Radio Fortune Africa
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Habari Zinapojiri -Ukweli Na Burudani
Afrika Leo Alfajiri
Afrika Leo Mchana
Afrika Leo Jioni
Afrika Mwisho Juma
Kipenga Cha Michezo
Kipenga Cha Afrika
Makala Maalum
Afya Na Jamii
Ukweli Na Burudani
Kipindi Cha Matumaini
Bao La Asubui
Good Evening Africa
Wimbi la Siasa
Vipindi vya Radio
CantonaCast Television
Fortune Television Network

Natumai U Buheri wa Afya hujambo na karibu popote ulipo duniani naitwa Cantona Joseph
POLISI wa Kenya ambao wapo nchini Haiti kupiga jeki juhudi za kuleta udhabiti Jumamosi walikabiliana na magenge katika kisa kilichogubikwa na ufyatulianaji mkali wa risasi mjini Gauthier.
Kamanda wa kikosi cha Kenya Godfrey Otunge alisema polisi walikabiliana na magenge hayo kwa saa kadhaa na kutwaa mji huo ambao umekuwa himaya ya magenge hatari kwa serikali.
“Halikuwa jambo rahisi kwa sababu polisi walikabiliana sana na magenge hayo na kuchukua usimamizi wa mji huo. Hata sasa wanasimamia kituo cha polisi cha Gatheri,” akasema Bw Otunge.
Picha iliziona ilionyesha jinsi ukuta wa kituo hicho cha polisi uliangushwa na sehemu yake kuchomwa. Mji wa Gatheri umekuwa chini ya usimamizi wa genge la wanachama zaidi ya 400 ambalo linafahamika kama Mawazo.
Wanachama wa genge hilo waliwatupia polisi kutoka Kenya mabomu ya petroli kwa lengo la kuwatia hofu. Gari ambalo polisi walikuwa wakitumia wakati wa shambulio hilo lilipasuliwa dirishani.
Hii ilikuwa mara ya pili ambapo polisi Wakenya walilazimika kutumia risasi dhidi ya magenge. Mara ya kwanza ilikuwa mnamo Julai 17, 2024 wakati ambapo walitwa bandari ya Autorite Portuaire Nationale (APN).
Mnamo Jumamosi wikendi iliyopita, Balozi wa Canada kule Haiti Andre Francois Giroux alikutana na Bw Otunge na kuzungumzia operesheni hiyo.
Bw Giroux aliteuliwa mnamo Novemba 2023 na alisema kuwa Canada inapanga kuwatuma maafisa wake wa usalama kusaidia kurejesha udhabiti Haiti.

WAKAZI wa mji wa Mpeketoni, Kaunti ya Lamu wameishinikiza serikali ya kaunti na ile ya kitaifa kuweka kamera za CCTV kwenye mitaa na vichochoro vya mji huo kusaidia kukabiliana na wizi na uhalifu mwingine.
Mpeketoni ni mji unaotambulika kuwa wa kibiashara na ukulima kote Lamu.
Siku za hivi karibuni, kumeshuhudiwa visa vya wizi hasa kuvunjwa kiholela kwa maduka ya kielektroniki na vyombo kuibwa.
Katika mahojiano na Radio Fortune Afrika, wakazi, wengi wao wakiwa ni wanabiashara walisema kuwekwa kwa CCTV mjini humo kutasaidia pakubwa kukabiliana na wezi na hata kuwatambua.
Bw John Musyoka alisema hairidhishi kuona wezi wakitekeleza maovu yao na kutoweka bila kutambuliwa na kuchukuliwa hatua.
“Mbali na kuimarisha usalama, tunaamini kamera za CCTV zitasaidia kuwatambua wakora hao, wakamatwe na wachukuliwe hatua kali za kisheria. Kaunti, serikali kuu na wahisani wajikaze kutuwekea hizo CCTV hapa. Tumechoka kuvunjiwa maduka na vifaa kuibwa,” akasema Bw Musyoka.
Lucy Ng’ang’a, mwanabiashara mjini Mpeketoni, alipendekeza endapo kamera hizo zitawekwa basi zihudumu kwa masaa yote.
Alisema kuwepo kwa CCTV kutasaidia kuwafurusha wakora mjini wakifahamu fika kuwa huenda wakajipata sura zao zikinaswa, hivyo kutambulika.
“Kamera ziwekwe. Kwa sasa wanavunja na kuiba madukani wakiwa na ujasiri wote wakijua fika kuwa hakuna anayewamulika,” akasema Bi Ng’ang’a.
Wakazi hata hivyo waliomba idara ya usalama pia kuongeza doria usiku na mchana mjini Mpeketoni na viunga vyake ili kukabiliana na uhalifu wa aina yoyote ile.
“Kukiwa na doria za kila mara, iwe ni za polisi au jeshi, wakora wanaoendeleza maovu yao wataogopa na kuhama huu mji wetu,” akasema Bw Simon Mbuthia.
Mwezi uliopita, washukiwa wanne wa wizi na ufunguaji wa simu za M-Kopa walinaswa kwenye msako mkali uliotekelezwa ghafla na polisi mjini Mpeketoni.
Wanne hao, ikiwemo wanaume watatu na mwanamke mmoja, walinyakwa kwenye maduka tofauti tofauti mjini humo, ambapo jumla ya simu 76, ikiwemo za kawaida na zile za M-Kopa, vipakatalishi na vifaa vingine vinavyowasaidia kutekelezea ujanja na wizi huo vikinaswa.

RAIS William Ruto ameahidi kuwa atawasaidia Wakenya wasiokuwa na kazi kupata ajira ughaibuni huku akilenga kuwatuliza vijana ambao wamekuwa wakimshinikiza ajiuzulu kwa kutotimiza ahadi alizotoa kabla ya kuchaguliwa 2022.
Akizungumza Kaunti ya Taita Taveta, Jumapili, Rais alitangaza kuwa ana mpango wa kuharakisha kutolewa kwa pasipoti kwa wale ambao wanataka kufanya kazi nje ya nchi.
“Nimefanya kazi yangu, nimetafuta kazi mataifa ya nje. Nimepanga kuwa wale ambao wanaenda kufanya kazi hizo ng’ambo wapate pasipoti zao ndani ya wiki moja,” akasema.
“Hata hawatahitaji pesa za kununua tikiti za ndege, tugharimia safari hizo,” akaongeza.
Ahadi yake ilikuja huku Idara ya Uhamiaji ikipambana kuandaa na kuwapa Wakenya pasipoti zao baadhi wakiwa wamesuburi kwa zaidi ya miezi 12.
Kumekuwa na uhaba wa karatasi na mashine za kuchapisha na kuandaa pasipoti hizo. Ufisadi na kiburi kwa wanaofanya kazi kwenye idara hiyo ni kati ya sababu nyingine ambazo zimefanya Wakenya wasipate pasipoti zao kwa wakati.
Mnamo Novemba 2023, Dkt Ruto alisema angetia saini mkataba na serikali za Ujerumani, Ufaransa, Saudi Arabia na mataifa ya Uarabuni ili Wakenya wasiokuwa na ajira wafanye kazi huko.
Hata hivyo, haikubainika ni nafasi ngapi za ajira ambazo zingetokea kutokana na maelewano hayo.
Mnamo Jumapili, Rais alisema serikali imewasaidia zaidi ya vijana 400,000 kupata kazi ng’ambo. Aliwataka wabunge waandae vijana kwenye maeneo yao kujihusisha na mpango wa ajira nje ya nchi.
“Kila wiki vijana 1,000 huhamia nchi za nje. Taita Taveta sasa wanafaa wajiandae kwa zamu yao.
“Kwa wabunge, nimefanya kazi yangu ya kusaka kazi ng’ambo. Nimepanga kuwa kila mtu ambaye angependa kufanya kazi ughaibuni, anapewa pasipoti na stakabadhi nyingine ndani ya wiki moja,” akasema Rais.
Kando na ajira za nje za nchi, Rais alisema kuwa anamakinikia kuanzisha ajira mitandaoni ambapo vijana watafanyia kazi kampuni za mataifa ya nje wakiwa nchini.
“Kwenye mpango wangu nataka vijana wawe na ajira ya maana. Hii ndiyo maana nimeanzisha mipango kama ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, ajira mitandaoni, Wakenya kufanya kazi nje ya nchi, viwanda ili kuwapa vijana wetu ajira ndipo tujenge taifa,” akasema.
Kiongozi wa nchi alifichua kuwa alikuwa amekubaliana na wabunge kujenga vituo vya teknolojia kwa kutumia Hazina ya Fedha ya Kustawisha Maeneobunge Nchini (CDF).
Serikali nayo itanunua kompyuta, kulipia intaneti na kuwalipa wakufunzi kwa vijana ambao watakuwa wakifanya kazi kwa kampuni za ng’ambo na kulipwa dola za Marekani.

Msanii Mali safi Chito ajiuliza maswali mengi.

KUNA nyakati anajiuliza maswali mengi bila majibu kwa nini alipinga ushauri wa baba yake.
Baba yake hakutaka ajishughulishe na usanii wa muziki kama njia ya kutega uchumi.
Tangu awe mwimbaji maarufu nchini mnamo Novemba 2023, Bi Millicent Jerotich, 36, maarufu kwa jina Marakwet Daughter, amesumbuka sana.
Akifichua kuwa alifurahia umaarufu kutoka kwa wimbo ‘Mali Safi Chito’ uliomfanya kutambulika, furaha yake ya ghafla ilidumu kwa wiki mbili tu.
Tangu wakati huo, Marakwet Daughter huangalia nyuma kila wakati kwa hofu ya kushambuliwa.
“Siku hizi ni adimu sana nitoke nyumbani na aghalabu siwaambii mashabiki wangu kuhusu shughuli zangu za burudani nikiogopa mahasimu,” anafichua. “Nimetukanwa tangu Novemba mwaka jana: simu yangu ina jumbe nyingi za vitisho.”
Akizungumza na Radio Fortune Africa kupitia njia ya simu, Bi Jerotich alisinasina akisikitikia maisha yake.
Kulingana naye, mara nyingi, amelazimika kuripoti katika vituo vya polisi ila hajasaidiwa.
“Imebidi nikabiliane na mahasimu hawa bila kuogopa baada ya polisi kunipuuza,” msanii huyu alilalama. “Baba yangu hunipigia simu kila siku kujua kama niko salama.”
Alitutumia moja ya jumbe zilizotishia maisha yake: Futa video mara moja la sivyo uchukuliwe hatua kali.”
Mtumiaji huyu wa mitandao ya kijamii alikuwa anatuma ujumbe kwa Bi Jerotich akimwelekeza kuondoa wimbo Konech Kalya (Kikwangwanga) kutoka kwenye mtandao wa YouTube.
Katika wimbo huu, inafahamika kuwa Marakwet Daughter haombi tu kwa ajili ya amani kati ya jamii zinazozozana za wafugaji kutoka jamii ndogo tofauti za Kalenjin, bali pia kwa nchi nzima.
Lakini wimbo huu ni chanzo cha uhasama kati yake na ‘mashabiki’ wake.
Jumbe za “Lala mahali pema peponi” ni miongoni mwa jumbe za vitisho ambazo amepokea kwa miezi kadhaa.
Aliripoti vitisho hivi katika kituo cha polisi cha Iten na ikanakiliwa katika kitabu cha matukio kwa nambari 20/12/04/23.
“Baadhi ya watu wanaonishambulia wanadai kuwa jamii yetu iliua watu wao wakati wa visa vya wizi wa mifugo,” anafichua.
Alivuma baada ya miaka 15 ya usanii
Ilichukua miaka 15 kwa juhudi za Marakwet Daughter kutamba kimuziki kuzaa matunda.
Aliimba zaidi ya nyimbo 500 lakini alijulikana tu nyumbani na mashabiki wachache.
Mara tu alipozindua wimbo wa ‘Mali Safi Chito’, mwanamuziki huyu alivuma nchini na ughaibuni.
Kibao hiki sasa kimetazamwa mara milioni 12 katika mtandao wa YouTube.
Kimeibuka kuwa nyimbo pendwa na Wakenya wengi kwa sababu ya umuhimu wake wa kiutamaduni pamoja na mvuto.
Alitamani sana kuvuma katika tasnia ya sanaa, ila hakuwa tayari kwa kilimchomkuta.
Mapato ya muziki
Mwimbaji huyu alikuwa miongoni mwa waliopata pesa nyingi, akitia mkobani angalau Sh100,000 kutokana na malipo ya hivi majuzi ya mirahaba iliyotolewa na Chama cha Hakimiliki ya Muziki Kenya (MCSK).
Tangu wakati huo, amezindua nyimbo nyingi zinazofanya vizuri zaidi kuliko zile zilizotolewa kabla ya umaarufu wake.
Ni pamoja na: ‘No giving up’, ‘Hapana taka’, ‘Promise keeper’, ‘Run your race’ na ‘Sonko teta’.
“Umaarufu huu umeleta taabu nyingi maishani mwangu – sina uhakika wa usalama wangu,” anasema. “Ninatishwa karibu kila wiki. Mmoja wa walionitisha alisema, ‘Nimelipwa ili kukumaliza, lakini ikiwa hutanipa kitu, nitachukua hatua.’”
“Siku hizi, sitembei sana na nimekatisha uhusiano na marafiki wengine… Sikuwahi hata kufikiria kwamba watu hawatakuwa na furaha nikifanikiwa,” Bi Jerotich anaongeza.

FAMILIA moja katika Kaunti ya Kirinyaga inalilia haki baada ya mwili wa mwanao ambaye alifuzu juzi kutoka kwa Idara ya Huduma ya Vijana kwa Taifa (NYS) kupatikana kwenye mochari.
Mwili wa marehemu James Macharia, 26, ambaye alitoweka Jumamosi ya Julai 21 ulikuwa na majeraha sehemu mbalimbali. Pikipiki ambayo alikuwa akitumia kabla ya mauti yake na ilikuwa ya jirani yake, bado haijapatikana.
Baada ya kumtafuta kwa zaidi ya wiki moja, familia hiyo ilipata mwili wake kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Kerugoya.
“Tulimsaka mwana wetu katika maeneo mbalimbali baada ya kukosa kuja nyumbani kijijini kwetu Karira lakini tukaishia kupata mwili wake katika chumba cha kuhifadhia maiti,” akasema Simon Wanjohi, mjomba wa marehemu.
Kwa mujibu wa mamake Rose Waitherera, mwanawe alitoka nyumbani kwao mji wa Ngurubani siku hiyo asubuhi na akaingiwa na wasiwasi aliposhindwa kurudi nyumbani.
“Nilipouliza, niliambiwa mwanangu alikuwa kwenye baa alipopokea simu kutoka kwa watu wasiojulikana na akaenda kukutana nao. Baadaye tulipata mwili wake kwenye mochari,” akasema Bi Waitherera.
Familia hiyo sasa inadai mwanao aliuawa na kuibiwa pikipiki na sasa wanataka haki itendeke.
“Tunataka wale ambao walimuua mwanangu wakamatwe na wachukuliwe hatua za kisheria,” akasema Teresa Wanjiru ambaye ni shangaziye marehemu.
Aidha familia hiyo ilifichua kuwa waligundua mwanao alipigwa na kuachwa akiwa mahututi na ni wasamaria wema ndio walimpeleka katika Hospitali ya Kaunti Ndogo ya Kimbimbi kwa matibabu.
Hali yake ilibadilika na kuwa mbaya hadi akahamishwa katika hospitali ya rufaa ya Kerugoya ambapo aliaga punde tu baada ya kufikishwa na mwili wake ukapelekwa mochari.

JARIBIO la watu fulani kusajili vyama vya kisiasa vyenye jina, Gen Z ili kuvuna kisiasa kutokana kampeni zilizoanzishwa na vijana kupigania uongozi bora nchini zimezimwa na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa Nchini.
Msajili huyo, Anne Nderitu, wiki jana alifichua kwamba tangu msururu wa maandamano ya vijana hao wa kizazi cha sasa kuanza kwa kupinga Mswada wa Fedha wa 2024, afisi yake imepokea angalau maombi 20 kutoka kwa watu wanaotaka kuhifadhi majina ya vyama vya kisiasa.
Hata hivyo, alisema maombi hayo yote, yanayoanza na maneno Gen Z, yamekataliwa kwani yanakiuka sheria, haswa kipengele 91 (1) (a) (e ) cha Katiba kinachohusu masharti yanapasa kuzingatiwa kuunda vyama vya kisiasa.
“Hitaji la sheria ni kwamba kila chama cha kisiasa sharti kiwe na sura ya kitaifa na kiheshimu haki za watu kushiriki katika michakato ya kisiasa, yakiwemo makundi ya walio wachache na waliotengwa,” Bi Nderitu akasema.
“Kwa hivyo, licha ya kupokea zaidi ya maombi 20 kutoka kwa watu mbalimbali wakitaka tuhifadhi majina ya vyama vya kisiasa vinavyoanza na Gen Z, tumekataa maombi hayo kwa sababu yanakiuka Katiba,” akaongeza.
Bi Nderitu alisema afisi yake ilianza kupokea maombi hayo baada ya siku ya kwanza ya maandamano hayo, Juni 18, 2024 kutoka kwa watu waliotaka kutumia umaarufu wa wimbi hilo la maasi ya vijana kuvuna kisiasa kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2027.
Watu hao walivutiwa na wimbi la vijana hao na hali kwamba hawakujinasibisha na kabila, kiongozi yeyote au chama chochote cha kisiasa.
“Chama cha kisiasa sharti kiwe na sura ya kitaifa na kijumuishe watu wa umri na matabaka yote. Sharti tuone watu wa umri wote katika chama cha kisiasa. Ukisema chama cha Gen Z, unaonekana kuwatenga watu wengine,” Bi Nderitu akaeleza.
Chama kinachoonekana kuwatenga watu wa umri fulani, msajili huyo anasema, basi chama hicho kinakosa sura ya kitaifa.
“Namna ambavyo, vijana hawataki kuachwa nje katika shughuli za vyama vilivyoko sasa au masuala ya uongozi, wao pia hawapaswi kuwaacha nje watu wengine. Kila mtu anafaa kushirikishwa, tangu hatua za kwanza kwa kubuni kwa chama chochote cha kisiasa,” Bi Nderitu akafafanua.
Kwa mfano ombi kutoka kwa Simon Maina Mwangi lilikataliwa na msajili wa vyama vya kisiasa kwa misingi hiyo hiyo ya kukiuka hitaji la kipengele cha 91 cha Katiba.
Bw Mwangi alitaka afisi ya Bi Nderitu kuhifadhi majina 10 ya vyama vya kisiasa ikiwa ni pamoja na; Gen-Z Movement, Gen Z National Movement, Gen Z People’s Alliance, Gen Z Peoples Movement, Gen Democratic Party, Gen Z Alliance Movement, Gen Z Democratic Movement, Gen Z United Movement, Gen Z Political Party na Gen Z Alliance Party.
Hata hivyo, Afisa huyo alikataa ombi hilo kupitia barua aliyomwandikia Bw Mwangi mnamo Julai 11, 2024.
Ombi jingine lililowasilishwa na John Onyango Ogenga, mnamo Juni 24 akitaka jina Gen Z lihifadhiwe pia lilikataliwa na Bi Nderitu kwa msingi huo huo.
Bw Ogenga sasa amewasilisha rufaa dhidi ya uamuzi huo katika Jopo la Kutatua Mizozo ya Vyama vya Kisiasa.
Anadai kuwa kukataliwa kwa ombi lake kunaenda kinyume na Katiba, kunaendeleza ubaguzi na kuhujumu haki zake za kisiasa.
Bw Mwangi pia ameapa kupinga uamuzi wa kukataliwa kwa ombi lake akidai sababu zilizotolewa na Nderitu hazina mashiko huku akitoa mfano wa chama cha Farmers Party kilichosajiliwa ilhali sio kila Mkenya ni mkulima.
“Kile nilitaka ni vijana wa Gen Z wawe na jukwaa ambako tunaweza kuangazia masuala yetu na kujitambulisha nayo. Watu wamekuwa wakituita magaidi au watu wasio na mwelekeo wala uongozi. Kwa hivyo, tunahitaji asasi ambayo imesajiliwa rasmi ili wenzetu waweze kujitambulisha nayo,” akasema Bw Mwangi, 32, mhitimu wa Chuo Kikuu cha Kiufundi Kenya (TUK).
Kenya Kwanza
Maandamano ya Gen Z
msajili wa vyama
Mswada wa Fedha 2024

RAIS William Ruto Jumapili aliendelea kutoa ahadi chungu nzima kwa Wakenya huku akisema utawala wake utapunguza utekelezaji wa miradi kutokana na hatua aliyochukua ya kuondoa Mswada wa Fedha 2024/25.
Rais Ruto alisema alilenga kupata pesa zaidi kupitia ushuru ambao ulikuwa umependekezwa kwenye mswada huo uliopingwa vikali na Wakenya na kuchangia maandamano nchini.
“Kwenye bajeti ya mwaka huu wa kifedha nilikuwa nimepanga kutekeleza mengi lakini kulikuwa pia na propaganda nyingi. Sasa lazima nitafute njia nyingine lakini ni vyema kutotilia manani propaganda na habari feki,” akasema Rais Ruto.
Alikuwa akiongea katika Kaunti ya Taita Taveta wakati wa ibada kwenye Kanisa la Kianglikana ya St Peters Bura, Kaunti ndogo ya Mwatate.
Aliwataka Wakenya wavumilie serikali yake kwa sababu sasa hawawezi kuzindua miradi mipya kutokana na upungufu wa fedha uliopo kwenye bajeti.
Hata hivyo, muda mfupi baada ya kusema hayo, Rais aliendelea kutoa ahadi tele kwa wakazi wa kaunti hiyo akisema atazuru eneo hilo kuzindua miradi mipya kaunti ndogo za Mwatate, Taveta na Voi.
Japo wakazi walikuwa wakisubiri kufahamu hatua zilizopigwa katika kutekeleza miradi iliyozinduliwa hapo awali, Rais alikwepa suala hilo kabisa.
Baadhi ya miradi aliyozindua na haijaanza ni mradi wa mabomba ya maji wa Mzima Two, Barabara ya Taveta-Illasit na ile ya Bura-Mgange-Mbale –Mtomwagodi.
“Nilikuwa nimetenga pesa kwa barabara ya Bura-Mghange-Mbale-Mtomwagodi lakini mnajua kile kilichotokea,” akasema kabla kuzungumzia masuala mengine.
Mradi wa ujenzi wa makazi ya gharama nafuu ndio unatarajiwa utazinduliwa na Rais Mwatate, Taveta na Voi akizuru tena kaunti hiyo jinsi alivyoahidi.
Alisema nyumba 800 zitajengwa Mwatate na nyingine 1,000 Voi na Taveta.
Rais alisema serikali itashirikiana na mwekezaji ambaye amekubali kuanzisha kiwanda cha chuma kwa kima cha Sh10 bilioni Voi. Kulingana naye, kiwanda hicho kitawapa zaidi ya vijana 2,000 ajira.
Aliongeza kuwa serikali imetenga Sh500 milioni kuunganisha umeme kwenye nyumba 10,000 katika kaunti hiyo na pia itawajengea nyumba za wanafunzi katika Chuo Kikuu cha Taita Taveta na kile cha kiufundi cha Taita Taveta.
Aliendelea kuahidi akisema ataketi chini na uongozi wa kaunti hiyo kuweka mipango jinsi ambavyo miradi ya maendeleo itaendelea kutekelezwa katika kaunti hiyo.
Wakati wa hafla hiyo, kiongozi wa nchi alitetea uamuzi wake wa kuwaingiza viongozi wa upinzani serikalini, akisema hilo litasaidia kuhakikisha kuna umoja na taifa linasonga mbele hasa baada ya maandamano ya Gen Z.
“Kile kilichofanyika kimetuwezesha kuanzisha mwelekeo mpya nchini. Baraza jipya la mawaziri litatuunganisha na sasa tumeweka siasa za vyama kando na kuipa umoja wa nchi mstari wa mbele,” akasema.
Gavana Andrew Mwadime, wabunge John Bwire (Taveta), Peter Shake (Mwatate) na Mbunge Mwakilishi wa Kike wa kaunti hiyo Lydia Haika waliahidi kushirikiana na serikali kuhakikisha miradi iliyokwama inakamilika na mingine mipya inaanzishwa.
“Tumekuwa kwenye kijibaridi kwa miaka mingi na sasa tuna matumaini kuwa miradi mingi itatekelezwa na watu wetu wanufaike,” akasema Bw Shake.

WAZIRI mteule wa Vyama vya Ushirika na Biashara ndogo ndogo Wycliffe Oparanya amesema kuwa viongozi wakuu wa upinzani walioteuliwa kujiunga na serikali ya Kenya Kwanza hawajagura vyama vyao.
Bw Oparanya, ambaye pia ni Naibu kiongozi wa Chama cha ODM, alifafanua kuwa wanachama wa chama hicho watakaojiunga na serikali ya Rais William Ruto baada ya kuidhinishwa na bunge la taifa, watahudumu kwa nyadhifa zao binafsi huku wangali wakionyesha uaminifu wao kwa chama.
“Haimanishi kuwa tumekiacha chama chetu cha ODM, sisi bado ni wanachama wa chungwa lakini tunatumikia serikali katika nyadhifa zetu. Lakini sijapigwa msasa kwa hivyo nisingependa kuzungumzia hilo,” akasema Bw Oparanya.
Gavana huyo wa zamani wa Kakamega, hata hivyo, alitetea uamuzi wa upinzani kuhudumu katika serikali ya Kenya Kwanza, akisema walifanya hivyo kuitikia wito wa Rais Ruto wa kuunda serikali ya muungano.
Alisisitiza kuwa kila Mkenya, wakiwemo wale wa mrengo wa upinzani, wana haki ya kikatiba ya kutumikia nchi katika wadhifa wowote, mradi tu wana sifa zinazohitajika.
“Sisi ni Wakenya, na hii ni nchi yetu; kila mtu aliye na elimu na ujuzi anastahili kuhudumu katika serikali yoyote. Mnakumbuka Rais alitamka wazi kuwa anaunda serikali ya muungano, kwa hiyo serikali hiyo itawashirikisha viongozi wa upinzani,” akasema.
Bw Oparanya alikuwa akizungumza mjini Mombasa mnamo Jumamosi wakati wa mkutano na jamii ya Waluhya wanaoishi Mombasa chini ya kikundi cha Wereca Real Focus.
Wereca Real Focus ni kikundi kilichoundwa katika Kaunti ya Mombasa kwa lengo la kuwaunganisha Waluhya wanaoishi Mombasa ili kusaidiana, kubadilishana mawazo ya kiuchumi, na kutiana moyo kuhusu uwekezaji na vyama ya wanawake.
Huku akiahidi kuwa atasaidia kundi hilo, Bw Oparanya alishukuru kwamba jamii hiyo imetambua umuhimu wa kujiimarisha ili kubuni ajira, na kukabiliana na umaskini.
“Ili kikundi kiweze kustawi na kuinua jumuiya yetu, lazima wajitose katika biashara; ajira pekee haiwezi kutosha. Hata kama umeajiriwa, ni muhimu kuwa na biashara ya kando ambao inaweza kukusaidia na wengine katika jamii,” alisema.
Bw Oparanya, ambaye alisisitiza kwamba bado yuko katika ODM. Aliahidi kuwa chama hicho hakitasita kutoa wito wa kukamatwa na kufunguliwa mashtaka maafisa wa polisi walioua na kuwajeruhi waandamanaji, pamoja na kupigania fidia kwa familia za waathiriwa.
“Mimi bado ni naibu kiongozi wa chama cha ODM, na ni kweli kwamba huu ndio msimamo wetu. Tumekuwa na maandamano na watu wetu wengi wameuawa na kulemazwa. Ni muhimu kwamba wale ambao wamepoteza maisha yao walipwe fidia ikiwa tunataka kupata amani,” alisema.
Kundi hilo la Wereca Real Focus, kupitia kwa Meneja wa eneo la Pwani Jonathan Wepukhulu, lilikaribisha uteuzi wa Bw Oparanya kuhudumu katika serikali ya Rais Ruto, likisema kuwa anafaa kwa kazi hiyo.
“Tunafurahi kama Wereca kwa sababu uteuzi wake unastahili. Amehudumu kama gavana na kufanya kazi nzuri. Ujuzi na uzoefu wake katika utawala utasaidia kuipeleka nchi hii mbele. Tunamtakia kila la heri anapoungana na wenzake kuleta mageuzi katika nchi hii,” akasema Bw Wepukhulu.

TABIA ya ubinafsi na tamaa ya chama cha ODM ya kutaka kutawala vyama tanzu katika miungano ya kisiasa imechipuka tena ikitaka kukwamilia nyadhifa za uongozi katika upinzani bungeni hata baada ya kuwa wazi imejiunga na serikali.
Kiongozi wa ODM Raila Odinga amejaribu kukanusha kwamba chama chake kimejiunga na Serikali katika kile ambacho wachanganuzi wanasema ni uroho wa kutaka kukwamilia nyadhifa za uongozi bungeni.
Kulingana na Raila, viongozi wa chama chake walioteuliwa mawaziri walifanya hivyo kama watu binafsi na haukuwa uamuzi wa ODM au muungano wa Azimio la Umoja One Kenya.
Kauli sawa ilitolewa na Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna aliyedai kuwa hakukuwa na azimio la chama, viongozi wake wateuliwe mawaziri.
Baada ya Rais William Ruto kuwateua maafisa wanne wa ODM kuwa mawaziri, vinara wenza wa Azimio walimtangaza kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka kuwa kiongozi mpya wa muungano wa upinzani.
Hata hivyo, kundi la wanachama wa ODM eneo la Nyanza liliwashutumu kwa kujaribu kumpindua Raila kutoka wadhifa wake wa sasa katika muungano huo wa upinzani.
Wadadisi wanasema hatua ya Raila na ODM ni kutaka kuthibiti upinzani akiwa serikalini. “ Ni tamaa ambayo alionyesha mara ya kwanza baada ya handisheki yake na Uhuru Kenyatta 2018 japo wakati huo wandani wake hawakuteuliwa mawaziri,” asema mchambuzi wa siasa Collins Mwenda.
Anasema lengo la Raila na ODM ni kukwamilia nyadhifa za kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa na seneti na viranja wa wachache katika mabunge hayo ambazo zinashikiliwa na ODM kama chama kikubwa katika Azimio.
“Hii ndiyo sababu inafanya washirika wa Raila kupiga kelele wakilaumu Kalonzo na wenzake waliokataa kujiunga na serikali kwa kumpindua kiongozi wao kama kinara wa Azimio,” asema.
Mbunge wa Ugunja Opiyo Wandayi aliyeteuliwa waziri wa kawi na petroli ndiye kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa huku mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohammed, mwandani wa karibu wa Raila akiwa kiranja wa wachache.
Nyadhifa hizi na zile za seneti huwa za kifahari kwa kuwa afisi zinafadhiliwa na Tume ya Huduma ya Bunge na wanaozishikilia wanapata marupurupu mengi yakiwemo magari ya serikali.
Mnamo Alhamisi, Musyoka alitangazwa na wenzake kuongoza muungano huo huku Bw Odinga akijikita kwenye “kampeni za kuwania uenyekiti wa Tume ya Afrika”.
Kulingana na gavana wa Homa Bay Gladys Wanga, ODM hatua ya Musyoka na vinara wenza wa Azimio ni ya kumtimua Raila katika muungano huo.
“Sisi ni wanachama thabiti wa muungano wa Azimio na siku ambayo Raila Odinga ataondoka kwenye kiti atasema. Ni kana kwamba amepinduliwa kutoka kwa uongozi kwa kisingizio kwamba anaenda AU,” alisema Wanga.
Mwenda anasema hatua ya ODM ya kukwamilia uongozi wa Azimio bungeni ni kilele cha uroho, tamaa na unafiki wa kisiasa.
“Nashawishika kuwa kauli ya Sifuna kwamba kuteuliwa kwa wenzake katika baraza la mawaziri hakukuwa uamuzi wa chama kama njia ya kukwamilia wadhifa wake kama naibu kiongozi wa wachache katika seneti. Hii ni kwa sababu wenzake, baadhi yao walio karibu sana na Raila kama Peter Kaluma na Mbadi mwenyewe walikiri kwamba chama kiliamua wajiunge na serikali,” akasema.
Anasema Raila amejiweka katika hatari ya kuamuliwa mustakabali wake wa kisiasa na Rais Ruto.

BAADHI ya viongozi waliochaguliwa kutoka Nyanza ambao waliitwa ‘waasi’ kwa kushirikiana na Rais William Ruto wanasema wameondolewa lawama baada ya wakosoaji wao kuteuliwa katika baraza la mawaziri.
Wanasema walikuwa na maono katika hatua yao ya kijasiri waliyochukua mapema ya kushirikiana na serikali ya Kenya Kwanza.
Viongozi hao walisema licha ya kutukanwa na wafuasi wa upinzani waliowaita wasaliti, kwa sasa ni wazi kuwa wapinzani umebaini ni lazima ushirikiane kwa karibu na serikali ili kuhakikisha nchi ni tulivu.
Kauli zao zilijiri siku chache baada ya washirika wa kiongozi wa ODM Raila Odinga ambao ni viongozi wakuu wa ODM kuteuliwa katika baraza la mawaziri la serikali ya Rais Ruto.
Wanne hao ni Mwenyekiti wa National Orange Democratic Movement Party na mbunge mteule Bw John Mbadi (Hazina ya Kitaifa na Mipango ya Kiuchumi), Naibu Viongozi wa Chama cha ODM Hassan Joho (Madini, Uchumi wa Baharini na Masuala ya Bahari) na Wycliffe Oparanya (Ushirika na Biashara Ndogo) na Kiongozi wa Wachache katika Bunge la Kitaifa Opiyo Wandayi (Nishati na Petroli).
Wanne hao wamekuwa msitari wa mbele kuwakosoa ‘waasi’ kwa kushirikiana na Rais Ruto na kutumia mifumo ya chama kutishia kuwaadhibu.
Mnamo Februari, mwaka jana, viongozi hao walikutana na Rais Ruto Ikulu, Nairobi kinyume na msimamo wa Bw Odinga.
Waliozuru Ikulu ni pamoja na Mbunge wa Kisumu Mashariki Shakeel Shabbir ambaye alichaguliwa kuwa mgombeaji huru, Seneta wa Kisumu wa ODM Tom Ojienda na wabunge wa Bunge la Kitaifa Bw Mark Nyamita (Uriri), Elisha Odhiambo (Gem), Dkt Gideon Ochanda ( Bondo), Paul Abuor (Rongo), Phelix Odiwuor almaarufu Jalang’o (Langata) na Caroli Omondi (Suba Kusini).
Baadaye walitimuliwa kutoka kwa kamati na kukabiliwa na hatua za kinidhamu kutoka ODM ambacho kilianzisha mchakato wa kuwaondoa chamani na kushinikiza wajiuzulu kwao kama wabunge.
“Tulishutumiwa na kuitwa majina lakini sasa nafurahi kwamba tumeondolewa lawama. Kulikuwa na mvutano wa kisiasa kati ya ODM na muungano wa Kenya Kwanza na tulikuwa wa kwanza kuona umuhimu wa kufanya kazi na serikali mapema kwa manufaa ya watu wetu. Nimefurahi kwamba waliokuwa wakitukosoa, wamejiunga nasi,” akasema Seneta Ojienda.
Dkt Ochanda anasema hajuti kuchakua hatua ya kijasiri.
“Baada ya uchaguzi, baadhi ya watu walikuwa bado na mashaka kwamba tuna Serikali, tulichukua hatua ya kijasiri ya kuitambua Serikali iliyopo madarakani, tulienda na kama Ojienda na sasa waliotuhukumu wamezunguka huku na kule lakini wameishia kuwa pamoja nasi,” alisema Dk Ochanda.
Bw Nyamita alitaja uteuzi huo kuwa mzuri na kuwataka Wakenya kukumbatia mazungumzo.
Bw Nyamita alifurahi kwamba Rais Ruto ameondoa uadui wa kisiasa na kuungana na wanaodhaniwa kuwa wapinzani wake wa kisiasa.

KAMPUNI ya mahaba ya Social Discovery Group (SDG) imewapa karibu wanamichezo 10,500 kutoka timu 206 fursa murwa ya kuchumbiana bila kulipia huduma za tovuti yake ya Dating.com wakati huu wa Michezo ya Olimpiki jijini Paris, Ufaransa.
Kenya inawakilishwa na wanamichezo 70 kwenye michezo hiyo ambayo waandalizi tayari wamesambaza kondomu 200,000.
Wakenya wameingia katika fani za raga (wanaume), voliboli (wanawake), uogeleaji (wanaume na wanawake), judo (wanawake), uzio (wanawake) na riadha (wanaume na wanawake).
Dating.com inaeleza kuwa inatambua kuwa wanamichezo wanahisi wana upweke wakati wa michezo hiyo na inawasaidia kupata uhondo wa nje ya uwanja.
Tovuti hiyo inasema kuwa wanaolimpiki hao wanaweza kuwasiliana na kuendeleza mahusiano muhimu bila ya kupoteza umakinifu wao kwenye fani wanazoshiriki.
“Wanamichezo wanaweza kujiandikisha katika tovuti yetu Dating.com/Paris2024. Baada ya kuthibitisha habari zao, uanachama wao utafanywa hai na wanaweza kuanza kurusha chambo na kuunganika na wenzao wakifanikishwa na vifaa vya mawasiliano vya Dating.com, hasa Let’s Mingle,” ikasema kampuni hiyo ambayo watu 500 milioni wanatumia bidhaa zake 66.
Uamuzi wa kuanzisha mradi huo, Dating.com inasema kuwa unafuatia habari kuwa wanamichezo wako huru kuendeleza miereka ya chumbani kwenye michezo hiyo inayofanyika Julai 24 hadi Agosti 11.
Hii ni tofauti na makala yaliyopita jijini Tokyo nchini Japan wakati masharti yalikuwa makali ya kutokaribiana kwa sababu ya janga la ugonjwa wa Covid-19.
SDG inasema ni muhimu watu kutangamana na kuwa Dating.com inawapa mahali pazuri pa kufanya hivyo.
Kondomu zimekuwa zikisambazwa kwenye Olimpiki tangu mwaka 1988 jijini Seoul, Korea Kusini. Olimpiki za Seoul zilishuhudia kondomu 8,500, zikaongezeka hadi 50,000 wakati wa Olimpiki za 1992 jijini Barcelona, Uhispania.
Idadi ilikuwa 15,000 mjini Atlanta, Amerika (1996), 90,000 mjini Sydney, Australia (2000), 130,000 mjini Athens, Ugiriki (2004), 100,000 mjini Beijing, Uchina (2008), na 150,000 mjini London, Uingereza (2012).
Olimpiki za Rio de Janeiro, Brazil mwaka 2016 ziliweka rekodi ya dunia ya kondomu 450,000. Makala ya 2020 mjini Tokyo yalishuhudia washiriki wakipewa kondomu 160,000, lakini kama zawadi baada ya mashindano waende watumie makwao.
mapenzi
Paris Olympics 2024
Muktasari
Habari za Afrika Leo Mchana.

1.Polisi nchini Uganda wanaendelea na operesheni ya kuwakamata vijana wanaondamana kupinga ufisadi nchini humo huku Rais Yoweri Museveni akiahidi kuwapa msahaha vijana waliokamatwa ikiwa watawafichua watu wanaowafadhili.
2.Tume ya Uchaguzi nchini Venezuela, imemtangaza Nicolas Maduro mshindi wa uchaguzi wa rais kwa kupata asilimia 51 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkuu Edmundo Gonzalez aliyejinyakulia asilimia 44 ya kura.
- Watu wawili wameuawa kusini mwa Lebanon kufuatia shambulio la kulipiza kisasi la Israel baada ya vijana 12 wa Israel kuuawa kwa roketi siku ya Jumamosi. Miito imekuwa ikitolewa ili kutotanua mzozo huo lakini serikali mjini Tel-Aviv imesema inalenga kuiadhibu Hezbollah bila kusababisha vita kamili lakini Uturuki imetishia kuingilia kati.
4.Nchini DR Congo, mamlaka imewaachia huru wafungwa 420 kutoka katika gereza kubwa na lenye msongamano wa watu la Makala.
Hatua hii imekuja baada ya picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuonyesha hali mbaya wanayokabiliwa nayo wafungwa kwenye gereza hilo.
Gereza la Makala maarufu kama Centre pénitentiaire et de rééducation de Kinshasa (CPRK), lilijengwa mwaka wa 1957 kwa ajili ya wafungwa 1,500 ila kwa sasa linaripotiwa kuwa na wafungwa 15,000.
#DRCongo #kinshasa #makalaprison Benjamin Kasembe Journaliste Jacques Mulakirwa Reuben Lukumbuka Ben Saleim
5.Pande hasimu nchini Sudan, zimetekeleza vitendo vya ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na wasichana wa kati ya umri wa miaka 9 na 60, ikiwemo kuwazuia wahanga kupata huduma za kiafya jijini Khartoum, hii ni kwa mujibu wa shirika la kimataifa la haki za binadamu, Human Rights Watch.
6.Marekani Jumapili imetangaza hatua mpya madhubuti ya kuimarisha kamandi yake ya kijeshi nchini Japan, ili kuongeza ushirikiano na vikosi vya Japan, wakati mataifa yote mawili yakikubaliana kuwa China ndiyo changamoto kubwa zaidi ya kimkakati, inayokumba eneo hilo.
Tangazo hilo ni kufuatia mazungumzo ya kiusalama kati ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Antony Blinken na mwenzake wa Ulinzi Lloyd Austin, na wenzao wa Japan Yoko Kamikawa na Minoru Kihara. Baada ya mazungumzo hayo, Austin ameambia wanahabari kwamba Marekani itaimarisha vikosi vyake vilivyoko Japan, kwa kuunganisha makao makuu, pamoja na kupanua operesheni zake.
Taarifa ya pamoja kutoka kwa mawaziri hao imesema kuwa mfumo mpya wa kamandi utatekelezwa sambamba na mpango wa Tokyo wa kubuni kamandi ya pamoja ya vikosi vyake kufikia Machi mwaka ujao. Taarifa hiyo pia imekashifu kile kimetajwa kuwa tabia ya kichokozi ya Beijing, kwenye bahari ya Kusini na Mashariki mwa China, ambako inafanya mazoezi ya kijeshi na Russia, pamoja na kupanua utengenezaji wa silaha za nyuklia.
Taarifa hiyo imeendelea kusema kuwa sera za kigeni za Beijing zinazingatia kubadili mfumo wa kimataifa ili kujinufaisha wenyewe, huku wakiumiza wengine.
TheHeartBeatofAfrica
All Rights Reserved © Cantona Group Ltd||2024
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.