Umoja wa Mataifa waitaka Tanzania kuchunguza mauaji ya siku ya uchaguzi

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Na : Cantona Joseph|RFA

fv

Kamishna Mkuu wa Haki za Kibinadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Türk ametaka uchunguzi juu ya mauaji na ukiukaji wa haki za binadamu uliofanywa wakati wwa uchaguzi wa Oktoba 29 nchini Tanzania, huku ripoti zikiibuka kwamba miili inachukuliwa na vikosi vya usalama na kupelekwa katika maeneo ambayo hayajajulikana.

Taarifa zilizopatikana na Ofisi ya Haki za Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa kutoka vyanzo tofauti nchini Tanzania zinaonyesha mamia ya waandamanaji na watu wengine waliuawa na idadi isiyojulikana kujeruhiwa au kushikiliwa. Ofisi imeshindwa kuthibitisha kwa uhuru takwimu za majeruhi kutokana na hali tete ya usalama na kuzimwa kwa intaneti wakati wa kupiga kura.

“Taarifa za familia zinazosaka wapendwa wao kila mahali kwa kutembelea kituo kimoja cha polisi baada ya kingine na hospitali moja baada ya nyingine ni za kutisha. Naomba sana serikali ya Tanzania itoe taarifa kuhusu hatma na mahali walipo wote waliopotea, na kukabidhi miili ya waliouawa kwa wapendwa wao ili wazikwe kwa heshima,” amesema Türk.

“Pia kuna ripoti kwamba vikosi vya usalama vimeonekana vikiondoa miili kutoka mitaani na hospitalini na kuipeleka kwenye maeneo ambayo hayajajulikana katika jaribio la kuficha ushahidi.”

Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za binadamu ameitaka Tanzania kuchunguza madai haya mazito ya ukiukaji wa haki za binadamu, kikamilifu na kwa uwazi, na kuwawajibisha wale waliohusika.

Ametoa wito kwa mara nyingine kuachiwa huru bila masharti vigogo wote wa upinzani waliokamatwa kabla ya uchaguzi mkuu akiwemo kiongozi wa chama cha upinzani cha Chadema Tundu Lissu na watu wengine wote waliowekwa kizuizini tangu siku ya uchaguzi.

Inaarifiwa kuwa zaidi ya watu 150 wametiwa mbaroni tangu siku ya kupiga kura – wakiwemo watoto walioshtakiwa kwa uhaini.

“Ni muhimu wale wote waliokamatwa au kuzuiliwa kwa makosa ya jinai wawasilishwe mara moja mbele ya a mahakama. Na wale wote wanaozuiliwa lazima wapewe haki kamili chini ya sheria za kimataifa za haki za binadamu,” amesema Türk.

Vitu vya kale vya Ufalme wa Asante wa Ghana vyarudishwa kutoka Uingereza na Afrika Kusini

rf
Maelezo ya picha,Baadhi ya vitu vilivyoporwa kutoka ufalme wa Asante vilirejeshwa kwa mfalme mwaka jana

Mfalme wa Asante wa Ghana amekaribisha kurejeshwa kwa vitu 130 vya dhahabu na shaba kutoka Uingereza na Afrika Kusini ambavyo baadhi viliporwa wakati wa ukoloni na vingine kununuliwa kwenye soko la wazi.

Vitu hivyo vinajumuisha mavazi ya kifalme, ngoma na mapambo ya sherehe, kutoka miaka ya 1870.

Vipande 25 kati ya hivyo vilitolewa na mwanahistoria wa sanaa wa Uingereza Hermione Waterfield na vingine na kampuni ya uchimbaji madini ya Afrika Kusini AngloGold Ashanti.

Wakikabidhi vipande hivyo katika hafla iliyofanyika katika Kasri ya Manhyia, katika mji wa Kumasi, maofisa kutoka kampuni ya AngloGold Ashanti ya Afirka Kusini wamesema kitendo hicho kimefanywa kama heshima na maridhiano ya kitamaduni.

Kumekuwa na mvutano katika eneo la kati la Ashanti huko Ghana kati ya AngloGold Ashanti na wakaazi, ambao wameshutumu kampuni hiyo kwa kunyonya rasilimali za madini bila kufanya mengi kuendeleza eneo hilo au kuunda kazi.

Mfalme wa Asante Otumfuo Osei Tutu wa Pili aliishukuru AngloGold Ashanti kwa kurudisha kwa hiari vitu vya kale vilivyonunuliwa katika masoko ya wazi.

Wanajeshi wa Uingereza walihusika katika mfululizo wa migogoro mwishoni mwa Karne ya 19 katika kile kilichoitwa vita vya Anglo-Asante. Ikulu ya mfalme, au Asantehene, iliporwa mara mbili.

Wito wa nchi za Kiafrika wa kurejeshwa kwa vitu vilivyoporwa umepokewa kwa mafanikio katika miaka ya hivi karibuni.

Mnamo 2022, Ujerumani ilikuwa nchi ya kwanza kurudisha shaba za Benin kwa Nigeria katika juhudi za kukabiliana na “historia yake ya ukoloni” .

Mtoto wa mwisho wa Gaddafi aliachiliwa baada ya miaka 10 kizuizini

.

Hannibal Gaddafi, mtoto wa mwisho wa aliyekuwa rais wa Libya aliyeondolewa madarakani Muammar Gaddafi, ameachiliwa huru na Lebanon baada ya kuzuiliwa kwa takriban miaka 10 bila kufunguliwa kesi.

Mamlaka ya Lebanon ilimkamata mtoto wa Gaddafi, ambaye sasa ana umri wa miaka 49, mwaka 2015, wakimtuhumu kwa kuficha habari kuhusu hatima ya mhubiri wa Kishia wa Lebanon ambaye alitoweka nchini Libya mwaka 1978.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yamelaani shutuma hizo.

Wakili wake aliliambia shirika la habari la AFP dhamana yake ya $900,000 (£682,938) imelipwa.

Laurent Bayon alisema: “Ni mwisho wa madhila kwake ambayo yamedumu kwa miaka 10.”

Mnamo mwezi Oktoba, jaji alitoa dhamana ya $11m dhidi ya kuachiliwa kwa Gaddafi lakini hii ilipunguzwa wiki iliyopita baada ya timu yake ya utetezi kuwasilisha rufaa, kulingana na AFP.

Bw Bayon alisema mteja wake ataondoka Lebanon kuelekea mahali pa “siri”.

“Ikiwa mtoto wa Gaddafi alizuiliwa kiholela nchini Lebanon kwa miaka 10, ni kwa sababu mfumo wa haki haukuwa huru,” Bayon alisema, kulingana na AFP.

Mnamo 2015, Hannibal Gaddafi alitekwa nyara na kundi lenye silaha nchini Lebanon kabla ya kuachiliwa. Baadaye aliwekwa kizuizini na mamlaka ya Lebanon.

Baada ya babake kupinduliwa na waasi na kuuawa mwaka 2011, alikimbilia Syria na alikuwa ameishi chini ya kifungo cha nyumbani huko Oman na mkewe Aline Skaf.

Kutoweka kwa kasisi wa Shia Musa al-Sadr nchini Libya mwaka 1978 kumekuwa chanzo cha mvutano kati ya Libya na Lebanon kwa miongo kadhaa.

Hannibal Gaddafi alikuwa na umri wa miaka miwili pekee wakati huo na hakuwa na wadhifa wowote nchini Libya akiwa mtu mzima.

Serikali ya Uingereza kukomesha majaribio ya kisayansi kupitia wanyama

e
Maelezo ya picha,Uchunguzi wa dawa kupitia sungura unaweza kumalizika mwishoni mwa mwaka huu

Serikali ya Uingereza imeelezea kwa mara ya kwanza jinsi inavyolenga kutimiza ahadi yake ya kuondoa tafiti na majaribio kupitia wanyama.

Mipango hiyo ni kupunguza matumizi ya mbwa na sokwe katika vipimo vya dawa za binadamu kwa angalau 35% ifikapo 2030.

Chama cha Labour kilisema katika manifesto yake kwamba “kitashirikiana na wanasayansi, viwanda, na mashirika ya kiraia kukomesha tafiti kupitia wanyama.”

Waziri wa Sayansi Lord Vallance aliambia BBC, ipo siku matumizi ya wanyama katika sayansi yatakomeshwa kabisa lakini anakubali kwamba itachukua muda.

Majaribio kupitia wanyama nchini Uingereza yalifikia milioni 4.14 mwaka 2015 kutokana na ongezeko kubwa la tafiti za urekebishaji jeni – hasa kwenye panya na samaki.

Kufikia 2020, idadi hiyo ilishuka kwa kasi hadi milioni 2.88 huku mbinu mbadala zikibuniwa.

Lord Vallance aliiambia BBC anataka kubadilisha majaribio ya wanyama ili kuwepo majaribio kupitia tishu za wanyama, AI, na kompyuta.

Kulingana na mipango ya serikali, ifikapo mwisho mwa 2025, wanasayansi wataacha kutumia wanyama kwa majaribio makubwa na kubadili njia mpya katika maabara zinazotumia seli za binadamu.

Rais wa zamani wa Ufaransa Sarkozy aachiliwa kutoka gerezani baada ya wiki tatu

j
Maelezo ya picha,Nicolas Sarkozy aliwasili nyumbani kwake magharibi mwa Paris saa moja baada ya mahakama kuruhusu kuachiliwa kwake.

Rais wa zamani wa Ufaransa Nicolas Sarkozy ameachiliwa kutoka jela, wiki tatu baada ya kifungo cha miaka mitano jela kwa kushiriki katika njama ya uhalifu.

Atakuwa chini ya uangalizi mkali wa mahakama na kuzuiwa kuondoka Ufaransa kabla ya kesi yake ya rufaa itakayosikilizwa mwaka ujao.

Tarehe 21 Oktoba, rais huyo wa zamani wa siasa za mrengo wa kulia mwenye umri wa miaka 70, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano kwa kula njama ya kufadhili kampeni yake ya uchaguzi wa 2007 kwa pesa kutoka rais wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi.

Timu yake ya wanasheria iliwasilisha ombi la kutaka rufaa ili aachiliwe.

Akiandika kwenye mitandao ya kijamii baada ya kuachiliwa, Sarkozy alisema “nguvu zake ni katika lengo moja la kuthibitisha kutokuwa na hatia. Ukweli utashinda… Mwisho wa hadithi bado haujaandikwa.”

Gari la Sarkozy lilionekana likitoka kwenye gereza la La Santé mjini Paris, chini ya saa moja na nusu baada ya mahakama kukubali kuachiliwa kwake. Muda mfupi baadaye, alionekana akiwasili nyumbani kwake magharibi mwa Paris.

Christophe Ingrain, mmoja wa mawakili wa Sarkozy, alipongeza kuachiliwa kwa mteja wake kama “hatua muhimu” na kusema sasa watakuwa wakijiandaa kwa kesi ya rufaa inayotarajiwa Machi.

Sharti moja la kuachiliwa kwa Sarkozy ni kwamba asiwasiliane na mashahidi katika kile kinachojulikana kama “kesi ya Libya” au wafanyakazi wowote wa wizara ya haki.

Wakati wa kifungo chake, alitembelewa na Waziri wa Sheria Gérald Darmanin. Ziara hiyo iliwafanya mawakili 30 wa Ufaransa kuwasilisha malalamiko yao dhidi ya Darmanin, wakiangazia kile walichosema ni mgongano wa kimaslahi kwani Darmanin alikuwa mfanyakazi mwenza wa zamani na rafiki wa Sarkozy.

Akizungumza na mahakama mjini Paris kupitia video Jumatatu asubuhi, Sarkozy alielezea hajawahi kuwa na “wazo” la kumwomba Gaddafi pesa na akasema “hatakubali kamwe kitu ambacho sijafanya.”

Sarkozy pia alitoa pongezi kwa wafanyakazi wa magereza kwa kuonyesha ubinadamu.

Mke wa Sarkozy, mwimbaji na mwanamitindo Carla Bruni-Sarkozy, na wana wawili wa rais huyo wa zamani walikuwepo katika chumba cha mahakama kumuunga mkono.

Sarkozy ndiye kiongozi wa kwanza wa zamani wa Ufaransa kuwekwa rumande tangu kiongozi wa wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Philippe Pétain kufungwa kwa uhaini mwaka 1945.

Tangu aingie gerezani, Sarkozy amekuwa akishikiliwa katika chumba cha peke yake, chenye choo, bafu, dawati, jiko dogo la umeme na TV ndogo – ambayo alilipa ada ya kila mwezi ya €14 (£ 12) – na friji ndogo.

Pia alikuwa na haki ya kupokea taarifa kutoka nje na kutembelewa na familia, pamoja na mawasiliano ya maandishi na simu – lakini alikuwa katika kifungo cha upweke. Aliruhusiwa kutoka nje ya chumba saa moja tu kwa siku kwa ajili ya mazoezi, ambayo alifanya peke yake.

Walinzi wawili waliwekwa karibu na chumba chake, jambo ambalo waziri wa mambo ya ndani Laurent Nuñez alisema lilitokana na hadhi ya Sarkozy.

Sarkozy alikuwa rais kutoka 2007 hadi 2012. Tangu aondoke madarakani, amekuwa akikabiliwa kesi za uhalifu na kwa miezi kadhaa ilimbidi kuvaa kifaa cha kielektroniki kwenye kifundo cha mguu baada ya kutiwa hatiani Desemba mwaka jana kwa kujaribu kumuhonga hakimu ili apate taarifa za siri kuhusu kesi tofauti.

Sita wafariki baada ya kimbunga cha pili ndani ya wiki moja kuikumba Ufilipino

efd
Maelezo ya picha,Zaidi ya watu milioni 1.4 walihamishwa kabla ya kimbunga Fung-wong kuwasili Ufilipino.

Takriban watu sita wamefariki dunia baada ya kimbunga kikali kuikumba Ufilipino, siku chache tu baada ya kimbunga kilichosababisha vifo vya zaidi ya watu 200.

Kimbunga kikubwa cha Fung-wong kilileta mafuriko na maporomoko ya ardhi, ambayo yamesababisha vifo.

Zaidi ya watu milioni 1.4 walihamishwa kabla ya kimbunga hicho. Sasa kinaelekea Taiwan, ambako zaidi ya watu 3,000 wamehamishwa.

Fung-wong kilikuwa kimbunga cha 21 kukumba taifa hilo la Kusini Mashariki mwa Asia mwaka huu, wakati ambapo wakazi wengi bado wanatatizika kujikwamua kutokana na majanga ya asili yanayotokea mara kwa mara.

Kimbubga hicho kilipiga katika jimbo la Aurora siku ya Jumapili kwa upepo mkali wa karibu kilomita 185 kwa saa (115mph).

Fung-wong kilimwaga mvua nyingi nchini humo, na kuacha nyumba zipatazo 4,100 zikiwa zimeharibiwa.

Kinakuja siku chache baada ya kimbunga cha Kalmaegi kukumba eneo hilo hilo, na kuwaacha maelfu ya watu wakihangaika. Na mwezi Septemba, tetemeko la ardhi la kipimo cha 6.9 lilipiga mkoa wa Cebu.

Wakati Ufilipino inakabiliwa na majanga ya asili, mfululizo huu wa majanga “sio wa kawaida,” Shirika la Kimataifa la Mashirika ya Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu lilisema katika taarifa yake siku ya Jumapili.

“Ni ukumbusho wa hali mbaya mbaya ya hewa inayoongezeka,” ilisema.

Watu 12 wameuawa katika mlipuko wa kujitoa muhanga nje ya mahakama Pakistan

fv

Takriban watu 12 wamefariki katika mlipuko uliotokea nje ya mahakama katika mji mkuu wa Pakistan Islamabad.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Pakistan Mohsin Naqvi ameviambia vyombo vya habari kuwa watu 12 wamefariki na watu 27 wamejeruhiwa katika tukio hili.

Mohsin Naqvi amesema, “Shambulio la kujitoa mhanga lilitokea mahakamani saa za jioni. Shambulio hili limesababisha uharibifu mkubwa, na watu 12 wameuawa na karibu 27 kujeruhiwa.”

Shirika la habari la Reuters lkimnukuu msemaji wa polisi akisema kuwa hali za baadhi ya waliojeruhiwa ni mbaya.

Mlipuko huo ulitokea karibu na lango la Mahakama ya Wilaya ya Islamabad, ambayo kwa kawaida huwa na watu wengi wanaokuja mahakamani.

Baada ya tukio hili, Waziri wa Ulinzi wa Pakistan Khawaja Asif amechapisha kwenye Instagram akisema kuwa Pakistan iko katika hali ya vita.

Aliandika kwenye X, “Ikiwa mtu yeyote anafikiri kwamba Jeshi la Pakistan linapigana vita katika eneo la mpaka wa Afghanistan na Pakistani na maeneo ya mbali ya Balochistan, basi shambulio la leo la kujitoa mhanga katika Mahakama ya Wilaya ya Islamabad ni wito kwamba hivi ni vita kwa Pakistan yote.”

Wahamiaji wa Warohingya waliofariki baada ya boti kupinduka wafikia 21

g
Maelezo ya picha,Shughuli za utafutaji na uokoaji zimeingia siku ya tatu kwa mamia ya wahamiaji waliopotea baharini

Takriban watu 21 wamefariki baada ya mashua iliyokuwa imebeba wahamiaji wasio na vibali kuzama karibu na kisiwa cha mapumziko cha Malaysia cha Langkawi, karibu na mpaka na Thailand.

Shughuli za utafutaji na uokoaji zimeingia siku ya tatu. Watu kumi na watatu wameokolewa lakini makumi ya wengine bado hawajapatikana. Jeshi la Majini la Malaysia wanakadiria takriban watu 70 walikuwa kwenye boti hiyo.

Wale waliokuwa kwenye boti hiyo wanaaminika wengi wao ni Warohingya – ambao waliondoka katika jimbo maskini la Rakhine nchini Myanmar wiki mbili zilizopita, imesema serikali ya Malaysia.

Boti nyingine iliyobeba abiria 230 bado haijapatikana.

Mamlaka ya usafiri wa baharini ya Malaysia inatarajia operesheni hiyo, inayohusisha utafutaji juu ya bahari, kudumu kwa siku saba.

Mwili mmoja uliopatikana ulikuwa wa mtoto, taarifa imesema.

Kati ya 13 waliookolewa, 11 ni Warohingya na wawili ni WaBangladeshi.

Warohingya, ambao ni Waislamu, ni miongoni mwa makabila madogo nchini Myanmar na wananyimwa uraia na serikali ya Myanmar.

Tangu Agosti 2017, ukandamizaji mbaya wa jeshi la Myanmar ulipelekea maelfu ya Warohingya kukimbilia Bangladesh.

Migogoro na hali duni ya maisha nchini Bangladesh hata hivyo pia imewafanya baadhi ya Warohingya kufanya safari za hatari kwenye meli zilizojaa watu hadi Malaysia, nchi yenye Waislamu wengi ambayo baadhi wanaiona kuwa ni kimbilio salama katika eneo hilo.

Zaidi ya Warohingya 150,000 wamekimbilia katika kambi za wakimbizi za Bangladesh tangu mwishoni mwa 2023, huku maelfu wakiwa wameyakimbia makazi yao kimataifa, kwa mujibu wa makadirio ya Amnesty International.

Watu wanane wauawa baada ya gari kulipuka India

fed

Watu wanane wameuawa siku ya Jumatatu jioni baada ya gari kulipuka katika mji mkuu wa India, Delhi.

Kamishna wa polisi wa Delhi anasema mlipuko huo ulitokea wakati gari lililokuwa likitembea polepole kusimama kwenye taa nyekundu kabla ya kulipuka.

Bado hakuna uthibitisho rasmi juu ya nini kilisababisha mlipuko huo.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa India Amit Shah na maafisa wengine wamesema “wanachunguza uwezekano wote ” juu ya kile ambacho kumesababisha mlipuko huo.

Waziri Mkuu wa India Narendra Modi amesema waliohusika na mlipuko huo ‘hawatasalimika.’

Makumi ya wafungwa wapatikana wamenyongwa katika gereza la Ecuador

.

Takriban wafungwa 31 wamepatikana wameuawa katika gereza moja kusini mwa Ecuador, wakiwemo 27 waliokuwa wamenyongwa, maafisa wanasema.

Wafungwa wanne waliuawa na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa katika makabiliano kati ya magenge hasimu katika gereza la El Oro katika mji wa Machala alfajiri ya Jumapili.

Saa chache baadaye, walinzi waliokuwa wametahadharishwa kuhusu kuzuka upya kwa ghasia za magenge waliwapata wengine waliokuwa wamenyongwa kwenye ghorofa ya tatu ya jengo hilo, idara ya magereza ya Ecuador ilisema.

Magereza yenye msongamano wa watu nchini humo yamekuwa eneo la ghasia mbaya na mapigano ya magenge ambapo mamia ya wafungwa wameuawa katika miaka ya hivi karibuni.

‘Tulizuia njama ya Ukraine na Uingereza kuiba ndege ya MiG-31’ – Urusi

.

Idara ya Ujasusi ya Urusi (FSB) imesema kuwa ilizuia njama ya majasusi wa Ukraine na Uingereza kuwajaribu marubani wa Urusi kuiba ndege ya MiG-31 iliyokuwa na kombora la hypersonic la Kinzhal kwa $ 3 milioni, vyombo vya habari vya serikali viliripoti Jumanne.

Shirika la habari la RIA lilinukuu FSB likisema kwamba ndege hiyo iliyotekwa nyara ingesafirishwa kuelekea kituo cha jeshi la anga la NATO katika mji wa Constanta nchini Romania, ambapo ingedunguliwa na walinzi wa anga, shirika hilo liliripoti.

FSB, mrithi wa KGB ya enzi ya Usovieti, ilisema Ukraine na Uingereza zilipanga “uchokozi” mkubwa kwa kutumia ndege iliyotekwa nyara, na kwamba ujasusi wa kijeshi wa Ukraine ulijaribu kulaghai marubani wa Urusi kwa dola milioni 3 ili kuiba ndege hiyo.

“Hatua zilizochukuliwa zimezuia mipango ya huduma za kijasusi za Ukraine na Uingereza kutekeleza uchochezi mkubwa zaidi,” RIA ilinukuu FSB ikisema.

Hata hivyo, shirika la habari la Reuters halikuweza kuthibitisha madai hayo kwa kujitegemea.

Kwa muda mrefu Urusi imeiweka Uingereza kama adui yake mkuu na kuishutumu kwa kuchochea vita vya Ukraine na ujasusi wa Uingereza kuisaidia Ukraine kuanzisha mfululizo wa operesheni ndani ya Urusi.

Nyuki mpya apewa jina ‘Shetani’ kwa muonekano wa pembe zake

.

Wanasayansi wa Australia wamegundua aina mpya ya nyuki wa asili mwenye pembe ndogo – na kumpa jina la shetani.

Watafiti walimgundua nyuki ‘Megachile Lucifer’ walipokuwa wakitazama ua adimu la mwituni ambalo hukua katika eneo la Goldfields la Australia Magharibi peke yake, 470km (292mi) mashariki mwa Perth.

“Pembe za nyuki huyo wa aina yake” ziko kwenye nyuki jike pekee na zinaweza kutumika kama njia ya kujilinda, kukusanya chavua au nekta, au kukusanya nyenzo kama vile resini kwa viota.

Mwanasayansi mkuu wa utafiti huo alisema alivutiwa na jina la ‘Shetani’ alipokuwa akitazama kipindi cha Netflix kilichokuwa na jina kama hilo wakati huo.

Aliongeza kuwa kuna aina mpya kabisa ya nyuki katika kipindi cha miaka 20.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a Reply