Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

TUME ya Maadili na Kupambana na Ufisadi imeandikia Karani wa Bunge ikielezea wasiwasi wake kuhusu uteuzi wa gavana wa zamani wa Kakamega Wycliffe Oparanya kuwa waziri, ikisema anakabiliwa na kesi ya ufisadi.
Katika barua iliyoandikwa kwa Samwel Njoroge na Afisa Mkuu Mtendaji Twalib Mbarak, EACC inasema kwamba Bw Oparanya amekuwa akichunguzwa kwa makosa ya kiuchumi ikimaanisha kwamba uteuzi wake kuwa Waziri wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo Ndogo utakuwa unakiuka Kifungu nambari sita cha Katiba kuhusu maadili.
Bw Oparanya ni miongoni mwa vigogo wanne wa ODM walioteuliwa na Rais William Ruto wiki jana kujiunga na serikali yake aliyoitaja kuwa ya ‘msingi mpana’ na inajiri baada ya maandamano makubwa ya vijana wa kizazi cha Gen Z yaliyomlazimu kuondoa Mswada wa Fedha 2024 pamoja na kuvunja baraza lake la mawaziri.

KAMATI ya pamoja ya Bunge la Kitaifa na Seneti kuhusu Afya, imempendekeza Dkt Patrick Amoth, kwa wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini.
“Baada kumhoji Alhamisi wiki jana kubaini ufaafu wake, tumeridhishwa na ufaafu wake kwa wadhifa huo. Tumeandaa ripoti ya pamoja inayopendekeza kwamba Bunge la Kitaifa na Seneti zimwidhinishe Dkt Patrick Amoth kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Afya,” Mbunge mmoja ambaye ni mwanachama wa Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Afya ameambia Taifa Leo Dijitali.
“Ripoti hiyo itajadiliwa katika Bunge la Kitaifa na Seneti wakati wowote kuanzia leo (Jumatano Julai 31, 2024) na ninaamini itapitishwa,” akaeleza Mbunge huyo ambaye aliomba tulibane jina lake kwa sababu kanuni za bunge hazimruhusu kuongea kwa niaba ya kamati hiyo.
Dkt Amoth amehudumu kama kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Afya nchini kwa zaidi ya miaka minne, tangu 2019, baada ya kumrithi Dkt John Masasabi.
Aliyekuwa Waziri wa Afya Susan Nakhumicha, alimpendekeza Dkt Amoth kwa wadhifa huo mnamo Juni 23, 2024.
Hii ni baada ya mtaalamu huyo kuibuka bora zaidi miongoni mwa watu waliotuma maombi kujaza nafasi hiyo.
Tume hiyo iliwahoji watu 11 kwa wadhifa huo akiwemo Dkt Amoth.
Mnamo Februari 20, 2024 Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) iliweka tangazo la kualika maombi kutoka kwa wanaohitimu kwa wadhifa huo.
“Niliwasilisha jina la Dkt Patrick Amoth bungeni baada ya kuibuka kuwa bora zaidi miongoni mwa waliohojiwa kwa wadhifa wa Mkurugenzi Mkuu wa Afya Nchini,” Bi Nakhumicha akasema kwenye taarifa Juni 23, 2024.
Kabla ya kuteuliwa kwake kuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa Afya, Dkt Amoth alihudumu kama mshauri wa kiufundi katika Wizara ya Afya.
Aliangaziwa zaidi katika vyombo vya habari katika mwaka wa 2020 baada ya mlipuko wa ugonjwa hatari wa Covid-19 akiandamana na aliyekuwa Waziri wa Afya Mutahi Kagwe kutoa habari muhimu kuhusu janga hilo.
Kulingana na Sheria ya Afya ya 2007, baada ya kuidhinishwa na mabunge yote mawili, Dkt Amoth atateuliwa rasmi na Waziri wa Afya.
Uteuzi huo utacheleweshwa hadi Waziri Mteule wa Afya Dkt Debra Mlongo Barasa, atakapopigwa msasa na bunge, kuidhinishwa na kuapishwa rasmi.

Habari za Kitaifa Zaidi
KIONGOZI wa kundi na wapiganaji la Hamas, Ismail Haniyeh, ameuawa nchini Iran, kundi hilo la wanamgambo wa Palestina lilisema Jumatano, Julai 31, 2024 na kutaja shambulio hilo kama “ongezeko kali la mapigano” ambalo halitaafikia malengo yake.
Kikosi cha Revolutionary Guards cha Iran kilithibitisha kifo cha Haniyeh, saa chache baada ya kuhudhuria hafla ya kuapishwa kwa rais mpya wa nchi hiyo, na kusema kuwa kinafanya uchunguzi.
Hakukuwa na maoni ya mara moja kutoka kwa mamlaka ya Israeli.
Ikulu ya White House, Amerika haikujibu mara moja ombi la kutoa maoni kuhusu kuuawa kwa Haniyeh.
Habari hizo, ambazo zilijiri chini ya saa 24 baada ya Israeli kudai kumuua kamanda wa Hezbollah ambaye ilisema ndiye aliyehusika na shambulio baya katika milima ya Golan inayokaliwa na Israeli, zinaonekana kurudisha nyuma uwezekano wa makubaliano yoyote ya kusitisha mapigano katika ukanda wa Gaza.
“Mauaji haya yaliyofanywa na Israel kwa ndugu Haniyeh, ni ongezeko kubwa la mapigano ambalo linalenga kuvunja moyo Hamas,” afisa mkuu wa Hamas Sami Abu Zuhri aliambia Reuters.
Alisema Hamas itaendelea na njia iliyokuwa ikifuata, na kuongeza: “Tuna uhakika tutaibuka na ushindi.”
Haniyeh, ambaye kwa kawaida anaishi Qatar, amekuwa akihusika na diplomasia kimataifa katika kundi hilo la Palestina huku vita vilivyoanzishwa na shambulio la Hamas dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7 vikipamba huko Gaza, ambapo wanawe watatu waliuawa katika shambulio la angani lililotekelezwa Israel.
Akishikilia wadhifa wa juu katika Hamas alioteuliwa mwaka 2017, Haniyeh amekuwa akihamia kati ya Uturuki na mji mkuu wa Qatar Doha, akikwepa njia za usafiri za Ukanda wa Gaza uliozingirwa na kumwezesha kuwa mpatanishi katika mazungumzo ya kusitisha mapigano au kuzungumza na mshirika wa Hamas, Iran.

MAAFISA wa serikali ya Tanzania wanazuilia ng’ombe 900 wa mfugaji Mkenya kutoka kijiji cha Rombo, Kaunti Ndogo ya Kajiado Kusini, Kaunti ya Kajiado kwa madai ya kupatikana katika taifa hilo jirani bila kibali.
Bw Saisa Lekimangusi, 47, alisema ng’ombe wake walikuwa wakisimamiwa na wachungaji walipokuwa wakipelekwa malishoni kutoka kaunti ya Kwale, Jumatatu, Julai 29, 2024.
Hapo ndipo maafisa wa Mbuga za Kitaifa Tanzania (Tanapa) waliwazuiliwa ng’ombe hao kuwa kuingia katika eneo linalosimamiwa na asasi hiyo, bila idhini.
“Maafisa hao walidai wachungaji hao walilisha mifugo hao ndani ya mbuga hiyo ingawa awali nilikuwa nimewaarifu kwamba nitawahamisha ng’ombe hao. Walikuwa mpakani sio ndani ya himaya ya Tanzania,” akasema Bw Lekimangusi.
Baba huyo wa watoto 11 aliambia Radio Fortune Africa kwamba maafisa wa Tanapa waliekeza ng’ombe wake hadi eneo la Seme nchini Tanzania ambako sasa wanazuiliwa.
Inaripotiwa kwa maafisa hao wanadai faini ya Tsh105,000 (Sh5,250) kwa kila ng’ombe.
Hii inamaanisha kuwa Bw Lekimangusi anahitaji kulipa Sh4.7 milioni, kwa usimamizi wa Tanapa, ili kukomboa mifugo wake.
“Hii ni faini ghali zaidi na siwezi kuimudu. Sasa nimeachwa bila mifugo wowote. Serikali yetu iingilie kati na ielewane na serikali ya Tanzania kabla wapige ng’ombe wangu mnada,” akaomba
Naibu Chifu wa Kata Ndogo ya Olelai Daniel Parasiato Jumanne jioni aliambia Taifa Leo kwamba kisa hicho kimeripotiwa katika afisi ya Kamishna wa Kaunti ili hatua zifaazo zichukuliwe.
“Suala hilo ni nyeti na huenda likahitaji maafisa wa ngazi za juu zaidi wa serikali kuingilia kati,” akasema Bw Parasiato.
Mbunge wa Kajiado Kusini Samuel Parashina naye alisema viongozi kadhaa wamelivalia njuga suala hili na kupasha habari asasi husika huku wakisaka maridhiano.
“Ni tukio la kusikitisha. Tunataraji kwamba maafisa wa Tanzania wataachilia mifugo hao bila masharti kwa moyo wa ujirani mwema,” Mbunge huyo akaeleza.
Kumekuwa na mizozo kadhaa kati ya maafisa wa serikali ya Tanzania na Wakenya wanaoishi katika eneo hilo la mpaka haswa kuhusiana na madai ya wafugaji kulisha mifugo wao ndani ya himaya ya Tanzania bila kibali.
Aidha, mnamo Mei mwaka huu maafisa watano wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kutoka kituo cha polisi cha Buruburu Kenya, walikamatwa nchini Tanzania kwa kuingia humo bila kibali walipokuwa wakiwafuata washukiwa wa wizi wa magari.
Baadaye waliachiliwa huru baada ya ujumbe wa maafisa wa usalama kutoka Kenya kuelewana na wenzao wa Tanzania.
Mnamo mwaka wa 2017, serikali ya Tanzania ilipiga mnada ng’ombe 1,300 mali ya wafugaji raia wa Kenya.
Wakati huo, aliyekuwa Rais wa Tanzania, John Magufuli, alidai maeneo ya mpaka wa nchi hiyo na Kenya yalikuwa yakiharibiwa na mifu.

KENYA imethibitisha kisa cha kwanza cha virusi vya homa ya tumbili inayofahamika kama Monkey Pox (Mpox) katika mpaka wa Taveta na Tanzania.Virusi hivyo viligunduliwa kwa mtu mmoja aliyekuwa akisafiri kutoka Uganda kwenda Rwanda kupitia Kenya.Maambukizi, ambayo husababishwa na virusi vya mpox, huenea watu wanapotangamana kwa karibu, na husababisha dalili za mafua na upele.Wizara ya Afya haikutoa habari zaidi kuhusu mtu huyo. Hata hivyo, iliwashauri Wakenya kuwa waangalifu na kunawa mikono mara kwa mara ili kupunguza hatari ya kuambukizwa.“Nawa mikono mara kwa mara kwa kutumia sabuni na maji. Ikiwa una dalili yoyote inayohusiana na virusi hivyo, pata ushauri kutoka kwa kituo cha afya kilicho karibu nawe na epuka kutangamana kwa karibu na watu wengine,” Wizara ilisema katika taarifa.“Maambukizi yanaweza kutokea iwapo umetangamana au kugusa mwili wa mtu aliye na virusi hivyo kama vile kupitia mdomoni au kwenye sehemu za siri. Ugonjwa huo pia unaweza kuambukizwa kupitia matone ya kupumua.”Virusi hivyo vimeenea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, pamoja na maeneo ya misitu katika Afrika Mashariki, Kati na Magharibi.Homa ya nyani KenyaTaita Taveta Tanzania virusi.
HABARI ZINAZOTOKEA

NI tukio la kihistoria Kenya baada ya bondi ya Sukuk kuingia katika soko la hisa Kenya kwa mara ya kwanza.
Sukuk ni bidhaa ya kifedha ya Kiislamu inayotolewa na serikali au mashirika kutafuta pesa kutoka kwa wawekezaji.
Hutolewa kwa muda ili kufadhili wawekezaji binafsi, biashara za mashirika au miradi ya serikali.
Mnamo Jumatano Julai 31, 2024, Rais William Ruto alizindua bondi ya kwanza inayofuata sheria za kiislamu.
Bondi hii almaarufu Linzi Sukuk, sasa imeorodheshwa katika Soko la Hisa la Nairobi (NSE).
Hii ni baada ya Shirika la Linzi Finsco Trust kutuma maombi kwa Mamlaka ya Masoko ya Mtaji nchini (CMA) mwaka wa 2023.
“Ni tukio la kihistoria kuorodhesha bidhaa ya kwanza inayofuata sheria ya Kiislamu katika soko la hisa,” akasema Rais alipozindua Linzi Sukuk.
Mwenyekiti wa NSE Kiprono Kittony akasema “Soko la Hisa la Kenya limepanua wigo wa jukwaa la uwekezaji kwa umma kupitia kuorodhesha bidhaa hii.”
Uwekezaji huo wa Kiislamu wenye thamani ya Sh3 bilioni unalenga kufadhili miradi ya maendeleo.
Uislamu na Riba
Sukuk hufuata kanuni za Kiislamu za fedha zinazoepuka riba badala yake kuwezesha uzalishaji wa pesa kutoka kwa pesa.
Wawekezaji hupata faida kutoka kwa ushirikishaji wa mali katika biashara mbalimbali.
Mwalimu wa dini ya Kiislamu Ustadh Feiswal Omar, amefurahishwa na hatua hii ya serikali inayoendana na matakwa ya dini.
“Mungu amekataza desturi ya kutoza riba na anayejihusisha nayo atakuwa ametangaza vita na Mungu. Mwenye kula riba atapata hasra na ataingia moto wa jahanamu,” akaeleza Bw Feiswal, Ustadh wa msikiti wa Masjid Mariam, Githurai kaunti ya Kiambu.
Akinukuu aya moja ya msahafu wa Quran, Bw Feiswal amesema mlaji wa riba hujiondolea baraka maishani mwake.

MAHAKAMA ya Rufaa imepiga msumari wa mwisho kwenye jeneza la Sheria ya Fedha 2023, kwa kukubaliana na uamuzi wa Mahakama Kuu uliotaja sheria hiyo kuwa kinyume na katiba.
Wakikatalia mbali sheria hiyo ambayo ilikuwa na aina mbali mbali za ushuru ikiwemo Ushuru wa Nyumba ambao ulizua vurumai kote nchini, majaji walisema mchakato wa kuunda sheria hiyo ulikuwa na dosari na kwamba ulikiuka Katiba.
“Kwa sababu hiyo, tunatangaza kwamba kutekelezwa kwa Sheria ya Fedha, 2023 kuwa kulikiuka vifungu 220 (1) (a) na 221 vya Katiba vikisomwa pamoja na Sehemu 37,39A na 40 vya PDMA ambavyo vinaeleza bayana hatua za kutengeneza bajeti, hivyo kufanya Sheria ya Fedha 2023 kuwa kinyume na sheria,”majaji Kathurima M’Inoti, Agnes Murgor na John Mativo wakasema Jumatano, Julai 31.
Habari zaidi ni kadiri tunavyozipokea…

RAIS William Ruto amesema ameridhishwa na shughuli za ukarabati zinazoendelea kwenye uwanja wa Talanta Sports City Complex, huku akitoa hakikisho kuwa uwanja huo utakamilika kabla ya mwaka ujao kumalizika ili kuandaa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON 2027).
Ruto alisema hayo Jumanne baada ya kutembelea uwanja huo unaopatikana kando ya Ngong Road, Nairobi kujionea ujenzi unaoendelea.
“Nimefika hapa leo kujionea ujenzi unaoendelea kwenye uwanja huu, na nimeridhika kuwa utamalizika wakati ufaao. Mradi huu utabainisha upya wasifu wetu kwenye kituo hiki kilichofanyiwa ukarabati wa hali ya juu kwa ajili ya kufaidi taifa nzima wa jumla,” Rais alieleza.

“Kenya inakusudia mpango mkubwa wa kuendeleza na kutekeleza michezo ya kila aina na sekta ya ubunifu,” alisema.
“Serikali inaimarisha viwanja vya umma kote nchini ili wachezaji wapate fursa ya kujiandalia kwenye mazingara mazuri,” aliongeza.
Awali, Rais Ruto alikuwa ametembelea shule ya walemavu ya Lenana School Primary, ambapo madarasa yanaendelea kujengwa ili kudhibiti idadi kubwa ya wanafunzi wanaojiunga na shule hiyo.
WIMBI LA SIASA MAREKANI
WASHINGTON, AMERIKA

UMAARUFU wa mgombeaji urais wa chama cha Democratic, Kamala Harris unaendelea kupanda huku kura za maoni zikionyesha kuwa anaongoza katika majimbo makubwa.
Harris yuko mbele ya Trump katika majimbo manne muhimu wakati rais huyo wa zamani akiwa mbele katika mawili, kulingana na kura ya maoni ya Bloomberg News/Morning Consult.
Harris anaongoza katika jimbo la Michigan kwa asilimia 11, pia anaongoza Arizona, Wisconsin na Nevada, kulingana na kura ya maoni.
Naye Trump ana umaarufu North Carolina.
Ikiwa uchaguzi ungefanyika leo, basi anayeongoza katika jimbo la Georgia angeshinda.
Katika kura ya maoni iliyoidhinishwa na Taasisi ya Maendeleo ya Kidemokrasia ( PAC), Harris anaongoza kwa asilimia kubwa katika jimbo la Georgia, huku Trump akiwa mbele kwa alama mbili majimboni Arizona na Pennsylvania.
Katika kura ya maoni iliyofanywa kote nchini na Reuters/Ipsos, Harris anaongoza kwa asilimia 43.
Harris, ambaye atatajwa rasmi kupeperusha bendera ya chama cha Democratic hapo Jumatatu, anatarajiwa kutangaza mgombea mwenza wake ndani ya siku chache kabla ya kuanza ziara ya majimbo ambayo yataamua uchaguzi wa Novemba 5.
Gavana wa Pennsylvania, Josh Shapiro, Seneta wa Arizona, Mark Kelly na Waziri wa Uchukuzi, Pete Buttigieg, miongoni mwa wengine, wametangaza azma ya kuwa mgombea-mwenza wa Harris.
Tangu Rais wa nchi hiyo, Joe Biden kujiondoa katika uchaguzi ujao wa Novemba 5, 2024 na kumpendekeza makamu wake kupeperusha bendera ya chama chao, Harris, amepata uungwaji mkono kutoka kwa viongozi mbalimbali.
Siku mbili zilizopita, Harris alikuwa amechangiwa Sh26 bilioni za kufanya kampeni. Isitoshe, zaidi ya wahisani 170,000 wamejitolea bila malipo kumsaidia Harris katika shughuli za kumpigia debe.
KIPENGA CHA MICHEZO

KLABU ya Chelsea imesajili kipa Filip Jorgensen kutoka klabu ya Villarreal kwa mkataba wa miaka saba ambao uligharimu Sh2.7 bilioni.
Raia huyo wa Denmark alivutia vigogo hao wa Ligi Kuu ya Uingereza baada ya kung’ara kama mlinda lango chaguo la kwanza wa klabu ya Villarreal msimu uliopita.
“Nimefurahia kujiunga na Chelsea, mojawapo wa klabu kubwa zaidi duniani. Ndoto yangu ya muda mrefu imetimika,” alisema mlinda lango huyo mwenye umria wa miaka 22.
Hata hivyo, kipa huyo atahitajika kupigania namba na Robert Sanchez aliyekuwa kipa chaguo la kwanza wa klabu hiyo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).
Kipa huyo aliyezaliwa Sweden aliwakilisha Denmark katika mashindano mbali mbali ya kimataifa ya umri tofauti hadi ya wachezaji wasiozidi umri wa miaka 21.
Alijiunga na Villarreal akiwa na umri wa miaka 25 na kupanda hadi alipopata nafasi ya kuchezea timu kuu ya taifa mnamo Januari 2023.
Tayari mlinda lango huyo ametua Califonia nchini Amerika kujiunga na wenzake katika kambi ya mazoezi kwa ajili ya msimu mpya wa 2024/2025.
Chelsea wamebakisha mechi tatu za maandalizi dhidi ya Club America, Manchester City, Real Madrid kabla ya kurejea London juma lijalo.
Mabingwa hao mara sita wa EPL mara sita (1955, 2005, 2006, 2010, 2015 na 2017) wamepangiwa kuanza msimu dhidi ya Manchester City mnamo Agosti 18, ugani Stamford Bridge.
Chelsea wanajadili mpango wa mshambuliaji wa Ubelgiji Romelu Lukaku, 31, kujiunga na Napoli, huku mshambuliaji wa Nigeria Victor Osimhen, 25, akitarajiwa kuhamia klabu hiyo kwa mkopo. (Athletic – usajili unahitajika)
Lukaku tayari amekubali kukatwa mshahara na kusaini mkataba wa miaka mitatu na klabu hiyo ya Serie A. (Ben Jacobs)
Brighton wamekubali mkataba wa pauni milioni 5.9 kumruhusu kiungo wa kati wa Ujerumani Pascal Gross, 33, kujiunga na Borussia Dortmund. (Guardian)

Chelsea na Aston Villa wamewasilisha ombi la kumnunua mshambuliaji wa Bayer Leverkusen na Ujerumani Maximilian Beier, 21. (Sky Germany)
Uhamisho wa Monza kwa mlinda lango wa Nottingham Forest na Costa Rica Keylor Navas, 37, unaweza kutibuka kutokana na tofauti kati ya pande hizo mbili wakati wa mazungumzo. (Fabrizio Romano)
Chelsea pia wamefikia mkataba wa pauni milioni 16.7 na Genk kwa ajili ya mlinda lango wa Ubelgiji Mike Penders, 18. (HLN – kwa Kiholanzi)
West Ham wanataka kujiondoa katika kinyang’anyiro cha kumnunua winga wa Leeds ya Uholanzi Crysencio Summerville, 22. (Talksport)
Aston Villa wanavutiwa na mshambuliaji wa Crystal Palace na Ufaransa Jean-Philippe Mateta, 27. (Express)
Everton wanafikiria kuwasilisha ombi la kumnunua mshambuliaji wa klabu ya Roma Muingereza Tammy Abraham, 26. (Sportitalia)
Manchester United wanajitahidi kufikia makubaliano na kiungo wa kati wa Ufaransa Adrien Rabiot, 29, ambaye aliondoka Juventus msimu huu wa joto. (Caughtoffside)
Beki wa England chini ya miaka 21 Rhys Williams, 23, na mlinzi wa Ufaransa Billy Koumetio, 21, wanatarajiwa kuondoka Liverpool. ((Athletic)

Liverpool wanapanga kumsajili kiungo mkabaji kabla ya dirisha la usajili kufungwa mwishoni mwa Agosti. (Football Insider)
Manchester United wanatarajiwa kusajili mchezaji wa kuchukua nafasi ya Scott McTominay , 27, iwapo watakamilisha mauzo ya kiungo huyo wa kati wa Scotland huku Fulham wakipanga kuwasilisha ofa mpya.
Mossad: Mbinu,mikakati na kuwatumia wanawake katika shirika la ujasusi la Israel walipa ufanisi katika operesheni zake

Maelezo kuhusu taarifa
- Author,Yusuf Jumah
- Nafasi,BBC Swahili
- 31 Julai 2024, 10:20 EAT
Je ni vipi taifa la Israel linavyomudu kusalia salama na kujilinda dhidi vitisho kutoka kwa nchi mbali mbali zinazopakana nayo?
Ni kweli kwamba shirika la ujasusi la Mossad linatumia mbinu zisizo za kawaida kuwaangamiza maadui wa Israel?
Kwanini kuna idadi kubwa ya wanawake wanaolifanyia kazi shirika la Mossad?
Hayo ni baadhi ya maswali ambayo watu wengi huuliza lakini hawapati majibu .
Hata hivyo tathmini ya karibu kuhusu vitendo na matamshi ya waliowahi kulifanyia kazi shirika hilo itakupa taswira ya jinsi Mossad inavyofanya kazi .
Kwanza Mossad inatumia maajenti wa kipekee na waliopewa mafunzo kuweza kutimiza malengo yake katika operesheni zake kote duniani .Hizi hapa baadhi ya sababu zinazoifanya Mossad kuwa shirika la kipekee la ujasusi kwa Israel
Wanawake wana uwezo wa kipekee
Mnamo mwaka wa 2017 shirika la Mossad lilitoa tangazo kuwatafuta maajenti wa kike .
Tayari shirika hilo lina asilimia 40 ya wanawake wanaolifanyia kazi huku asilimia 24 wakishikilia nafasi za juu za uongozi ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinaeleza .
Wanawake wamesifiwa kama maajenti bora wa siri na mkuu wa zamani wa Mossad.Soma pia:
- Ana Montes: Jinsi jasusi wa Cuba alivyoisaliti Marekani11 Januari 2023
- Mfahamu mwanamke Mmisri aliyekuwa jasusi Israeli27 Novemba 2021

Tamir Pardo alisema mnamo 2012 kwamba maajenti wa kike “wana faida tofauti katika vita vya siri kwa sababu ya uwezo wao wa kufanya kazi nyingi” na “wanaficha tabia yao ili kufikia malengo,” kulingana na The Jerusalem Post.
“Kinyume na maoni potofu, unaona kuwa uwezo wa wanawake ni bora kuliko wanaume kwa kuelewa eneo, hali za kusoma, ufahamu wa mazingira. Wakati unapopata walio bora , ni wazuri sana,” mkuu wa shirika hilo wakati huo alisema.
Wakati wa tangazo hilo miaka mitatu iliyopita Tovuti ya Mossad iliwaambia wanaotaka kujiunga na shirika hilo kwamba “Sio kile ulichokifanya bali ni kuhusu ni wewe ni nani.”
Mossad ilianzishwa lini?
- Kikosi cha kimataifa cha huduma ya ujasusi cha Israeli kilianzishwa mnamo 1949
- Ni moja wapo ya huduma za ujasusi za siri zinazoogopwa sana na za visa vingi ulimwenguni. Maafisa wake wote wamepongezwa kwa operesheni za kipekee na hata wanatuhumiwa kwa mauaji ya kinyama
- Kwanza ilithibitisha azma yake ya kufikia ulimwengu kwa kumkamata mtuhumiwa wa uhalifu wa kivita wa Nazi Adolf Eichmann mnamo 1960 huko Argentina
Iran yalalama
Iwapo kuna nchi ambayo inailaumu Mossad kwa kila mkosi unaoikumba ,basi Iran ni ya kwanza katika orodha hiyo . Imeilaumu Mossad kwa kuhusika na mauaji ya wanasayansi wake wanaoendesha mpango wake wa kuwa na silaha ya nyuklia .
Mnamo Januari 10 mwaka wa 2011 Iran ilitangaza kwamba imewakamata raia wake 10 kwa mauaji ya Profesa Massoud Ali Mohammadi.
Wizara ya Ujasusi ya Iran ilisema kuwa washukiwa 10 walifanya kazi kwa ushirikiano na Mossad.
Vituo vya runinga vya serikali vya Iran vilitangaza madai ya kukiri kwa mmoja wa wanaume waliokamatwa, aliyeitwa Majid Jamali Fashi.
Ajenti anayeshukiwa alionyeshwa akiongea kwenye chumba chenye kilichokuwa na giza.
Bwana Jamali Fashi alielezea kuwa, karibu miaka mitatu iliyopita, alitakiwa kwenda katika Ubalozi Mdogo wa Israeli huko Istanbul.
Sababu ya ziara hiyo haijulikani. Lakini alifanya hivyo, na akasema kwamba alihojiwa na maajenti wa Israeli.
“Waliuliza maelezo yote ya maisha yangu haswa. Na pia, walinipa hakikisho ili nishirikiane nao kwenye mipango yao na wakaniuliza nikusanye habari kutoka ndani ya Iran.”
Huo tu ni mfano mmoja wa jinsi Mossad ilivyofaulu kuwafanya raia wengi wa Iran kuwa maajenti wake na kuanza kukusanya habari za kijasusi kwa niaba ya Israel .
Baada ya mafunzo ya miezi kadhaa, waliokuwa wakizugumza naye walimwambia kwamba alikuwa na kazi ya kufanya na kumuambia kwamba alifaa kumlenga – Massoud Ali Mohammadi, profesa katika Idara ya Fizikia katika Chuo Kikuu cha Tehran.
Alielezea kwamba walitaka yeye atege bomu la pikipiki nje ya nyumba ya profesa huyo,na hivyo ndivyo alivyouawa mwanasayansi huyo wa Iran .

Tangia tukio hilo kumekuwa na visa vingi vya Wanasayansi wa Iran kuuawa katika hali za kutatanisha na kila mara Iran imekuwa ikiilaumu Israel kwa kuhusika na mauaji yao.
Jambo jingine ambalo limefanikisha ufanisi wa shirika la Mossad ni jinsi taifa la Israel linavyotetewa na Marekani .
Serikali ya Israel inafahamu jinsi inavyolindwa na Marekani kidiplomasia na hivyo basi imejipatia ukakamvu wa kuweza kufanya lolote bila kuogopa athari za kuidhuru.
Panapotokea lalama za nchi nyingine kuhusu operesheni za Mossad ama madai ya mauaji ,vikwazo vya kimataifa au hata kutoka kwa umoja wa Mataifa haviwezi kuelekezewa Israel kwasababu ya Marekani kuingilia kati na kuipa kinga .
Pia haisaidii kwamba Iran ambayo ina uhasama na Marekani imekuwa ikiilenga Israel kupitia makundi ya wapiganaji kama vile Hamas na Hezbollah .
Hilo linaifanya Marekani kuiona Israel na shirika lake la Mossad kuonekana kama chaguo bora la kutumiwa kukabiliana na vitisho vinavyotolewa na Iran kwa maslahi ya Marekani na nchi nyingine za magharibi.














All Rights Reserved © Cantona Group Ltd||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.