Rais Maduro wa Venezuela asema Marekani ‘inaandaa vita’ inapotuma meli kubwa zaidi ya kivita duniani

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Na: Cantona Joseph|RFA

Rais wa Venezuela Nicolás Maduro ameishutumu Marekani kwa “kuandaa vita”, baada ya kutuma meli kubwa zaidi ya kivita duniani kuelekea Karibiani katika ongezeko kubwa la jeshi lake katika eneo hilo.

Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth aliamuru meli ya kivita ya USS Gerald R Ford, ambayo inaweza kubeba hadi ndege 90, kuondoka kutoka Mediterania siku ya Ijumaa.

“Wanabuni vita vipya vya milele,” Maduro aliambia vyombo vya habari vya serikali. “Waliahidi kwamba hawatawahi tena kujihusisha na vita, na wanabuni vita.”

Marekani imekuwa ikiongeza uwepo wake wa kijeshi katika Karibiani, ikituma meli za kivita, manowari ya nyuklia na ndege za F-35 katika kile inachosema ni kampeni ya kuwalenga wafanyabiashara wa dawa za kulevya.

Washirika wa Ukraine waahidi kuondoa mafuta na gesi ya Urusi kwenye soko la kimataifa

Washirika wa Ukraine waahidi kuondoa mafuta na gesi ya Urusi kwenye soko la kimataifa

Zaidi ya mataifa 20 yanayoiunga mkono Ukraine yameahidi “kuondoa mafuta na gesi ya Urusi katika soko la kimataifa” kama sehemu ya juhudi za kumshinikiza Rais Vladimir Putin kukomesha vita.

“Tunazuia ufadhili wa nguvu ya kijeshi ya Urusi,” alisema Waziri Mkuu wa Uingereza Sir Keir Starmer, baada ya kuandaa mkutano wa kilele wa “muungano wa walio tayari” jijini London.

Uingereza na Marekani katika siku za hivi karibuni zimeweka vikwazo dhidi ya makampuni mawili makubwa ya mafuta ya Urusi, huku EU ikilenga mauzo ya nje ya gesi asilia iliyoyeyushwa (LNG) ya Moscow.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky, ambaye pia alikuwa London, alisema “shinikizo” kwa Urusi ndiyo njia pekee ya kusimamisha mapigano.

Hata hivyo, hakuna uwasilishaji wa makombora ya masafa marefu kwenda Ukraine uliotangazwa katika mkutano huo.

Polisi Uingereza yamsaka mhalifu mhamiaji aliyeachiliwa jela kimakosa

Hadush Kebatu

Polisi wanaendelea na msako wa kumtafuta muomba hifadhi ambaye aliachiliwa kimakosa kutoka gerezani Ijumaa, wiki chache baada ya kufungwa jela kwa kumnyanyasa kingono msichana wa miaka 14 na mwanamke mmoja huko Essex.

Raia wa Ethiopia Hadush Kebatu alikusudiwa kupelekwa katika kituo cha kizuizini cha uhamiaji kutoka HMP Chelmsford kabla ya mpango wa kufukuzwa nchini Ijumaa lakini Waziri wa Sheria David Lammy alisema mtu huyo mwenye umri wa miaka 41 sasa “hayupo” London.

Lammy alisema maafisa kutoka Polisi wa Metropolitan, Polisi wa Uchukuzi wa Uingereza (BTP) na Polisi wa Essex walikuwa wakifanya kazi pamoja kumtafuta Kebatu, ambaye alifungwa jela kwa miezi 12 mnamo Septemba.

Sir Keir Starmer alieleza kuachiliwa kwake “hakukubaliki kabisa”.

Waziri mkuu alisema Kebatu “lazima akamatwe na kufukuzwa nchini”, akiongeza kuwa polisi “wanafanya kazi ya haraka kumtafuta”.

Polisi wa Essex wamethibitisha kwamba Kebatu alipanda treni iliyokuwa ikielekea London katika kituo cha Chelmsford saa 12:41 siku ya Ijumaa. Jeshi hilo lilisema liliarifiwa na Huduma ya Magereza kwamba kulikuwa na “makosa” saa 12:57 na msako ukaanza.

Kebatu alikamatwa tarehe 8 Julai na akaachiliwa kimakosa siku 108 baadaye. Baada ya kuachiliwa kwake angestahili malipo ya kuachiliwa kwa pauni 76.

Marekani yaweka vikwazo dhidi ya Rais wa Colombia Gustavo Petro

Gustavo Petro

Mamlaka ya Marekani imeweka vikwazo dhidi ya Rais wa Colombia Gustavo Petro, wakidai alishindwa kuzuia biashara haramu ya dawa za kulevya.

Vizuizi hivyo pia vilimuathiri mke wake na mtoto wake mkubwa wa kiume.

“Rais Petro ameruhusu magenge ya dawa za kulevya kushamiri na kukataa kuyazuia,” alisema Waziri wa Hazina ya Marekani Scott Bessent.

Mbali na familia ya rais, Marekani pia iliweka vikwazo kwa Waziri wa Mambo ya Ndani wa Colombia Armando Benedetti.

Watu waliowekewa vikwazo watashindwa kuzifikia mali zao zilizo Marekani.

Colombia hapo awali ilichukuliwa kuwa mshirika wa Marekani katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya, ikipokea mamia ya mamilioni ya dola kila mwaka kutoka Washington ili kuimarisha vikosi vyake vya kijeshi.

Hata hivyo, uhusiano wa Pedro na Rais wa Marekani Donald Trump umekuwa mgumu sana.

Marekani inaiona Colombia kama muuzaji mkubwa wa kokeini duniani na inasema nchi hiyo inaleta “tishio kubwa la dawa za kulevya” kwa Marekani.

Petro anakanusha shutuma za Washington na anadai kuwa amekuwa akipambana na ulanguzi wa dawa za kulevya “kwa miongo kadhaa” na pia ameisaidia Marekani kupambana na matumizi ya kokeini.

“Ni kitendawili, lakini si hatua ya kurudi nyuma na hakuna kupiga magoti,” Petro aliandika kwenye akaunti yake kwenye mtandao wa X.

Vikwazo hivyo ni mwendelezo wa mgogoro unaozidi kuongezeka kati ya Petro na Trump. Rais wa Colombia hapo awali alimshutumu kiongozi huyo wa Marekani kwa “mauaji ya kiholela” na kukiuka sheria za kimataifa kuhusiana na mashambulizi dhidi ya meli zinazoshukiwa kufanya biashara ya dawa za kulevya. Trump aliita Colombia “pango la dawa za kulevya.”

Heche anashikiliwa mahabusu ya Polisi Dodoma, anyimwa dhamana-CHADEMA

Heche

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimesema Makamu Mwenyekiti Taifa, John Heche anashikiliwa kwenye mahabusu ya jeshi la Polisi Mtumba jijini Dodoma.

” Leo Ijumaa, 24 Oktoba, Mh. Heche alihojiwa na Idara ya Uhamiaji mbele ya Wakili wa Chama na Kaka yake akituhumiwa kuvunja sheria za Uhamiaji kwa kile walichokisema alivuka mpaka wa Tanzania na kuingia nchini Kenya bila kufuata taratibu”.

“Pamoja na kosa hilo alilotajiwa kuwa na dhamana, Jeshi la polisi limekataa kumpa dhamana likisema kuwa kuna maelekezo kutoka juu kuwa aendelee kubaki mahabusu.” Ilieleza taarifa hiyo.

Heche alikamatwa na Jeshi la Polisi siku ya Jumatano kwenye lango la kuingilia Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam kabla ya kupelekwa Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es salaam kisha kusema wanampeleka mkoani Mara.

” Kuendelea kumshikilia Mh.Heche kinyume cha sheria ni muendelezo wa mpango wa serikali ya CCM chini ya Rais Samia kuwakamata viongozi wakuu wa Chama na kuwaweka kizuizini mpaka baada ya uchaguzi Mkuu uliopangwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025.

“Tunamtaka Rais Samia aache kutumia vibaya vyombo vya dola vya Ulinzi na usalama kuwakamata na kuwaweka kizuizini washindani wake wa kisiasa.” Ilisema taarifa ya chama hicho.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment