Uchaguzi mkuu wa Tanzania 2025: Serikali yawaagiza wafanyakazi wa umma kufanyia kazi nyumbani

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

By : Cantona Joseph|RFA

Msemaji wa serikali, Gerson Msigwa, aliweka ujumbe kwenye mtandao wake wa Instagram akielezea tangazo hilo kuwa kufuatia angalizo la kiusalama lililotolewa na jeshi la polisi kwa wakaazi wa jiji la Dar es Salaam watafanyia kazi nyumbani.

“…Kesho tarehe 30 Oktoba 2025, watumishi wote wa umma nchini wafanyiekazi nyumbani isipokuwa wale ambao majukumu yao ya kazi yanawakata kuwepo katika vituo vyao vya kazi kama ambavyo wataelekezwa na waajiri wao.”

Taarifa hiyo pia ilionyesha kuwa waajiri wa sekta binafsi wanashauriwa kuzingatia tahadhari hiyo.

Aidha, iliongeza kuwa wananchi wasio na ulazima wa kutoka nje wanashauriwa kufanya shughuli zao nyumbani.

Hapo jana, 29/10/2025 ilikuwa ni siku ya kupiga kura kuchagua viongozi wao lakini kwa mara ya kwanza katika historia, siku ya uchaguzi ilikumbwa na maandamano katika baadhi ya miji huku waandamanaji waliokuwa wanapinga kufanyika kwa uchaguzi wakifunga barabara kadhaa na kuchoma moto maeneo kadhaa.

Hali ya wasiwasi yaendelea kuripotiwa Tanzania

Hali ya wasiwasi inaendelea kushuhudiwa nchini Tanzania kufuatia maandamano ya ghasia yaliofanyika hapo jana.

Hatahivyo baadhi ya barabara ambazo zilikuwa zimefungwa hapo jana sasa zimefunguliwa.

Baadhi ya raia ambao walikuwa wamekwama kutokana na maandamano yaliosababisha amri ya kutotoka nje kuwekwa hapo jana wamefanikiwa kufika makwao.

Aidha kuna ripoti za maandamano kuzuka katika mji wa kaskazini wa Mwanza na kwamba baadhi ya wakaazi kutoka eneo hilo wanadai kwamba wamekuwa wakisikia milio mikubwa nje ya nyumba zao.

Aidha kuna madai kwamba baadhi ya waandamanaji mjini Dar, Mbeya na Dodoma wamekuwa wakiwashambulia walioshiriki katika shughuli ya kupiga kura hapo jana

Vilevile huku mitandao ikiendelea kuminywa kwa siku ya pili mfululizo ni simu za kawaida pekee zinazotumika kwa mawasiliano.

Uchaguzi mkuu wa Tanzania 2025: Mtandao waendelea kuminywa kwa siku ya pili mfululizo

.

Tanzania inaendelea kushuhudia siku ya pili ya kukatwa kwa mtandao hatua ambayo imefanya mawasiliano kuwa changamoto.

Hapo jana siku ya uchaguzi, shirika la kimataifa la uchunguzi wa mtandao wa Netblocks, lilisema kuwa limegundua kufinywa kwa mtandao kote nchini humo.

“Imethibitishwa: Takwimu za mtandao wa moja kwa moja zinaonyesha usumbufu wa kitaifa kwa kuunganishwa kwa mtandao nchini Tanzania Siku ya Uchaguzi,” Netblocks aliandika katika machapisho kwenye vyombo vya habari vya kijamii.

Tatizo la ukosefu wa mtandao limeathiri pia wafanyabiashara wanaoendesha shughuli zao kwa njia hiyo.

Hata hivyo, hii si mara ya kwanza Tanzania kukutana na tukio kama hili ikikumbukwa pia uchaguzi wa 2020 mtandao wa X ulifungwa.

Wafanyakazi wa serikali ya Marekani Tanzania watakiwa kuchukuwa tahadhari

.

Wafanyakazi wa Serikali ya Marekani wanaoishi nchini Tanzania wameshauriwa kuchukua tahadhari na kujilinda kufuatia ghasia na maandamano yalioripotiwa nchini humo.

Kulingana na taarifa ya ubalozi huo iliotolewa hapo jana tarehe 29 Oktoba, ubalozi huo aidha umesema kwamba shughuli zake hii leo zitakuwa hudumu za dharura pekee na za kibalozi.

Vilevile wafanyakazi hao wametakiwa kuepuka maandamano, mikusanyiko ya watu, kutazama taarifa za vyombo vya habari ili kujua yanayoendelea mbali na kuchukua tahadhari kuu katika maeneo walipo.

Hatua hiyo inajiri kufuatia maandamano yaliofanyika hapo jana wakati ambapo upigaji kura ulikuwa ukiendelea.

Raia wa Tanzania hapo jana walipiga kura kumchagua rais wabunge na madiwani licha ya maandamano hayo yaliofanywa na vijana.

Wafanyabiashara wakadiria hasara kubwa kufuatia maandamano Jijini Dar es Salaam

.

Wafanyabiashara jijini Dar es Salaam wanakadiria hasara ya mamilioni ya pesa kufuatia maandamano ya siku ya uchaguzi yaliyogeuka kuwa ya vurugu kufanyika jana, Jumatano, katika jiji hilo na maeneo mengine nchini Tanzania.

Kilichoanza kama wito wa kudai haki kimegeuka kuwa chanzo cha hasara kubwa kwa wafanyabiashara ambao sasa wanasema hawajui pa kuanzia.

Mfanyabiashara Paul Boniface, kupitia ukurasa wake wa mitandao ya kijamii, alieleza kusikitishwa na hatua ya serikali kudhibiti huduma za intaneti kufuatia machafuko hayo, akisema hali hiyo imeathiri shughuli za biashara zinazotegemea mtandao.

“Natumia VPN kwa sababu intaneti imezimwa. Hili limeathiri sana mfumo wetu wa utendaji. Kwa sasa kazi zimesimama kabisa kutokana na ukosefu wa intaneti imara,” alisema Boniface.

Baadhi ya biashara za wasanii wa Tanzania pia zimeharibiwa na kuteketezwa usiku wa kuamkia leo.

Raia wa Tanzania wamelaumu wasanii walioonekana kumuunga mkono Rais Samiya wakieleza walifumbia macho yaliyokuwa yakiendelea nchini humo.

Vurugu hizo zimesababisha uharibifu wa mali ikiwemo kuvunjwa kwa vioo vya maduka, kuchomwa kwa sehemu ya ukuta wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mjini Arusha, pamoja na kuharibiwa kwa vituo vya mabasi ya mwendokasi, vituo vya kupigia kura, mabasi, na maeneo ya biashara.

Maeneo yaliyoathirika zaidina maandamano hayo ni Kimara, Magomeni, Ubungo, Kinondoni, Shekilango, na Tandale.

Vituo kadhaa vya polisi pia vimeripotiwa kushambuliwa katika purukushani hizo.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuimarisha ushawishi wake wa kisiasa nchini, huku hali ya kisiasa ikizidi kuwa na mvutano mkubwa baada ya kuondolewa kwa wapinzani kadhaa katika kinyang’anyiro cha urais.

‘Vijana wa Afrika wanaongea, ni wakati wa watawala kuwasikiliza’ – Bobi Wine

.

Mwanasiasa mashuhuri wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, ametangaza kuunga mkono raia wa Tanzania wanaoandamana kupinga kile wanachokiita udhalimu wa uchaguzi na ukosefu wa uwajibikaji wa viongozi.

Kupitia ukurasa wake katika mtandao wa kijamii X ambao zamani ulijulikana kama (Twitter), Bobi Wine, ambaye ni mpinzani wa Rais wa Uganda Yoweri Kaguta Museveni, alisema anasimama bega kwa bega na kiongozi mkuu wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, ambaye anadaiwa kushikiliwa tangu mwezi Aprili kwa tuhuma za uhaini.

Bobi Wine amewataka pia viongozi wa kikanda kusikiliza matakwa ya vijana wa kizazi cha Gen Z, ambao wamekuwa wakitumia haki yao ya kikatiba kuandamana wakidai mabadiliko ya kisiasa na utawala wa haki.

Maandamano hayo yanafanyika sambamba na uchaguzi mkuu wa kuchagua wabunge, madiwani, na rais wa muungano.

Rais Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kushinda katika uchaguzi wa mwaka 2025, ambao umeibua mjadala kutokana na madai ya kuenguliwa kwa baadhi ya wapinzani wakuu waliotarajiwa kushiriki katika kinyang’anyiro hicho.

Kiti cha urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kimevutia wagombea 17, wakiwemo watatu wanawake, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa ushiriki wa wanawake katika siasa za kitaifa.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment