwa dhamana.
Wengine waliopewa wito ni Afisa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji.
Naibu mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Chadema nchini Tanzania John Heche, ambaye alikamatwa siku kumi na saba zilizopita leo alisafirishwa kutoka dodoma hadi mji mkuu wa Dar es Salaam, ambako amehojiwa na maafisa wa polisi kuhusiana na tuhuma kadhaa.
Wakili wa bwana Heche, Hekima Mwasipu ameiambia BBC kuwa Heche anazuiliwa katika kituo kimoja cha polisi baada ya kufahamishwa kuwa anakabiliwa na mashtaka mawili ya ugaidi.
Ombi hilo litasikilizwa Novemba 7, 2025 saa 4:30 asubuhi katika mahama kuu ya Dar es Salaam.Kufikia sasa hakuna kilichowekwa wazi kuhusu usikilizwaji wa ombi hilo.

Ni makamu mwenyekiti wa chama cha upinzani Tanzania CHADEMA
Waliodhulumiwa na LRA wa Uganda wataka Joseph Kony kukamatwa haraka baada ya ICC kuthibitisha mashtaka 39 dhidi yake

Waliodhulumiwa na Lord’s Resistance Army (LRA) nchini Uganda wametoa wito atiwe nguvuni kiongozi wake, Joseph Kony.
Hii inatokea siku moja baada ya mahakimu wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) Hague kuthibitisha mashtaka 39 ya uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu dhidi yake, yakiwemo mauaji, utumwa, na mateso.
Hii ni mara ya kwanza kwa ICC kuthibitisha mashtaka dhidi ya mtuhumiwa asiyekuwepo mahakamani.
Hata hivyo, kesi haiwezi kuendelea bila Joseph Kony kuwa mahakamani.
Patrick Ochieng alilazimishwa na LRA kuwa askari mtoto.
“Anapaswa kwanza kushikiliwa, na mashtaka yote yafikishwe dhidi yake. Hata hivyo, waathirika walioteswa hawawezi kusubiri, baadhi ya waathirika hawa pia wanakufa,” alisema Patrick Ochieng.
Zaidi ya watu 100,000 waliuawa katika kampeni za kigaidi za LRA. Lakini Kony hajawahi kuonekana hadharani kwa takriban miaka ishirini, na hakujulikani kama bado yuko hai.
Kony, kiongozi wa Lord’s Resistance Army (LRA), anashutumiwa kwa mashtaka 39 yakiwemo mauaji, ubakaji, kutumia watoto kama askari, utumwa wa ngono na mimba ya kulazimishwa, kati ya mwaka 2002 hadi 2005.
COP 30: Viongozi wa dunia wamshutumu Trump kwa msimamo hasi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi

Viongozi kadhaa wa dunia waliokusanyika Brazil kwa mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira COP30 wamemshutumu Rais Donald Trump kwa msimamo wake hasi kuhusu mabadiliko ya tabia nchi.
Marais wa Chile na Colombia wamemtaja kiongozi huyo wa Marekani kuwa muongo kwa kupingana na sayansi kuhusu ongezeko la joto duniani.
Marekani haihudhurii mkutano huo wa COP30 unaofanyika katika mji wa Belem nchini Brazil.
Viongozi wa China na India pia hawahudhurii mkutano huo wa kilele kuhusu mazingira.
Tesla imetoa kifurushi kikubwa cha malipo kwa Elon Musk

Wamiliki hisa wa Tesla wamemkubalia Elon Musk kifurushi cha malipo cha dola trilioni 1 ili aendelee kuongoza kampuni hiyo kwa miaka ijayo, huku Tesla ikiingia katika kipindi kipya kinachohusiana na akili unde (AI).
Ingawa baadhi ya watu walipinga kifurushi hicho wakisema ni kikubwa sana na haifai, wakirejelea baadhi ya shughuli za Musk nje ya Tesla zilizoweza kuathiri sifa ya kampuni, ikiwa ni pamoja na usimamizi wake kwenye huduma ya Marekani DOGE.
Hata hivyo, Musk ameongoza kampuni hadi kupata faida za kihistoria akiifanya Tesla kuwa kampuni ya magari yenye thamani kubwa zaidi duniani na kumfanya kuwa mtu tajiri zaidi duniani.
Mzozo wa DRC: Rwanda yashutumu ujumbe wa UN kwa mafunzo ya jeshi la DRC

Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Rwanda, Olivier Nduhungirehe, amekosoa ujumbe wa kueneza amani wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Monusco) kwa kutoa mafunzo kwa wanajeshi 120 wa Kongo.
Akiendeleza ukosoaji wake, katika chapisho lake jana Alhamisi Novemba 6, 2025 kwenye X, Nduhungirehe alidai kwamba Monusco inasaidia ukiukaji wa kusitisha mapigano kwa kusaidia jeshi la Kongo, ambalo anadai lina uhusiano na kundi la FDLR (Democratic Forces for the Liberation of Rwanda), kutumia silaha nzito na ndege zisizo na rubani.
Hata hivyo, Monusco ilitangaza tarehe 4 Novemba kwenye X kwamba mafunzo hayo, yaliyoelezwa rasmi kuwa kwa lengo la kuongeza ulinzi wa raia na uwezo wa kijeshi, yalilenga matumizi ya ndege zisizo na rubani, utunzaji wa silaha, na mbinu za uokoaji.
Mvutano kati ya Rwanda na DRC unaongezeka, huku Kinshasa ikidai kwamba Kigali inasaidia waasi wa M23.
Marekani inasukuma kwa suluhisho la haraka, huku mazungumzo mapya yakiwa yanaendelea Doha.
Rais wa Nigeria awataka mawaziri kuongeza juhudi za kupambana na ugaidi

Rais wa Nigeria Bola Tinubu amewaeleza mawaziri wake mjini Abuja kuwa sharti waongeze juhudi za kukabiliana na ugaidi na uhalifu wakati taifa hilo la magharibi mwa Afrika lilikabiliwa na shinikizo la kimataifa kushughulikia masuala ya kiusalama.
Hilo ndilo tamko lake la kwanza tangu Rais wa Marekani Donald Trump kutishia kuyatuma majeshi ya Marekani nchini Nigeria akidai waumini wa kikristo wa Nigeria wanauawa na wanamgambo wenye misimamo mikali ya Kiislamu.
Awali mshauri wake Daniel Bwala aliambia BBC kwamba hatua zozote za kijeshi dhidi ya makundi ya kijihadi zinapaswa kutekelezwa kwa pamoja.
Bwala alisema Nigeria itakaribisha msaada wa Marekani katika kukabiliana na wanamgambo wa kijihadi lakini akabainisha kuwa Nigeria ni nchi “huru”.
Kwa muda mrefu,Nigeria imekabiliwa na changamoto kubwa za kiusalama kaskazini mashariki mwa taifa hilo ambako kundi la waasi la Boko Haram limesababisha mauaji makubwa.
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa laondoa vikwazo dhidi ya Rais wa Syria Ahmed al Sharaa

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepiga kura kuondoa vikwazo dhidi ya Rais wa Syria Ahmed al Sharaa.
Azimio hilo lililoandikwa na Marekani liliidhinishwa kuelekea mkutano kati ya Rais Donald Trump na bwana Al Sharaa unaotarajiwa kufanyika katika Ikulu ya White House Jumatatu ijayo.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Syria pia ameondolewa vikwazo.
Rais Al Sharaa aliwekewa vikwazo na Umoja wa Mataifa alipokuwa kiongozi wa kikosi cha wanamgambo cha HTS kilichokuwa na mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda miaka tisa iliyopita.
Kikosi hicho cha HTS kilikuwa mstari wa mbele katika kumng’oa madarakani Rais wa Syria Bashar al Assad mwaka jana.
Mzozo wa Sudan: Wanamgambo wa RSF wakubali kusitisha mapigano kuruhusu misaada ya kibinadamu

Wanamgambo wa kikosi maalum nchini Sudan wa Rapid Support Forces RSF,wamesema wamekubali kusitisha vita ili kuruhusu misaada ya kibinadamu nchini humo.
Hata hivyo Jeshi la Sudan halijakubaliana na mapendekezo hayo yaliyowasilishwa na Marekani na nchi za kiarabu.
RSF pia iko tayari kufanya mazungumzo kuhusu kukomesha uhasama kati yake na Jeshi katika kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa zaidi ya miaka miwili.
Tangazo hilo la RSF linakuja chini ya majuma mawili tangu wanamgambo hao kuudhibiti mji mkuu wa Darfur Kaskazini,El Fasher.
Aidha, wameshutumiwa kwa kuwaua raia wengi wa mji huo,miongoni mwa uvunjifu mwingine wa haki za kibinadamu kama unyanyasaji wa kingono.
Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Marekani amesema wanazihimiza pande zote mbili zinazozozana Sudan kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya jeshi la Sudan na RSF vilianza mwezi Aprili 2023.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.