Pamoja na maandiko kututaka kuwa na huruma na kusaidia maskini, yatima, wajane, walemavu na watu mbalimbali lakini ipo haja ya kumshirikisha Mungu katika kila tendo jema unalotaka kufanya kwa wahitaji.
Maana siyo kila anaepitia changamoto za kimaisha ikiwemo magonjwa na mapito mbalimbali anastahili kusaidiwa, bali wengine nyuma ya mapito yao kuna gadhabu ya Mungu ambayo hiyo inahitaji toba na unyenyekevu wao kwa Mungu ili shida hiyo iondoke juu yao.
Na wanapokaidi na kushupaza shingo ndipo mapigo yanazidi kuongezeka kwao, ambapo katika hali hiyo akijitokeza mtu na kutaka kuwasaidia anakuwa amejiunganisha na kuwa sehemu ya mapigo hayo pasipo yeye kujua.
Mtume Paulo alimpa wosia Timotheo na kumwambia kwamba asiwe na haraka katika kumuwekea mtu mkono maana unaweza kujikuta unashiriki dhambi za watu wengine (1 Timotheo 5:22).
Ni dhahiri kwamba unaweza kufanya tendo jema kabisa kwa mtu na ukadhania unatenda wema kumbe ndiyo unajiingiza kwenye vita ambayo ilikuwa haikuhusu.
Naomba tusome kisa hiki ndani ya biblia cha mtu aliyepitia hali kama hiyo na kujikuta anapoteza hata kile alicho nacho.
Kuna wakati Mungu alimtuma Mfalme Sauli kupitia kinywa cha Nabii Samweli, kwamba aende vitani na kuwaua waamaleki wote pamoja na kuteketeza vitu vyao, kwa sababu miaka mingi iliyopita mababa zao walifanya makosa na hawakuyatubia (1 Samweli 15:3), lakini Sauli alipofika vitani akatumia akili zake za kibinadamu na huruma za kilokole ambapo maandiko yanasema, “Lakini Sauli na watu wake wakamwacha Agagi hai, na katika kondoo walio wazuri, na ng’ombe, na vinono, na wana-kondoo, na cho chote kilicho chema, wala hawakukubali kuwaangamiza; bali cho chote kilichokuwa kibaya na kibovu, ndicho walichokiangamiza kabisa.” (1 Samweli 15:9).
Japokuwa Mfalme Sauli alitenda haya kwa nia njema kabisa ya kubakiza vile vitu vizuri kwa ajili ya kumtolea Mungu sadaka (1 Samweli 15:15) lakini hakujua kuwa neno la Mungu ni sheria inayopaswa kuzingatiwa bila kuingiza hisia zetu za kibinadamu.
Makosa kama haya watu wengi wanayapitia leo kwa kutanguliza huruma zao kabla ya kuchunguza sababu iliyo nyuma ya mateso ya mtu wanaemuhurumia na kutaka kumsaidia.
Kwa mfano leo hata ukikuta mtu amepooza mwili mzima, mke kamkimbia, na watoto wake hawamjali, unaruhusiwa kabisa kumuhurumia kama binadamu mwenzako, lakini usichukue hatua ya kumsaidia kabla ya kumuomba Mungu ruhusa ili kuepuka yasije kukukuta kama yaliyomkuta Sauli.
Nimetumia mfano wa mtu aliyepooza ila namaanisha mtu yeyote anaepitia changamoto yeyote ile.
Maana leo hii kuna watu wanateseka sana lakini nyuma ya pazia utakuta mateso hayo ni mavuno ya mbegu mbaya waliyopanda siku za nyuma.
Kuna watu leo wana utajiri walioupata kwa kutoa kafara za kishetani ambazo zinahusisha matendo ya kikatili kama vile kumwaga damu ya mtu, kubaka na kulawiti watoto, kushiriki mapenzi ya jinsia moja, kulala na wazazi wao, na watu hao utakuta wanakula bata hapa mjini zaidi ya wewe unaetafuta kwa njia ya haki. Lakini hakimu wa hayo yote huwa ni muda. Kama maandiko yanavyosema, “Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya; Wala usiwahusudu wabaya.
Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu; Taa ya mtu mbaya itazimika.” (Mithali 24
19:20).
Maisha ya mtenda mabaya huwa hayana thawabu na mwisho wake huwa ni taa yake kuzimika (Taa kuzimika siyo kifo bali ni kuishi maisha ya giza ambayo ni mateso na taabu)
Tofauti kabisa na maisha ya wanaotenda wema.
Biblia inasema, “”Umwangalie sana mtu mkamilifu, Umtazame mtu mnyofu, Maana mwisho wake mtu huyo ni amani.”
(Zaburi 37:37).
Haya ni maandiko yanayoonyesha kwamba mwisho wa mtu asiye mkamilifu katika njia zake au asiye muadilifu huwa hauna amani bali una mabaya.
Ndiyo hapo utamkuta mtu kawa homeless wakati zamani alikuwa tajiri wa kuuza madawa ya kulevya, au mfanya biashara ya human trafficking, nakadhalika alafu kabla hajamalizana na Mungu wewe unataka kuingilia kati kumsaidia. Hapo ndiyo na wewe unaanza kushiriki mapigo yake.
Leo hii kuna watu wameingia kwenye maisha magumu punde tu baada ya kutoa msaada kwa mtu aliyekuwa ana mapito fulani. Wengine biashara zimeyumba, huduma zimekufa, ndoa zimevunjika, nguvu za kiume zimepotea nakadhalika nakadhalika, kwa sababu tu ya kuingilia vita ya mtu na Mungu kwa kushawishiwa na hisia zao za huruma.
Hebu fikiria, miaka michache ijayo ukija kukutana na mtumishi wa Mungu ambaye kwa sasa anavuma kwenye media, ana pesa na waumini wa kutosha, alafu umkute amefulia kiasi kwamba hana hata makazi ya kuishi, au amelala kitandani kansa, ukimwi au gonjwa baya la ki Misri linammliza, pembeni yake wapambe wote wamekimbia, alafu wewe ukaingia kati na kutaka kumsaidia, kumbe mtu huyo anapigwa na Mungu kwa makosa ya kugushi miujiza, kudanganya watu waliomuamini, kulala na wake za watu, kuwapa mimba wanawake na kuzitoa ili jina lake liwe salama, kutapeli, kutumia nguvu yake ya kiuchumi vibaya na kudhurumu watu nk. Hapo ndiyo utajikuta unashangaa kwamba, baada ya kumsaidia mtumishi huyo ndiyo mikosi inaanza kukuandama.
Ndugu yangu, kusaidia ni kuzuri sana pale ambapo Mungu ameridhia umsaidie mtu na siyo pale ambapo hisia zako za huruma zinakutuma utoe msaada….
Kuwa mtu mwema, wapende watu, wahurumie, lakini katika kuwasaidia hakikisha kuwa Mungu amekupa kibali cha kufanya hivyo maana wengine hawastahili kusaidiwa bali wanatakiwa kutubu maana mapito yao yanasababishwa na maovu yao mbele za Mungu.
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.