Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Huduma ya gari la wagonjwa imesema watu wengine 11 wamejeruhiwa, wakiwemo sita walio katika hali mbaya wakiwa na majeraha ya risasi.

Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la risasi mjini Jerusalem imeongezeka hadi sita, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar.
Tukio jilo limetokea kwenye kituo cha basi nje kidogo ya mji wa Jerusalem siku ya Jumatatu, huduma ya ambulensi ya Israel imesema, huku polisi wakisema wahalifu hao wameuawa.
Haikuweza kufahamika mara moja ni nani aliyetekeleza shambulio hilo. Lakini kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas limewasifu “wapiganaji” wawili wa Kipalestina ambao limesema wamefanya shambulio hilo lakini Hamas haijadai kuhusika.
Islamic Jihad, kundi jingine la wanamgambo wa Kipalestina pia lilipongeza shambulio hilo lakini halikudai kuhusika.
Huduma ya gari la wagonjwa imesema watu wengine 11 wamejeruhiwa, wakiwemo sita walio katika hali mbaya wakiwa na majeraha ya risasi.
Polisi wa Israel wanasema washambuliaji wawili walifika kwa gari na kufyatua risasi kwenye kituo cha basi. Taarifa zinasema maafisa wa usalama na raia waliwapiga risasi na kuwaua washambuliaji.
Serikali ya Ufaransa iko ukingoni kuporomoka

Madeni makubwa ya Ufaransa yanaiweka serikali ya nchi hiyo mashakani, ameonya Waziri Mkuu wa taifa hilo François Bayrou kabla ya kura kuhusu kuaminika siku ya Jumatatu.
Bayrou, waziri mkuu wa nne wa Rais Emmanuel Macron katika kipindi cha chini ya miaka miwili, aliita kura ya imani juu ya shinikizo kubwa linaloikabili Ufaransa kuhusu kushughulikia fedha zake, na nakisi ya mwaka jana karibu mara mbili ya kikomo cha 3% cha pato la kiuchumi la Umoja wa Ulaya na deni la umma la 113.9% ya Pato la Taifa.
Waziri huyo ameonya katika bunge kwamba serikali yoyote inayofuata itakabiliwa na matatizo kama hayo.
“Mna uwezo wa kuiangusha serikali, lakini hamna uwezo wa kufuta ukweli. Ukweli utabaki kwamba: gharama zitaendelea kupanda, na mzigo wa madeni, ambao tayari hauwezi kuvumilika, utakua mkubwa na wa gharama kubwa,” Bayrou aliwaambia wabunge.
Vyama vya upinzani vimeweka wazi kuwa havikubaliani naye kuhusu jinsi ya kushughulikia deni hilo, na vitapiga kura dhidi ya serikali ya wachache ya Bayrou.
Kuporomoka kwa serikali ya wachache kunatazamiwa kuzidisha matatizo ya Ufaransa katika wakati muhimu kwa Ulaya, ambayo inatafuta umoja katika kukabiliana na vita vya Russia dhidi ya Ukraine, China inayozidi kutawala na mivutano ya kibiashara na Marekani. Msukosuko huo pia unatishia uwezo wa Ufaransa wa kudhibiti deni.
Mwanamke aliyewaua wakwe zake afungwa miaka 33

Mwanamke raia wa Australia aliyepatikana na hatia ya kuwaua jamaa watatu wa mume wake walioachana kwa kuwapa chakula chenye uyoga wenye sumu amehukumiwa kifungo cha miaka 33 jela siku ya Jumatatu, katika mojawapo ya vifungo virefu zaidi kuwahi kutolewa kwa mwanamke nchini humo.
Hakimu mfawidhi alisema Erin Patterson (50) hakuwahurumia wakwe zake wazee baada ya kuwapa nyama ya Ng’ombe iliyotiwa uyoga wenye sumu.
Patterson alipatikana na hatia mwezi Julai kwa kumuua mama mkwe wake, Gail Patterson, baba mkwe, Donald Patterson na dadake Gail, Heather Wilkinson, katika kesi ambayo imekuwa ikifuatiliwa duniani kote na kupewa jina la mauaji ya uyoga.
Baraza la majaji pia lilimpata na hatia ya jaribio la kumuua Ian Wilkinson, mume wa Heather, ambaye alinusurika mwaka 2023 nyumbani kwa Patterson huko Leongatha, mji wa ulio kilomita 135 (maili 84) kusini mashariki mwa Melbourne.
Wafungwa wa Kipalestina hawapewi chakula cha kutosha – Mahakama ya Israel

Mahakama ya Juu ya Israel imetoa hitimisho kuwa taifa hilo linashindwa kuwapa chakula cha kutosha wafungwa wa Kipalestina, na lazima lichukue hatua za kuboresha lishe yao.
Majaji watatu walisema siku ya Jumapili kwamba serikali ya Israel ina wajibu wa kisheria kuwapa wafungwa chakula cha kutosha.
Maelfu ya Wapalestina wamezuiliwa katika jela za Israel kwa miaka mingi, ikiwa ni pamoja na mashtaka ya ugaidi – na maelfu ya wengine wamezuiliwa tangu vita vya Gaza kuanza Oktoba 2023.
Mazungumzo ya kusitisha mapigano yamekwama lakini Jumapili usiku Rais wa Marekani Donald Trump alitoa “onyo la mwisho” kwa Hamas, akiwataka kukubali makubaliano ya kuwaachilia mateka wa Israel kutoka Gaza.
Hamas ilijibu katika taarifa na kusema iko tayari “kuketi mara moja kwenye meza ya mazungumzo” kufuatia “mawazo kutoka upande wa Marekani yenye lengo la kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano”.
Wafungwa wa Kipalestina walioachiliwa huru wameiambia BBC walitendewa vibaya na kuteswa mikononi mwa wanajeshi wa Israel na wafanyakazi wa magereza.
Daktari anayetuhumiwa kuwawekea wagonjwa sumu huku 12 wakifariki apandishwa kizimbani

Aiyekuwa daktari wa nusukaputi amefikishwa mahakamani katika mji wa Besançon, mashariki mwa Ufaransa, akituhumiwa kuwapata sumu kwa makusudi watu 30, wakiwemo wagonjwa 12 waliofariki.
Frédéric Péchier, 53, aliwekwa chini ya uchunguzi miaka minane iliyopita, aliposhukiwa kuwapa wagonjwa sumu katika kliniki mbili za jiji kati ya 2008 na 2017.
Licha ya mashtaka mazito dhidi yake, Péchier amesalia huru chini ya uangalizi wa mahakama na aliiambia redio ya Ufaransa Jumatatu “hakuna uthibitisho wa sumu yoyote.”
Kesi hiyo inatarajiwa kudumu kwa zaidi ya miezi mitatu na inahusisha zaidi ya raia 150 wanaowakilisha waathiriwa 30.
Madai ya sumu yaliibuka Januari 2017, wakati mgonjwa mwenye umri wa miaka 36 anayeitwa Sandra Simard, aliyekuwa mzima wa afya, alipofanyiwa upasuaji kwenye mgongo wake na moyo wake ukaacha kupiga.
Baada ya daktari wa wagonjwa mahututi kushindwa kuuamsha moyo, Frédéric Péchier alimdunga sindano na mgonjwa huyo alipata koma na baadaye kuamka. Dawa aliyotumia kumdunga ilionyesha kiwango cha potasiamu mara 100 ya kipimo kilichotarajiwa.
Mmoja wa mawakili wa Péchier amesema yuko tayari kuthibitisha kuwa hana hatia, na daktari huyo wa zamani ameiambia redio ya RTL Jumatatu kwamba ni fursa ya kuweka mambo sawa.
Kesi kumi na mbili za kutiliwa shaka zinazohusisha wagonjwa ambao hawakuweza kuamka zinamkabili.
Damien Iehlen alifariki Oktoba 2008. Akiwa na umri wa miaka 53 alikwenda katika Kliniki ya Saint-Vincent ambako mtuhimiwa alikuwa akifanya kazi, kwa ajili ya upasuaji wa kawaida wa figo na alifariki baada ya mshtuko wa moyo. Uchunguzi ulionyesha alikuwa amepewa kiwango kikubwa cha dawa ya lidocaine.
Frédéric Péchier anatoka katika familia ya wataalamu wa afya; baba yake pia alikuwa daktari wa ganzi.
Kesi hiyo imepangwa kuendelea hadi Desemba na mshtakiwa ataendelea kuwa huru, chini ya uangalizi wa mahakama. Ikiwa atapatikana na hatia atakabiliwa na kifungo cha maisha.
19 wameuawa katika maandamano ya kupinga marufuku ya mitandao ya kijamii

Takriban watu 19 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa nchini Nepal baada ya maandamano ya kupinga marufuku ya serikali ya mitandao ya kijamii na kusababisha vurugu kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama.
Maelfu ya waandamanaji wanaojiita Generation Z walikusanyika karibu na jengo la bunge huko Kathmandu kupinga uamuzi wa kupiga marufuku Facebook, X na YouTube.
Waziri wa Mawasiliano wa Nepal Prithvi Subba aliiambia BBC polisi walilazimika kutumia nguvu – ikiwemo maji ya kuwasha, marungu na kurusha risasi za mpira.
Serikali imesema majukwaa ya mitandao ya kijamii yanahitaji kudhibitiwa ili kukabiliana na habari ghushi, matamshi ya chuki na ulaghai mtandaoni.
Waandamanaji walibeba mabango wakipinga kile walichokiita tabia ya kimabavu ya serikali.
Serikali ya Nepal imejitetea kuwa haipigi marufuku mitandao ya kijamii bali inataka iendeshwe kulingana na sheria za Nepal.
Baba aliyetorokea msituni na watoto kwa miaka minne apigwa risasi na kuuawa

Mwanaume mmoja ambaye alitoroka na watoto wake watatu na kwenda nao msituni huko New Zealand kwa karibu miaka minne ameuawa kwa kupigwa risasi na polisi.
Tom Phillips, alitoweka na watoto wake mwishoni mwa 2021, alikwepa kukamatwa licha ya kutafutwa kote nchini.
Phillips aliuawa katika majibizano ya risasi siku ya Jumatatu, ambapo afisa wa polisi alijeruhiwa vibaya, serikali imesema.
Maafisa walikuwa wakijibu tukio la wizi lililoripotiwa huko Piopio, mji mdogo kaskazini mwa New Zealand, wakati Phillips na mmoja wa watoto wake walipoonekana na pikipiki ya magurudumu manne.
Maafisa wa polisi waliwafukuza kabla ya kuweka miiba barabarani kuwazuia. Pikipiki hiyo iligonga miiba na kwenda nje ya barabara.
Polisi walipofika kwenye pikipiki walikutana na milio ya risasi, Naibu Kamishna wa Polisi Jill Rogers aliwaambia waandishi wa habari.
Afisa wa kwanza katika eneo la tukio alipigwa risasi kichwani, na bado yuko katika hali mbaya, polisi wamesema.
Kitengo cha pili cha doria kilipambana na Phillips, ambaye alipigwa risasi na kufariki katika eneo la tukio. Awali mwili huo ulikuwa haujatambuliwa rasmi.
Watoto wengine wawili walipatikana baadaye mchana kwenye kambi katika msitu mnene. Watoto wote watatu hawajajeruhiwa, amesema Rogers.
Mtoto aliyekuwa naye, alitoa habari “muhimu” iliyowasaidia kupatikana watoto wengine wawili wa Phillips.
Haijawa wazi iwapo watoto hao wamefahamishwa kuhusu kifo cha baba yao.
Polisi wametoa taarifa kwa mama yao na wazazi wa Phillips kuwa watoto hao wako salama.
Mama wa watoto hao, anayejulikana kwa jina la Paka, alikiambia chombo cha habari cha RNZ kuwa “amefarijika sana” kwamba “tatizo hilo limefikia kikomo” baada ya kutokuwa na watoto wake kwa karibu miaka minne.”
Lakini, aliendelea: “Tunasikitishwa na jinsi mambo yalivyotokea leo.”
Serikali inasema Phillips amekuwa akikwepa kukamatwa tangu kushindwa kufika mahakamani mwaka 2022.
Kabla ya kutoweka, Phillips na watoto wake walikuwa wakiishi Marokopa, mji mdogo wa mashambani katika eneo la Waikato.
Phillips, anayeaminika kuwa na umri wa miaka 30, ni mwindaji mwenye uzoefu wa wayama wa msituni.
Polisi wanaamini kuwa aliwachukua watoto wake baada ya kupoteza ulezi kisheria.
Tangu 2023, Phillips na watoto wake wamehusishwa na visa vingi vya wizi katika maduka ya vifaa na maduka ya vyakula.
Watu sita wameuawa kwa kupigwa risasi huko Jerusalem

Idadi ya watu waliouawa katika shambulizi la risasi mjini Jerusalem imeongezeka hadi sita, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya nje wa Israel Gideon Saar.
Tukio jilo limetokea kwenye kituo cha basi nje kidogo ya mji wa Jerusalem siku ya Jumatatu, huduma ya ambulensi ya Israel imesema, huku polisi wakisema wahalifu hao wameuawa.
Haikuweza kufahamika mara moja ni nani aliyetekeleza shambulio hilo. Lakini kundi la wanamgambo wa Palestina Hamas limewasifu “wapiganaji” wawili wa Kipalestina ambao limesema wamefanya shambulio hilo lakini Hamas haijadai kuhusika.
Islamic Jihad, kundi jingine la wanamgambo wa Kipalestina pia lilipongeza shambulio hilo lakini halikudai kuhusika.
Huduma ya gari la wagonjwa imesema watu wengine 11 wamejeruhiwa, wakiwemo sita walio katika hali mbaya wakiwa na majeraha ya risasi.
Polisi wa Israel wanasema washambuliaji wawili walifika kwa gari na kufyatua risasi kwenye kituo cha basi. Taarifa zinasema maafisa wa usalama na raia waliwapiga risasi na kuwaua washambuliaji.
Aliyekuwa sajenti meja anakiri kumnyanyasa kingono askari aliyejiua

Sajenti wa zamani wa Jeshi nchini Uingereza amekiri kosa la kumnyanyasa mwanajeshi wa kike ambaye alijitoa uhai baada ya kuingiwa na hofu kutokana na tukio hilo.
Mwanajeshi huyo wa Kifalme Jaysley Beck, ambaye alikuwa na umri wa miaka 19, alipatikana akiwa amekufa kwenye kambi yake huko Larkhill huko Wiltshire mnamo 15 Desemba 2021.
Alikuwa amewasilisha malalamiko dhidi ya Sajenti Batri Michael Webber baada ya kumkandamiza na kujaribu kumbusu kwenye hafla ya kijamii ya kazini.
Webber, ambaye ameacha kazi ya Jeshi, alikiri shtaka moja la unyanyasaji wa kijinsia katika kikao cha kabla ya kesi Ijumaa iliyopita. Sasa anasubiri hukumu.
Katika taarifa yake, mama yake Gunner Beck, Leighann McCready, alisema: “Tunafarijika kwamba Michael Webber amekiri hatia yake na hajatuweka kwenye kiwewe cha kesi zaidi za kisheria, lakini hakuna kinachoweza kutengua hasara ya kumpoteza binti yetu mrembo Jaysley.”
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.