Baraka na utajiri ni vitu viwili tofauti.

Baraka na utajiri ni vitu viwili tofauti kama vile laana na umasikini vilivyo tofautiana.
Watu wengi tumekuwa na mtazamo hafifu juu ya baraka za Mungu kwenye maisha ya mtu huku tukidhania wanaomiliki mali ndiyo waliyobarikiwa na wale wanaoishi maisha ya kubangaiza tunawahisi kama watu waliyolaaniwa.

Leo katika makanisa mengi matangazo yao yanawataja watu wasiokuwa na nyumba, gari, kazi, ndoa, watoto nk kama kundi lenye laana na mikosi huku wakiwaaminisha kuwa kumiliki vitu vinavyoonekana ndiyo ishara ya kubarikiwa.

Mimi ninaukosoa mtazamo huu kwa herufi kubwa kulingana na ufahamu wangu juu ya ahadi za Mungu zilizofichwa ndani ya maandiko.

Katika biblia takatifu tunamuona Kaini aliyekuwa first born wa Adam baada ya kulaaniwa na Mungu ndipo aliweza kujenga mji (Apartment) katika nchi ya Nodi na kuuita kwa jina la mwanaye Henoko.

Huu ni ushahidi tosha unaoonyesha kwamba hata mtu mwenye laana anaweza kujenga, kuoa/kuolewa na kupata watoto, ila tofauti kati ya aliyelaaniwa na aliyebarikiwa iko kwenye kuvifurahia vile anavyovimiliki.

Mfalme Sulemani katika sehemu kubwa ya kitabu chake cha mhubiri ameongelea kwamba baraka za Mungu katika maisha aliyotupatia hapa duniani ni kuyafurahia maisha yetu, (Mhubiri 2:26).

Hata Musa katika sheria zake aliainisha kuwa baraka ni mtu kufurahia maisha yake na laana ni mtu kutofurahia maisha yake ukijumuisha na vitu alivyovitafuta na kuvipata.

Ndiyo maana kwenye Torati 28 kuanzia mstari wa 20 Musa akaeleza dalili zote za laana ambazo kwa ujumla wake ni kutofurahia maisha yako katika kila unachokimiliki ikiwemo kuchumbia mwanamke alafu mwanaume mwingine akakunyang’anya na kulala naye, ujenge nyumba alafu usiishi ndani yake, ulime shamba na faida wapate watu wengine wewe uishie kutaabika tu, uwe mtu wa kudhulumiwa nakadhalika (Torati 28:30).

Kwa maana hiyo wapo watu waliyobarikiwa ingawa wamepanga chumba kimoja na sebule na vilevile wapo watu waliyolaaniwa ingawa wamenga maghorofa na wanatembelea magari makubwa ya kifahari.

Kama una pesa na hauwezi hata kuwasaidia wazazi au ndugu zako kisa tu unaogopa kuvunja masharti uliyopewa na mganga tambua kuwa wewe ni mmoja wa watu waliyolaaniwa.

Kama una gari zuri na hauwezi kulitembelea mwisho wa siku unaishia kupanda daladala huku gari yako ukiwa umeikodisha kwa watu wengine hiyo pia ni dalili ya laana.

Kama umeoa/olewa kwa harusi kubwa na nzuri lakini ndani ya ndoa hakuna amani kiasi kwamba ukiwa nje ya nyumba unakuwa na furaha zaidi ya unapokuwa nyumbani na mke/mume wako hiyo pia ni dalili ya laana.

Kama una ajira lakini muajiri wako haoni jema katika juhudi zote unazozifanya katika wajibu wako hiyo pia ni dalili ya laana…

Baraka ni kuwa navyo na kuvifurahia huku ukivitawala…. Mafanikio yako kukutawala ni laana bali wewe kuyatawala mafanikio ni baraka maana umeumbwa ili utawale


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment