Hakuna wa kuzima ndoto yako!!!

Tunasoma kutoka

Mwanzo 39:1-6

Neno linasema,

“1 Basi Yusufu akaletwa mpaka Misri naye Potifa, akida wa Farao, mkuu wa askari, mtu wa Misri, akamnunua mkononi mwa hao Waishmaeli waliomleta huko.
2 BWANA akawa pamoja na Yusufu, naye akasitawi; naye alikuwa katika nyumba ya bwana wake, yule Mmisri.
3 Bwana wake akaona ya kwamba BWANA yu pamoja naye, na ya kuwa BWANA anafanikisha mambo yote mkononi mwake.
4 Yusufu akaona neema machoni pake, akamtumikia. Naye akamweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na yote yaliyomo akayaweka mkononi mwake.
5 Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo, BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu. Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.
6 Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu.Naye Yusufu alikuwa mtu mzuri, na mwenye uso mzuri.”
Haleluya!

Habari hii tunayoisoma hapana shaka tumepata kuisikia pahala pengi.
Wahubiri, Walimu, Wainjilisti n.k wameizungumza kwa namna mbalimbali lakini leo tuisome kwa anuani hii,
“NUNUA HATMA YAKO”

Wana wa Mungu, wengi mwakumbuka kisa cha Yusuf, kuuzwa na ndugu zake kwa Waishmael/Waarabu, wafanya biashara ya utumwa wakati huo.
Waishimael wafikapo Misri kushusha mzigo, basi wakutana na Afande, Askari polisi mmoja aitwa Potifa.
Afande akafika bei bhana, akachukua bidhaa inaitwa Yusuf!
Oooh! Haleluya!
Nasema na mtu hapa?
Hebu tupungiane mkono pahala hapo ulipo

OK, hatma ni nini?
Kwa lugha rahisi hatma yafasiliwa kama mafanikio, mambo mema yanayotarajiwa kutukia kitambo kidogo.
Mbegu inapandwa leo ili hatimaye kesho tule chakula.
Mtoto anasomeshwa leo ili kesho awe na hatima njema, mwisho mwema, mambo mema.
Haleluya!

Ok,
Kanisa katika uso wa Dunia, wapo watu wa namna mbili.
Watu hao ni hawa;
I. Wauzaji wa Hatima zao
II. Wanunuzi wa Hatima zao

Wauzaji wa Hatma zao
Hawa ni ndugu wa Yusuf, watoto wa Mzee Yakobo.
Waishmael/Waarabu ( Wauza Yusuf)
Akina Adam&Eva (Wawapo Eden)
Akina Essau (mnakumbuka biashara yake na mdogo wake Yakobo bila shaka
Kwenye hilo somo hapo juu, Israel ni muuzaji wa hatma yake.

Watu hawa hutoa/huuza vitu ambavyo Mungu ameachilia kwenye maisha yao vije kuwa msaada. Vije kuwa lango la baraka kwenye maisha yao.

Wanunuzi wa Hatma zao
Hawa ni akina Potifa, Yakobo, Rahabu-kahaba n.k
Mnakumbuka nyumbani kwa Isaka, biashara kati ya watoto wawili ilifanyika, Essau na Yakobo.
Kuna watu ambao hutoa, huuza mibaraka yao, hasa kwa kutokujua.
Mungu huachilia watu wema kwao, vitu vyema kwao lakini pasipokutambua huvitoa maishani mwao.

Kimsingi watu hawa, wanunuzi wa hatma wapo kila familia, ukoo, mji, nchi nk.
Mpendwa kila mtu anapozaliwa hapa Duniani,
Kila familia unayoiona hapa Duniani,
Kila Ukoo, Ardhi/Nchi hapa Duniani
MUNGU AMEWEKA HATMA YAO/YAKE KUPITIA KWA MTU FULANI

Tunapofanya Maombi mbele za Mungu Mtakatifu, huwa hashuki kwenye kiti chake cha enzi aje hapa Duniani kutusaidia.
Kwa vile amemwekea kila mmoja hatma yake, basi humwinua mtu huyo ili awe lango lake la kuingia Kanaani.
Yusuf wako aweza kuwa Rafiki, Mzazi, Babu, Bibi, Mjomba, Shangazi, Kaka, Dada, Msichana wa kazi-kijakazi, Mvulana wa kazi n.k

Potifa, Afande wa Kimisri amenunua hatma yake (Yusuf) kutoka kwa Waarabu. Yusuf anapoingia tu katika maisha yake kila kitu kikabadilika!
Kila kitu kikaanza kuwa chema.
Soma hapa kidogo;

“Ikawa tokea wakati alipomweka awe msimamizi juu ya nyumba yake, na vyote vilivyomo,

BWANA akabariki nyumba ya yule Mmisri kwa ajili ya Yusufu.

Mbaraka wa BWANA ukawa juu ya vyote alivyokuwa navyo katika nyumba, na katika shamba.
6 Akayaacha yote aliyokuwa nayo mkononi mwa Yusufu; wala hakujua habari za kitu cho chote chake, ila hicho chakula alichokula tu”
Hatma ya Potifa hiyo.
Afande ameneemeka kwa sababu ya mkono wa Yusuf!
Haleluya!
Mtumwa, Houseboy Yusuf amekuwa lango la neema kwa Mmisiri asiyemjua hata Mungu.
Kanisa, tunyamaze kimya. Kuanzia leo tusihoji wasiomjua Mungu kubarikiwa dabodabo afu Watakatifu tunateseka.
Kuna akina Potifa katika uso wa Dunia wamenunua hatma zao.
Wamekutana na malango kwenye maisha yao.

Mpendwa, kuna mtu akiingia kwenye maisha yako, ofisi yako, biashara yako, huduma yako anakuletea kibali.
Anafanyika Baraka!
Anafanyika Lango la Neema!
Mtu huyo ukiwa naye, ukamtambua kama Potifa alivyomtambua, mtumie barabara!
Haleluya! Haleluya!
Oooh! Nasikia upako hapa!
Oooh! Glory to God! Glory to God!
Potifa ameachia kila kitu kwenye mikono ya mtumwa Yusuf.
Tumsifu huyu Afande jamani!

Potifa, kanunua hatma ya maisha yake na taifa lake Misri.
Israel imeuza hatma ya taifa lake kupitia watoto wa Yakobo.

Mwana wa Mungu,
Wewe unayo hatma yako hata sasa?
Umeiuza hatma yako?
Umeinunua hatma yako?
Jichunguze!

Pamoja na Potifa kubarikiwa mwafahamu vema yaliyomkuta Yusuf baadaye.
Mama mwenye nyumba, Mrs. Potifa akapanga uovu kisha HATMA ikauzwa tena na kuingia gerezani.

😁Yusuf muota ndoto mwamkumbuka bila shaka. Mwakumbuka aitwavyo Ikulu ya Misri, kwa Pharaoh na kutafsiri ndoto.
Mzee Pharaoh anasema hivi,

Mwanzo 41:38-44

38 Farao akawaambia watumwa wake,

Tupate wapi mtu kama huyu, mwenye roho ya Mungu ndani yake?

39 Farao akamwambia Yusufu, Kwa kuwa Mungu amekufahamisha hayo yote, hapana mwenye akili na hekima kama wewe.
40 Basi wewe utakuwa juu ya nyumba yangu, na kwa neno lako watu wangu watatawaliwa. Katika kiti cha enzi tu nitakuwa mkuu kuliko wewe.
41 Farao akamwambia Yusufu, Tazama, nimekuweka juu ya nchi yote ya Misri.
42 Farao akavua pete yake ya muhuri mkononi mwake, akaitia mkononi mwa Yusufu; akamvika mavazi ya kitani nzuri, na kumtia mkufu wa dhahabu shingoni mwake.
43 Akampandisha katika gari lake la pili alilokuwa nalo. Na watu wakapiga kelele mbele yake, Pigeni magoti. Hivyo akamweka juu ya nchi yote ya Misri.
44 Farao akamwambia Yusufu, Mimi ni Farao, na bila amri yako, mtu asiinue mkono wala mguu katika nchi yote ya Misri.
👆👆👆
Umekubali Hatma ya Misri ilikuwa mikononi mwa Yusuf?
Kumbe Potifa alikuwa lango japo mkewe aliuondoa mbaraka kwenye nyumba yake.
Tunafahamu yaliyotokea Misri enzi yote ya Yusuf.

Mwana wa Mungu

UNAWEZAJE KUNUNUA HATMA YAKO?
Kwa somo tulilojifunza, mtu anaweza kununua hatma yake kwa kufanya yafuatayo;

  1. Kutenda Haki na Huruma
    Tumeona ufunguo mkuu wa kuinuliwa kwa Yusuf huko Ugenini ni kutenda haki na huruma pote alipowekwa kuhudumu.
    Kutenda haki
    Kuwahurumia wengine
    Kukataa dhambi
    Kuwasaidia wengine
    Ni Lango la Hatma njema katika maisha yetu.

Adam auzapo hatma yetu wanadamu Eden imebidi ashuke Yesu Kristo kuja kununua hatma yetu kwa Damu yake.
Kwa ajili yake sote tukakombolewa kutoka kwa uharibifu tuliodumbukizwa.

Kuna Mzee mmoja aitwa Mordekai, amekabeba kajomba kake kuishi nako baada ya Dada yake kufariki, kajomba kaitwa Esta.
Mwakumbuka ukombozi uliomtokea Mordekai na wayahudi wote kwa mkono wa haka kajomba alikokaisidia.

  1. Tambua watu walioletwa kwako na Mungu kama Malaika
    (Destiny helper/Ngazi zako za kupanda juu)
    Hawa ni wawezeshaji.
    Tumesema huko juu, unapoomba, Mungu hukuinulia watu wa kuleta majibu katika hoja zako.
    Huinua watu katikati yako wakusaidie.
    Hutumia akina Yusuf kukukwamua ulipokwama.

Yusufu yupo wa kuondoa teso katika mji wako, familia yako, ukoo wako, biashara yako, ofisi yako, jumuiya yako n.k

Soma
2Fal.5:1-5
Hapa kuna habari za Nahamani, mwenye ukoma.
Binti wa kazi, amekuwa lango lake la uponyaji.
Mama mwenye nyumba ametambua lango lipo kwa binti, kijakazi wake.
Akaitumia fursa na hatma ya mumewe ikawa njema.

Soma
1Samw.9:1-10
Kuna Habari ya Sauli na kijana wake wa kazi.
Mtumwa, house boy amekuwa lango la hatma njema katika nyumba ya Mfalme.
Ila, Wafalme wametambua na kumtumia vema.

MwanaNDOA kwa nini lakini?
Siyo vizuri ujue.
Adam kanunua hatma njema, Eva anauza!
Potifa kanunua mbaraka, Mkewe anauuza!
Ndoa hizi tuziombee wajameni!
Haleluya! Haleluya

  1. Tambua yanayoendelea katika uso wa Dunia
    Hapa Mungu anataka kusisitiza kuhusu umuhimu wa taarifa na maarifa katika uso wa Dunia.
    Ukitaka kufanikiwa;
    Tafiti
    Soma
    Tafuta maarifa
    Uliza
    Fuatilia vyombo vya habari n.k

Kuna vitu Mungu anafanya kupitia maarifa. Wengine wamebarikiwa kwenye maisha yao kwa hili tu bila hata kuitwa Walokole, Watakatifu n.k
Wengi hapa ulimwenguni wanafanikiwa kwa sababu wametambua siri mbalimbali za mafanikio na wanazifanyia kazi.
Hatusemi Mungu asipewe namba 1, hapana!
Mungu amesisitiza sana tumkamate sana elimu/maarifa na tusimuache aende zake maana huyo ni uzima wetu.
Tusome Vitabu.
Tuangalie Habari.
Tusikilize Habari.
Tupite mitandaoni.
Tuulize, tunawezaja kuwa na hatma njema?
Mbinu zipi tutumie tufike Kanaani yetu, nchi ya maziwa na asali?

Somo hili ni refu kidogo.
Tusichoke.

Ok,
Huenda Uliiuza Hatma yako.
Hebu mtafute Yusuf wako kama alipotea.
Huenda Mungu alimleta kwako ukamuuza kama wana wa Yakobo, Kama mke wa Potifa n.k
Nenda kamwombe Msamaha.
Nenda katengeneze ili mbaraka urudi kwenye mji wako.

Kama hujamtambua bado Yusuf wako basi, Omba Mungu akukutanishe naye. Mungu akuinulie.
Ajapo, ukae naye Sawasawa na Ukamweke kuwa juu ya nyumba yako isipokuwa Ufalme tu ndiyo ubaki nao kama Pharaoh alivyofanya!

Yusuf ameanzia utumwa lakini Utukufu wake wa Mwisho ukawa mkuu kuliko ule wa kwanza.

Kwa Jina la la Yesu Kristo, Mwana wa Mungu

“MWAKA 2020 UTUKUFU WAKO UTAKUWA MKUU KULIKO ULE WA KWANZA!”
Sema “Amen” kujiambatisha na unabii huu!

Mungu Akubariki sana!
Asante kwa kushiriki nami karamu hii.

CantonaJoseph’s contacts

Facebook https://www.facebook.com/CantonaJoseph/

Instagram https://www.instagram.com/Cantona.Joseph.

Twitter https://twitter.com/@CantonaJoseph

LinkedIn https://www.linkedin.com/in/CantonaJo

Management Fortune Baraka Entertainments

Website https://CantonaJoseph.Wordpress.Com

Email:fortunebaraka.entertainmentsltd@gmail.com

cantona.online254@gmail.com

Contacts +254748836127

Wewe ni wa maana sana!

All Rights Reserved @2019/FortuneBarakaEntertainments.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a Reply