Chagua kuambatana na watu watakaokusaidia kutimiza ndoto zako.

Kwenye maisha Mungu ameumba mfumo wa kumpatia mtu watu wa kufanana naye… Na mfumo huu ulianza kwake mwenyewe pale alipokuwa ameumba kila kitu lakini akawa hana kiumbe cha kufanana naye kinachoweza kuwatawala na kuwaongoza viumbe wenzake, ndipo akasema, “Na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu; wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi” (Mwanzo 1:26).

Baada ya kumuumba Adam katika nafasi hiyo biblia inaendelea kuelezea kuwa, “Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye” (Mwanzo 2:18), huu ulikuwa ni muendelezo wa Mungu kumpatia binadam mtu wa kufanana naye ili amsaidie kutimiza maono ndipo akamuumba mwanamke ili amsaidie mwanaume.
Hili swala la msaidizi wa kufanana halipo katika ndoa na mahusiano pekee bali hata katika maono, biashara nk, ndiyo maana Mungu mwenyewe alipotaka msaidizi wa kufanana naye katika kuutawala ulimwengu ndipo alimuumba binadamu.

Watu wa kufanana nasi ni watu muhimu sana katika maisha yetu ya kila siku, ninaposema kufanana simaanishi kufanana sura, rangi au umbo, bali kufanana mitazamo ili kuweza kujenga maono pamoja.

Watu wengi maono yao yanakuwa magumu na huduma zao zinakuwa mzigo uliojaa tabu kwa sababu ya kushirikiana na watu ambao hawajafanana nao kimtazamo.
Hapo ndiyo utakuta mtu badala ya kufurahia kile anachokifanya anaishia kuwa na stress za kila siku.

Yusufu alikuwa na maono ya kuwa mtawala lakini mlango wa kumfikisha katika maono yake ulikuwa ni kutafsiri ndoto za watu. Na kwa mfumo huo ndugu zake hawakuwa watu sahihi katika maono yake, maana wakati yeye anaota ndoto, tayari ndugu zake walikuwa na kipawa cha kutafsiri ndoto zake, na kwa ujuzi wao huo walitumia nguvu nyingi kumpinga ili ndoto zake zisitimie.
Hivyo Mungu akamtenga na kumpeleka kwa wamisri ambao hawajui kutafsiri ndoto na kisha akampa kipawa hicho ambacho kilikuwa ni cha asili katika ukoo wao ili aweze kuwafaa na thamani yake iweze kupanda, na kweli kupitia kipawa hicho akafanikiwa kuwa kiongozi mkubwa wa wamisri.
Hao ndiyo walikuwa watu wa kufanana naye, yaani watu wa kumsikiliza na kumsaidia kutimiza ndoto zake.

Ili huduma ya Yesu Kristo ienee duniani kote ilimbidi awaache mafarisayo ambao walikuwa ni wabobezi wa mambo ya ki imani kwa enzi hizo, na akawatafuta wavuvi wa samaki, watoza ushuru, pamoja na wezi ambao ilikuwa rahisi kwao kuielewa huduma yake na kumsaidia kufika katika maeneo ambayo wabobezi wa dini isingelikuwa rahisi kwao kumsindikiza na kumfikisha. Hivyo wavuvi, watoza ushuru, wezi na makahaba ndiyo walikuwa watu wa kufanana naye kihuduma na kupitia hao ndiyo leo hii wokovu umetufikia hata sisi wadengereko.

Bado kuna mtu anaitwa Yefta ambaye ndugu zake walimkataa na akatafuta watu wasiofaa waliojulikana kama mabaradhuli na kushirikiana nao kutimiza wito wake na akafanikiwa.
Samsoni alipokosa watu wa kufanana naye katika wito wake kuna wakati alishirikiana na mbweha ili kutimiza maono yake ya kuteketeza mashamba ya maadui zake.
Huu ndiyo mfumo wa mafanikio yaani kutafuta watu wa kufanana na wewe.
Tatizo lililopo sasa hivi ni kwamba watu wengi wanatafuta watu wenye vyeo na pesa badala ya kutafuta watu wa kufanana nao, ndiyo maana hata manabii na mitume wengi wameng’ang’ania miji mikuu kwa sababu ni miji ya kiuchumi, na sasa wengi wana ndoto za kuhamia ulaya kihuduma.Hizo zote ni mbio za kutafuta wenye nguvu kimamlaka na kiuchumi na siyo kutafuta wa kufanana nao ki maono.
Ili maono yaende tunapaswa kuwa na watu wa kufanana nasi either kwa kuwatafuta au wao kututafuta kama vile Daudi alivyotafutwa na watu wenye dhiki, shida, madeni pamoja na uchungu nafsini mwao, na hao ndiyo wakawa ministry partners wake…
Anaekufaa kwenye maisha ya kihuduma, kimahusiano, kibiashara, kitaaluma, huyo ndiyo wa kumshikilia sana maana kupitia yeye hata Mungu inakuwa rahisi kwake kukutendea jambo la kukufikisha katika hatima yako.

MUNGU WANGU AKUSAIDIE ULIELEWE SOMO HILI.


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment