Urusi yashambulia miji kadhaa ya Ukraine saa chache kabla ya mkutano wa Trump

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Mashambulizi mabaya ya Urusi katika mji wa Ukraine na miji mingine yaliendelea kushuhudiwa ikiwa imesalia masaa kadhaa kabla ya mkutano wa wa Volodymyr Zelensky na Donald Trump huko Washington.

Katika mji wa kaskazini mashariki mwa Kharkiv, watu wasiopungua wanne wakiwemo mtoto wamekufa wakati ndege isiyo na rubani ya Urusi iliposhambulia eneo la ghorofa, Meya wa jiji hilo Ihor Terekhov alisema.

Sehemu ya jengo imeanguka na watu zaidi inahofiwa wako chini ya vifusi.

Katika mkoa wa Zaporizhzhia, mtu mmoja alikufa na sita kujeruhiwa ikiwa ni pamoja na watoto wawili katika shambulio la Urusi kwa kutumia mabomu ya glide, mkuu wa utawala wa mkoa Ivan Fedorov amesema.

Zelensky, Viongozi wa Ulaya kukutana na Trump; Huu ndio ujumbe wanaotaka kumpa Trump

.

Leo rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky atakuwa na mkutano na rais wa Marekani Donald Trump huko Washington nchini Marekani.

Mkutano huu unakuja siku chache tu baada ya Trump kukutana na Rais Vladimir Putin wa Urusi, uliofanyika jimbo la Alaska nchini Marekani.

Lakini Zelensky hatakuwa peke yake katika mkutano huo. Atasindikizwa na viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani, Italia, Finland, Kamisheni ya Ulaya na Nato.

Hatua ya viongozi hao wa nchi za Ulaya kuambatana na Zelensky si ya kawaida na si bahati mbaya pia. Wanalenga kutuma ujumbe mzito kwa Trump na serikali yake lakini pia kwa Putin.

Ni kweli Trump amefanya jitihada kubwa za kutaka kumaliza vita kati ya Urusi na Ukraine, lakini Zelensky na viongozi wa Ulaya wana wasiwasi kwamba amekuwa na huruma kwa Putin na kwamba anaweza kuingia katika mtego wa kumpa rais huyo wa Urusi kile anachokitaka.

Pamoja na kutaka hakikisho kwamba Ukraine haitajiunga na Nato, kutokuendelea kusaidiwa kijeshi na Ulaya na madai mengine, Putin anataka apewe maeneo kadhaa ya upande wa Mashariki ya Ukraine ambayo anadai kihistoria yalikuwa ni ya Urusi.

Lakini Ukraine na Ulaya inakataa matakwa hayo na kusema kumpa Putin hayo maeneo ili asimamishe vita ni sawa na kumzawadia mchokozi na mvamizi.

Lakini wanahoji pia kwamba Putin akipewa hayo maeneo kuna uwezekano mkubwa kwamba siku za usoni akataka kupewa maeneo mengine zaidi.

Kwa hivyo ujumbe wa kwanza wa Umoja wa Ulaya kuambatana na Zelensky ni kumwambia Trump; “Usimzawadie Putin kwa uchokozi alioufanya”.

Ujumbe wa pili watakaoupeleka ni kwamba wanataka hakikisho la Marekani na wajibu wake katika kuhakikisha Putin hatavamia tena Ukraine muda mfupi baada ya kusitishwa kwa vita vinavyoendelea sasa.

Huko nyuma, Ukraine na Urusi walisaini mikataba kadhaa ya kuishi kwa amani, ujirani mwema na kuheshimu mipaka ya kila nchi. Hata hivyo, muda mfupi baadae Urusi ilivunja mikataba hiyo na kufanya vurugu na hata kuchukua baadhi ya maeneo ya Ukraine kinyume na mikataba waliyokuwa wamesaini.

Hivyo Umoja wa Ulaya na Zelensky wanataka kumwambia Trump kwamba Urusi haaminiki na tungependa kupata hakikisho la Marekani kwamba itakuwepo kutusaidia kupambana na Putin pale atakapovunja makubaliano ya amani yatakayosainiwa hapo baadae.

Ujumbe mwingine wa muhimu ambao viongozi hao wa Ulaya na Zelensky wanatumaini kumpa Trump ni kwamba wanaitazama vita ya Urusi na Ukraine kuwa ni vita ya Ulaya.

Wao wanaamini kwamba Putin asipodhibitiwa vya kutosha basi hatoishia kuvamia Ukraine tu, bali ataendelea kuvamia nchi zingine pia za Ulaya, hasa zile zinazopakana na Urusi kama vile Poland, Finland na Estonia.

Kwa maneno mengine, Ulaya inataka kumwambia Trump kwamba wao hawako tayari kumlegezea Putin katika madai yake na kwamba makubaliano yoyote yatakayofanyika sasa kumaliza vita hiyo ya Urusi na Ukraine yatakuwa na matokeo hasi au chanya ya moja kwa moja kwa nchi za Ulaya.

Katika mazingira ambayo Trump ameonekana kumuelewa Putin na madai yake, viongozi hawa wa Ulaya na Zelensky wanakwenda kumuona Trump wakiwa na wasiwasi mkubwa ikiwa watafanikiwa kumshawishi pia ili aegemee upande wao pia.

M23 yawasilisha makubaliano yake ya kufikia amani na DR Congo kwa Qatar

.

Msemaji wa waasi wa M23 ameiambia BBC kwamba wameonyesha wako tayari kuhakikisha amani ya kudumu hii ikitokea kabla ya tarehe ya mwisho iliyowekwa ya Agosti 18, 2025 kwa makubaliano ya amani kufikiwa kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na kundi la M23.

Oscar Balinda alisema kundi hilo tayari limechukua hatua na kuwasilisha makubaliano yake ya kufikia amani na DR Congo kwa Qatar, mpatanishi anayeongoza mchakato wa amani wa Doha unaoendelea.

“Tumefanya kila kitu kinachohitajika kwetu, na sasa tunangojea serikali kuchukua hatua ili suluhisho lifikiwe,” alisema.

Aliongeza kuwa wanataka kuona nia njema kutoka kwa serikali pia, wakisema kuwa waasi walikuwa wameachilia karibu wanajeshi 1,400 ambao wamerudi kwa familia zao huko Kinshasa na kwengineko.

Serikali, hata hivyo, inaendelea kuwazuia wanachama zaidi ya 700 wa M23 katika magereza mbalimbali nchini humo.

“Ikiwa tumekubali kutekeleza mpango wa amani, basi sote tuonyeshe utayari. Kwa mfano, tuliondoa vikosi vyetu kutoka eneo la Walikale, Kivu Kaskazini, kama ishara ya nia njema – na hiyo ilikuwa sehemu ya makubaliano yetu makubwa,” ameongeza.

Hata hivyo, serikali ya DRC bado haijajibu madai ya hivi karibuni ya M23.

Taarifa ya Bw Balinda inawadia wakati ripoti zikiibuka kuwa wapatanishi huko Qatar wametoa makubaliano ya amani ya serikali ya DRC na kundi la waasi linaloungwa mkono na Rwanda la M23, katika nia ya kumaliza vita ambavyo vimedumu kwa miaka kadhaa katika mkoa wa mashariki.

Serikali ya Congo na M23 walitia saini azimio la pamoja huko Qatar mnamo Julai 19, wakiahidi kukubaliana kufikia Agosti 18.

Kulingana na AFP, afisa wa Qatar alisema Jumapili kwamba pande zote mbili zimeonyesha nia njema kwa mpatanishi na utayari wa kuendelea na mazungumzo.

“Tunatambua changamoto zilizopo na tunatumai kuwa wanaweza kuzishinda kupitia mazungumzo na kujitolea kwa kweli,” afisa huyo alisema.

Mapema mwaka huu, waasi wa M23 waliteka miji muhimu ya Goma na Bukavu kuanzisha tawala za mitaa.

Mashirika ya kutoa misaada yanasema kuingiliwa kwa haraka kwa maeneo hayo kumezidi ukosefu wa usalama na kusababisha mapungufu ya bidhaa zinzohitajika na familia zilizohamishwa kutoka makazi yao.

DRC kwa muda mrefu imeshutumu Rwanda jirani yake kwa kuunga mkono M23, madai ambayo Rwanda inakanusha.

Mzozo huo umechochea mvutano wa kikanda huku washirika wa kimataifa wakihimiza pande zote mbili kujizuia.

Maandamano makubwa yafanyika Israel wakidai makubaliano ya kuachiliwa kwa mateka

.

Mamia kwa maelfu ya watu wamekusanyika nchini Israel kutoa wito wa kusitishwa kwa vita vya Gaza na kufikiwa kwa makubaliano ya kuhakikisha kuachiliwa kwa mateka wanaoshikiliwa na Hamas.

Umati mkubwa wa watu ulionekana katika uwanja wa “Hostages Square” wa Tel Aviv siku ya Jumapili, huku waandaaji wakisema mipango ya serikali ya kuutwaa mji wa Gaza inahatarisha maisha ya karibu mateka 20 ambao bado wanazuiliwa na Hamas.

Maandamano ya kitaifa ya siku moja – sehemu ya maandamano makubwa – barabara zilizofungwa, ofisi na vyuo vikuu katika baadhi ya maeneo. Karibu watu 40 walikamatwa wakati wa mchana.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alikosoa maandamano hayo akisema “yatazidisha misimamo ya Hamas” na yatapunguza kasi ya kuachiliwa kwa mateka hao.

Trump asema ‘Ukraine haitaweza kujiunga na NATO,’ huku Zelensky akijiandaa kufika Ikulu

.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema rais wa Ukraine anaweza kumaliza vita vya Urusi “ikiwa anataka” kufanya hivyo, lakini “Ukraine haitaweza kujiunga na NATO” kama sehemu ya makubaliano ya amani.

Saa chache kabla ya kuwa mwenyeji wa Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House, Trump pia alisema rasi ya Crimea “haitarudishwa tena”, ambayo Moscow ilinyakua kinyume cha sheria mwaka 2014, miaka minane kabla ya kuanzisha uvamizi wake.

Hii inafuatia mkutano wa kilele wa Trump na kiongozi wa Urusi Vladimir Putin huko Alaska ambao ulisababisha rais huyo wa Marekani kutupilia mbali ombi la kusitishwa kwa mapigano na badala yake akataka makubaliano ya amani ya kudumu.

Mjumbe wa Marekani alisema siku ya Jumapili kwamba Putin alikubali uwezekano wa makubaliano ya usalama kama ya Nato kwa Ukraine.

Rais wa Urusi amekuwa akipinga mara kwa mara wazo la Ukraine kujiunga na muungano huo wa kijeshi.

Katika ujumbe wake kwenye jukwaa la Truth Social siku ya Jumapili usiku, Trump alisema: “Rais Zelenskyy wa Ukraine anaweza kumaliza vita na Urusi mara moja, ikiwa anataka kufanya hivyo, au anaweza kuendelea kupigana.

“Kumbuka jinsi ilivyoanza. Hakuna kupata tena Crimea iliyochukuliwa wakati wa Obama (miaka 12 iliyopita, bila hata risasi kufyatuliwa!), na UKRAINE HAITAWEZA KUINGIA NATO. Mambo mengine hayabadiliki!!!” Trump aliongeza.

Kabla ya Trump kurejea madarakani mwezi Januari, nchi za Nato zilikubaliana juu ya “mwelekeo usioweza kubadilika” wa Kyiv kuwa mwanachama katika muungano huo.

Katibu Mkuu wa Nato Mark Rutte, pamoja na viongozi wa Ulaya akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer, wataungana na Zelensky mjini Washington kwa mazungumzo kuhusu mustakabali wa Ukraine leo Jumatatu.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment