Usiambatane na watu wanaoudharau uwezo wako.

Na. Mtume Na Cantona Joseph

Katika maisha yako ya hapa duniani utajiri wako mkubwa unaopaswa kujivunia ni ule uwezo ambao Mungu amekuamini na kukupatia. Kila mtu ana uwezo wake binafsi ambao huo ndiyo utajiri wake.

Kwa mfano leo hii ukimkata mikono mwana masumbwi (bondia) unakuwa umempa umasikini wa kudumu maana utajiri wake uko katika uwezo ambao Mungu ameuweka kwenye mikono yake.

Moja kati ya uwezo ambao Mungu alimpatia Mfalme Daudi ilikuwa ni kupigana, na katika kitabu cha Zaburi 144:1, alimshukuru Mungu kwa kusema, “Na ahimidiwe Bwana, mwamba wangu, Anifundishaye mikono yangu vita, Vidole vyangu kupigana.”

Huyu ndugu alijua kuwa uwezo wa kupigana siyo takwa lake binafsi bali zawadi maalumu ambayo Mungu alimpatia…

Hata mwanamuziki akigeuka na kuwa bubu ghafla huo ndiyo unakuwa umaskini wake maana utajiri wake unatokana na uwezo ambao Mungu ameuweka kwenye sauti yake.

Leo kuna wanasoka matajiri ambao akikatika mguu mmoja anakuwa amepoteza uwezo unaomletea utajiri, hiyo ni mifano michache ya uwezo ninaouongelea hapa leo.

Mwenyezi Mungu anaamini sana katika uwezo aliyouweka ndani mwanadamu, ndiyo maana alimwambia Gidion, “Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma?” (Waamuzi 6:14).

Mungu huwa anatupa uwezo (Karama na vipawa mbalimbali) kwa ajili ya kutimiza makusudi yake hapa duniani, ambapo kuuthamini na kuutumia uwezo huo ni wajibu na kutokuutumia ni dhambi isiyokuwa na udhuru mbele za Mungu.

Yesu akiongelea uwezo huu katika lugha ya fumbo aliuita talanta ambao alisema mtu atakaeifukia talanta yake (Akimaanisha kuwa mtu ambaye hatautumia uwezo wake) ipo siku ataulizwa na kuwajibishwa na Mungu. Soma Mathayo 25:1-30.

Watu wote waliofanikiwa katika maandiko ni wale ambao hawakuudharau uwezo ambao Mungu amewapatia, wala hawakukubali kuongozana na watu wasioamini katika uwezo wao (watu wanaowadharau).

Historia ya maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo inaonyesha alikuwa ni muumini mzuri sana katika dini ya wayahudi tangu akiwa mtoto, ambaye wazazi wake walimzaa na kumlea katika taratibu na sheria za dini hiyo. Ushahidi wa maandiko unaonyesha kuwa, hata Yesu alipokuwa mtoto wa miaka kumi na mbili aliweza kukaa hekaluni na kuwahoji viongozi wa dini yake huku wakiishangaa hekima yake (Luka 2:46-47).

Lakini baada ya kushuka kutoka mlimani na kwenda kuhubiri kwenye sinagogi kama ilivyokuwa desturi yake, watu wa dini yake walimkataa na kutaka kumuua, hapo ndipo aliachana nao na kutafuta kampani ya wavuvi, watoza ushuru na watu wasiojua mambo ya dini hao ndiyo akaambatana nao.

Kwa lugha nyingine ni kwamba aliwaacha wanathiolojia na wanazuoni waliomdharau na kumkataa, kisha akaambatana na masela waliomuheshimu na kuukubali uwezo wa Mungu uliyo ndani yake.

Alikadhalika Yefta alipokataliwa na ndugu zake kwa kigezo cha kuwa mtoto wa kahaba, aliamua kuondoka na kuitafuta jamiii ya watu wasiofaa (mabaradhuli) ambao walimuheshimu na kufanya nae kazi kama kiongozi wao, na jamii hiyo ndiyo ilimtambulisha na kumpa uongozi wa taifa la Israeli. Soma habari zake katika kitabu cha Waamuzi 11 na kuendelea.

Hata Daudi naye alikataliwa katika ikulu ya mfalme Sauli, na alipokimbilia kwenye pango la Adulamu alifuatwa na watu wachovu mia nne ambao walimuheshimu na kuuamini uwezo ambao Mungu ameuweka ndani yake. Maandiko yanasema, “Kila mtu aliyekuwa katika hali ya dhiki, na kila mtu aliyekuwa na deni, na watu wote wenye uchungu mioyoni mwao, wakakusanyika kwake; naye akawa jemadari wao; nao waliokuwa pamoja naye walipata kama watu mia nne.” (1 Samweli 22:2).

Muheshimu sana na umtunze kwa gharama yeyote mtu ambaye anaukubali uwezo wako wa ndani ambao Mungu amekupatia bila kushawishiwa na vitu unavyovimikiki, maana huyo ndiyo mfuasi wa kweli ambae Mungu amekupatia.

Utajiri wa vitu unavyomiliki au utakavyokuja kuvimiliki ni ushahidi wa tu wa uwezo ambao Mungu amekupatia bali uwezo ulioko ndani yako ndiyo utajiri halisi.

Utajiri wa nyumba, magari, mifugo, mashamba ni vitu ambavyo mtu yeyote anaweza kuvitafuta na kuvipata, ila uwezo ulioko ndani yako ndiyo utajiri pekee ambao hakuna mtu ambaye anaweza kutafuta na kuupata kwa juhudi zake.

Ndiyo maana katika historia ya taifa la Tanzania kuna Baba wa taifa mmoja tu ambapo hatakuja kutokea mwingine, maana uwezo wake ndiyo ulimpa heshima hiyo, na kuna Magufuli mmoja na hatokuja kutokea mwingine maana uwezo wake ndiyo umempa heshima ya kukumbukwa daima…

Hivyo basi uwezo wako ndiyo utajiri wako na ndiyo upekee wako hapa duniani, hata kama hauna pesa, hauna magari, hauna nyumba, hauna elimu lakini kama una uwezo ambao Mungu amekupatia bado wewe ni tajiri ambaye ukiushikilia vizuri na kuupalilia uwezo huo ipo siku Mungu atakuja kukushangaza wewe, kuishangaza dunia na kukufuta machozi ya taabu yako.

Uwezo wako unaweza kuonekana kama ni jambo la kawaida katika macho ya wanaokutazama lakini ukiuheshimu uwezo huo ipo siku utakuheshimisha mbele ya jamii ya watu waliokudharau.

Yusufu alikuwa na uwezo wa kuota ndoto na alipoutambulisha uwezo huo kwa jamii yake ambao wana uwezo wa kuota na kufafsiri ndoto aliishia kuchukiwa na kutaka kuuwawa. Lakini huo huo alipoutumia kwenye nchi ya Misri, watu ambao waliuamini na kuuheshimu uwezo huo alijikuta hadi anapata nafasi ya kuwa waziri mkuu katika taifa hilo…

Sijui ninaongea na nani kupitia andiko langu hili na sijui Mungu amekusudia nini kwako ila nachojisikia kukuambia ni kwamba uheshimu sana uwezo wako. Na njia moja wapo ya kuuheshimu na kuutunza ni pamoja na kubadilisha mazingira ya watu wanaokudharau na utafute watu watakaouheshimu uwezo wako.

Biblia inasema, “Amdharauye mwenzake afanya dhambi.” (Mithali 14:21), andiko hili linathibitisha kuwa dharau ni dhambi, hivyo wenye dhambi ya kukudharau haupaswi kabisa kuambatana nao maana dhambi yao ina nguvu ya kuua uwezo ambao Mungu ameuweka ndani yako, hivyo busara ya ki Mungu ni kuondoka katikati yao na kujitenga nao ili Mungu akuletee watu watakaoheshimu uwezo uliyopewa na Mungu.

Ukisoma kitabu cha Ezra 9:3-4 utaona Ezra alipoanza maombi ya toba alifuatwa na kundi la watu waliotetemeka baada ya kusikia maneno ya Mungu, hata kwetu sisi hao ndiyo aina ya watu tunawahitaji kwenye maono, watu wanaotuamini na kuheshimu dhamana ya uwezo ambao Mungu ametupatia, kinyume na hapo maono hayawezi kwenda mbele, sanasana yatazidi kushuka na kurudi nyuma.

Nahitimisha kwa kusema kuwa kundi linalokukataa na wewe likatae, sehemu unayofukuzwa ondoka, eneo usilohitajika usiende, jitenge na watu wanaoudharau uwezo wako hii ndiyo njia sahihi ya kukuza kile ambacho Mungu amekuamini na kukupenda.

Maamuzi hayo yanaweza kuwa siyo rahisi sana lakini unapaswa kuamua kukubali msoto, upweke, kupotea kwa muda hadi pale Mungu atakapokutambulisha tena ukiwa na watu sahihi ambao umewapata katika majira yako ya giza na ukimya.

MUNGU WA ISRAELI AKUBARIKI SANA.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment