Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na: Cantona Joseph|RFA

Vikosi vya Marekani vimewauwa watu 14 katika mashambulizi dhidi ya boti nne zinazodaiwa kuwa za madawa ya kulevya katika Bahari ya Pasifiki, amesema Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth.
Jeshi la wanamaji la Mexico linasema linamtafuta mtu mmoja aliyenusurika takribani maili 400 (643km) kutoka mji wa pwani ya Pasifiki wa Acapulco.
Hili ni shambulio la hivi punde zaidi katika mfululizo wa mashambulizi dhidi ya boti ambazo Marekani inasema zinabeba dawa za kulevya katika Pasifiki na Caribbean.
Mashambulizi hayo, ambayo Hegseth anasema yalitokea Jumatatu kwa maagizo ya Rais Donald Trump, yanaashiria kuongezeka kwa kile inachokitaja kama kampeni ya kukomesha mihadarati kuingia Marekani.
Mashambulizi hayo yamelaaniwa na wataalam wametilia shaka uhalali wake. Wajumbe wa Bunge la Congress la Marekani, Democrats na Republicans pia wameibua wasiwasi na kutilia shaka mamlaka ya rais ya kuamuru mashambuliz hayo.
Rais wa Mexico Claudia Sheinbaum aliuambia mkutano wake na waandishi wa habari “hatukubaliani na mashambulizi haya.”
Alisema alimwomba waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo, pamoja na wawakilishi wa jeshi la wanamaji, kukutana na balozi wa Marekani.
“Tunataka mikataba yote ya kimataifa iheshimiwe,” aliongeza.
Takriban watu 57 wameuawa katika Mashambulizi hayo, ambayo yamesababisha mvutano mkubwa kati ya Marekani na serikali za Colombia na Venezuela.
Hofu ya mauaji ya halaiki yatanda wakati maelfu wakinasa katika mji uliozingirwa Sudan

Hofu inaongezeka juu ya mauaji ya halaiki katika mji muhimu wa el-Fasher nchini Sudan baada ya wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) kuuteka kutoka vikosi vya serikali.
Katika hotuba yake Jumatatu jioni, mkuu wa jeshi la Sudan Jenerali Abdel Fattah al-Burhan alisema ameidhinisha kuondoka kwa wanajeshi ili kuzuia “uharibifu na mauaji ya raia.”
Umoja wa Mataifa umesema kuna ripoti za kuaminika za “mauaji ya kiholela,” wakati Maabara ya Utafiti ya Chuo Kikuu cha Yale, Marekani ikionesha picha za satelaiti za “marundo ya miili ya watu waliouwawa kwa makundi.”
RSF imekanusha shutuma za kuua raia au kuyalenga makabila ya watu wasiokuwa Waarabu, licha ya ushahidi uliotolewa na Umoja wa Mataifa na mashirika ya kutetea haki za binadamu.
Kuanguka kwa El-Fasher katika eneo la Darfur kunaashiria mabadiliko makubwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan, ambavyo vimeua maelfu na kuwafanya karibu watu milioni 12 kuyahama makazi yao tangu Aprili 2023.
Wapiganaji wa RSF waliuzingira mji wa el-Fasher wenye maelfu ya raia kwa muda wa miezi 18, na kupelekea mgogoro wa njaa.
Maabara ya Utafiti wa Masuala ya Kibinadamu ya Chuo Kikuu cha Yale imeiambia BBC, tangu mji huo kutekwa, picha za satelaiti zimeonyesha “marundo ya miili iliyouawa kwa pamoja, au iliyopigwa risasi na walenga shabaha.”
Na katika chapisho kwenye X, mkurugenzi mtendaji wa maabara hiyo ameelezea mshtuko wake kwa kuona “madimbwi ya damu” kupitia picha za satelaiti.
Vile vile, timu ya Umoja wa Mataifa ya kutoa misaada ya kibinadamu nchini Sudan imesema “imeshtushwa” na ripoti za ukatili kama vile “mauaji ya kiholela,” mashambulizi dhidi ya raia kwenye njia za kutoroka, unyanyasaji wa kingono na uvamizi wa nyumba hadi nyumba.
Kikosi cha Pamoja, muungano wa makundi yenye silaha ya Darfuri yanayoiunga mkono jeshi, yamesema raia 2,000 wameuawa tangu mji huo ulipoanguka. Hakuna uthibitisho wa hili.
Wakaazi waliofanikiwa kutoroka El-Fasher wameiambia BBC, wana hofu baada ya kupoteza mawasiliano na jamaa ambao bado wamekwama jijini.
Israel yaishambulia Gaza baada ya kuishutumu Hamas kukiukaji usitishaji mapigano

Israel imefanya mashambulizi ya anga huko Gaza, kujibu kile maafisa wa Israel wanachosema ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yanayosimamiwa na Marekani.
Waziri wa Ulinzi wa Israel Israel Katz ameishutumu Hamas kwa kuwashambulia wanajeshi wa Israel huko Gaza siku ya Jumanne, na kukiuka masharti ya kurejesha miili ya mateka waliofariki dunia.
Lakini kundi hilo la wapiganaji wa Palestina linasema, halikuhusika na shambulio hilo na kusisitiza kuwa limejitolea kuendelea na makubaliano ya kusitisha mapigano.
Takriban Wapalestina 33 waliuawa katika mfululizo wa mashambulizi ya Israel, kulingana na Shirika la Ulinzi wa Raia wa Gaza linaoendeshwa na Hamas na maafisa wa hospitali.
Mashambulizi hayo yalipiga nyumba na shule katika Jiji la Gaza, Beit Lahia, al-Bureij, Nuseirat na Khan Younis.
Licha ya mashambulizi hayo, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance amesema anaamini usitishaji mapigano unaendelea.
Taarifa fupi iliyotolewa na ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu siku ya Jumanne jioni ilisema aliamuru “mashambulizi ya makali” lakini hakutaja sababu.
Katz alisema Hamas imevuka “mstari mwekundu” kwa kufanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Israel huko Gaza siku ya Jumanne.
“Hamas italipa kwa kuwashambulia wanajeshi na kwa kukiuka makubaliano ya kuwarudisha mateka,” alionya.
Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kwamba wanajeshi katika mji wa kusini mwa Gaza wa Rafah walishambuliwa kwa makombora na walenga shabaha siku ya Jumanne mchana, huku vyombo vya habari vya Palestina vikiripoti mashambulizi ya makombora ya Israel katika eneo hilo.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.