Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na: Cantona Joseph|RFA

Shughuli za Bunge jipya la Kumi na tatu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zinatarajiwa kuanza rasmi tarehe 11 Novemba 2025 mjini Dodoma, kufuatia tangazo lililotolewa na Katibu wa Bunge, Baraka Leonard.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kikao cha kwanza cha mkutano wa kwanza wa Bunge jipya kitafanyika kuanzia tarehe 11 hadi 14 Novemba 2025.
Tangazo hilo limefuatia wito wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania uliotolewa kupitia Gazeti la Serikali, toleo maalum namba
11, la tarehe 4 Novemba 2025.
Kikao hicho cha kwanza kinatarajiwa kushuhudia shughuli muhimu kadhaa, zikiwemo: Kusomwa kwa tangazo la Rais la kuitisha Bunge, uchaguzi wa Spika na Naibu Spika, kiapo cha uaminifu kwa wabunge wote, kuthibitishwa kwa uteuzi wa Waziri Mkuu, na ufunguzi rasmi wa Bunge jipya utakaoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ufunguzi wa Bunge jipya utakuwa ni tukio muhimu litakaloweka msingi wa kazi za Bunge la kumi na tatu, likihusisha wabunge wapya na wale waliorejea, huku macho ya Watanzania yakielekezwa Dodoma kuona sura mpya za uongozi wa chombo hicho cha kutunga sheria.
Chama cha mapinduzi,CCM kimeendelea kutawala bunge kikipata ushindi wa zaidi ya 90% ya wabunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Takriban watu saba wafariki baada ya ndege ya mizigo kuanguka huko Kentucky

Takriban watu saba wameuawa wakati ndege ya mizigo ya UPS ilipoanguka ilipokuwa ikipaa kutoka uwanja wa ndege wa Louisville, Kentucky Jumanne jioni, gavana wa jimbo hilo alisema.
Andy Beshear alisema wafanyakazi watatu wa ndege hiyo huenda wakawa miongoni mwa waliofariki baada ya ndege hiyo ya mizigo kulipuka ilipokuwa ikiondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Louisville Muhammad Ali mwendo wa saa 17:15 kwa saa za eneo (22:15 GMT).
Takriban watu wengine 11 wamejeruhiwa wakati ndege hiyo ilipoanguka na kusababisha moshi mwingi angani.
Maafisa wameonya kuwa watu wamepata majeraha “makubwa” katika tukio hilo na kuwa idadi ya vifo inaweza kuongezeka.
Mwanasheria mkuu wa serikali ya Tanzania aapishwa rasmi

Mwanasheria mkuu wa Tanzania Hamza Johari amekula kiapo cha kazi Jumatano ya tarehe 05/11/2025 katika ikulu ya Chamwino Dodoma.
Hamza Said Johari aliteuliwa siku ya Jumatatu na Rais Samia Suluhu baada ya kuingia ikulu kwa muhula wa pili utakaokamilika 2030.
Viongozi mbalimbali wamehudhuria hafla hiyo ya uapisho wa mwanasheria mkuu wakiongozwa na Rais Samia Suluhu.
Aliyeongoza uapisho huo ni Jaji mkuu George Mcheche Masaju.
Mwanasheria mkuu huyu pia alikuwa katika wadhifa huo muhula uliopita wa Rais Samia.
Kabla ya kuwa Mwanasheria mkuu wa serikali ya muungano wa Jamhuri ya Tanzania alikuwa mkurugenzi mtendaji wa mamlaka ya usafiri wa anga Tanzania.
Kwa mujibu wa Ibara ya 112(1)(b), Mwanasheria Mkuu wa Serikali atakuwa Mjumbe wa Tume ya Utumishi wa Mahakama kati ya Wajumbe Sita.
Vikosi vya usalama vyaendelea kushika doria, huku shughuli za kawaida zikianza kurejea Tanzania

Kufuatia siku kadhaa za machafuko katika miji mbalimbali nchini Tanzania, maisha yameonekana kurudi kawaida lakini vikosi vya usalama vimeonekana vikishika doria katika maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam.
BBC imeshuhudia maafisa wa polisi na wanajeshi wakiwa katika vituo vya mwendekasi, ofisi ya serikali na maeneo ya biashara kama vituo vya kujaza mafuta wakiwa na silaha pamoja na magari.
Hali hii inafuatia vurugu zilizotokea kuanzia Jumatano ya tarehe 29, siku ambayo Tanzania iliingia kufanya uchaguzi mkuu wa kumchagua rais, wabunge na madiwani.
Kwa mujibu wa mashirika ya haki za binadamu yanaeleza kuwa mamia ya watu wameuwawa katika vurugu hizo, huku serikali ya Tanzania ikikiri kutokea kwa vurugu lakini bado haijatoa idadi kamili ya waliouwawa.
60 wafariki dunia baada ya tufani kuharibu maeneo nchini Ufilipino

Angalau watu 66 wamefariki dunia, huku mamia ya maelfu wakikimbia makazi yao, baada ya moja ya tufani zenye nguvu zaidi mwaka huu kupita katikati ya Ufilipino, kwa mujibu wa mamlaka.
Tufani Kalmaegi imeathiri miji yote kwenye kisiwa cha kati chenye idadi kubwa ya watu, Cebu, ambapo watu 49 walifariki.
Wengine 26 bado hawajulikani walipo, alisema afisa wa ulinzi wa kiraia katika mahojiano ya redio Jumatano.
Video zinaonyesha watu wakiokolewa kwenye paa za majengo, huku magari na kontena za mizigo zikisogea barabarani kwa nguvu za tufani.
Idadi rasmi ya vifo inajumuisha wanajeshi sita wa helikopta ya kijeshi iliyoanguka kwenye kisiwa cha Mindanao, kusini mwa Cebu, baada ya kutumwa kusaidia jitihada za msaada.
Helikopta hiyo ilianguka Jumanne karibu na Agusan del Sur, ikiwa moja kati ya nne zilizotumwa kusaidia.
“Mawasiliano na helikopta yalipotea, jambo ambalo lilisababisha mara moja kuanzishwa kwa operesheni ya uokoaji,” alisema Jeshi la Anga la Ufilipino.
Baadaye, msemaji alisema miili sita ilipatikana, ikidhaniwa kuwa ni ya rubani na wafanyakazi wake.
Tufani, inayojulikana hapa kama Tino, imepungua nguvu tangu ilipopiga kisiwa mapema Jumanne, lakini bado inapeleka upepo wenye kasi ya zaidi ya 80 mph (130 km/h).
Inakadiriwa itapita katika kisiwa cha Visayas na kuingia kwenye Bahari ya China Kusini ifikapo Jumatano.
Rafaelito Alejandro, naibu msimamizi wa Ofisi ya Ulinzi wa Kiraia, alitoa idadi iliyosasishwa ya vifo katika mahojiano na kituo cha redio cha DZMM Jumatano.
Waokoaji wanasubiri anga kutulia kabla ya kusambaza msaada.
Alisema: “Changamoto ni mabaki na magari barabarani. Kuna mengi ya kusafisha.” Carlos Jose Lañas, muokoaji wa hiari, aliambia BBC kwamba licha ya kujiandaa kwa hali mbaya zaidi, walishangazwa na ukubwa wa mafuriko.
“Hii ndiyo mafuriko mabaya zaidi niliyowahi kuyapata,” alisema kijana huyo wa miaka 19.
“Karibu mito yote hapa Cebu imevunja kingo. Hata wahudumu wa dharura hawakutarajia hali kama hii.”
Israel yathibitisha mwili uliorudishwa na Hamas ni wa mmoja wa mateka wao

Israel imethibitisha Jumatano ya 05/11/2025 kuwa mwili uliokabidhwa na Hamas Jumanne ni wa Sajenti Itai Chen, mateka Muisraeli-Mmarekani aliyotekwa Oktoba 7, 2023.
Hamas iliukabidhi mwili kwa shirika la msalaba mwekundu baada ya operesheni ya utafutaji katika mtaa wa Shuja’iyya.
Al-Qassam alisema mwili ulipatikana ndani ya mstari njano, maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa Israeli.
Chanzo cha Hamas kiliambia AFP kuwa miili mingine ya mashahidi wa Palestina pia ilipatikana chini ya mabaki ya majengo.
Hadi sasa, miili 21 imekabidhiwa huku 7 ya askari bado yapo katika eneo hilo.
BBC imefahamu kuwa Marekani ilisambaza, siku ya Jumatatu, kwa idadi ya wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, rasimu ya azimio linalotaka kuanzishwa kwa kikosi cha kimataifa katika Ukanda wa Gaza, na mamlaka ya kuongezwa kwa muda usiopungua miaka miwili.
Mradi huo, ambao wanadiplomasia waliozungumza na BBC waliuelezea kuwa “nyeti lakini sio siri,” unafungua mlango kwa majadiliano muhimu kuhusu usimamizi na usalama wa siku zijazo wa sekta hiyo baada ya vita.
Rasimu hiyo inaonesha kuwa Marekani itaongoza katika awamu ya kwanza kikosi hicho kitakachojulikana kama ISF (“International Security Force”) , ambapo shughuli zitasimamiwa kwa ushirikiano na nchi nyingine na mashirika ya kimataifa.
Kikosi hicho kinalenga kulinda mipaka ya Gaza na Israel na Misri, kulinda raia na korido za kibinadamu, kutoa mafunzo kwa kikosi kipya cha polisi cha Palestina, pamoja na kuwapokonya silaha makundi yenye silaha na kuzuia kujengwa upya kwa miundombinu yao ya kijeshi.
Katika maendeleo mengine, Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, aliomba kumalizika mapema kwa kesi yake ya ufisadi kutokana na mkutano wa dharura wa kidiplomasia na Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa wa Marekani, Tulsi Gabbard, anayemtembelea Israel.
Netanyahu amelalamika kuwa kesi hiyo inayodumu tangu 2020 inamkosesha uwezo wa kutekeleza majukumu yake kama waziri mkuu.
Zohran Mamdani ashinda kinyang’anyiro cha umeya wa New York

Zohran Mamdani, mwenye umri wa miaka 34, sasa ndiye Meya mpya wa Jiji la New York na Meya wa kwanza Muislamu wa jiji kubwa zaidi nchini Marekani.
Hii ni baada ya uchaguzi kukamilika.
Mamdani, anayejitambulisha kama msoshalisti wa kidemokrasia, alikuwa hajulikani sana miezi michache iliyopita.
Hata hivyo, amepata ushindi mkubwa kupitia kampeni zilizoahidi kutoza kodi zaidi kwa mamilionea ili kufadhili mipango mipya ya kijamii.
Meya mteule wa New York, Zohran Mamdani, ameibuka jukwaani akipunga mkono na kutabasamu huku umati mkubwa ukishangilia kwa sauti na kupaza jina lake, “Zohran! Zohran!”
Akiwahutubia wafuasi wake waliokuwa wamefurika kusherehekea ushindi huo, Mamdani alisema kuwa leo inaashiria mwanzo wa siku mpya yenye matumaini kwa binadamu wote.
“Kwa muda mrefu, wafanyakazi wa New York wameambiwa na matajiri na wenye ushawishi kwamba madaraka si yao,” alisema Mamdani.
“Lakini katika kipindi cha miezi kumi na miwili iliyopita, mmeonyesha ujasiri wa kutafuta kitu kikubwa zaidi. Usiku huu, kinyume na matarajio yote, tumekipata.”
Akaongeza kwa kusema, “Mustakabali uko mikononi mwetu,” huku umati ukishangilia kwa nguvu.
Ingawa hotuba yake ilijikita zaidi katika kuelezea maono yake kwa jiji la New York, haikuchukua muda kabla ya kumjibu mkosoaji wake mkubwa, Rais wa Marekani Donald Trump.
“Donald Trump, najua unatazama,” alisema kwa ucheshi. “Nina maneno manne kwako: ongeza sauti.”
Kwa ishara hiyo, umati ulilipuka kwa kelele kubwa zaidi. Mamdani aliendelea kumkabili moja kwa moja Trump kwa kusema: “Ili umfikie yeyote kati yetu, italazimu upitie kwetu sote.”
Wakati Mamdani akiendelea na hotuba yake, Trump aliandika katika ukurasa wake wa Truth Social: “… NA HIVYO NDIVYO INAVYOANZA!”
Rais wa Marekani Trump alikuwa ametishia kukata ufadhili wa serikali kuu kwa Jiji la New York iwapo Mamdani angeshinda dhidi ya Andrew Cuomo (mwaniaji huru) na Curtis Sliwa (Mrepublican).
Wakati huo huo, chama cha Democrat kinatarajiwa pia kushinda uchaguzi wa ugavana katika majimbo ya Virginia na New Jersey.
Aidha, wapiga kura wa California wamepitisha uamuzi wa kubadilisha mipaka ya majimbo ya uchaguzi ili kuimarisha nafasi ya chama cha Democrat kuelekea uchaguzi wa mwaka huu.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.