Radio Fortune Africa- Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

WAZIRI mteule wa Uchumi wa Baharini na Uchimbaji Madini Hassan Ali Joho amekana madai kuwa anahusika katika ulanguzi wa mihadarati.
Bw Joho alisema hakuna ushahidi wowote ambao umewasilishwa na asasi yoyote ya umma kumhusisha na uovu huo.
Akijitetea mbele ya Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi Jumapili, gavana huyo wa zamani wa Mombasa alieleza kuwa wakati mmoja, aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani Profesa George Saitoti aliwasilisha ripoti bungeni ambayo ilimwondolea lawama kuhusu madai kuwa alihusika katika sakata ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

“Ni kweli kwamba madai hayo yamewahi kutolewa dhidi yangu. Uchunguzi ulifanywa na asasi husika za serikali. Baadaye aliyekuwa waziri wa usalama marehemu Saitoti aliwasilisha bungeni ripoti hiyo ya uchunguzi ulioendeshwa na asasi za humu nchini na kimataifa na hakukuwa na ushahidi wowote wa kunihusisha na madai hayo,” Bw Joho akaiambia kamati hiyo inayoongozwa na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula.
Alikuwa akijibu swali kutoka kwa Mbunge wa Teso Kusini Mary Emase aliyemtaka aieleze kamati hiyo endapo madai kwamba yeye ni mmoja wa walanguzi wa dawa za kulevya ni kweli au la.
Bw Joho alisema yeye hufanya biashara halali inayohusisha uchukuzi wa bidhaa na “endapo nilikuwa nikifanya biashara haramu singesazwa na serikali zilizopita.”
WAZIRI mteule wa Michezo na Masuala ya Vijana, Kipchumba Murkomen, amekana madai kuwa “aliuza” Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) katika mpango uliohusisha kampuni moja ya India.
Akijitetea mbele ya wabunge Jumamosi jioni mnamo Agosti 3, Bw Murkomen, ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi hadi Julai 11, 2021 alipofutwa kazi pamoja na wenzake 20, alisisitiza kuwa kama Waziri hana mamlaka ya kuuza au kukodi mali ya umma kwa kampuni ya kibinafsi kivyake.
“Sijatia saini mkataba na kampuni yoyote ili kuuza au kukodi JKIA. Sina uwezo na mamlaka ya kufanya hivyo chini ya mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali na Kampuni za Kibinafsi (PPP). Kwa hivyo, sijauza JKIA kwa vyovyote,” Murkomen akaeleza kufuatia madai kuwa aliuza JKIA kwa Kampuni ya Adani Airport Holdings Ltd, kutoka India.
Alifichua kuwa kile anachoelewa ni kwamba kampuni hiyo imewasilisha ombi kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Viwanja vya Ndege Nchini (KAA) ikitaka kuwekeza katika uwanja wa JKIA.
“Kampuni hiyo imetuma maombi na hiyo ni hatua ya kwanza. Na ni ombi la kukodisha sehemu ya JKIA sio kuinunua. Mchakato wa ukodishaji ni mrefu chini ya mpango wa PPP na sharti uhusishe maoni kutoka kwa Wakenya ambao ndio wamiliki halisi wa mali hiyo,” Bw Murkomen akasema alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Uteuzi kupigwa msasa kuhusu ufaafu wake kushikilikia wadhifa wa Waziri wa Michezo.

Waziri huyo mteule alieleza kuwa mpango huo pia sharti uidhinishwe na baraza la mawaziri, hatua ambayo haijafikiwa ‘kwa sababu mahitaji ya kisheria hayatimizwa.’
“Kabla ya hati za mpango huo kufika mbele ya mawaziri, sharti uidhinishwe na Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Fedha. Kwa hivyo, ni wazi kwamba shughuli kama hii haiwezi kuendeshwa na mtu mmoja pekee; waziri wa uchukuzi,” Bw Murkomen akaeleza.
Suala la uuzaji au ukodishaji wa JKIA liliangaziwa hadharani kwa mara ya kwanza majuma mawili yaliyopita na Seneta wa Kisii Richard Onyonka.
Seneta huyo aliwasilisha malalamishi yake katika Bunge la Seneti akitaka maelezi kutoka kwa Wizara ya Uchukuzi kuhusu kile alichotaka kama “njama fiche ya kuuzwa kwa JKIA kwa kampuni ya Adani ya India.”

WASHINDANI wa Raila Odinga katika uwaniaji wa Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) wamepungua baada ya wawili waliomezea mate wadhifa huo kujiondoa huku orodha ya masuala ambayo kila mgombeaji amewasilisha ikionyesha changamoto za kudumu za muungano wa bara.
Kabla ya tarehe ya mwisho ya kuwasilisha wagombeaji ambayo ni Agosti 6, imeibuka kuwa Fawzia Adam wa Somalia na mgombea wa Ushelisheli Vincent Meritoni wameng’atuka kwenye kinyang’anyiro hicho, na kumuacha Raila Odinga wa Kenya kumenyana na Mahmoud Ali Youssouf wa Djibouti.
Maafisa wawili wa Serikali ya Somalia walisema kuwa Somalia haitamteua Bi Adam, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje kuwania kiti AUC, lakini wote wawili hawakutoa sababu.
Duru nyingine zilidai kuwa Somalia ilichagua kuunga mkono mgombea mwingine kutoka nchi tofauti.
Bi Adam mwenyewe hakujibu maswali ya Taifa Leo kuhusu ugombeaji wake.
Mnamo Julai 22, Wizara ya Mambo ya Nje ya Ushelisheli ilithibitisha kuwa Bw Meriton, Makamu wa Rais wa zamani, alijiondoa katika kinyang’anyiro hicho, akitaja sababu za kiafya kuwa kiini cha hatua hiyo.
“Serikali ya Jamhuri ya Ushelisheli inapenda kuwafahamisha kwamba Bw Vincent Meriton, Makamu wa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Ushelisheli, ameamua kutoendelea na azma ya kuwania Uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) katika uchaguzi utakaofanyika wakati wa Mkutano wa 38 wa Kawaida wa Muungano wa Afrika mnamo Februari 2025, kutokana na sababu za kiafya,” ilisema taarifa hiyo.
Huku muda wa kuwasilisha majina ya wagombeaji ukiwa Jumanne ijayo, inaonekana kinyang’anyiro hicho hadi sasa kitakuwa kati ya Bw Odinga na Bw Youssouf. Wote wawili waliwasilisha maombi yao kwa Wakili wa Kisheria wa Muungano wa Afrika mnamo Jumatatu, Julai 29.
Hata hivyo, kulikuwa na habari kwamba aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Nje wa Tanzania, January Makamba, anaweza kujiunga na kinyang’anyiro hicho. Bw Makamba na maafisa wa Serikali ya Tanzania hawakuthibitisha.
Chini ya kanuni za utaratibu, ilibidi wawaniani kwanza kuwasilisha stakabadhi kwa Mkuu wa Kanda ya Mashariki, ambaye ni Mwakilishi Mkuu wa Mauritius katika Muungano wa Afrika, Dharmraj Busgeeth, na baadaye kwa Wakili wa Kisheria wa Tume ya AU. Kanda ya Mashariki itagombea kiti cha Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika, chini ya sheria mpya.
Mnamo Jumatatu, Wizara ya Masuala ya Nje na Masuala ya Wakenya Wanaoishi Ng’ambo ilisema imemteua Bw Odinga kwa sababu ana uzoefu wa kutosha kushughulikia changamoto za bara hili.
“Afrika inaendelea kukumbwa na dhiki ya kiuchumi, changamoto za kimazingira, migogoro, ugaidi na mizozo ya jumla ya kijamii, inayochochewa na ushindani wa kijiografia.
“Labda hakuna wakati wowote katika historia ya Muungano wa Afrika ambapo bara linahitaji kiongozi mwenye maono zaidi, mwanasiasa aliyekamilika na mtetezi wa Afrika,” Kenya ilisema.
Bw Odinga na mpinzani wake wa Djibouti wanalenga kutatua matatizo ya bara, ikiwa ni pamoja na yale ya AUC.
Bw Odinga anasema anataka kuangazia utangamano wa Afrika na maendeleo ya miundombinu, akitumia uzoefu wake kama Waziri wa zamani wa Kawi na baadaye Mjumbe Mkuu wa Muungano wa Afrika kuhusu Maendeleo ya Miundombinu.
Bw Youssouf aliahidi kutekeleza mambo kama hayo lakini pia alisema kuwa atatumia ushiriki wa sekta ya kibinafsi ili kutimiza matumizi ya Eneo Huru la Biashara ya Bara la Afrika (AfCTA), mkataba wa 2018 unaokusudiwa kupanua biashara ya ndani ya Afrika lakini ambao unahitaji kujengwa upya kwa miundombinu.
- AUC
- Dharmraj Busgeeth
- January Makamba
- Mahmoud Ali Youssouf
- raila odinga
- SOMALIA
- tanzania
- USHELISHELI
- Vincent Meriton
VIONGOZI mbalimbali wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kutoka eneo la Magharibi wamejitosa katika kinyang’anyiro cha kumrithi aliyekuwa Gavana wa Kakamega, Wycliffe Oparanya.
Baadhi ya viongozi hao walio na lengo la kuchukua nafasi ya Bw Oparanya (Naibu Mwenyekiti wa chama hicho) wanatoka katika Kaunti za Kakamega na Vihiga huku wajumbe wa ODM kutoka kaunti hizo mbili wakitaka Fernandes Barasa (Gavana Kakamega) na Godfrey Osotsi (Seneta Vihiga) wamrithi Bw Oparanya.
Mnamo Ijumaa, wajumbe wa ODM kutoka Kaunti ya Kakamega waliidhinisha Bw Barasa kuhudumu kama naibu kiongozi wa chama.
Hii ni baada ya Bw Oparanya kuteuliwa na Rais William Ruto kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika na Maendeleo ya Biashara Ndogo Ndogo.

Bw Oparanya alikuwa akishikilia wadhifa huo pamoja na mwenzake Hassan Joho aliyekuwa Gavana wa Kaunti ya Mombasa kabla ya kuteuliwa katika baraza la mawaziri.
Uteuzi wa Bw Oparanya katika baraza la mawaziri hata hivyo unakabiliwa na changamoto kadhaa baada ya Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) kudai kwamba gavana huyo wa zamani alijihusisha na shughuli za ufisadi zinazohitaji kuchunguzwa.
Wajumbe wa ODM kutoka Kakamega wakiongozwa na Mbunge wa Lugari (Mbunge) Nabii Nabwera waliteta kwamba kwa kuwa nafasi ya naibu kiongozi wa chama ilikuwa ikishikiliwa na Bw Oparanya kutoka Kaunti ya Kakamega, inafaa wadhifa huo usalie katika kaunti hiyo.

WAZIRI mteule wa Kawi na Mafuta James Wandayi amepuuzilia mbali madai kwamba alitumia maandamano ya vijana wa kizazi cha Gen Z kuomba kazi ya uwaziri.
Akihojiwa na Kamati ya Bunge kuhusu Uteuzi hapo Jumamosi, Agosti 3, 2024 Wandayi alifafanua kuwa jina lake liliwasilishwa na mtu mwingine wala si yeye alituma maombi ateuliwe.
Aidha, Wandayi, ambaye alikuwa Kingozi wa Wachache, alisisitiza kwamba licha ya kuteuliwa kuwa waziri bado anaunga mkono masuala yaliyoibuliwa na waandamanaji wanaoipinga serikali.
Wandayi alisema masuala yaliyoibuliwa na vijana hao yalikuwa na umuhimu mkubwa na yanahitaji jibu la haraka kutoka kwa serikali.
Wandayi alisema kuwa baadhi ya malalamishi ya waandamanaji yanawiana na yale wamekuwa wakiibua katika Bunge la Kitaifa.
“Vijana hawakuibua masuala tofauti na yale ambayo tulikuwa tukiibua bungeni. Ni masuala muhimu ambayo lazima yashughulikiwe,” Wandayi alifafanua.
“Hivyo, si sahihi kusema kwamba tulitumia maandamano ya Gen Z ili kupata kazi. Sikuwahi kuomba kujiunga na serikali, lakini nilifurahi jina langu lilipendekezwa,” aliongeza.
Mbunge huyo alimpongeza Rais William Ruto kwa kumteua waziri.
“Bado ninashikilia kwamba hatukusaliti vijana kwa vyovyote vile,” alisisitizia wanakamati.
Wandayi ni miongoni mwa viongozi wanne wa chama cha upinzani cha Orange Democratic Movement (ODM) walioteuliwa katika nyadhifa za uwaziri na Rais Ruto.
- #MawaziriWateule
- Azimio
- Baraza la Mawaziri
- bunge
- Cabinet
- kawi
- Ministry of Energy
- odm
- Opiyo Wandayi
- William Ruto

GAVANA wa Kwale Bi Fatuma Achani amewaonya wanasiasa dhidi ya kutumia mradi wa basari kujipigia debe kisiasa.
Aliwaonya viongozi kutowahadaa wakazi na kuingiza siasa kwenye suala muhimu la hazina ya elimu.
“Wanasiasa jamani, tuache kuingiza siasa kwenye suala la kielimu. Tusiwahadae wakazi sababu ya manufaa ya kisiasa. Mradi wa basari ni wa kunufaisha wakazi wa Kwale,” alisema Bi Achani bila kutaja mwanasiasa mahususi.
Aliungwa mkono na Naibu wake Bw Chirema Kombo ambaye alisema mradi huo umekuwa katika miaka 10 ya uongozi wa aliyekuwa Gavana wa Kwale Bw Salim Mvurya.
Kulingana na Bw Kombo, mradi huo umeleta maendeleo katika sekta ya elimu eneo hilo.
“Matokeo yanaonekana. Viwango vya elimu vimeimarika sababu ya mradi wa basari ambao pia umesaidia wanafunzi kutofukuzwa shuleni sababu ya ukosefu wa karo. Watoto wetu sasa wana muda mwafaka wa kusoma,” alisifu Bw Kombo.
Naibu Gavana alidokeza serikali hiyo itaendelea kusaidia wanafunzi wa familia ambazo hazijiwezi.
Bi Achani aliwahakikishia wazazi kuwa hakuna mwanafunzi yeyote anayetoka familia maskini atakosa basari.
Aliongeza kuwa wanafunzi wote wanaohitaji basari watanufaika na mradi huo.
Haya yanajiri wakati wanasiasa wanaendelea kukashifiwa kwa kutumia basari kisiasa.
Baadhi ya wanasiasa wamegunduliwa wamekuwa wakiwalazimisha wananchi kuthibitisha kama ni wapigakura maeneo husika kabla ya kupewa basari.
Mjadala unaendelea nchini kuhusu kubuniwa kwa njia mpya ya utoaji basari ili kuleta mageuzi muhimu katika sekta ya elimu.

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu, amemtengea ardhi na kumpa nyota wa Hollywood Idris Elba kibali cha kuzindua studio ya filamu nay a kufyatua michezo ya sinema nchini humo.
Haya yanajiri huku Serikali ya Kenya ikiendelea kusuasua katika harakati zake za ‘kupangapanga’ mambo.
Tanzania ambayo ni jirani ya Kenya imepiga hatua hiyo muhimu baada ya majadiliano kati ya Elba na Rais Suluhu mnamo Januari 2023 katika Kongamano la Kiuchumi la Dunia nchini Uswisi.
Elba, anayesifika kwa uigizaji wake katika filamu za ‘Luther’ na ‘The Wire’, amekuwa na nia ya kuendeleza tasnia ya uigizaji kupia filamu na michezo ya sinema barani Afrika.
Akiwa na asili ya Sierra Leone na Ghana, mwigizaji huyo wa Uingereza anatazamia kuansisha studio ambayo ni ya hadhi ya kushindana na zile za Hollywood, Nollywood na Bollywood.
Waziri wa Uwekezaji wa Zanzibar alisema kwa kutania, “Sina uhakika tutaiitaje Zanzibar sasa, iwe Zollywood au Zawood!”
Msemaji wa Rais alisema hatua hiyo haitafaidi Tanzania pekee bali pia Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Kenya kwa upande wake bado inaendelea ‘kupanga panga’ mambo katika juhudi za kutimiza ahadi ya kujenga studio za kisasa katika kila kaunti kama alivyoahidi Rais William Ruto mnamo Agosti 2023.
“Tutashirikiana na serikali za kaunti ili tuweze kutoa fursa kwa kila msanii awe katika shule ya msingi au sekondari kutoa nyimbo zake bila kikwazo chochote,” Rais Ruto alisema alipohudhuria Tamasha za Kitaifa za Muziki (KMF) katika Ikulu ya Nakuru.
- Bollywood
- Hollywood
- Idris Elba
- kenya
- KMF
- Luther
- Nollywood
- Rais William Ruto
- Samia Suluhu Hassan
- sinema
- tanzania
- The Wire
- zanzibar

NAIBU Rais Rigathi Gachagua ana wakati mgumu kutimiza masuala ambayo wakazi wa eneo la Mlima Kenya walitarajia ashughulikie, huku akikabiliwa na tishio la kutimuliwa afisini kupitia hoja bungeni.
Naibu Rais anatarajiwa kuanika changamoto za kisiasa ambazo zimemzonga kwa karibu miaka miwili tangu aingie afisini na jinsi atakavyokabiliana navyo, atakapohutubia wakazi wa kaunti za Mlima Kenya Jumapili, Agosti 4, 2024 kupitia vituo vya utangazaji vinavyotumia lugha za mama za eneo hilo.
Kwa mujibu wa mhadhiri wa chuo kikuu Profesa Macharia Munene, uwezekano wa Bw Gachagua kuteuliwa tena kama mgombea mwenza wa Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu ujao wa 2027 ni finyu mno.

“Anakabiliwa na shida kubwa zaidi kuliko mvutano wa ubabe kati yake na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi serikali. Sasa kiongozi wa upinzani Raila Odinga pia ameingia serikalini na anadhibiti wizara sita zenye ushawishi mkubwa, na bado atataka nyadhifa zaidi,” Prof Munene akasema.
Kuingia kwa Raila serikalini
Bw Odinga amefanya wandani wake wakapewa nyadhifa za wizara za Fedha, Madini na Uchumi wa Baharini, Ustawi wa Vyama vya Ushirika, Kawi, Masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, na Mwanasheria Mkuu.
Wakati Naibu Rais atakuwa akizungumza na wakazi wa Mlima Kenya – wanaojumuisha wanajamii wa Agikuyu, Aembu na Ameru – kwenye mahojiano hayo, wakazi hao watafuatilia kwa makini ili kusikiza majibu atakayotoa kuhusu masuala muhimu yanayoathiri maisha yao.
“Tutakuwa na hamu kujua nafasi yetu katika serikali hii tuliyoitundika mamlakani kwa kuipa asilimia 87 ya kura zetu, na hivyo kumpa rais uongozi wa nchi. Yule tuliyesukuma kwa upinzani ameletwa ndani na tunakubali. Kile tunataka kujua ni nafasi yetu imesalia nini,” akasema Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga, mwandani wa karibu sana wa Bw Gachagua ambaye anaonekana kugeuka kuwa msemaji wake.
Bw Kahiga aliongeza: “Tunataka kujua jinsi tutakomesha malumbano ya kisiasa na kujikita katika shughuli za utoaji huduma, tukisubiri wakati Bw Odinga atajiondoa rasmi kwenye kinyang’anyiro cha urais 2027.”
Gavana huyo anamtaka Bw Gachagua kuondolea wakazi wa Mlima Kenya hofu kuhusu kuingia kwa Bw Odinga serikalini, hatua ambayo alisema imechangia umaarufu wa Rais Ruto kushuka Mlimani kiasi cha kuathiri azma yake ya kusaka kura tena eneo hilo kwa ajili ya uchaguzi wa 2027.
Vita dhidi ya pombe haramu
Naye Mbunge Maalum Sabina Chege alimshauri Naibu Rais anafaa kuongoza eneo hilo katika kampeni ya kutetea miradi ya maendeleo badala ya kujikita katika siasa za kuendeleza masilahi ya watu binafsi.
“Tuko katika hali ambapo yule nilijaribu kumsaidia kuukwea mlima lakini akashindwa, sasa ameingia serikalini. Sisi tuliomuunga mkono tulitajwa kama maadui. Sasa sote tuko serikalini na tunahimiza kupendana,” akaambia Taifa Leo mnamo Ijumaa, Agosti 02, 2024, katika eneobunge la Gatanga.
Diwani wa wadi ya Gatanga, Bw John Kibaiya, alisema eneo la Mlima Kenya linataka kusikia mbinu anazotumia Gachagua kuendeleza vita dhidi ya pombe haramu vinavyoonekana kulegea.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Jamii ya Agikuyu (Njuri Ncheke), Bw Wachira Kiago, anahoji kuwa Naibu Rais ana kibarua cha kuelezea wakazi hatua ambazo serikali imepiga kuleta mageuzi katika sekta ya kilimo ambayo ni nguzo kuu ya uchumi wa Mlima Kenya.
“Tunataka kujua ikiwa tutaendelea kusubiri kuvuma matunda ya mageuzi katika sekta ya kilimo,” akasema.
Hatima ya Mt Kenya ndani ya UDA
Suala lingine ambalo wakazi wanataka kupata hakikisho kutoka kwa Bw Gachagua ni uthabiti wa kisiasa na kukomesha kwa mivutano isiyo na maana.
“Aidha, tunataka kujua nafasi yetu katika chama cha UDA tulichosaidia kuunda,” akasema Mbunge wa Embakasi Kaskazini James Gakuya.
Kwa upande wake Mbunge wa Naivasha Jane Kihara alisema suala la uteuzi wa makamishna wapya wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) pia ni lenye uzito mkubwa kwa wakazi wa Mlima Kenya.
Naye Seneta wa Kiambu Karungo Wa Thang’waa alisema wakazi wa Mlimani wanataka kujua ni lini mfumo wa ugavi wa mapato wa “mtu mmoja-kura moja-shilingi moja” utaanza kutekelezwa.
MBUNGE wa Likoni, Mishi Mboko, alianika ‘masaibu ya ndoa’ ya Waziri Mteule wa Leba Alfred Mutua hadharani.
Lakini Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetang’ula akakatiza tukio hilo ili kumlinda Dkt Mutua.
Mwanajopo huyo wa Kamati ya Uteuzi ya Bunge la Kitaifa alisema ‘skendo za mapenzi’ zinaweza kumharibia sifa Dkt Mutua ambaye alihojiwa kubaini ufaafu wake kuwa waziri.

“Kamati hii haiwezi kuingilia masuala ya ndoa ya mtu yeyote,” Bw Wetang’ula alimkata kalima Bi Mboko aliyeonekana kumuaibisha waziri wa awali wa Utalii na Mashauri ya Kigeni.
“Wakenya wanakutaka upunguze vituko kuhusu maisha yako ya ndoa kwa sababu vinaweza kukuharibia jina ama kukuweka katika hali mbaya,” alisema Bi Mboko.
Mwanakamati mwenza, Omar Abdi Shurie (Mbunge wa Balambala), alionekana ameaibika alipoinama na kuficha uso wake suala hili lilipoibuliwa.
“Mwenyekiti, ni bora utunze masuala yetu ya ndoa yasijulikane na umma,” alisema Bw Shurie kabla ya kukanywa na Spika asiendeleze mjadala huo.
“Hakuna hitaji la mtu kuwa katika ndoa ili atathminiwe kuwa afisa wa umma katika taifa hili,” alisema Bw Wetang’ula.
Habari za utengano kati ya Bi Lilian Nganga na Dkt Mutua mwaka wa 2021 (akiwa Gavana wa Machakos) zilivuma sana na aghalabu suala hili huibuka mara kwa mara.
Baada ya kutengana, Bi Nganga alifunga ndoa na msanii maarufu wa nyimbo za kufoka Julius Owino maarufu Juliani mnamo Februari 2022.

GAVANA wa Taita Taveta, Andrew Mwadime ameeleza nia ya serikali yake kutafuta Suluhu la kudumu la kushughulikia migogoro kati ya wanyamapori na binadamu, kama njia ya kuwaepushia wakazi hasara, maafa huku wanyamapori wakitunzwa.
Akizungumza wakati wa kufanya mkutano afisini mwake, Mwatate, alipotembelewa na maafisa kutoka kwa Hazina ya Kimataifa ya maslahi ya wanyama(IFAW), Bw Mwadime alielezea kwamba Taita Taveta ilikuwa ikifanya mazungumzo kuhakikisha wanyamapori wanatunzwa.
Alisema kuwa alilenga kushirikiana na IFAW kushughulikia migogoro hiyo ambayo ilikuwa imechochewa sana na mabadiliko ya tabianchi.
“Wakazi wetu wanapigana na wanyamapori kila mara kwa sababu ya uhaba wa maliasili kama vile maji na chakula haswa wakati wa kiangazi. Kwa kupata njia mwafaka ya kushughulikia shida hii inayohangaisha wakazi wetu moja kwa moja, tunaweza kuwa na athari kubwa sana,” akasema Bw Mwadime.
Kwa mujibu wa Naibu wa Rais anayesimamia miradi ya dunia katika IFAW, Bw Jimmiel Mandima, pendekezo hilo huenda laikawapa wakazi manufaa mengi kwa kuhakikisha kuwa binadamu na wanyamapori wanaishi kwa amani.
Kulingana na Naibu wa Gavana Taita Taveta, Bi Christine Kilalo, ushirikiano huo huenda ukawasaidia wanawake na watoto wanaoishi karibu na mbuga za wanyama kwa kuwa wanakodolewa macho na athari kubwa ya kuvamiwa na wanyamapori.
“Kuzuia wanyama hao na kuwatengea sehemu za kupata raslimali na hata kusafiri kwao kutawaokoa akina mama na watoto. Akina mama wanasaka kuni na hata maji mapema na jioni. Migogoro hii imewaacha wengi mayatima. Ni bora tukiwa hata na hazina ya kushughulikia watoto wanaopoteza wazazi kutokana migogoro hii,” akasema Bi Kilalo.

WAKAZI wa Mtongwe katika Kaunti ya Mombasa wataendelea kusafiri takriban kilomita 10 au hata zaidi ili kupata huduma za kuvuka kutoka Kisiwani Mombasa, baada ya kubainika kuwa hakuna matumaini ya kurejesha huduma za kivuko cha feri eneo la Mtongwe.
Kwa sasa wakazi hao watazidi kusongamana katika feri eneo la Likoni ambayo huhudumia takriban watu 300,000 baada ya serikali kufeli kurekebisha sehemu za kuegeshea feri. Haya yanajiri kukikosekana imani ya mradi huo kutengewa fedha zozote na serikali kuu.
Mnamo Oktoba 15, 2021, Huduma za Feri Nchini (KFS) ilisimamisha huduma za feri Mtongwe ikihoji kuwa kulikuwa na masuala ya kiusalama baada ya sehemu ya eneo la kuegeshea kusombwa na mawimbi ya baharini. Tangu wakati huo, wakazi wamekuwa wakilazimika kutembea mwendo mrefu kuvuka feri eneo la Likoni. Isitoshe, kusitishwa kwa huduma hizo kumewaacha wafanyabiashara wadogo wadogo waliokuwa wakitegemea biashara katika eneo hilo katika njia panda. Wateja waliokuwa wakinunua bidhaa katika sehemu hiyo walilazimika kubadilisha njia. Mnamo Mei 2022, Kamati ya Bunge ya Uchukuzi, kazi za umma na nyumba iliahidi kuwa huduma za feri zingerejea kabla ya mwaka kukamilika. Ahadi hizo hazikutimia licha ya Mamlaka ya Bandari Humu nchini (KPA) kutenga fedha za kurekebisha maeneo ya kuegeshea feri katika mwaka wa kifedha wa 2022/2023.
Mamlaka hiyo ilieleza kuwa kuchelewa huko kulitokana na masuala ya kikandarasi kati ya KPA na mwanakandarasi ila ikasema hilo lilishughulikiwa. Taarifa zinaeleza kuwa misingi ya maeneo hayo ya kuegeshea feri ilikuwa imeharibika kiasi cha sehemu moja kujitenga na eneo zima, ishara kuwa ingeng’oka baada ya muda.
Juhudi za wakazi kuelezea Rais William Ruto kuhusu masaibu yao alipozuru ukanda wa Pwani wiki kadhaa zilizopita hazikuzaa matunda, rais akieleza kuwa kulikuwa na mipango ya kutafuta suluhu ya kudumu.
“Tuanelewa masaibu ya wakazi wa Likoni tangu kufungwa kwa daraja la kuelea la Liwatoni ambalo lilikuwa likisababisha msongamano wa meli katika bandari. Nimezielekeza Mamlaka ya kusimamia barabara nchini (KENHA) na KPA kutafuta suluhu katika eneo la feri,” akasema Bw Ruto.
Wakazi wa Mtongwe walikuwa wakitumia daraja hilo la Liwatoni kama njia mbadala ya kivukio cha feri kabla ya serikali kulifunga kwa kuhitilafiana na njia ya meli zinazoingia na kutoka katika Bandari ya Mombasa.
TAARIFA ZAIDI
- Nigeria: Rais Tinubu aomba vijana kukomesha maandamanoRais wa Nigeria Bola Tinubu ametoa wito wa kusitishwa kwa maandamano dhidi ya gharama ya maisha, ili kutoa fursa ya mazungumzo.Hii ni mara ya kwanza Rais Tinubu anazungumzia suala hilo tangu raia waliokata tamaa kuingia mitaani wiki iliyopita kulalamikia hali ya maisha.Katika matangazo ya televisheni, Tinubu alitoa wito wa kukomeshwa kwa ghasia katika majimbo kadhaa tangu kuanza kwa maandamano, akisema yuko tayari kwa mazungumzo.”Wanaijeria wangu wapendwa, hasa vijana wetu, nimewasikia. Ninaelewa uchungu mlio nayo… na ninataka kuwahakikishia kuwa serikali yetu imejitolea kusikiliza na kushughulikia kero za raia wetu,” alisema.Mshirikishe mwenzako, Nigeria: Rais Tinubu aomLl Somalia yawakamata maafisa wakuu wa usalama kwa kuzembea kazini
- Maafisa wakuu wa usalama wamekamatwa katika mji mkuu wa Somalia Mogadishu baada ya shambulio la kujitoa muhanga lililofanyika katika ufuo maarufu wa Lido, siku ya Ijumaa.Takriban watu 37 waliuawa na wengine zaidi ya 200 kujeruhiwa kulingana na wizara ya afya ya Somalia.Waziri Mkuu Hamza Abdi Barre alisema maafisa hao walikamatwa kwa kushindwa kudhibiti usalama kutokana na uzembe.Rais Hassan Sheikh Mohamud aliitisha kikao cha dharura cha vyombo vya usalama vya nchi hiyo, Jumamosi ili kutathmini ya shambulio hilo.Ufukwe wa Lido unapatikana katika wilaya ya AbdiAziz ya mji mkuu, eneo lenye utajiri na usalama kiasi, ambalo pia ni nyumbani kwa maafisa wakuu wa serikali.Hapo awali imekuwa shabaha ya mashambulizi ya Al Shabaab.Uturuki, mshirika wa usalama wa Somalia, kupitia wizara yake ya mambo ya nje ilisema itaendelea kusimama pamoja na nchini hiyo katika mapambano yake dhidi ya ugaidi.Mshirikishe mwenzako, Somalia yawakamata maafisa wakuu wa usalama kwa Olimpiki 2024: Shelly-Ann Fraser-Pryce ajiondoa katika mbio za mita 100
Chanzo cha picha,Getty ImagesMaelezo ya picha,Shelly-Ann Fraser-Pryce ameshinda mataji 13 ya kimataifaMwanariadha wa Jamaica Shelly-Ann Fraser-Pryce alijindoa kwenye mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024 ya mbio za mita 100 kabla ya nusu fainali ya ya mbio hizo Jumamosi kwa sababu ya jeraha.Mjamaica mwenye umri wa miaka 37, mshindi wa dunia mara tano na bingwa mara mbili wa Olimpiki wa mbio za mita 100, anashiriki mashindano yake ya mwisho kabla ya kustaafu.Mwanariadha huyo ambaye ana medali 24 za kimataifa, alifuzu kwa nusu fainali ya mbio hizo lakini hakushiriki siku ya Jumamosi.Fraser ni sehemu ya timu ya wanawake ya 4x100m ya Jamaica, ambayo ilishinda dhahabu huko Tokyo miaka mitatu iliyopita.Siku ya Jumapili Fraser-Pryce alisema ilikuwa “vigumu” “kupata maneno ya kuelezea masikitiko yangu”.Katika chapisho katika mtandao wa Instagram, alisema: “Ninajua kuwa mashabiki wangu pia wamevinjwa moyo na uamuzi huu.”Fraser-Pryce alikuwa anawania kushinda mbio za100 katika mashindano ya Olimpiki kwa mara ya tano mfululizo baada ya kunyimwa taji la tatu na mchezaji mwenzake Elaine Thompson-Herah huko Tokyo miaka mitatu iliyopita.Maelezo zaidi:Paris Olimpiki 2024: Wajue nyota wa kimataifa wa kuwatazama“Hijabu ni sehemu ya maisha yangu” – nyota wa voliboli ya ufukweniJedwali la medali ya mashindano ya Olimpiki ya Paris 2024Mshirikishe mwenzako, Olimpiki 2024: Shelly-Ann Fraser-Pryce ajiondoa katika mbioL Rwanda yafunga makanisa 4,000
Chanzo cha picha,Getty ImagesMaelezo ya picha,Makanisa ya Kipentekoste, ambayo mara nyingi yanaendeshwa na wahubiri wanaodai kuwa na uwezo wa kufanya miujiza, yamekua maarufu barani Afrika.Zaidi ya makanisa 4,000 yamefungwa katika kipindi cha mwezi mmoja uliopita nchini Rwanda kwa kushindwa kuzingatia kanuni za afya na usalama, ikiwa ni pamoja na kutozuiliwa ipasavyo.Hatua ihiyo imeathiri zaidi makanisa madogo ya Kipentekoste – baadhi yanafanya ibada nje ya mapango au kwenye kingo za mito.”Hii haifanywi kuwazuia watu kusali bali kuhakikisha usalama na utulivu wa waumini,” Waziri wa Serikali ya Mitaa Jean Claude Musabyimana aliviambia vyombo vya habari vya serikali.Ni msako wa kwanza mkubwa tangu sheria ilipobuniwa miaka mitano iliyopita kudhibiti maeneo ya ibada.Sheria inayataka makanisha kuendesha ibada kwa mpangilio katika mazingira salama na vile vile kuharamisha matumizi yao vipaza sauti.Sheria hiyo pia inawalazimu wahubiri wote kupata mafunzo ya kidini kabla ya kufungua kanisa.Sheria ilipopitishwa mwaka wa 2018 takriban makanisa 700 yalifungwa hapo awali.Wakati huo, Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema nchi hiyo haihitaji nyumba nyingi za ibada, akishikilia kuwa idadi hiyo kubwa inafaa tu kwa uchumi ulioendelea zaidi na njia za kuziendeleza.Bw Kagame, ambaye ndio mwanzo ameshinda muhula wa nne madarakani kwa 99% ya kura, anatawala jamii inayodhibitiwa vikali ambapo wakosoaji wake wanasema kuna uhuru mdogo wa kujieleza.Operesheni inayoendelea inayolenga makanisa inafanywa na mamlaka za mijini kwa ushirikiano na Bodi ya Utawala ya Rwanda (RGB).Mamlaka zinasema zinachukua hatua hiyi kwali kwani makanisa yalipewa muda wa miaka mitano kuzingatia kanuni hizo kikamilifu.Idadi kubwa ya Wanyarwanda ni Wakristo lakini wengi pia wanafuata desturi za jadi.Makanisa ya Kipentekoste, ambayo mara nyingi yanaendeshwa na wahubiri wanaodai kuwa na uwezo wa kufanya miujiza, yamekua kwa kasi katika sehemu nyingi za Afrika katika miaka ya hivi karibuni.Mengine ni makubwa, yanavutia maelfu ya waumini kila Jumapili, lakini mengine ni majengo madogo yaliyojengwa bila idhini.Mshirikishe mwenzako, Rwanda yafunga makanisa. - Uingereza: Zaidi ya 90 wakamatwa kufuatia maandamano ya mrengo mkali wa kulia
Chanzo cha picha,PA MediaZaidi ya watu 90 wamekamatwa baada ya maandamano ya siasa kali za mrengo wa kulia kusababisha ghasia katika miji kadhaa nchini Uingereza siku ya Jumamosi.Vurugu zilishuhudiwa katika miji ya Hull, Liverpool, Bristol, Manchester, Stoke-on-Trent, Blackpool na Belfast, huku mabomu ya machozi yakirushwa, maduka kuporwa na polisi kushambuliwa katika baadhi ya maeneo.Waziri Mkuu Sir Keir Starmer ameahidi kuvipa vikosi vya polisi “msaada kamili” wa serikali kuchukua hatua dhidi ya “wenye msimamo mkali” wanaojaribu “kupanda mbegu ya chuki”.Mvutano umekuwa mkubwa baada ya mauaji ya wasichana watatu wadogo kwenye tamasha ya densi yenye mada ya Taylor Swift huko Southport, Merseyside, Jumatatu.Mshirikishe mwenzako, Uingereza: Zaidi ya 90 wakamatwa kufuatia maandamano ya mrengo mkali wa kulia - Saa 3 zilizopitaNchi zawataka raia kuondoka Lebanon huku hofu ya vita kuzuka ikiongezeka Mashariki ya Kati
Chanzo cha picha,Getty ImagesMarekani imetoa wito kwa raia wake kuondoka nchini Lebanon kwa “ndege yoyote inayopatikana”, huku hofu ya vita kuenea katika eneo la Mashariki ya Kati ikiongezeka.Mataifa ya Uingereza, Uswidi, Ufaransa, Canada na Jordan zimetoa onyo sawa na hilo kwa raia wao.Iran imeapa kulipiza kisasi dhidi ya Israel, kwa madai ya mauaji ya mkuu wa Hamas Ismail Haniyeh huko Tehran siku ya Jumatano.Mauaji yake yalikuja saa chache baada ya Israel kumuua kamanda wa Hezbollah Fuad Shukr huko Beirut.Inahofiwa kuwa kundi la Hezbollah, linaloungwa mkono na Iran lenye makao yake nchini Lebanon, linaweza kuwa na jukumu kubwa katika mpango huo ambao huenda ukafanya hali ya usalama kuwa tete katika eneo hilo.Ubalozi wa Marekani hapo jana (Jumamosi) ulisema kwamba wale watakaoamua kusalia Lebanon wanapaswa “kuweka mipango ya dharura” na kuwa tayari “kujikinga kwa muda mrefu”.Ubalozi huo pia uliongeza kuwa mashirika kadhaa ya ndege yamesiitisha au kuahirisha safari, lakini “ndege za kibiashara kutoka Lebanon bado zinapatikana”.Hezbollah ilirusha makumi ya roketi katika mji wa Beit Hillel kaskazini mwa Israel usiku wa kuamkia Jumapili.Picha zilizosambazwa mitandaoni zilionyesha mfumo wa ulinzi wa anga wa Israel (Iron Dome) ukizuia roketi hizo.Jeshi la anga la Israel lilijibu mashambulizi hayo kwa kulenga shabaha kusini mwa Lebanon.Soma pia:Bomu lililotegwa Tehran miezi miwili iliyopita” lilimuua Haniyeh – New York TimesMauaji ya Haniyeh ni kikwazo kwa usitishaji mapiganoNini kimewapata viongozi mashuhuri wa Hamas?Mshirikishe mwenzako, Nchi zawataka raia kuondoka Lebanon huku hofu ya vita kuzuka ikiongezeka Mashariki ya Kati
All Rights Reserved © Cantona Group Ltd||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.