Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na : Cantona Joseph|RFA

Wizara ya Mambo ya Nje ya China imemwita balozi wake wa Japan nyumbani kwa sababu ya matamshi yaliyotolewa na Waziri Mkuu wa Japan Takaichi Sanae kuhusu uwezekano wa kutokea kwa mzozo juu ya Taiwan.
Takaichi alikiambia kikao cha Bunge la Chini wiki iliyopita kwamba uvamizi wa China huko Taiwan kunaweza kuchukuliwa kama “hali ya kutishia maisha”, na kusababisha Japani kuchukua hatua ya kijeshi.
Makamu wa Waziri wa Mambo ya Nje wa China Sun Weidong alisema Takaichi anapaswa kubatilisha matamshi yake “vinginevyo chochote kitakachotokea Japan itawajibika,” kulingana na Wizara ya Mambo ya Nje huko Beijing.
Hata hivyo, Waziri Mkuu Takaichi, baadaye alisema matamshi hayo yalitolewa kwa dhana ya hali mbaya zaidi inayoweza kutokea na haibadilishi msimamo uliopo wa serikali.
Wizara ya China ilisema Sun iliita matamshi ya Takaichi kuwa “ya nia mbaya” na kunukuliwa kuwa kile alichosema Takaichi kinadhoofisha msingi wa kisiasa wa uhusiano wa China na Japan.
Urusi yafanya mashambulizi makubwa Ukraine

Urusi imefanya mashambulizi makubwa ya makombora na ndege zisizo na rubani kwenye mji mkuu wa Ukraine, Kyiv na maeneo mengine ya nchi.
Mapema siku ya Ijumaa, ilithibitishwa kwa mtu mmoja ameuawa huko Kyiv na moto mkubwa umetokea ambao umeharibu jengo la makazi katika wilaya nyingi za mji mkuu, Meya Vitali Klitschko alisema.
Takriban watu 26 walijeruhiwa huku wafanyakazi wa dharura wakijibu mashambulizi mengi, kulingana na maafisa.
Klitschko alisema huenda watu wengine wawili waliuawa katika shambulio hilo, lakini bado haijathibitishwa kwani waokoaji hawakuweza kutoa miili kutoka kwenye vifusi.
Wakati huo huo, shirika la habari la Reuters limeripoti kuwa vikosi vya ulinzi wa anga vya Urusi vimedungua au kunasa ndege za Ukraine usiku kucha, Wizara ya Ulinzi ilisema siku ya Ijumaa.
Wizara hiyo ilisema imeangusha ndege zisizo na rubani katika eneo la kusini mwa Urusi la Krasnodar, ambapo maafisa walisema awali bohari ya mafuta na bandari ilikuwa ikilengwa.
Gavana wa mkoa wa Saratov nchini Urusi alisema kuwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani yameharibu miundo mbinu ya raia, huku mkuu wa mkoa wa Volgograd akisema kuwa ulinzi wa anga umezuia shambulio la usiku kucha la ndege zisizo na rubani kwenye miundombinu ya nishati.
Saa ya dhahabu iliopatikana katika meli ya Titanic kupigwa mnada

Saa ya mfukoni ya dhahabuiliyopatikana kwenye mwili wa mmoja wa abiria tajiri zaidi katika meli ya Titanic iliyozama inatarajiwa kuuzwa mnadani kwa karibu dola milioni 1.3.
Isidor Strauss na mkewe Ida walikuwa miongoni mwa zaidi ya watu 1,500 waliokufa wakati meli ya Titanic ilipozama baada ya kugonga jiwe la barafu mnamo Aprili 14, 1912.
Bw. Strauss alikuwa mfanyabiashara na mwanasiasa wa Marekani aliyezaliwa Bavaria na mmiliki mwenza wa duka kuu la Macy huko New York.
Mwili wake uligunduliwa katika Bahari ya Atlantiki siku chache baada ya meli ya Titanic kuzama, na miongoni mwa mali zake ni saa ya mfukoni ya dhahabu ya karati 18, ambayo itapigwa mnada Novemba 22.
Andrew Aldridge, mkurugenzi wa kampuni ya mnada huko Wiltshire, Uingereza, aliiambia BBC: “Kupitia saa hii, tunasimulia hadithi ya Isidor. Ni kumbukumbu nzuri sana… Walikuwa wanandoa mashuhuri sana wa New York. Kila mtu anawajua kuanzia kwa filamu ya Titanic iliyoandikwa na kuelekezwa na James Cameron, katika tukio ambapo wanandoa wazee wanakumbatiana wakati meli inazama. Walikuwa ni Isidor na Ida.”
Usiku wa kuzama kwa meli ya Titanic, inaaminika kuwa mke wake aliyejitolea alikataa kuingia kwenye mashua ya kuokoa maisha kwa sababu hakutaka kumwacha mumewe, akisema afadhali afe karibu naye. Mwili wa Ida haukupatikana.
Saa hii ya mfukoni ilisimama saa 02:20, wakati meli ya Titanic ilipotea chini ya mawimbi.
Wanajeshi wa Libya wasambaza mafuta kwa kikosi cha RSF nchini Sudan – The Sentry

Kikundi cha uratibu chenye makao yake Marekani kinasema kwamba wanajeshi wanaomuunga mkono kamanda wa Libya, Khalifa Haftar, wamekuwa wakisambaza mafuta kwa Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) nchini Sudan kwa niaba ya Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).
Kundi hilo, lijulikanalo kama The Sentry, linasema Haftar amekuwa msambazaji muhimu wa mafuta na silaha kwa RSF wakati wote wa vita.
Kamanda huyo wa Libya ameshtumiwa mara si moja kwa kusambaza silaha na mafuta kwa kikosi cha RSF kwa niaba ya falme za kiarabu, madai ambayo amekanusha.
Falme za kiarabu pia imekanusha kuhusika na vita vinavyoendelea Sudan.
Ripoti ya The Sentry inasema kuwa, hatua ya Haftar kuwapa mafuta kikosi cha RSF, kumewasaidia kudhibiti eneo la Darfur ambayo sasa ni ngome yao kuu.
Eneo zima la Darfur magharibi mwa Sudan, linapakana na Libya pamoja na Chad, na liko chini ya udhibiti wa RSF ambao waliuteka mji wa mwisho wa El-Fasher ambao ulikuwa unadhibitiwa na jeshi la Sudan.
Ripoti ya Umoja wa mataifa, imeishtumu falme za kiarabu kwa kuipa RSF silaha na ndege za kivita zisizo na rubani.
Jeshi la Sudan, pia limeshtumu Falme za Kiarabu kwa kuwatuma mamluki kutoka Colombia kupitia mataifa jirani kupigana vita vinavyoendelea nchini humo.
Mshauri wa Rais wa Falme za Kiarabu (UAE), Anwar Gargash, alilaani ukatili unaoendelea mjini El-Fasher na kupinga vikali kile alichokiita “habari za uongo” kuhusu Falme za Kiarabu kuhusika na vita vinavyoendelea Sudan.
Libya imegawanyika kati ya serikali inayotambuliwa na Umoja wa Mataifa mjini Tripoli, inayoongozwa na Waziri Mkuu Abdulhamid Dbeibah, na utawala wa Haftar ulioko mashariki mwa nchi hiyo.
Taifa hilo la kaskazini mwa Afrika, limegawanyika tangu mapinduzi yaliyotokea mwaka wa 2011, yaliyomuondoa madarakani kiongozi wa muda mrefu wa taifa hilo Muammar Gaddafi.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.