Kifo cha Raila Odinga: Ratiba ya mazishi kuanzia leo hadi Jumapili

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza maafisa wa serikali katika kupokea mwili huo ambao utapelekwa hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee kuandaliwa.

Na:Cantona Joseph|RFA

Kenya bado iko kwenye majonzi kufuatia kifo cha Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, ambaye aliaga dunia akipata matibabu nchini India.

Mwili wa Raila Odinga utawasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA) leo saa tatu na nusu asubuhi kwa ndege ya Shirika la Ndege la Kenya kutoka Mumbai, India.

Siku ya Alhamisi, Oktoba 16, 2025

Rais William Ruto anatarajiwa kuongoza maafisa wa serikali katika kupokea mwili huo ambao utapelekwa hadi chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee kuandaliwa.

Mwili wa Raila kisha atapelekwa katika majengo ya bunge. Na wananchi wataruhusiwa kuutazama kuanzia kuanzia saa sita mchana hadi kumi na moja jioni na kurejeshwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee.

Siku ya Ijumaa, Oktoba 17, 2025

Mwili wa Raila Odinga utapelekwa katika uwanja wa michezo wa Nyayo na raia wataweza kutoa heshima zao za mwisho kuanzia saa mbili asubuhi.

Baadaye, mwili utarejeshwa nyumbani kwake Karen mjini Nairobi.

Siku ya Jumamosi, Oktoba 18, 2025

Mwili wa Raila Odinga utaondoka Nairobi kuelekea kaunti ya Kisumu.

Wananchi watakuwa na fursa ya kuutazama katika uwanja wa Jomo Kenyatta Grounds, Kisumu, kuanzia saa tatu asubuhi hadi saa tisa mchana.Na mwili huo utaondoka kutoka mji wa Kisumu hadi Bondo, kaunti ya Siaya.

‘Nizikwe ndani ya saa 72’: Wosia wa Raila Odinga

.

Mwili wa Raila Amollo Odinga unatarajiwa kuwasili saa tatu na nusu asubuhi ya leo kutoka India, ambako alikuwa anapata matibabu kabla ya kupatwa na mauti.

Familia yake imefichua kwamba ndani ya wosia wake, aliandika kuwa azikwe ndani ya saa 72.

Chanzo cha familia kilisema Rais William Ruto alifahamishwa kuhusu hilo punde tu alipowasili nyumbani kwa Raila Odinga huko Karen.

“Mzee aliweka katika Wosia wake kwamba azikwe ndani ya saa 72; Rais ameambiwa shughuli ya mazishi ziendane na ratiba hiyo,” chanzo cha familia kiliongeza.

Kufuatia hilo, Raila Odinga atazikwa Jumapili, Oktoba 19, 2025 katika makaburi ya familia huko Kango Ka Jaramogi, Nyamira, Bondo, kando ya kaburi la marehemu babake Jaramogi na mwanawe Fidel.

Mwili wa Odinga utakapofika, utapelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee kuandaliwa kabla ya kuendelea na ratiba jinsi ilivyopangwa.

Kifo cha Raila Odinga: Maandalizi ya kuupokea mwili yanaendelea JKIA

.

Maandalizi ya kuupokea mwili wa Raila Odinga yanaendelea katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Jomo Kenyatta.

Wanajeshi wameshawasili na wanaonekana wakiendelea na maandilizi yao.

Wakati huo huo, wananchi wameshafika katika maeneo ya uwanja ya ndege kumuomboleza Raila Odinga.

Wanashuhudiwa wakilia wengine wakipiga mayowe, kila mmoja akimuomboleza kwa namna yake.

Serikali yatangaza Ijumaa kuwa sikukuu kwa heshima ya Odinga

.

Serikali imetangaza Ijumaa, Oktoba 17, 2025 kuwa sikukuu ya umma kwa heshima ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Amollo Odinga, aliyeaga dunia alipokuwa akipokea matibabu nchini India.

Katika notisi maalum ya gazeti la serikali Na. 15007 iliyochapishwa Alhamisi, Katibu wa Baraza la Mawaziri wa Mambo ya Ndani na Utawala wa Kitaifa, Kipchumba Murkomen, ametangaza tamko hilo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Likizo ya Umma (Sura ya 110).

Mazishi ya kitaifa yatafanyika katika uwanja wa Nyayo siku ya Ijumaa.

Bendera kote nchini Kenya zimekuwa zikipepea nusu mlingoti tangu Jumatano, wakati habari za kufariki kwa Odinga zilipothibitishwa, huku vitabu vya rambirambi vikifunguliwa katika afisi za serikali, balozi na ofisi za chama cha ODM.

Raila Odinga, 80, aliwahi kuwa Waziri Mkuu wa pili wa Kenya kati ya 2008 na 2013 chini ya Serikali ya Muungano kufuatia uchaguzi wa urais wa 2007 uliokumbwa na utata.

Odinga, pia alikuwa mgombea urais mara tano na kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM).

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment