Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na: Cantona Joseph|RFA

Picha: AP Photo/picture alliance
Chama kikuu cha upinzani Tanzania CHADEMA, kimesema takriban watu 700 wameuwawa ndani ya siku tatu za ghasia za baada ya uchaguzi. Hayo yanajiri wakati bado maandamano yakishuhudiwa na mtandao ukiendelea kufungiwa.
Unachohitaji kujua
- Upinzani: Takriban watu 700 wameuawa Tanzania katika ghasia za baada ya uchaguzi
- Tanzania: Jeshi latoa onyo kwa waandamanaji, huku hofu ikiongezeka baada ya uchaguzi
- Dkt. Hussein Ali Mwinyi atangazwa mshindi wa urais Zanzibar
- Matokeo yaendelea kutolewa Tanzania, Samia aongoza
- Wabunge wa Ulaya wasema uchaguzi Tanzania haukuwa wa huru na haki
- Waandamanaji wajadili mbinu za maandamano zaidi Tanzania
Upinzani wasema Takriban watu 700 wameuawa Tanzania
Kulingana na msemaji wa CHADEMAJohn Kitoka, kwa sasa idadi ya waliouwawa mjini Dar es Salaam kutokana na ghasia za baada ya uchaguzi wamefikia 350 na mjini Mwanza 200 wameuawa kufuatia ghasia hizo zilizojitokeza kuanzia Oktoba 29 wakati wa zoezi la uchaguzi.
Akizungumza na shirika la habari la AFP, Kitoka amesema ukimjumlisha vifo vya maeneo mengine nchini humo, idadi ya waliouawa wanafikia 700. Amesema anahofu kuwa idadi hiyo huenda ikawa juu zaidi.
Chanzo cha usalama kimeliambia shirika la AFP kwamba kuna taarifa ya zaidi ya watu 500 waliouwawa nchini humo ndani ya siku tatu za maandamano.
AFP imesema hospitali kadhaa na wahudumu wa afya wanahofu ya kuzungumza na vyombo vya habari kuhusu hali wanayoishuhudia.
Huku hayo yakiarifiwa vyaombo vya habari vya ndani ya Tanzania vimebakia kimya, kuhusu zoezi la uchaguzi, huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa bado hajaonekana hadharani wala kusema chochote tangu alipopiga kura siku ya uchaguzi, Oktoba 29.
Mkuu wa Jeshi la Ulinzi wa Wananchi nchini humo Jenerali Jacob Mkunda alijitokeza hadharani kukosoa maandamano yanayoendelea akiwaita waandamanaji wahalifu, na kuwaonya pia dhidi ya kuendelea kuandamana, akisema jeshi halitasita kuchukua hatua kwa mujibu wa sheria iwapo hali ya vurugu na maandamano itaendelea.
Jeshi la Tanzania latoa onyo kwa waandamanaji, huku hofu ikiongezeka baada ya uchaguzi
Akizungumza mjini Dar es Salaam, Jenerali Mkunda amesema Jeshi la Ulinzi wa Wananchi wa Tanzania (TPDF) halitakaa kimya huku makundi ya waandamanaji yakiingia mitaani, kuvuruga amani na kupinga mchakato halali unaoendelea wa uchaguzi.
Amesisitiza kwamba jeshi, kwa kushirikiana na polisi na vyombo vingine vya usalama, liko tayari kufanya kazi yake kwa kuzingatia sheria ili kurejesha utulivu iwapo machafuko yataendelea. Amesema vitendo vinavyoshuhudiwa kwa sasa ni uhalifu unaopaswa kukomeshwa mara moja.
” Ndugu wananchi, ikumbukwe kuwa nchi yetu inaongozwa kwa misingi ya sheria, ambayo lazima izingatiwe na kuheshimiwa. Kutokana na hali hiyo Jeshi la Ulinzi la wananchi wa Tanzania, linawataka watu wote wanaojishusisha na vitendo vya kihalifu kuacha vitendo hivyo mara moja, ili kuepusha madhara yasiokuwa ya lazima kwa ustawi wa jamii na taifa letu. Endapo vitendo vya uhalifu vitaendelea , jeshi la ulinzi la wananchi wa Tanzania kwa kushirikia ana vyombo vingine vya usalama vitaendelea kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria ,” alisema Jenerali Mkunda.

Kulingana na shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International watu kadhaa wameuwawa na wengine kukamatwa tangu vurugu hizi zilipoanza Oktoba 29.Picha: AP Photo/picture alliance
Onyo hilo linakuja huku umma ukidai kutoridhika na mchakato wa uchaguzi, na kushuhudiwa pia maandamano makubwa ya kupinga uchaguzi huo, yaliyoonekana mjini Dodoma, Arusha na Mwanza. Waandamanaji wanadai uchaguzi ulikuwa na dosari.
Hata hivyo muda mfupi baada ya maandamano kushuhudiwa, utawala nchini Tanzania ulichukua hatua za kudhibiti maandamano hayo ikiwa ni pamoja na kuwarushia waandamanaji mabomu ya kutoa machozi. Risasi za moto pia zinadaiwa kutumika katika juhudi za kuwadhibiti waandamanaji. Kulingana na shirika la Kimataifa la kutetea haki za binaadamu Amnesty International, watu kadhaa wameuwawa na wengine kukamatwa tangu vurugu hizi zilipoanza Oktoba 29.
Serikali bado haijatoa maoni kuhusu idadi ya vifo lakini imesisitiza kuwa uchaguzi uliendeshwa kwa amani na uwazi.
Chama tawala nchini Tanzania (CCM), ambacho kimekuwa madarakani tangu nchi hiyo ilipojinyakulia uhuru wake 1961, kinatarajiwa kuendelea kukita mizizi. Tayari matokeo ya awali yanamuonesha mgombea wake Samia Suluhu Hassan akiongoza kwa asilimia 94 ya kura dhidi ya wapinzani wake 16 anaochuana nao.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.