Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na: Cantona Joseph|RFA

Mwenyekiti wa INEC amesema kwamba kulingana na Katiba ya Tanzania mshindi anahitaji tu kuwa na kura nyingi kuliko washindani wengine.
Matokeo ya uchaguzi wa Tanzania 2025: Watanzania mpakani Namanga wanasema nini?
Raia wa Tanzania wanaoishi katika mpaka wa Namanga wametoa hisia za mchanganyiko kuhusu ushindi wa Samia Suluhu Hassan katika uchaguzi mkuu wa Tanzania.
Namanga ni moja ya sehemu zilizoshuhudia vurugu la maandamano ya kupinga uchaguzi mkuu Tanzania
Hawa hapa chini ni baadhi yao.
CHARLES MASAI, Dereva wa malori ya uchukuzi, Namanga
”Ni bora tuunge mkono matokeo ya uchaguzi ili maisha yaendelee hata kama uchaguzi huo ulikuwa na utata. Kama vyama vyote vingeshiriki, ingekuwa vizuri zaidi.”
MZEE MADIKO, Fundi wa magari Namanga
”Familia yake inateseka sana kufuatia virugu hizi, Badala ya vurugu, hebu Mama aapishwe. Kwa nini? Kwa sababu mimi ni mzazi. Je, unapenda vita? Je, unapenda kulala nje? Je, unataka askari watawale nchi yetu ya Tanzania? Tunaomba Mama aapishwe ili tupate amani hiyo.”
HUSSEIN JAFFAR
”Nimepokea matokeo ya uchaguzi kwa masikitiko. Hakukuwa na upinzani wa kweli, Sio mimi tu niliyekasirishwa na matukio ya ukandamizaji wa upinzani kuelekea uchaguzi mkuu — watu wengi hawalitaki.”
INEC ilindesha vyema uchaguzi – Jumuiya ya uangalizi wa uchaguzi wa EAC
Mkuu wa ujumbe wa uangalizi wa uchaguzi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dk. Speciosa Wandira Kazibwe amesema Tume Huru ya uchaguzi ya Tanzania INEC imeendesha vyema mchakato wa uchaguzi kuanzia mwanzo hadi mwisho.
”Tumekuja hapa na kushuhudia jinsi mnavyosimamia uchaguzi huu na tumejiridhisha kwamba utaratibu wote ulifuatwa,”Dkt Wandira alisema.
Pia aliongeza kwamba walikutana na wagombea wote waliowania urais na wameufahamisha ujumbe huo kupitia wawakilishi wao kwamba wanafahamu kilichofanyika wakati wa uchaguzi na wamekubaliana na matokeo ya uchaguzi huo.
Akihutubia hafla ya INEC ya kumkabidhi chetu mshini wa uchaguzi huo Rais Mteule Samia Suluhu Hassan, Dkt Wandira aliitaja Tanzania kama mfano wa kuigwa katika eneo la Afrika Mashariki kwa kuendesha mchakato huo kwa njia ya amani.
Samia akabidhiwa cheti cha cha ushindi katika makao makuu ya INEC

Rais Samia Suluhu Hassan akabidhiwa cheti cha ushindi wa uchaguzi wa 2025 na Tume Huru ya Taifa nchini Tanzania (INEC) uliofanyika tarehe 29/10/2025.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mwenyekiti wa INEC amesema kwamba kulingana na Katiba ya Tanzania mshindi anahitaji tu kuwa na kura nyingi kuliko washindani wengine.
INEC ikitangaza mshindi mtokeo hayawezi kubatilishwa ama mahakamani au kupitia mahakama ya utatuzi wa mizozo ya INEC.

Rais Samia alipata ushindi kwa kupata kura 31,913,866 kati ya 32,678,844 zilizopigwa.
Watanzania waliojeruhiwa katika maandamano watibiwa Kenya

Hospitali tafauti nchini Kenya zimeanza kuwapokea raia wa Tanzania waliojeruhiwa katika maandamano, hususan katika miji ya mpakani ya Isebania – Sirari,
Kufikia Ijumaa tarehe 31 Oktoba, takriban raia 25 wa Tanzania waliovuka mpaka na kuingia Kenya walikuwa wametibiwa katika hospitali tofauti za Kaunti ya Migori magharibi mwa nchi hiyo.
Kwa mujibu wa gazeti la The Standard, taarifa kutoka Kituo cha Polisi cha Isebania inaonyesha kuwa waathiriwa hao waliingia nchini kupitia njia zisizo rasmi za mpakani, ambapo sita kati yao walikuwa na majeraha ya risasi.
Hospitali ya BNM iliwahudumia na kuwaachilia wagonjwa wanne waliokuwa na majeraha ya kipigo, huku ikimlaza mgonjwa mmoja aliyepigwa risasi.
Hospitali ya Jamii ya Emalia iliwapokea wagonjwa wawili wenye majeraha ya risasi na kuwapeleka katika Hospitali ya Migori kwa matibabu maalumu.
Hospitali ya Getontira ilipokea wagonjwa sita, watatu wakalazwa na watatu wakapelekwa hospitali nyingine, ilhali Hospitali ya Queen Easter ilimlaza mgonjwa mmoja aliyepigwa risasi ambaye baadaye aliruhusiwa kwenda nyumbani baada ya hali yake kuimarika.
Hospitali ya Bwana Mifupa ilishughulikia visa tisa vya wagonjwa wenye mifupa iliyovunjika, ingawa haikurekodi majeraha yoyote ya risasi.
Maafisa wa afya na usalama katika Kaunti ya Migori wanaendelea kufuatilia kwa karibu hali hiyo, huku kukiwa na hofu kwamba idadi ya majeruhi watakaovuka mpaka huenda ikaongezeka endapo machafuko nchini Tanzania yataendelea.
Dr. Hussein Ali Mwinyi aapishwa kuwa Rais wa Zanzibar kipindi cha Pili

Dr. Hussein Ali Mwinyi ameapishwa kwa Rais wa Zanzibar awamu ya 8 kipindi cha Pili.
Jaji Khamis Ramadhan Abdhallah amemuapisha Hussein Mwinyi kuwa Rais wa Zanzibar.
“Mimi Hussein Ali Mwinyi naapa ya kwamba kwa Jina la Mwenyezi Mungu kwamba nitakuwa muaminifu kwa Zanzibar na kuitumikia kwa moyo wangu wote na kwamba nitaihifadhi, nitailinda, nitaitii na… Katiba ya Zanzibar na Katiba ya Jamhuri wa Muungano wa Tanzania na watu wake kwa mujibu wa sheria iliyowekwa. Nakuomba Mwenyezi Mungu unisaidie.”
Hafla hii ya uapisho inafanywa katika uwanja wa Amaan Complex na imehudhuriwa na viongozi wa kitaifa, mabalozi na viongozi wa kisiasa.
Katibu wa masuala ya nje wa CHADEMA aitaka EAC, SADC, AU kuingilia hali ilivyo Tanzania

Katibu wa masuala ya nje wa chama cha CHADEMA nchini Tanzania Deogratias Munishi, ametoa wito kwa EAC, SADC, AU pamoja na vyombo vingine kuingilia kati hali ilivyo nchini humo.
Katika mahojiano na BBC, Munishi alisema kutangaza matokeo ya uchaguzi kutaongeza ‘ghadhabu’ miongoni mwa wananchi.
Munishi alipoulizwa na mwandishi wa BBC ikiwa CHADEMA imepanga kupinga rasmi matokeo ya uchaguzi, alisema hata kama pengine wangeshiriki uchaguzi, kulingana na ‘mfumo wa uchaguzi nchini, huwezi kupinga matokeo ya uchaguzi yaliotangazwa na Tume katika mahakama yoyote’.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi INEC hapo jana ilikuwa inaendelea na shughuli ya kuhesabu kura huku serikali ikiendelea kusisitiza kuwa usalama umeimarishwa.
Serikali ya Tanzania: Hatuwezi kuthibitisha idadi ya watu waliouawa katika maandamano

Maelezo ya picha,Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania Thabit Kombo amezungumza na BBC kueleza kinachoendelea nchini Tanzania
Serikali ya Tanzania imesema kwamba haiwezi kuthibitisha idadi ya watu waliouawa katika maandamano baada ya uchaguzi uliofanyika Jumatano wiki hii, vurugu za uchaguzi zikiingia siku ya tatu.
‘Kwa sasa hakuna mtu anaweza kusema ni watu wangapi wamefariki au kuumia. Tunaendelea kupokea ripoti kuhusu mali binafsi ya watu iliyoharibiwa, magari, mali ya umma, magari ya TANESCO ambayo ni kampuni yetu ya umeme yalichomwa. Kwa sasa hakuna hesabu kamili, mpaka serikali itakapopokea ripoti kamili na itatoa idadi kamili,’ alisema Mahmoud Thabit.
Baadhi ya makundi ya upinzani yalidai kuwa mamia ya watu waliuawa, huku umoja wa mataifa ukisema kuwa watu kumi wameuawa, madai ambayo Thabit Kombo amekanusha.
Vile vile serikali ya Tanzania imeeleza kuwa hatua za kuminya intaneti hazilengi kuwakandamiza wananchi bali ni za kuwalinda huku wakiwahakikishia huduma za intaneti zitarudi hivi karibuni.
‘Wakati tulipowasha mtandao wa intaneti ilileta shida kwa watu wachache wahuni ambao walikuwa wakitumia mtandao kuleta vurugu. Sasa kwa mujibu wa sheria za mamlaka ya kusimamia mawasiliano Tanzania kuna sheria ambazo zinatumiwa wakati kuna wasiwasi wa usalama wa kitaifa kuhusu mtandao wa intaneti ndani ya nchi. Haya si mambo ya haki au ukosefu wa haki, tunazungumzia maisha ya watu, mali ya watu na usalama wa nchi yetu.’
Akizungumza na BBC, Waziri wa mambo ya kigeni Balozi Mahmoud Thabit Kombo alitetea jinsi serikali ilivyokabiliana na waandamanaji baada ya uchaguzi wa Jumatano wiki hii.
Mwanasiasa wa Upinzani Tanzania adai maisha yake yako hatarini

Mwanasiasa mwandamizi wa chama cha upinzani nchini Tanzania amedai kuwa anahofia maisha yake kufuatia uchaguzi mkuu uliofanyika Jumatano, ambao umeibua utata na tuhuma za ukiukwaji wa haki za binadamu.
Bw. John Kitoka, Mkurugenzi wa Masuala ya Nje na Diaspora wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ameiambia kipindi cha BBC Newshour kwamba kuna taarifa zinazoonyesha kuwa takribani watu 500 wameuawa na maafisa wa polisi pamoja na watu wanaodaiwa kuwa ni mamluki wa kigeni akionya kuwa idadi hiyo huenda ni kubwa zaidi.
Kwa mujibu wa Bw. Kitoka, mauaji hayo yanafanyika nyakati za usiku, wakati hakuna mashuhuda, jambo linalozidisha hofu miongoni mwa wananchi.
“Nina hofu kubwa kwa maisha yangu,” amesema akiwa mafichoni ndani ya nchi. “Wanawafuatilia viongozi wetu mmoja baada ya mwingine; baadhi wamekimbia nchi. Watu hawa wanaua bila hofu wala kuwajibishwa,” ameongeza.
Aidha, amesema kuwa viongozi wakuu wa upinzani walizuiwa kugombea dhidi ya Rais Samia Suluhu Hassan, akieleza kuwa mchakato huo haukustahili kuitwa uchaguzi huru na wa haki, bali “sherehe ya kumtawaza kiongozi mmoja.”
Hadi sasa, mamlaka za serikali hazijatoa tamko rasmi kuhusu tuhuma hizo, huku jumuiya ya kimataifa ikiripotiwa kufuatilia kwa karibu maendeleo ya kisiasa nchini Tanzania kufuatia uchaguzi huo wenye utata.
Bunge la Ulaya laiomba INEC kutotangaza matokeo ya uchaguzi Tanzania

Bunge la Ulaya limetoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi nchini Tanzania INEC kutotangaza matokeo ya uchaguzi hadi pale uchunguzi wa kina utakapofanyika.
Bunge hilo pia limetoa wito kwa Jeshi la taifa hilo la Afrika Mashariki kuwa tu washikilizi wa madaraka iwapo watachukua jukumu la kudhibiti maandamano yanayoendelea nchini humo.
”Iwapo Jeshi la Tanzania litaamua kuchukua hatua yoyote ya udhibiti iwe ni ya kudumisha amani na kuleta utulivu na sio kung’ang’ania mamlaka’, ilisoma taarifa hiyo ya Bunge la Ulaya.
Wakati huo huo,bunge hilo limesema kuwa linawaunga mkono waandamanaji na kuongeza kuwa maandamano hayo ni ya kupigania haki na uwajibikaji na sio vurugu kama inavyotajwa na wengi.
Haya yanajiri baada ya mkuu wa Jeshi la Tanzania Jenerali Jacob Mkunda kulaani vitendo vya vurugu vinavyoendelea kushuhudiwa katika baadhi ya maeneo nchini humo na kuvitaja kuwa kinyume cha sheria.
”Tunashirikiana na vyombo vingine vya usalama kurejesha hali ya utulivu,”alisema Jenerali Mkunda Alhamisi usiku katika taarifa iliyopeperushwa kupitia televisheni ya taifa nchini humo TBC.
Watalii wakwama katika Uwanja wa ndege wa kimataifa wa Zanzibar

Saa chache baada ya Ubalozi wa Marekani kutoa tahadhari kwa raia wake wanaoishi nchini Tanzania na kuwataka wasalie majumbani mwao, watalii waliokuwa wamefika katika Uwanja wa Ndege wa Zanzibar wamekwama kutokana na safari za ndege kusitishwa.
haya yanajiri siku moja baada ya uchaguzi mkuu wenye utata nchini Tanzania, huku kukiripotiwa machafuko na maandamano yenye vurugu katika maeneo ya bara, wakati huduma za intaneti na mawasiliano mengine zikiwa zimekatizwa.
Kupitia taarifa iliotolewa kwenye tovuti ya ubalozi wa Marekani iliwajulisha raia wake kuthibitisha safari zao kwanza kwa njia ya simu kabla ya kusafiri kuelekea uwanja wa ndege kwani safari za ndege nyingi za kimataifa zimefutwa
Aidha, imeongeza kuwa kusafiri kwa barabara kuna hatarisha maisha yao na kuwataka wasalie majumbani mwao na wajiepushe kushiriki maandamano yanayoendelea Tanzania bara.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.