Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Na: Cantona Joseph|RFA

Polisi wa Nigeria wamefyatua gesi ya kutoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa wamekusanyika katika mji mkuu wa Abuja kutokana na kuendelea kuzuiliwa kwa kiongozi anayetaka kujitenga Nnamdi Kanu.
Waandamanaji hao, wakiongozwa na mwandishi wa tovuti ya habari ya Sahara Reporters, Omoyele Sowore, wanataka kuachiliwa mara moja kwa Kanu, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya ugaidi na ni kiongozi wa kundi la Indigenous People of Biafra (Ipob).
Kanu, ambaye amekuwa kizuizini tangu 2021, amekanusha mashtaka. Pia ana uraia wa Uingereza.
Ipob inatafuta uhuru kwa kile wanachokiita taifa la Biafra kusini-mashariki mwa Nigeria.
Ujumbe wa Trump uko Israel huku UN ikionya misaada inayoingia Gaza ni kidogo mno

Wajumbe maalum wa Rais Trump, Steve Witkoff na Jared Kushner, wamewasili Israel baada ya makubaliano ya usitishaji vita wa Gaza kuporomoka kwa muda hapo jana.
Shambulio linalosemekana kutekelezwa na Hamas liliwauwa wanajeshi wawili wa Israel na kisha mashambulizi kadhaa ya Israel yakawauwa takriban Wapalestina 45, hospitali za Gaza zilisema.
Leo, vifaru vya Israel vimeripotiwa kuua takriban watu watatu mashariki mwa mji wa Gaza karibu na njia iliyokubaliwa ya kusitisha mapigano.
Licha ya kuzuka mara kwa mara kwa ghasia, wajumbe wa Marekani wanatarajiwa kushinikiza kuanza kwa hatua ya pili ya mpango wa amani.
Inahusisha kuanzisha serikali ya mpito katika eneo hilo, kupeleka kikosi cha kimataifa cha kuleta utulivu, uondoaji wa wanajeshi wa Israel na kuwapokonya silaha Hamas.
Mwalimu aliyemuua mtoto wa miaka 8 afungwa maisha Korea Kusini

Mahakama ya Korea Kusini imemhukumu kifungo cha maisha jela mwalimu mmoja kwa kumdunga kisu mtoto wa miaka minane, katika kesi iliyoshtua taifa hilo.
Myeong Jae-wan, 48, alimuua Kim Hae-neul, baada ya kumshawishi kuingia darasani katika mji wa kati wa Daejeon mwezi Februari.
Waendesha mashtaka walikuwa wameomba hukumu ya kifo kwa Myeong, wakisema kuwa familia ya mwathiriwa iliomba adhabu kali.
Lakini mahakama ilisema ingawa “hatari ya kudhulumiwa tena ni kubwa, ni vigumu kuhitimisha” kwamba Myeong lazima auawe.
Myeong alisema kwamba atatafakari makosa yake katika maisha yake yote.
Alisema uwezo wake wa kufanya maamuzi haukuwa sawa wakati wa kisa hicho alipokuwa akipokea matibabu ya afya ya akili.
DCI yamsaka mwombolezaji aliyempokonya mlinzi wa Gavana bastola kwenye mazishi ya Raila

Polisi eneo la Bondo kaunti ya Siaya wanachunguza kisa ambapo bunduki inadaiwa kutoweka wakati wa hafla ya mazishi ya marehemu Raila Amolo Odinga siku ya Jumapili.
Kulingana na ripoti ya polisi iliyowasilishwa katika Kituo cha Polisi cha Bondo, kisa hicho kilitokea takriban 4:30 jioni Jumapili, wakati Konstebo Benson Kodia Olayo, afisa wa GSU aliye katika Kitengo cha Ulinzi wa VIP kwa Gavana wa Kakamega Fernandes Barasa, aliibiwa silaha hiyo.
Pia aliachwa na michubuko wakati akihangaika bila mafanikio kuzuia kupokonywa silaha hiyo, polisi walisema.
Huu ni wakati ambapo ibada ya kumuaga ilikuwa imeisha na mwili ulikuwa unapelekwa kwenda kuzikwa.
Alikuwa pamoja na maafisa wengine wanne wa polisi na walikuwa wakitoka kwenye hafla hiyo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Jaramogi Oginga Odinga (JOOUST) kwenye lango kuu alipopokonywa silaha hiyo.
Alisema wakati wakipanda kwenye gari rasmi la Gavana, vijana waliokuwa wamemzunguka kiongozi huyo walimpokonya bastola yake iliyokuwa na risasi 15 na kukimbia kutoka eneo la tukio.
Uhuru azuru kaburi la Raila huko Bondo siku moja baada ya kuzikwa

Aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta amezuru kaburi la aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Amolo Odinga eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya, siku moja baada ya kiongozi huyo kuzikwa.
Alipowasili kimya kimya katika nyumba ya familia ya Odinga iliyoko Kang’o Ka Jaramogi, Uhuru alijiunga na wanafamilia katika kipindi ambacho kiligeuka kuwa cha kutafakari sana.
Katika video iliyoonekana na gazeti la Star, Uhuru alikwenda hadi kwenye kaburi ambapo Raila alizikwa Jumapili, Oktoba 19, 2025 na kusimama kimya huku akitoa heshima zake.
Rais huyo wa zamani aliinamisha kichwa chake katika maombi, akabaki tuli kwa dakika kadhaa.
Wakati fulani, alinyoosha mkono wake kuelekea kaburini kabla ya kuendelea na tafakari yake ya kimyakimya. Baadaye aliunganisha mikono yake pamoja na kusali, kichwa chake akikiinamisha.
Kipindi hiki kilikuwa cha hisia nzito wakati familia na Uhuru wakimuenzi Raila ambaye hakuwa tu mshirika wa kisiasa wakati fulani, lakini pia rafiki wa muda mrefu.
Kipindi cha uraisi cha Uhuru, kulikuwa na wakati ambao walitofautiana kisiasa pamoja na kuungana mkono hasa wakati wa “kupeana mikono” wa kihistoria 2018 kulikobadilisha sura ya kisiasa ya Kenya.
Rais Ruto amtunuku Raila Odinga Tuzo ya heshima ya juu zaidi

Waziri Mkuu wa zamani marehemu Raila Odinga ametunukiwa tuzo ya hadhi ya juu zaidi ya Tuzo ya Moyo wa Dhahabu (CGH), ya heshima ya Juu zaidi nchini Kenya.
Tuzo hiyo imetolewa siku ya Mashujaa na Rais William Ruto.
Notisi ya gazeti la serikali ya Oktoba 20, 2025, ilithibitisha kutunukiwa heshima ya CGH ya Daraja la Kwanza kwa Raila, ikimtambua kwa mfano wa ujasiri, uvumilivu, kujitolea kwa dhati kwa maadili ya demokrasia na utawala bora, kujitolea, muungano wa Afrika na huduma ya uaminifu kwa wanadamu wote.
Katika hotuba yake kwa Wakenya katika uwanja wa Ithookwe mjini Kitui, Ruto alimtambua Raila kwa mchango wake katika ujenzi wa taifa na urithi wa kudumu.
Ruto alieleza zaidi kwamba Waziri Mkuu huyo wa zamani ni mzalendo na shujaa wa zama za kale.
“Ikiwa sisi, watu aliotupenda na kututumikia sana, tutachagua kuishi kulingana na masomo aliyotufundisha; kupenda Kenya kuliko tunavyojipenda wenyewe; kutanguliza umoja kuliko migawanyiko; kutamani kufikia makuu, na kutumikia kwa ujasiri, basi tunaweza kuwa taifa kubwa la mashujaa milioni 50,” Rais alisema.
Hafla hiyo inajiri siku moja baada ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kuzikwa huko Kang’o Ka Jaramogi huko Bondo, Kaunti ya Siaya.
Serikali ya Tanzania yazidisha ukandamizaji kabla ya uchaguzi mkuu – Amnesty International

Serikali ya Tanzania imezidisha ukandamizaji kwa wakosoaji wake wa kisiasa, waandishi wa habari, asasi za kiraia, na watetezi wa haki za binadamu katika juhudi za kudumisha madaraka na kuzuia ushiriki wa raia, imesema Amnesty International katika taarifa yake ya hivi punde.
Aidha inadai kuwa uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025 nchini humo unatarajiwa kutawaliwa na chama tawala, Chama Cha Mapinduzi (CCM), huku wagombea wakuu wa vyama vya upinzani wakikumbwa na vikwazo vingi vya kisheria, ikiwa ni pamoja na kufungiwa kugombea.
Miongoni mwao ni Luhaga Mpina na Tundu Lissu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo Tundu Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika, ameonya kuwa serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imepoteza fursa ya mageuzi ya kidemokrasia.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan inaendeleza ukandamizaji unaolenga viongozi wa upinzani, asasi za kiraia, waandishi wa habari, na maoni tofauti, ikiwemo mashambulizi, utiwaji mbaroni bila kufuata taratibu za kisheria, mauaji kinyume cha sheria na upotezwaji, na hakuna mtu yeyote anayewajibishwa,’’ alisema Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International.
Kulingana na ripoti ya Amnesty kuna matumizi mabaya ya mfumo wa sheria, hasa mashtaka ya kisiasa yanayotumika kama silaha dhidi ya wapinzani wa kisiasa.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa serikali inapaswa kuachia mashtaka ya kisiasa yanayotumika kama zana za ukandamizaji, kufanya uchunguzi wa kina wa matukio ya utekaji, mateso na mauaji, na kuwahukumu wahusika wote.
Aidha, serikali ya Jamhuri ya Tanzania inahimizwa kuheshimu haki za binadamu, kuondoa hofu na kuanzisha mazingira ya uchaguzi huru, wa haki na wa amani.
Haya ni kulingana na matokeo ya uchunguzi uliofanywa na Amnesty International kwa kufanya mahojiano na wahanga, mashuhuda, wanasheria na wawakilishi wa asasi za kiraia, pamoja na uchambuzi wa ripoti za vyombo vya habari na vyanzo huru vya habari.
Wakati huo huo, Amnesty International imetoa wito kwa serikali ya Tanzania na jumuiya ya kimataifa kuhakikisha kuwa uchaguzi wa mwaka 2025 unafanyika katika mazingira ya huru, salama na yenye heshima ya haki za binadamu, vinginevyo utaonekana kuwa zoezi lisilo halali, lenye ukandamizaji na hofu inayozuia ushiriki wa kisiasa kwa kila mtanzania.
”Bila ya shinikizo endelevu kutoka kwa wabia wa Tanzania wa kikanda na kimataifa kuacha ukandamizaji kwenye uhuru wa kujieleza na haki za binadamu kwa ujumla, ipo hatari uchaguzi wa 2025 utakuwa zoezi la kiutaratibu ambalo halina uhalali, linalofanywa katika mazingira ambayo hofu, ukatili, na kuenguliwa vimechukua nafasi ya ushiriki wa wazi wa kisiasa,” alisema Tigere Chagutah.
rump amtaka Zelensky wa Ukraine kukubali kuachia baadhi ya maeneo kwa Urusi – Vyanzo

Rais wa Marekani Donald Trump amemsukuma Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kutoa maeneo mengi kwa Urusi wakati wa mkutano wa siku ya Ijumaa uliowaacha wajumbe wa Ukraine wakiwa wamekata tamaa, kulingana na watu wawili walioarifiwa kuhusu mjadala huo.
Trump pia alikataa kutoa makombora ya Tomahawk kwa matumizi ya Ukraine, na akatafakari juu ya kutoa hakikisho la usalama kwa Kyiv na Moscow, maoni ambayo ujumbe wa Ukraine ulipata utata, viliongeza vyanzo viwili, ambavyo viliomba kutotajwa majina ili kujadili mazungumzo ya faragha.
Baada ya mkutano wake na Zelensky, Trump alitoa wito hadharani kusitishwa kwa mapigano kwenye mstari wa mbele wa sasa, msimamo ambao rais wa Ukraine Zelensky baadaye aliuunga mkono alipozungumza na wanahabari.
Chanzo cha tatu kilisema kuwa pendekezo hilo lilitolewa na Trump wakati wa mkutano huo, baada ya Zelensky kusisitiza kuwa hatakubali kwa hiari kukabidhi eneo lolote kwa Urusi.
“Mkutano uliishia na uamuzi wa Trump kuendelea na ’makubaliano pale walipo, katika mstari wa sasa wa uwanja wa vita’,” alisema chanzo hicho.
Trump alisisitiza msimamo huo tena siku ya Jumapili alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ndani ya ndege ya Air Force One:
“Tunaamini wanachopaswa kufanya ni kusimama tu walipo sasa, kwenye mistari ya mapigano,” alisema. “Kila kingine ni kigumu kujadili, hasa ukianza kusema ‘chukua hiki, tutachukua kile’.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.