Ujasiri wa mkristo hutoka wapi!

UJASIRI WA MTEULE WA KRISTO HUTOKA WAPI?

Bwana YESU KRISTO atukuzwe ndugu zangu wote.
Karibuni tujifunze Neno la MUNGU

Ujasiri wa Mtu aliyeokoka hutoka wapi?

Umeshawahi kujiuliza swali Kama hilo?
Inawezekana ulikuwa na rafiki yako muoga muoga lakini baada ya huyo rafiki yako kuokoka amekuwa jasiri kiasi kwamba anaweza kuwashuhudia injili watu, anaweza kuhubiri, anaweza kuimba pambio mbele za watu, anaweza kutangaza hadharani kwamba hawaogopi wachawi wote n.k

Unadhani huo ujasiri unatoka wapi?
Binafsi Mimi ni mmoja wa watu ambao kabla ya kuokoka nisingeweza kuongea mbele za watu lakini kwa sasa baada ya kuokoka hata Kama Kuna kundi la watu elfu 50 naweza kusimama mbele yao na kufundisha Neno la MUNGU kwa ujasiri kabisa.
Ulishawahi kujiuliza kwanini ulipookoka tu ndipo Kuna ujasiri ambao hukuwanao kabla lakini baada ya kuokoka huo ujasiri ukawa nao?

Je ujasiri wa Mteule wa KRISTO hutoka wapi?

Ngoja nikufundishe vyanzo vya ujasiri wa Mteule wa KRISTO.

  1. Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na Mteule huyo kuwa na ROHO MTAKATIFU.

Mfano hao ni hawa Mitume ambao walipompokea ROHO MTAKATIFU ndipo wakapata ujasiri wa kuhubiri injili ya KRISTO kwa ujasiri.

Matendo 4:31 “Hata walipokwisha kumwomba MUNGU, mahali pale walipokusanyika pakatikiswa, wote wakajaa ROHO MTAKATIFU, wakanena neno la MUNGU kwa ujasiri.”

  1. Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na kuwa na uhakika kwamba MUNGU yuko upande wako.

Mfano hai ni huu ambapo Rahabu anawaambia wapelelezi wa Israeli kwamba Yeriko ikeyeyuka na watu wote Wana hofu kwa sababu ya Waisraeli maana Waisraeli Wana MUNGU.

Rahabu anasema “Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa BWANA, Mungu wenu, yeye ndiye MUNGU, katika mbingu juu na katika nchi chini.-Yoshua 2:11

Waisraeli walikuwa na MUNGU ndio maana walikuwa na ujasiri lakini mataifa ambao hawakuwa na MUNGU walikuwa hawana ujasiri mbele za Israeli, hivyo chanzo kimoja wapo Cha ujasiri wa Mteule wa KRISTO ni anapokuwa na uhakika kwamba MUNGU yuko upande wake.

  1. Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na Mteule huyo kuishi maisha matakatifu ya Wokovu na haki.

Mithali 28:1 “Waovu hukimbia wasipofuatiwa na mtu; Bali wenye haki ni wajasiri kama simba.”

Biblia inasema waovu hawana ujasiri lakini wenye haki ni majasiri Kama simba.

Dhambi huondoa ujasiri lakini kuishi maisha matakatifu kutakufanya uwe jasiri muda wote maana huna unachohofia.

Mfano mwizi akikutana na polisi ni rahisi kukimbia hata Kama hawamtafuti yeye, maovu yake ndio humfanya awe na hofu na wasiwasi mwingi hivyo kukosa ujasiri.

Hivyo wanaoishi maisha matakatifu ya Wokovu wa KRISTO hao ndio majasiri, utakatifu huleta ujasiri.
Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na Mteule huyo kujitenga mbali na dhambi.

  1. Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na Mteule huyo kujua kuitumia mamlaka iliyo ndani ya YESU KRISTO Mwokozi wake.

Luka 10:19 “Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.”

  1. Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na Mteule kuwa na uhakika kwamba YESU KRISTO ni Mwokozi wake.

Bwana YESU anasema kuhusu sisi wateule wake kwamba “Nami nawapa uzima wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. – Yohana 10:28”

YESU KRISTO akiwa ni Mwokozi wako lazima uwe jasiri.

  1. Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na Mteule huyo kuwa na Neno la MUNGU ndani yake.

Neno la MUNGU ni Moto na nyundo kwa nguvu zote za giza.

Yeremia 23:29 “Je! Neno langu si kama moto? Asema BWANA; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?”

Hivyo Neno hilo la MUNGU likiwa ndani ya Mteule wa KRISTO na akawa analitumia Neno hilo katika maombi na kuliishi hakika Mteule huyo atakuwa mshindi na jasiri Sana maana hataogopa chochote kutoka ulimwengu wa roho wa giza.

Neno la MUNGU kwenye kinywa Cha Mteule wa KRISTO litafanya kazi.

Yeremia 5:14 “Kwa sababu hiyo BWANA, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala.”

Ndio maana Biblia inatusisitiza Sana kwamba tuhakikishe Neno la MUNGU linajaa ndani yetu.
Wakolosai 3:16 “Neno la KRISTO na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia MUNGU kwa neema mioyoni mwenu.”

  1. Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na Mteule huyo kuisikia saiti ya MUNGU na kuifuata.

Kumbu 28:1″ Itakuwa utakaposikia sauti ya BWANA, Mungu wako, kwa bidii, kutunza kuyafanya maagizo yake yote nikuagizayo leo, ndipo BWANA, Mungu wako, atakapokutukuza juu ya mataifa yote ya duniani;”

  1. Ujasiri wa Mteule wa KRISTO unatokana na Mteule huyo kuwa na amani ya KRISTO.

Wakolosai 3:15 “Na amani ya KRISTO iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani.”

Amani ya KRISTO ndio pia amani ya MUNGU, hiyo ikiwa ndani ya Mteule wa KRISTO hakika Mteule huyo atakuwa jasiri.

Wafilipi 4:7 “Na amani ya MUNGU, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika KRISTO YESU.”

Nfugu, Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.

Bwana YESU Amekaribia Kurudi.

Je, Umejiandaaje?

Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?

Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.

Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.



CantonaJoseph’s contacts
Facebook https://www.facebook.com/CantonaJoseph/
Instagram https://www.instagram.com/Cantona.Joseph.
Twitter https://twitter.com/@CantonaJoseph
LinkedIn https://www.linkedin.com/in/CantonaJo
Management Fortune Baraka Entertainments
Website https://CantonaJoseph.Wordpress.Com
Email fortunebaraka.entertainmentsltd@gmail.com cantona.online254@gmail.com
Contacts +254748836127
Wewe ni wa maana sana!

Copyrights Reserved @2019 FortuneBaraka Entertainments.




Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

2 thoughts on “Ujasiri wa mkristo hutoka wapi!

Leave a reply to CantonaJoseph Cancel reply