Ofisi ya Mbunge Dagoreti yachomwa Dagoreti kusini Nchini Kenya.

Afrika Leo Alfajiri -Radio Fortune Africa

Na Cantona Joseph

MAAFISA wa polisi waliokuwa wanalinda afisi za Mbunge wa Dagoretti Kusini John ‘KJ’ Kiarie walilazimika kutorokea usalama wao Jumanne, wakati vitoa machozi walivyokuwa wakirushia waandamanaji kuisha.

Wahalifu waliodai kuwa waandamanaji usiku wa Jumanne, Juni 25, 2024 walimfuata mbunge huyo baada ya kupiga kura ya “ndio’’ kwa Mswada wa Fedha 2024 licha ya kuandika barua ndefu ya kuomba msamaha kwa wapiga kura wake.

Wakati wa maandamano hayo, polisi mmoja wa kitengo cha AP alipoteza kidole kimoja.

Waandamanaji hao walisema afisi hiyo imekuwa ikiendeleza ufisadi wakati wa kutoa basari kwa wakazi.

Mlinzi wa afisi hiyo Bw Isaac Khaemba, alisema waliotekeleza kitendo hicho ni waandamanaji zaidi ya 1,000 walivuja ukuta ili kupata nafasi ya kuingia.

“Mchana maandamano yalikuwa na utulivu sana. Saa kumi jioni walirudi hapa na kubomoa ukuta ambao umezingira afisi hii. Wakati huo, polisi walitumia vitoa machozi kuwatawanya,” alisimulia Bw Khaemba jinsi hali ilianza.

“Baadaye walikuja kwenye afisi hiyo na kuamuru wanunuliwe maji ya kupangusa gesi ya kutoa machozi na mfanyakazi mwenza akawapa na kuenda,” alisema Bw Khaemba.

Waandamanaji wapya walifika katika afisi hiyo mwendo wa saa mbili usiku na kuanza kurusha mawe. Maafisa wa polisi waliingilia kati hadi wakati vitoa machozi viliisha.

“Vitoa machozi viliisha, niliokolewa na polisi kutoka kituo cha Kabete. Polisi walitoroka na kuniacha kwenye lango na waandamanaji hao walianza kuchoma choo na kisha kuelekea katika afisi ya mbunge na kuchoma kila kitu,” alisema Bw Khaemba.

Waandamanaji hao walitoka katika eneo hilo baada ya kuhakikisha afisi hiyo imeteketea.

Msimamizi wa kituo cha polisi Bi Sarah Kimsar alithibitisha kuwa mmoja wa maafisa kutoka kituo chake alipoteza kidole wakati wa makabiliano makali na wandaamanaji.

All Rights Reserved © Cantona Group Ltd||2024


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

One thought on “Ofisi ya Mbunge Dagoreti yachomwa Dagoreti kusini Nchini Kenya.

Leave a comment