Moto wa madhabahu usizimike.

MOTO WA MADHABAHU USIZIMIKE.🔥

“Tengeneza Madhabahu Binafsi ya Roho Mtakatifu ndani yako.”

Mambo ya walawi 6: 13 Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.

Mungu katika agano la kale amekuwa akijifunua kwa Moto,
Mfano; moto uliokula sadaka ya Ibrahim (Mwanzo 15:17), kijiti cha moto kisichoteketea (kutoka 3:2-3), nguzo ya moto usiku kuwaangazia na kuwapa joto wana wa Iraeli (kutoka 13:21), Utukufu wa Mungu ulipo shuka pale mlima Sinai (kutoka 19:18). n.k…

Sikuhizi za agano jipya amejifunua kwa Roho Mtakatifu kama moto akiwa batiza watu kwa Roho Mtakatifu na Moto.

Mathayo 3:11 …….yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu na kwa moto.

Wakati flani Baada ya Mungu kuwakomboa wana wa Israeli, alimuagiza Musa kujenga hema ya mfano wa vitu vya Mbinguni kama alivyo Muagiza (kutoka 25-31) na ujenzi wake uliotekelezwa baadae (kutoka 35-40).

Mungu alitoa masharti haya ili kuwaweka wana wa Israeli katika muelekeo wa kutii na kuongozwa na Mungu. Vitu vyote hivi vilifanyika ili tuu binadamu afundishwe na kujua mambo ya Rohoni ambayo aliyapoteza hapo zamani baada ya kuanguka na kupotea pale alipo kula tunda la mti wa ujuzi wa mema na mabaya, hata akawa hana tena uelewa wa mambo ya Rohoni.

Kumbuka hivi vitu vyote Mungu alivifanya katika Mwili tuu, ili kuwafundisha vitu vya Rohoni, na vilikuwa ni mfano wa mambo ya Rohoni,

Hapa Mungu alitumia nafasi hii, ili kuwajengea watu tumaini la wokovu, wokovu ulioletwa na Bwana Yesu baada ya kukamilishwa pale msalabani, ambao leo hii tumepata bahati ya kuishi katika Neema yake.

Na mwisho wa Maisha haya tufe tukiwa na tumaini hilo ndani ya Mioyo yetu, tumaini la wokovu katika jina la Bwana Yesu, maana bila Imani ya Wokovu huu hatuwezi kukamilishwa, wala kuwa na uhusiano wa kweli na Baba.

Katika vitu vya Muhimu kwenye hema hili ni sadaka za kuteketezwa zilizo hitaji kuteketezwa kwa moto katika madhabahu.

Na madhabahu ndiyo inayo fungua mlango wa mawasiliano baina ya ulimwengu wa Roho na ulimwengu wa Mwili.

Bila Madhabahu, mtu asingeweza kufanya jambo lolote la kuweza kuingia ndani ya lile hema, na bila moto madhabahu isingeweza kuwa na thamani yake iliyo takiwa.

Moto huu wa kuteketezwa sadaka haukutoka kwa watu (binadamu) yaani haukuwashwa kama watu wanavyo washa moto, bali ulikuja kutoka katika utukufu wa Mungu mwenyewe (Mambo ya walawi 9:24) na ulitumika kwa ajili ya kuteketeza sadaka kwenye ile madhabahu, na pia uli tumika kuchomea uvumba kwenye chetezo, na kuwacha vile vinara vya taa.

Mambo ya walawi 6:12 Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake.

Hakuna alie takiwa kuwasha moto wa kigeni mbele za Mungu, yaani moto pekee ulitoka pale kwenye ile madhabahu, na ni ule ulio washwa na Mungu na haukuwahi kuzimika, bali walichochea kuni kila mara zakutosha kuuchochea ili usizimike .

Mambo ya walawi 9:24 Kisha moto ukatoka hapo mbele za Bwana, na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama kifudifudi.

Sasa utaona huu haukuwa moto wa kawaida kabisa, ila ni moto wa kipekee, chanzo chake ni Mungu, ila mtu wa kawaida akija hatojua kwa haraka kuwa huo moto ni wa Mungu, ila kama ikitokea mtu yeyote akawasha moto mwingine, ule moto wa Mungu ungemuua.

Mambo ya walawi 10:1 Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya Bwana, ambao yeye hakuwaagiza.

2 Kisha moto ukatoka hapo mbele za Bwana, nao ukawala, nao wakafa mbele za Bwana.

Baadae Mungu alikuja na kujenga hekalu kupitia mkono wa sulemani kama Isahara ya Mungu kuja kukamilisha hekalu la kweli na la milele kwa njia ya Yesu Kristo, na sisi wanadamu tutakao amini tuwendio mawe ya hilohekalu. (1 wafalme sura ya 5 hadi sura ya 9), (1 Petro 2:5).

Kumbuka , #hema lina weza kubebwa, ni ishara ya kitu cha muda tuu,
ila #Hekalu haliwezi kubebwa, Ishara ya makao ya kudumu, japo hekalu la Sulemani lililikuja kuondolewa, ni ili lije hekalu hili la kweli (ambapo miili yetu ni kama hema/ hekalu la muda mfupi hadi pale tutakapo kufa), kisha lipo hekalu la kudumu mbinguni ambapo tutaenda kukaa na Bwana wetu Yesu Kristo milele.

Leo hii tunayo madhabahu yenye uhalisia mbinguni ambayo tunaweza kuikaribia kwa Imani kwa damu ya Yesu Kristo iliyo mwagika msalabani, na kanisa kama bibi harusi ni Makao ya Roho mtakatifu ambaye yupo juu ya kila kiungo cha kanisa, yaani ndani ya wale walio mpokea Yesu kuwa ni Bwana na Mwokozi wao.

1Petro 2:5 Ninyi nanyi, kama mawe yaliyo hai, mmejengwa mwe nyumba ya Roho, ukuhani mtakatifu, mtoe dhabihu za roho, zinazokubaliwa na Mungu, kwa njia ya Yesu Kristo

Kila aliempokea Yesu anafanyika kuwa hekalu la Mungu.

1wakorintho 3:16 Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

Sasa baada ya kuona kuwa sisi ni hekalu la Roho mtakatifu na namna Mungu alivyoweza kutufundisha kutoka agano lakale hadi tukafika hapa agano jipya, kutoka kule kwenye yale ya vitu hadi kuanza kwenda Rohoni na kuelewa ni kwa jinsi gani sisi tumekuwa hekalu la Mungu, basi tuangalizie sasa kuhusu moto ndani yetu sisi uliowasha kwa Roho mtakatifu, ili tumtolee Mungu dhabihu za Roho.

Baada ya Bwana Yesu kufa msalabani, na kufufuka siku ya tatu, tena baada ya siku hamsini (50) yaani pentecoste, Roho Mtakatifu aliwashukia watu wa kwanza, na ndipo walianza kuwa na nguvu za Roho Mtakatifu , wakinena kwa lugha nyingine na pia baada ya hapo walianza kumtumikia Mungu kwa nguvu.

Matendo 2:1-4

1 Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja.
2 Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi.
3 Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao.
4 Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka.

Ujio wa Roho Mtakatifu, ni ukamilisho wa moto ulioshuka ( mambo ya walawi 9:24) kutoka kwenye utukufu wa Mungu hadi juu ya madhabahu iliyopo ndani yetu kama ma hekalu ya Mungu.

Hii ndio inayo tuwezesha sisi (hekalu la Mungu) kuweza kumfanyia Mungu Ibada ya kweli, maana hakuna Ibada pasipo Madhabahu ya kutolea sadaka na kuchomea uvumba (yaani sala – ufunuo 8:4, Wagalatia 4:6)

Maisha ya Mkristo ni maisha ya Ibada, tena Ibada ya kumuabudu Mungu katika Roho na Kweli.

Ni kwaneno lake Mungu tuu, tunaweza kujua ukweli na kuweza kuamini anacho sema Mungu, na ni kwa maombi tuombayo kwahiyo Imani yaletayo matokeo ya Kiroho, nasio kwa namna nyingine ile.

Sasa basi, upo uadui ambao shetani amekuwa akiupandikiza ili kuzui Moto huu usiwake ndani, yaani Imani ya mtu isisitawi bali iyumbe.

Kama tumesha hama katika matumizi ya vitu vya mfano vilivyotumika katika agano la kale kwa ajili ua kutujengea Imani, basi hatuna haja ya kuvitazama tena kwa macho ya agano la kale, bali kwa mtazamo wa agano jipya, tukijua kuwa Imani yetu haijengwi kwenye vitu bali kwenye neno la Mungu kwa kuliamini.

Mungu alitoa onyo kuwa Moto usizimike, ila kuna watu wana sababisha wengine moto uzimike kwa kuwalewesha na vitu visivyo vya Imani ya kweli, (maana Imani ya uongo ipo na inafanya kazi na kwa kuwa watu wengi ni wavivu wa kusoma neno, wanapotea kirahisi).

Ndio maana mtume Paulo alimuasa Timotheo, achochee karama iliyopo ndani yake,
2Timotheo 1:6 Kwa sababu hiyo nakukumbusha, uichochee karama ya Mungu, iliyo ndani yako kwa kuwekewa mikono yangu.

Mtu alie simama kwa Imani, anafanya kosa kama ataendelea kukaa katika kutegemea vitu. wakati mwingine, shetani hutumia huo mlango na kumuaminisha mtu kitu kisicho na msingi katika neno, yaani Imani mbadala, kwa kisingizio cha huduma ya kiMungu au neno la Mungu, wakiwafundisha watu kutumia vitu visivyo tokana na neno, ila kiukweli sio Mungu aliewatuma.

Mtu anapokuwa anawasha moto tofauti na uliokwisha kuwashwa na Mungu, yaani akipokea Roho nyingine au kristo mwingine, anakuwa anahatari ya kufa kama wale wana wa haruni, na mwisho wa siku kama hatopata neema atakufa kweli na kwenda motoni.

Leo hii hakikisha Moto ndani yako hauzimi kwa kulishwa vitu vya Kiroho visivyo na msingi kwenye neno la Mungu,kwa sababu ni kwa neno tuu, mtu anaweza kuujua ukweli wote na kwa kujuua ukweli akaweza kuwa na Imani Imara na siivinginevyo.

Je Unayo Madhabahu yako Binafsi na Roho Mtakatifu? Moto ndani yako umeshazimwa au bado unawaka?🔥


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment