Na Cantona Joseph Julai 03, 2026 16:00 (EAT
Siasa Mashariki ya Kati

Maelfu wajitokeza kwa shughuli ya umma ya kumuaga aliyekuwa Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei, aliyeuawa Februari 28 katika shambulizi la Israel na Marekani.Picha: Mohammed Salem/REUTERS
Maelfu ya watu wamekusanyika mjini Tehran, Iran, kutoa heshima zao za mwisho kwa Kiongozi Mkuu wa nchi hiyo, Ayatollah Ali Khamenei, aliyeuawa katika shambulio la anga lililofanywa kwa pamoja na Marekani na Israel.
Shughuli rasmi za maombelezo zimeanza leo na zitadumu kwa siku sita.
Jeneza la Khamenei aliyeuawa akiwa na miaka 86, litawekwa hadharani mjini Tehran hadi Jumatatu kabla ya kusafirishwa kwenda mji mtakatifu wa Qom, kisha Iraq, na hatimaye kuzikwa katika mji wake wa kuzaliwa wa Mashhad siku ya Alhamisi.
Waombolezaji wengi wameonekana wakibeba mabango mekundu yanayoashiria wito wa kulipiza kisasi. Wakati wa siku hizo sita, anga ya Iran na baadhi ya barabara katika miji husika zitafungwa kwa sababu za usalama.
Ukraine yashambulia miundo mbinu ya mafuta nchini Urusi
Siasa Ulaya

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky akihutubia waandishi wa habari huko Dublin, Ireland mnamo Julai 1, 2026Picha: Paul Faith/AFP
Jeshi la Ukraine limeshambulia leo miundombinu ya mafuta na vituo vya kijeshi karibu na mji wa St. Petersburg nchini Urusi. Haya ni kwa mujibu wa Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelenskyy.
Katika chapisho kwenye mtandao wa Telegram, Zelensky amesema vikosi vya ulinzi vya nchi yake vilishambulia miundombinu ya mafuta katika bandari inayoiingizia Urusi mapato ya kufadhili vita vyake, pamoja na Kronstadt, ambayo ni shabaha muhimu ya kijeshi iliyoko zaidi ya kilomita 850 kutoka mpaka wa Ukraine.
Wakati huo huo, Urusi imesema imedungua makumi ya droni za Ukraine zilizokuwa zimeelekezwa katika mji huo wa St. Petersburg. Haya ni kulingana na gavana wa mji huo, Alexander Beglov.
Beglov amesema shambulio hilo lililenga eneo la kituo cha kuhifadhi na kusafirisha mafuta katika Wilaya ya Kirovsky mjini St. Petersburg. Ameongeza kuwa athari za kiufundi zilizotokana na shambulio hilo zilidhibitiwa haraka na hakukuwa na majeruhi.
Pia amesema droni moja ilianguka katika eneo la kihistoria la Peterhof, lakini haikusababisha uharibifu wowote.
Marekani yaadhimisha miaka 250 ya Uhuru wake
Siasa Marekani

Rais wa Marekani, Donald TrumpPicha: Evan Vucci/REUTERS
Rais wa Marekani Donald Trump katika hotuba yake ya usiku wa kuamkia leo Jumamosi siku ambayo Marekani, inaadhimisha miaka 250, amewaonya raia wake dhidi ya itikadi ya kikomunisti .
Akizungumza mbele ya wafuasi wake kwenye eneo la Kumbukumbu ya Kitaifa ya Mlima Rushmore eneo takatifu lililotengwa kwa ajili ya kuwakilisha msingi, maendeleo na Demokrasia ya Marekani katika jimbo la South Dakota,Trump amesema mtu anaweza kuchagua kati ya kuwa mkomunisti ama mzalendo.
Katika siku za hivi karibuni, Trump amekuwa akilitumia neno “ukomunisti” kuwakosoa wapinzani wake wa kisiasa wa mrengo wa kushoto na sera zao.
Trump pia ameielezea Marekani kama taifa linalomtegemea Mungu, akisema haki zao wamepewa na Mungu aliyewaumba, na hazitakiwi kuvunjwa.
Rais huyo mwenye umri wa miaka 80 pia amesema hakuna nchi nyingine iliyoitendea mema zaidi dunia kuliko Marekani.
Maelfu zaidi ya raia wa kigeni waondoka Afrika Kusini

Raia wa Zimbabwe wakiondoka Cape Town, Afrika Kusini mnamo Juni 30, 2026Picha: Rodger Bosch/AFP
Maelfu ya raia wa kigeni wameendelea kuondoka Afrika Kusini kutokana na kampeni inayowataka wahamiaji haramu kuondoka nchini humo.
Shirika la Usimamizi wa Mipaka la Afrika Kusini limesema zaidi ya watu elfu 35 tayari wamerejeshwa au kufukuzwa nchini humo tangu Juni 7. Kampeni ya kuwataka wageni wasio na vibali kuondoka, imeambatana na maandamano ya vurugu yaliyosababisha vifo vya raia wanne wa kigeni, wakiwemo raia wa Msumbiji, Ethiopia na Malawi.
Kampeini ya kupinga wageni, imekuwa ikiongozwa na makundi ya raia wa Afrika Kusini ambayo yalitowa tarehe 30 mwezi Juni kuwa siku ya mwisho kwa wageni wasiokuwa na vibali kuondoka nchini humo.
Hata hivyo Waziri wa Sheria wa Afrika Kusini, Mmamoloko Kubayi, amesisitiza kuwa serikali pekee ndio iliyo na mamlaka ya kusimamia na kutekeleza sheria za uhamiaji na sio mtu mwengine yeyote na kwamba serikali iko tayari kulinda wananchi wote pamoja na raia wa kigeni dhidi ya vitisho na unyanyasaji wa aina yoyote.
Mali yakumbwa na mashambulizi mapya ya kupangwa
Siasa Afrika

Wapiganaji wa kundi la Ukombozi wa Watu wa Azawad (MSA) mjini Menaka mnamo Machi 14, 2020Picha: Souleymane Ag Anara/AFP
Wanamgambo wanaofuata itikadi kali na washirika wao wa Kituareg wanaotaka kujitenga, wamefanya mashambulizi mapya ya kupangwa nchini Mali leo Jumamosi, wakilenga miji kadhaa pamoja na gereza.
Mashambulizi hayo yaliripotiwa katika miji ya Gao, Anefis na Sevare, pamoja na gereza lililoko Kenieroba.
Mohamed Elmaouloud Ramadane, msemaji wa kundi la Touareg la Azawad Liberation Front (FLA) ameliambia shirika la Reuters kwamba wapiganaji wa kundi hilo waliushambulia mji wa Anefis, ulioko katika eneo la Kidal kaskazini mashariki mwa Mali, mapema leo.
Vikosi vya serikali pamoja na wanajeshi wa Urusi vilikuwa vimetumwa Anefis kufuatia mashambulizi ya Aprili, ambapo FLA na tawi la kikanda la Al-Qaeda waliteka udhibiti wa mji wa Kidal.
Katika mji wa Gao ulioko katikati mwa nchi, afisa mmoja wa eneo hilo amesema kulikuwa na milio ya risasi na makombora yaliyolengwa kwenye kambi ya kijeshi. Haikufahamika mara moja ni kundi gani lililohusika na mashambulizi hayo.
Msemaji wa serikali hakujibu ombi la Reuters la kutoa maoni kuhusu tukio hilo.
Ulaya yarekodi vifo 3,700 zaidi vinavyohusiana na joto kali
Janga Ufaransa

Wimbi la joto kali lilikumba bara la Ulaya katikati ya mwezi Juni na linatarajiwa kurejea mwezi huu wa JulaiPicha: Ebrahim Noroozi/AP Photo/picture alliance
Ulaya imerekodi maelfu ya vifo kote barani humo kufuatia wimbi la joto la wiki iliyopita, na hasa wazee. Nchini Ufaransa, waziri mkuu anakabiliwa na kura ya kutokuwa na imani kuhusu mgogoro huo.
Angalau vifo 3,700 zaidi vimerekodiwa nchini Ufaransa, Ubelgiji na Uholanzi pekee kutokana na wimbi la joto la Juni lililosababisha halijoto kupanda kwa zaidi ya nyuzi joto 40.
Wataalamu wamesema wimbi la joto kali la kati ya Juni 20-28, lilikuwa baya zaidi kuwahi kurekodiwa barani Ulaya, na mamlaka zimeonya kwamba takwimu hizo ni za awali na huenda zikaongezeka.

Leave a Reply