Bwana YESU atukuzwe ndugu mpendwa kokote uliko.
Karibu tujifunze Neno la MUNGU.
Watu wengi sana huuliza kuhusu upendo, wengine huuliza sana juu ya kumchagua mtu sahihi ambaye anampenda hata wachumbiane na kisha kufunga ndoa takatifu.
Somo la upendo ni pana sana na kuna aina zaidi ya 3 za Neno upendo.
Leo nazungumzia upendo wa mtu kwa mchumba wake.
YESU alisema Neno muhimu sana na la kuzingatia sana kwamba ‘’ Mpende Jirani yako kama nafsi yako-Marko 12:31’’
Hata katika uchumba au ndoa kipimo hiki cha upendo ambacho ni cha juu sana kinatakiwa kiwepo.
Kama wewe hupendi kwenda jehanamu basi usimkoseshe na upendaye hata aanze kwenda jehanamu kwa sababu yako, usimfanye atende dhambi, usimfanye amkufuru MUNGU.
Kama unapenda wewe usisalitiwe milele basi na wewe usimsaliti milele umpendaye.
Kiwango cha unavyojipenda mwenyewe unatakiwa na wengine uwapende hivyo.
Neno upendo wa kimahusiano yanayozaa uchumba kwa ufupi lina maana hii ‘’ Kuvutiwa na mtu na ukamweka moyoni na kumthamini sana kisha ukakusudia kufunga naye ndoa takatifu ’’
Lakini ni muhimu sana kujua kwamba sio kila mtu ni wa kumweka moyoni kwa upendo wa kimahusiano yanayozaa uchumba kisha ndoa, sio wote ni wako, zingatia sana hiyo.
Kiini cha somo langu ni njia za kuujua upendo wa kweli kutoka kwa mchumba wako.
Biblia inasema yafuatayo katika
1 Wakorintho 13:4-8 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya; haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli; huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote. Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika.”
Njia hizo za kuujua upendo wa kweli kutoka kwa mchumba wako zipime katika haya.
- Upendo huo lazima uvumilie.
Uvumilivu ni hali ya kustahimili hivyo mwenye upendo wa kweli lazima astahimili.
Kama mnafanya uasherati wakati wa uchumba ujue hapo hakuna upendo wa kweli
Kama una upendo wa kweli vumilia ndipo utapata faida.
Waebrania 6:15 “Na hivyo kwa kuvumilia akaipata ile ahadi.”
Kuvumilia ni kuendelea na jambo ingawa mnapitia misukosuko na taabu. Inawezekana upande wa mchumba wako hawakutaki, inawezekana Mchumba wako kwa muda mrefu anaumwa, upendo huvumilia, sio umwache kwa sababu amelazwa mara mbili ndani ya miezi 6 hii.
Ngono kabla ya ndoa hapo upendo haupo bali kuna tamaa tu kwa sababu uvumilivu haupo.
Waefeso 4:17 “Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao;”
Unashindwa nini kustahimili wakati kabisa huyo ni wako?
Kwa nini usishughulikie suala la kufunga ndoa?
Wewe unashughulikia dhambi ya uasherati na kupelekea uchumba wetu shetani kupanda magugu mengi ambayo hata kuyang’oa mtashindwa na kujikuta tu mmeachana kwa maumivu na fedheha?
Ndugu upendo wa kweli huvumilia.
Ewe Mwanaume au mwanamke uliye katika uchumba tuliza kichwa chako maana tendo la ndoa ni katika ndoa tu na sio kabla ya hapo.
Mimi kama Mtumishi wa MUNGU nikionacho kwa baadhi ya watu ambao hufanya dhambi ya uasherati wakati wa uchumba ni hiki.
Wanawake wengi hupenda uasherati ili wapate mimba wakidhani kwamba mimba itawafanya waolewe, hao kundi kubwa mno wala hawakuolewa bali waliachwa na maumivu makubwa.
Wanawake wengine hujifanya akina mama huruma kwa kuwahurumia wachumba zao ili wakidhi haja zao, hao wengi sana wameachwa baada ya uasherati.
Wanaume wengi hufanya ngono wakati wa uchumba kwa tamaa zao za kipepo, tendo hilo la ngono huvuruga uchumba, hufuta mipango ya ndoa, huifanya mipango ya ndoa kuchelewa.
Ndugu, kataa dhambi ya uasherati katika uchumba wako, Onyesha kwamba una upendo wa kweli kwa kuvumilia huku ukifanya juhudi za kufunga ndoa na sio vinginevyo.
- Upendo wa kweli lazima ufadhili.
Neno “fadhili” maana yake kutoa msaada wakati wa shida au tatizo.
Msaada mkuu wakati wa uchumba ni maombi, kutiana moyo na kushauriana kiroho kwa utakatifu na uaminifu wote.
Msaada mkiwa katika ndoa ni pamoja na kusaidiana kwa kila kitu ili mwenzi wako atoke katika tatizo.
Ukiwa katika ndoa Baba au Mama usikubali mwenzi wako anaumwa na pesa unayo lakini hutoi kuhudumia matibabu ya mwenzi wako, hata kama una mipango mizuri kiasi gani ni lazima umsaidie ili atoke kwenye tatizo, huo ndio upendo wa kweli.
1 Wakorintho 13:4 “Upendo huvumilia, HUFADHILI; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;”
- Upendo wa kweli hauna husuda.
Husuda maana yake mtazamo wa ubaya juu ya mtu na vitu vyake.
Husuda pia ni hali ya kutokupendezwa au kutokufurahishwa na mafanikio ya mwingine.
Mchumba wako mpime katika hilo ndio utajua kwamba hana upendo wa kweli au anao.
Mchumba wako kama ana mitazamo ya ubaya dhidi yako, wazazi wako, mali zako, kazi yako, uchumi wako n.k hakika huyo hana upendo wa kweli kwako.
Mchumba wako kama hafurahishwi na mafanikio yako kiroho au kimwili n.k huyo hana upendo wa kweli kwako.
Mchumba wako kama hafurahishwi wewe kuokoka, huyo ana husuda na hakufai.
Mchumba wako kama hafurahishwi wewe kumtumikia MUNGU na kuwa mtu wa ibada hakika huyo ana husuda na hakufai daima maana hana upendo wa kweli.
Alikukuta unamtumikia Bwana YESU kwanini sana atake uache huduma?
1 Petro 2:1 “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.”
- Upendo wa kweli hautakabari.
Kutakabari maana yake ni kumfanyia mtu jeuri au kiburi.
Maana nyingine ya kutakabari kuwaona wengine sio kitu.
Unaweza ukajipima kwenye uchumba wako wewe ndio unaupembeleza huo uchumba?, wewe ndio unaulazimisha uchumba uwepo? wewe ndio unajikomba kwa mchumba wako?
Ndugu ikiwa ni hivyo katika uchumba wako ujue mwenzako yuko katika kundi la kutakabari na huyo wala hana upendo wa kweli kwako.
1 Wakorintho 13:4 “Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo HAUTAKABARI; haujivuni;”
Ukiona anakufanyia jeuri na kiburi kwa sababu anajua kabisa ni wewe unayetaka uchumba huo uwepo na sio yeye ujue huyo hakupendi.
Ninaposema kumfanyia mtu jeuri na kiburi sina maana ya kwamba umtii katika kila jambo mchumba wako.
Kama mchumba wako wewe anakuita una jeuri na kiburi kwa sababu umemkatalia kufanya dhambi ya uasherati tambua kwamba wewe huna kiburi wala jeuri bali tambua kwamba yeye hakupendi na wala hana mpango wa kufunga ndoa na wewe.
Jeuri au kiburi katika mambo ya kukulazimisha kutenda dhambi wala hiyo sio jeuri wala kiburi bali ni ucha MUNGU sahihi.
Upendo wa kweli hautakabari hivyo ukiona kitu kiitwacho kutakabari kutoka kwa mchumba wako kama ulivyojifunza maana ya kutakabari katika somo hili basi ujue Mchumba wako hakupendi kabisa, anataka tu kukutumia kisha akuache.
Mtu wa kutakabari anaweza kukuambia “hata hivyo Nimekubali uchumba na wewe kwa kukusaidia tu’’, huyo hakupendi.
Usikubali kuingia katika ndoa na mtu mwenye kutakabari.
Warumi 1:30 “wenye kusingizia, wenye kumchukia MUNGU, wenye jeuri, wenye kutakabari, wenye majivuno, wenye kutunga mabaya, wasiowatii wazazi wao,”
- Upendo wa kweli haujivuni.
Kujivuni maana yake ni kujiona bora kuliko mwenzako.
Kujiona wa thamani kuliko kuliko mchumba wako.
Kujiona una vitu zaidi kuliko mchumba wako, hivyo atakutegemea wewe tu hana iweje.
Ndugu ukiwa katika uchumba na mtu mwenye majivuno kwako ujue huyo hana upendo wa kweli kwako.
Utagundua tu kwamba mchumba wako hakupendi kwa kuangalia majivuno yake kwako, utagundua kwamba ni wewe unalazima uchumba ila yeye hakutaki.
Mimi Peter Mabula niko hapa leo kukujulisha upendo wa kweli ulivyo ili uujue hivyo ukiona na ukapima kabisa kwamba katika uchumba wako wewe unaulazimisha uchumba huo huku mwenzako hana habari na wewe ujue huyo hana upendo.
Kama upendo ni kuthaminiana kwanini wewe huthaminiki kwa mchumba wako harafu anasema anakupenda?
Anakutangaza mitaani kwamba amekukubali ili tu kukusaidia, huyo hakupendi.
Ndugu upendo wa kweli haujivuni.
Wafilipi 2:3 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.”
- Upendo wa kweli lazima uhusike na adabu.
Adabu maana yake tabia njema.
Mithali 11:16″ Mwanamke wa adabu huheshimiwa daima; …..”
Adabu ni utaratibu mzuri wa ki MUNGU wa kuendesha mambo, lazima huo utaratibu wa ki MUNGU uwepo katika uchumba wenu, hicho ndicho kipimo cha upendo wa kweli.
Adabu ni heshima inayoambatana na aibu au haya ya kutenda jambo lisilo zuri mbele za MUNGU na mbele za wanadamu.
Ukiona mchumba wako hana aibu au haya kutenda dhambi na wewe ujue huyo hana adabu na kwa sababu hana adabu basi hana pia upendo wa kweli, maana upendo wa kweli huambatana na adabu yaani tabia njema.
- Upendo wa kweli hautafuti mambo yake.
Mchumba wako ni lazima alenge kumpendeza MUNGU, Kukupendeza wewe katika hali takatifu, kukupa amani na furaha katika haki.
Kama Mchumba wako anautumia uchumba wenu kama njia ya kujifurahisha yeye tu huyo hana upendo wa kweli.
Usikubali mchumba wako akakutumia kama chombo chake cha starehe.
Usikubali mchumba wako akakutumia kama kifaa chake cha mazoezi au cha kujipima kama ana nguvu na maamuzi, upendo wa kweli hauko hivyo.
Upendo wa kweli hautafuti mambo yake.
Wafilipi 2:4 “Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.”
- Upendo wa kweli hauleti uchungu.
Maana ya uchungu ni masononeko ambayo hayana mwisho wa haraka.
Waebrania 12:15 “mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya MUNGU; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo.”
Kuna watu uchumba wao umejaa uchungu kiasi kwamba hata wanajiuliza mara mbilimbili juu ya kuingia kwenye ndoa na wachumba zao hao.
Unakuwa na mchumba ambaye unamfumania live na mtu mwingine wakifanya ngono, mtu kama huyo hakupendi na hana upendo wa kweli kwako.
Ni wachumba lakini mara mmepigana, mara vikao vya usuluhishi kila mara kwa sababu ya tabia chafu za mchumba wako, mtu kama huyo hana upendo wa kweli kwako.
Wakati mwingine katika maisha kuna kupishana kauli kidogo lakini mtu ambaye hakupendi mkipishana kauli atakununia hata mwenzi, atakaa na uchungu bila kusamehe na kuachilia, huyo hana upendo wa kweli.
Kuna makosa ambayo hakika yanaweza kuvunja uchumba mfano kumfumania, mtu ana mahusiano zaidi yako, tabia chafu, dhambi n.k hayo yanaweza yakavunja uchumba.
Lakini mfano hujapokea tu simu ya mchumba wako kwa sababu ulikuwa unaoga kisha baadae ukimpigia simu anakutishia kukuacha, huyo hana upendo wa kweli kwako.
- Upendo hauhesabu mabaya.
Tunaposema upendo hauhesabu mabaya haina maana ya kwamba watu wafanye mabaya tu na uchumba uendelee kwa sababu upendo hauhesabu mabaya.
Eti Mchumba wako anakusaliti wewe huvunji uchumba kwa sababu upendo hauhesabu mabaya, ndugu haiko hivyo.
Kuna tabia ukizilea ujue zitaendelea hata wakati mkiwa ndani ya ndoa.
Mtu mwenye pepo la ngono wakati wa uchumba ujue hata mkioana pepo la ngono halitaondolewa na ndoa.
Msaliti ni msaliti tu haijalishi mko katika ndoa au uchumba, wakati wa uchumba usikubali kuingia katika ndoa na msaliti.
Kama uko katika ndoa na unaishi na mwenzi msaliti basi muombee na tafuta msaada wa kiroho ili aanze kumcha MUNGU ndipo usaliti utaondoka, lakini wakati wa uchumba usifanye hivyo bali kaa mbali na msaliti maana anaweza kuendelea na usaliti huo hata ndani ya ndoa.
Biblia inaposema upendo hauhesabu mabaya katika uchumba au ndoa ina maana kama hizi.
Mambo yako mabaya ya zamani kipindi hujampokea YESU hayatakiwi kuwa silaha ya mchumba wako leo kukutuhumu na kukunyanyasa.
Hata kama ulifeli masomo, familia yenu ni maskini, ni yatima huna wazazi, huna ndugu, uliwahi kubakwa zamani, uliwahi kufungwa jela zamani, ulikuwa kahaba au jambazi zamani, upendo wa kweli hufunika mabaya kama hayo yote na zaidi hata yasionekane tena.
1 Wakorintho 13:4-5 ” Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni; haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; HAUHESABU MABAYA;”
- Upendo wa kweli haufurahii udhalimu.
Udhalimu maana yake ni uonevu au ukatili.
Udhalimu kwa ujumla ni tendo la kufanya mambo yaliyo kinyume na haki.
1 Wakorintho 6:9 “Au hamjui ya kuwa wadhalimu hawataurithi ufalme wa MUNGU? Msidanganyike; waasherati hawataurithi ufalme wa MUNGU, wala waabudu sanamu, wala wazinzi, wala wafiraji, wala walawiti,”
Kama una mchumba na anakufanyia udhalimu hakika huyo hakupendi.
Kama una mchumba anakuonea kila mara, anakufanyia ukatili wa kijinsia au ukatili mwingine wote mfano kukupiga ujue huyo hana upendo wa kweli.
Hata kukukataza kwenda Kanisani au kwenda kwenye mikesha ya maombi huo ni ukatili usio na maana hata moja.
Uko kwenye kwaya unaambiwa na mchumba wako acha kwaya, unamtumikia Bwana YESU harafu mchumba wako anakuambia acha utumishi huo.
Ni wewe ndio unajua uliingia agano gani na Bwana YESU Mwokozi, Kwanini mtu aliyekuja kukuona tu ukubwani akuvunjie agano lako na MUNGU?
Nina shuhuda nyingi za watu waliofanyiwa udhalimu na wachumba zao, nafasi haitoshi hapa ningekupa shuhuda hizo, moja tu ni hii Binti mmoja alikuwa ana mchumba na ilibaki wiki moja kufunga ndoa. Yule binti kumbe aliwahi kupendana na kijana mwingine ambaye wakati mrefu alikuwa mbali. Kijana yule alipokuja tu yule binti alitaka ndoa isifungwe, mahari irudishwe na kamati ya harusi ivunjwe, huo ni udhalimu mbaya.
Ndugu ni hatari sana ukiingia katika uchumba na mtu dhalimu.
Kijana mmoja alikimbia mke na watoto na kwenda mkoa mwingine na huko alikokwenda alijitambulisha kama mtu ambaye hajawahi kuoa wala kuchumbia, akampenda binti mmoja na mipango ya harusi ikaanza, siku chache mno kabla ya ndoa mke halisi wa huyo mtu akaja, ilikuwa ni hatari sana, ndugu unaweza hata ukapata madhara kwa sababu tu umeingia katika mahusiano na mtu dhalimu ambaye amewahi kuolewa au kuoa.
Ndugu kumbuka Neno hilo ya kwamba upendo wa kweli haufurahii wala kujihusisha na udhalimu.
Biblia inasema kwamba upendo wa kweli haufurahii udhalimu.
1 Wakorintho 13:6 “haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;”
- Upendo wa kweli huambatana na kweli.
Ungeniuliza mimi Peter Mabula kwamba katika njia hizi za kuujua upendo wa kweli ipi inayotakiwa kuwa ya kwanza ningekuambia ni hii ya kumi na moja.
Hakika upendo wa kweli ni lazima uambatane na kweli.
Wafilipi 4:8 “Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.”
Kweli ya kwanza kabisa ambayo upendo wa kweli unatakiwa kuambatana nayo ni Wokovu wa YESU KRISTO.
Waebrania 2:3 “sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na Bwana, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia;”
Hiyo ndio kweli kuu, Baada ya hiyo ni lazima mchumba wako awe mkweli, ukweli huwa unamuweka mtu huru.
Kuna watu wameingia katika uchumba au ndoa na watu walioathirika, mtu wa hivyo hana kweli.
Kuna watu wameingia katika ndoa na maajenti wa kuzimu ambao wamejivika ngozi ya kondoo kwa juu, mtu huyo hana kweli.
Kuna watu wameingia katika ndoa na watu wabaya sana ambao wakati wa uchumba walikuwa tu wameficha makucha yao.
Ndugu hakikisha unakuwa mtu wa maombi na mtii ROHO MTAKATIFU ili akujulishe mtu sahihi.
Fanyia kazi “amani ya KRISTO” moyoni na fanyia kazi “huzuni ya MUNGU” rohoni mwako ili kukusaidia katika maamuzi ya kumjua mtu sahihi.
Katika maamuzi ukiona una huzuni uwe makini sana maana ipo huzuni ya MUNGU(Wafilipi 4:7) hiyo huzuni huja ndani yetu ili itusaidie katika kuamua.
Biblia inasema “amani ya KRISTO iamue ndani yenu -Wakolosai 3:15”
Baada ya kukueleza hizo njia kumi na moja za kuujua upendo wa kweli kutoka kwa mchumba wako, ngoja nikupe nyongeza hii muhimu sana.
Upendo pia huamini yote yaliyo ya ki MUNGU.
Upendo huamini mafundisho sahihi ya Neno la MUNGU.
Upendo huamini mafunuo ya ROHO MTAKATIFU mwenyewe.
Upendo hutumainia yaliyo ya ki MUNGU.
Kutumainia maana yake ni kuwa na matarajio kupata kitu.
Uchumba wenu unahitaji ndoa hivyo tarajia ndoa huku ukifanya juhudi njema za kuifikia hiyo ndoa haraka.
Hakuna haja ya kuwa wachumba miaka 2 au 3 au 4 au 5 au zaidi huku mkidanganya kwamba mnachunguzana.
Kama ulisema ni MUNGU amekufunulia kwanini baada ya kumpata mchumba unaanza tena kumchunguza, hapo unakuwa unadhihilisha wazi kwamba MUNGU hakukufunulia bali akili zako tu.
Kama ni MUNGU alisema na wewe uwe na uhakika ni salama kabisa.
2 Nyakati 20:20 “mwaminini BWANA, Mungu wenu, ndivyo mtakavyothibitika; waaminini manabii wake, ndivyo mtakavyofanikiwa.
Katika uchumba pia ni muhimu kujua kwamba wakati mwingine itawabidi kuvishinda vikwazo vyote vinavyotokana na mawakala wa shetani.
Njia ya kuvishinda vikwazo hivyo ni kukataa uasherati na machukizo mengine, kuomba sana na kuishi maisha matakatifu ya Wokovu wa YESU KRISTO Mwokozi aliye hai.
Kumbuka kwamba katika mambo ya kiroho hakuna kitu kinaitwa wengi wape. Kwenye mambo ya kiroho kuna kumsikiliza ROHO MTAKATIFU basi.
Usikubali ndugu zako au rafiki zako wakuchagulie mchumba, kwa sababu ni wengi wamempendekeza dada fulani au kaka fulani kwako.
Kuhusu Mchumba nakuomba chagua mwenyewe huku ukimshirikisha MUNGU , maana mchumba huyo mkiingia katika ndoa mtakuwa ni ninyi tu na MUNGU wenu, hao marafiki hawatakuwepo na hao ndugu hawatakuwepo hivyo amua mwenyewe.
Kumbuka pia kwamba adui wa kwanza kabisa wa uchumba ni uasherati, uepuke sana huo kama kweli unataka kuingia katika ndoa njema.
Adui mwingine mbaya sana ni kutokumcha MUNGU, usikubali kuwa hivyo.
Adui mwingine wa uchumba ni kusikiliza kila mtu anayekushauri.
Adui mwingine ni wivu.
Ninaweza kusema mengi mno lakini kwa leo inatosha hapa, somo hili pia ni Moja ya masomo yangu ya vitabu hivyo siku nikikutangazia kitabu nitaomba uniunge mkono pia.
Mche MUNGU katika KRISTO YESU Mwokozi na utaitwa heri.
Asante kama umelielewa Neno la MUNGU la siku ya leo ila nina neno moja la mwisho kwako leo.
Bwana YESU Amekaribia Kurudi.
Je, Umejiandaaje?
Je, Unaendeleza Dhambi Ili Siku Ile Uachwe Na Bwana YESU? Je, Umeshika Wokovu Na Utakatifu Hata Unyakuliwe Siku Ile Kwa Ajili Ya Kwenda Uzima Wa Milele?
Majibu Sahihi Yako Moyoni Mwako Ila Nakusihi Mpokee Bwana YESU Kama Hujampokea Na Nakusihi Ishi Maisha Matakatifu Ukiwa Ndani Ya Wokovu.
Vya Dunia Tulivikuta Na Tutaviacha.
Ndugu, Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Kuokoka.
Vya Dunia Visikupotezee Muda Wako Hata Ukasahau Wokovu Wa Bwana YESU Kwako.
CantonaJoseph’s contacts
Facebook https://www.facebook.com/CantonaJoseph/
Instagram https://www.instagram.com/Cantona.Joseph.
Twitter https://twitter.com/@CantonaJoseph
LinkedIn https://www.linkedin.com/in/CantonaJo…
Management Fortune Baraka Entertainments
Website https://CantonaJoseph.Wordpress.Com
Email:fortunebaraka.entertainmentsltd@gmail.com cantona.online254@gmail.com
Contacts +254748836127
Wewe ni wa maana sana!
All Rights Reserved @2019/FortuneBarakaEntertainments.
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.