Mkutano wa hali ya hewa wa COP30 unaanza huku ukiwa hauna malengo mahususi

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Na : Cantona Joseph|RFA

.

Mkutano wa COP30 unafunguliwa leo Jumatatu huku zaidi ya nchi 190 zikishiriki, lakini haijafahamika wazi ni nini hasa wangejadili wakati wa mkutano wa kilele wa wiki mbili wa Umoja wa Mataifa katika mji wa Amazon wa Belem nchini Brazili.

Pia haijulikani ni jinsi gani watashughulikia masuala ambayo yamekuwa kama majaribu, kama vile ahadi ya 2023 ya kuondoa vyanzo vya nishati vinavyochafua mazingira na mahitaji ya ufadhili kuwezesha hilo kufanyika.

Nchi kama vile Brazili wamependekeza kuwa nchi zilenge juhudi ndogo ambazo hazihitaji makubaliano, baada ya miaka mingi ya mikutano ya COP ambayo imesherehekea kuwa na ahadi chungu nzima lakini nyingi zikiishia bila kutekelezwa.

“Ninachopendelea sio kuwa uamuzi wa COP,” Rais wa COP30 Andre Correa do Lago alisema katika mahojiano na Reuters na vyombo vingine vya habari. “Ikiwa nchi zina hamu kubwa ya uamuzi wa COP, bila shaka tutalifikiria suala hilo na kulishughulikia.”

Do Lago alibainisha kuongezeka kwa umuhimu wa China katika mazungumzo hayo, huku Marekani ikiahidi kujiondoa kwenye Mkataba wa Paris mwezi Januari na Umoja wa Ulaya nao ukijitahidi kudumisha azma yake huku kukiwa na wasiwasi juu ya usalama wa nishati.

Mamia wajitokeza kwa maandamano ya kupinga uchafuzi wa mazingira India

.

Mamia ya watu mjini Delhi waliingia mitaani siku ya Jumapili kupinga uchafuzi wa mazingira huku ubora wa hewa ukiendelea kuzorota katika mji mkuu wa India na maeneo jirani.

Watu wa rika zote wakiwemo watoto walishika mabango na kupiga kelele wakiitaka serikali kuchukua hatua kukabiliana na uchafuzi wa mazingira.

Takriban watu 80 walizuiliwa kwa muda mfupi na polisi, ambao walisema waandamanaji hawakuwa na kibali cha kukusanyika katika eneo husika ambalo ni kitovu cha jiji hilo.

Ingawa uchafuzi wa hewa ni tatizo la mara kwa mara kaskazini mwa India, hasa katika majira ya baridi, haya yalikuwa maandamano makubwa ya kwanza kuhusu suala hilo kwa muda mrefu.

“Mapafu yetu yanaharibika. Serikali inapaswa kutangaza kuwa ni dharura ya kiafya hadi watakapopata suluhu,” mwandamanaji mmoja aliambia shirika la habari la PTI.

Ubora wa hewa mjini Delhi na vitongoji vyake ni duni kwa kiasi cha mwaka mzima kutokana na utoaji wa moshi wa magari, vumbi na vichafuzi vya viwandani.

Lakini tatizo huwa mbaya zaidi wakati wa majira ya baridi kali kwa sababu ya wakulima kuchoma makapi ya mazao katika majimbo jirani, pamoja na kasi ya chini ya upepo kunasa vichafuzi karibu na ardhi.

Kesi ya Lissu yaahirishwa sababu za kiusalama – Mwanasheria

s

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa chama kikuu cha upinzani nchini Tanzania, (CHADEMA), Tundu Lissu, ambayo ilitarajiwa kuendelea leo Jumatatu, Novemba 10, 2025, imeahirishwa hadi Jumatano ya Novemba 12, ambapo itatajwa tena mahakamani.

Awali, upande wa Jamhuri ulipanga kuwasilisha shahidi wa nne katika kesi hiyo, lakini hilo halikuwezekana kutokana na hali ya sintofahamu iliyoibuka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania kufuatia maandamano ya siku tatu yaliyoanza Oktoba 29, 2025. Mashahidi wanaotoka mikoa ya Ruvuma na Mbeya wameshindwa kusafiri kufika jijini kutokana na changamoto hizo za kiusalama.

Kwa mujibu wa maelezo ya upande wa mashtaka, hali hiyo imeathiri mchakato wa mashahidi kufika, na hivyo kufanya kesi ishindwe kuendelea kama ilivyopangwa. Wakili wa Serikali Mkuu, Thawabu Issa, aliieleza Mahakama kuwa ombi la kuahirisha linatolewa chini ya kifungu cha 302(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Sura ya 20 (Toleo la 2023), akibainisha kuwa mashahidi wameshindwa kufika kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wao.

Kwa upande wa Jamhuri uliomba kesi iahirishwe kwa siku 14, Jaji Danstan Ndunguru aliamua ihahirishwe kwa siku mbili na kwamba shauri hilo litaendelea Jumatano ijayo badala ya muda huo mrefu uliotakiwa.

Wakili wa Lissu, Rugemeleza Nshalla, aliyeeleza kuhusu kuhairishwa kwa sababu ya usalama amesema wao wameweza kufika Mahakamani maana yake hali inaruhusu wengine kufika Mahakamani.

“Na tunafahamu kuwa mashahidi wengine ni wale wa kufichwa hata sijui usalama wao unahatarishwa vipi”, alihoji Nshalla na kuongeza, “Bahati mbaya mwenyekiti anajiwakilisha mwenyewe, hivyo hakuweza kuzungumza, tunatumaini kwamba umma ungependa kujua nini kinaendelea”.

Hata hivyo mwishoni mwa wiki, Makamu wa Rais, Dk Emmanuel Nchimbi, akizungumza kwenye mkutano wa nchi wanachama ya Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kwamba hali ya nchi iko shwari.

“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imechukua hatua za kurejesha utengemano katika nchi yetu ambao sasa nchi yetu (hali) ni shwari, na kila mtu anafuata utawala wa sheria”, alisema Dk Nchimbi.

Indonesia yamtaja dikteta wa zamani Suharto ‘shujaa wa taifa’

.

Indonesia imemtaja rais wa zamani Suharto kuwa shujaa wa taifa, hata ingawa utawala wa udikteta umezusha maandamano makali kupinga hatua hiyo.

Wakati wa utawala wa Suharto katika miaka ya 1960 hadi 1990, Indonesia ilishuhudia enzi ya ukuaji wa haraka wa uchumi lakini pia ukandamizaji mkali wa kisiasa.

Mamia ya maelfu ya wapinzani wa kisiasa walisemekana kuuawa katika kipindi hicho.

Tuzo la shujaa wa kitaifa ni jambo la kila mwaka, linalokusudiwa kuwaheshimu watu binafsi kwa michango yao kwa nchi.

Siku ya Jumatatu, marehemu Suharto alikuwa miongoni mwa majina 10 mapya yaliyoongezwa kwenye orodha hiyo, katika hafla iliyoongozwa na rais wa sasa wa Indonesia Prabowo Subianto, mkwe wa zamani wa Suharto.

Muingereza afariki baada ya kupigwa risasi wakati wa tukio la wizi nchini Ghana

.

Mwanamume mmoja raia wa Uingereza amefariki baada ya kupigwa risasi wakati wa wizi nchini Ghana siku ya Ijumaa, polisi wanasema.

Ashraf Qarmar Parvez, 68, alipigwa risasi baada ya kujaribu kuzuia jaribio la kuiba simu yake katika eneo la kunywa pombe huko Tema, mji ulio mashariki mwa mji mkuu wa Ghana, Accra. Baadaye alifariki hospitalini, polisi walisema.

Mamlaka nchini Ghana inamsaka mshambuliaji – mmoja wa kundi la washukiwa sita ambao wanasema walikuwa katika eneo la tukio na walitoroka kwa pikipiki.

Ofisi ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema ilikuwa ikisaidia familia ya mtu aliyefariki.

Israel yapokea maiti ya mwanajeshi aliyeuawa Gaza mwaka 2014

.
Maelezo ya picha,Mwanajeshi wa IDF Hadar Goldin aliuawa huko Gaza mnamo mwaka 2014

Israel imepokea mwili wa Lt Hadar Goldin, mwanajeshi aliyeuawa na Hamas mwaka 2014 na ambaye mwili wake umeshikiliwa huko Gaza tangu wakati huo.

Jeshi la Israel lilisema Lt Goldin, ambaye alikuwa na umri wa miaka 23 alipofariki, alitambuliwa rasmi na sasa atazikwa. Aliacha wazazi, dada, kaka wawili, na mchumba.

Mrengo wa kijeshi wa Hamas ulisema Jumapili kwamba utakabidhi mwili wa Lt Goldin kama sehemu ya makubaliano ya kusitisha mapigano.

Hamas sasa imewarudisha mateka wote 20 walio hai, na mateka 24 kati ya 28 waliofariki chini ya awamu ya kwanza ya mpango huo.

RSF inaondoa miili kuficha madai ya ukatili dhidi ya raia – Jumuiya ya madaktari wa Sudan

,

Jumuiya ya madaktari wa Sudan imeshutumu vikosi vya Rapid Support Forces (RSF) kwa kuondoa mamia ya miili kutoka mitaa ya El Fasher huko Darfur kuficha madai ya ukatili dhidi ya raia.

Mtandao wa Madaktari wa Sudan ulisema katika taarifa Jumapili, kuwa maiti kadhaa zilizikwa kwenye makaburi ya halaiki.

Mtandao huo ulisema mazishi hayo ni “mauaji ya halaiki” na “ukiukaji wa kanuni zote za kimataifa na za kidini ambazo zinahakikishia wafu haki ya mazishi yenye heshima,” taarifa ilisema.

Taarifa hiyo imeendelea kueleza kuwa hali katika eneo la Al Fasher ni ” zaidi ya janga la kibinadamu” yenye kulenga maisha ya mwanadamu huku kukiwa na “ukimya wa kutisha wa kimataifa”.

Mnamo Oktoba 26, RSF ilichukua udhibiti wa eneo la Al Fasher, mji mkuu wa Darfur ya Kaskazini, na kufanya mauaji, kulingana na mashirika ya ndani na ya kimataifa.

Tangu Aprili 15, 2023, Jeshi la Sudan na RSF wmekuwa katika vita ambavyo upatanishi wa kikanda na kimataifa umeshindwa kuvimaliza.

Mzozo huo umewauwa maelfu ya watu na kuhamishwa kwa mamilioni ya wengine.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment