Kifo cha Raila Odinga: Risala za rambirambi zaendelea kumiminika.

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Vocalize Pre-Player Loader

Raila amefariki dunia wakati akifanyiwa matibabu katika hospitali moja nchini India kulingana na duru za familia.

Kifo cha Raila: Rais Ruto akiwa na mama Ida Odinga alipomtembelea nyumbani kwake Karen Jijini Nairobi kumpa pole.

Rais William Ruto atangaza maombolezo ya kitaifa kwa heshima ya Raila Odinga

Rais Ruto akihutubia taifa la Kenya
Maelezo ya picha,Rais Ruto akihutubia taifa la Kenya

Rais William Ruto ametangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kwa muda wa siku saba kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Amollo Odinga.

Katika kipindi hiki, bendera zote za taifa zitapeperushwa nusu mlingoti kama ishara ya heshima na maombolezo.

Aidha, Rais Ruto ametangaza kusitisha shughuli zake zote za umma na kuwasihi maafisa wengine wa serikali kuchukua hatua kama hiyo ili kutoa nafasi ya kutafakari na kuomboleza maisha ya kiongozi huyo mashuhuri.

Kwa ajili ya maandalizi ya mazishi ya kitaifa, Rais ametangaza kuundwa kwa kamati maalum ya kushughulikia shughuli hizo, itakayokuwa chini ya uongozi wa Naibu Rais Kithure Kindiki.

Serikali ya India, kwa ushirikiano wa karibu na Serikali ya Kenya, imeahidi kugharamia na kuratibu shughuli za kusafirisha mwili wa marehemu kutoka India hadi Kenya kwa ajili ya mazishi.

Wakati huo huo, ujumbe wa viongozi wakuu wa serikali, ukiongozwa na Mkuu wa Mawaziri, Mheshimiwa Musalia Mudavadi, unaondoka nchini Kenya kuelekea India haraka iwezekanavyo ili kushughulikia mipango ya mwisho ya usafirishaji wa mwili wa marehemu.

Rais Ruto amemsifu marehemu Raila Odinga kama mtu asiye na tamaa ya makuu, mpenda amani, na mzalendo wa kweli.

“Raila alikuwa kiongozi mwenye maono, aliyejitolea kwa dhati kwa ajili ya taifa hili. Alisimamia haki, usawa na amani. Ni shujaa ambaye historia haitamsahau,” alisema Rais Ruto.

Mazishi ya kitaifa yanatarajiwa kufanyika katika siku zijazo, huku taifa likiendelea kuomboleza mmoja wa viongozi wake wakuu waliotoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya demokrasia na haki za Wakenya.

Viongozi wa serikali ya Kenya wakisikiliza hotuba ya Rais
Maelezo ya picha,Viongozi wa serikali ya Kenya wakisikiliza hotuba ya Rais
Kifo cha Kinara Raila Odinga  chashtua wabunge wa Kenya
Maelezo ya picha,Kifo cha Kinara Raila Odinga chashtua wabunge wa Kenya

Raila Odinga aaga dunia

Raila Amollo Odinga

Maelezo kuhusu taarifa

Aliyekuwa waziri mkuu nchini Kenya Raila Odinga amefariki akiwa na umri wa miaka 80.

Raila amefariki wakati akifanyiwa matibabu katika hospitali moja nchini India kulingana.

Rais wa Kenya William Ruto ametangaza siku saba za maombolezo ya kitaifa kufuatia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.

Katika hotuba yake kwa taifa kupitia televisheni, Rais Ruto alimtaja Odinga kama “mzalendo mwenye ujasiri usio wa kawaida.”

Alisema bendera ya taifa itapepea nusu mlingoti kote nchini Kenya na katika balozi zote za Kenya nje ya nchi.

“Kama ishara ya heshima, nimeahirisha shughuli zangu zote za umma kwa siku zijazo, na ninawaomba wafanyikazi wengine wote wa umma na viongozi kufanya vivyo hivyo ili tujiunge na taifa katika kipindi hiki cha maombolezo,” Ruto alisema.

Rais Ruto pia ametangaza kuwa Odinga ataandaliwa mazishi ya kitaifa kwa heshima kamili.

Aliongeza kuwa serikali ya India, ambapo waziri mkuu huyo wa zamani alifariki alipokuwa akipokea matibabu, imejitolea kuwezesha kurejeshwa kwa mwili wake.

Ujumbe unaoongozwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Kenya Musalia Mudavadi na mnjane wa Odinga Mama Ida Odinga, unatarajiwa kusafiri kuelekea India kusimamia mipango hiyo.

Kumekuwa na uvumi kuhusu afya ya kiongozi huyo wa ODM katika wiki za hivi majuzi baada ya kutoweka kwenye hafla za umma mwezi uliopita.

Kakake mkubwa, Seneta wa Siaya Oburu Oginga, Jumamosi alisema alikuwa mgonjwa lakini “anapata nafuu n kupumzika” nchini India, na hakuwa katika hali mbaya kama inavyodaiwa na baadhi ya wanasiasa kwenye vyombo vya habari.

Odinga ambaye amemwacha mjane na watoto watatu ni mwanasiasa mashauhuri wa Kenya ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu wa nchi hiyo kuanzia 2008 hadi 2013.

Kabla ya kifo chake kiongozi huyo atakumbukwa kwa kupigania uhuru wa kidemokrasia, haki za kibinadamu na mabadiliko ya kitaifa.

Safari yake ya kisiasa

.
Maelezo ya picha,Raila Odinga

Raila Odinga alikuwa mtu mashuhuri katika siasa za Kenya na Afrika, na kutia moyo kizazi chote barani.

Akiwa mwana wa mpiganiaji uhuru Jaramogi Oginga Odinga, makamu wa kwanza wa rais wa Kenya, Raila alisomea Ujerumani Mashariki kabla ya kurejea nyumbani miaka ya sabini.

Aliwekwa kizuizini kwa miaka sita baada ya kutuhumiwa kuhusika na jaribio la mapinduzi mwaka 1982, na baadaye alikamatwa tena kwa kushinikiza demokrasia chini ya utawala wa chama kimoja.

Alirejea kutoka uhamishoni baada ya kuanzishwa tena kwa siasa za vyama vingi kabla ya kuchaguliwa kuwa Mbunge. Alikuwa na mchango mkubwa katika kukomesha utawala wa miongo kadhaa wa chama cha uhuru wa Kenya alipounga mkono jitihada za Mwai Kibaki za kuwania urais mwaka 2002.

Raila Odinga ambaye anajulikana sana kama Baba, aligombea urais mara tano, mara nyingi akiunganisha na kuunda upya upinzani, lakini hakuwahi kunyakua wadhifa huo wa juu zaidi.

Vita vyake vikali vilikuja kati ya mwaka 2007, wakati matokeo ya uchaguzi yaliogombaniwa kuzua ghasia nchi nzima, hatua iliosababisha makubaliano ya kugawana madaraka yaliyosimamiwa na Katibu Mkuu wa zamani wa Umoja wa Mataifa Kofi Annan.

Safari ndefu ya kisiasa ya Raila Odinga, iliyojaa ukakamavu, ukaidi na kujitolea mhanga, ilimletea sifa ndani na nje ya nchi.

Umoja wa Afrika wamkumbuka Odinga

Hj

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC), Mahmoud Ali Youssouf, ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha mwanasiasa wa upinzani Kenya, na Waziri Mkuu wa zamani wa Jamhuri hiyo, Raila Amolo Odinga

Kwa niaba ya Umoja wa Afrika, vyombo na taasisi zake, mwenyekiti huyo ametuma salamu za rambirambi kwa familia ya Odinga, Serikali na wananchi wa Kenya, na na Afrika nzima inayoomboleza msiba huu mkubwa.

Amemtaja Odinga kama mtu mashuhuri katika maisha ya kisiasa na mpiganaji thabiti wa demokrasia, utawala bora na maendeleo yanayozingatia watu na ameacha alama isiyofutika sio tu kwa Kenya bali katika bara zima la Afrika.

Mwenyekiti Youssouf anasema, “Afrika imepoteza mmoja wa wanawe wenye maono; kiongozi aliyejitolea maisha yake kutafuta haki, demokrasia na umoja. Urithi wake utaendelea kujenga Afrika yenye amani, ustawi na demokrasia.”

Rais Ruto na mamia ya Wakenya wamuomboleza Raila Odinga

Rais wa Kenya William Ruto pamoja na mamia ya Wakenya wamewasili nyumbani kwa Raila Odinga Karen jijini Nairobi kuomboleza na familia yake.

Uhuru Kenyatta: Nimempoteza rafiki na kaka

.
Maelezo ya picha,Uhuru kenyatta

Aliyekuwa rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametuma rambi rambi zake kwa familia ya Raila Odinga.

Katika ujumbe wake katika mtandao wa Instagram, Uhuru amemtaja marehamu kama mwenzake wa kisiasa katika safari yake yote ya kisiasa.

‘Nimepoteza rafiki na kaka. Kwangu mimi, Raila alikuwa zaidi ya mwenzangu wa kisiasa, alikuwa sehemu ya pekee ya safari yangu, katika utumishi wa umma na maishani’- Uhuru Kenyatta.

Rais wa Zambia amtaja Odinga kama mtetezi wa demokrasia

Hj

Rais wa Zambia Hakainde Hichilema atuma salamu za pole kufuatia kifo cha mwanasiasa wa Kenya, Raila Odinga.

Katika taarifa yake kupitia X amesema, “nasikitisha kusikia kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya RailaOdinga. Tunatuma rambirambi zetu kwa watu wa Kenya, familia ya Odinga, Rais wa Kenya William Ruto na wote walioguswa na mtetezi huyu mkuu wa demokrasia.

Hichilema amesema urithi wa Odinga utadumu na amemtakia apumzike kwa amani ya milele.

Waziri mkuu wa India Narendra Modi amtaja Odinga kama rafiki

Picha ya pamoja ya Raila Odinga na Narendra Modi
Maelezo ya picha,Picha ya pamoja ya Raila Odinga na Narendra Modi

Waziri mkuu Narendra modi ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa waziri mkuu wa Kenya Raila Odinga.

Kupitia ukurasa wake wa X au Twitter Narendra amemtaja Raila Odinga kama kiongozi mashuhuri na rafiki wa dhati wa India.

Modi alisema kuwa mchango wa Raila Odinga katika kukuza uhusiano kati ya India na Kenya ulikuwa wa kipekee, na kwamba kumbukumbu zake zitaendelea kuenziwa na wengi.

Aliongeza kuwa Raila alikuwa sauti ya hekima, demokrasia, na mshikamano barani Afrika, na kwamba dunia imepoteza kiongozi wa kweli.

Waziri Mkuu Modi alituma salamu za rambirambi kwa familia ya Raila Odinga, wananchi wa Kenya, na wote walioguswa na msiba huu, akiwatakia faraja na nguvu katika kipindi hiki kigumu.

Modi ameweka bayana kuwa Raila alipendelea tiba ya Ayurveda na tiba asili za India kutokana na ufanisi wake katika afya ya binti yake.

‘Alikuwa na mapenzi kwa India kuanzia tiba zetu na utamaduni wetu”

Raila Odinga amefariki dunia akipokea matibabu nchini India.

Kifo cha Raila Odinga: Wabunge washindwa kujizuia bungeni

.

Kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga kimesababisha uchungu na simanzi kwa wafuasi wake na Wakenya kwa ujumla.

Raila alifariki siku ya Jumatano, Oktoba 15, alipokuwa akipatiwa matibabu nchini India.

Bungeni, wabunge wa ODM waliangua vilio baada ya kupokea habari hizo za kuhuzunisha.

Baadhi ya wabunge walitiririkwa na machozi na kushindwa kujizuia huku wakimsifu waziri mkuu huyo wa zamani.

Mwakilishi wa Kike wa Busia Cathrtine Omayo na Mbunge wake wa Likoni Mishi Mboko walishindwa kujizuia wakati taarifa za kifo cha Raila kilipotangazwa.

Wakenya wanaendelea kutoa heshima zao kwenye mitandao ya kijamii wakimkumbuka kwa namna mbalimbali.

Rais Ramaphosa amuomboleza Raila Odinga

Baada ya kutangazwa rasmi kufariki kwa galacha wa siasa Raila Odinga, Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametoa risala za rambirambi kwa Kenya.

Akiwa ni kiongozi wa hivi punde kumuomboleza Odinga Rais Ramaphosa alisema: “Taifa la Kenya na bara letu limempoteza kiongozi mzalendo na asiye na ubinafsi ambaye nilimfahamu na kufanya naye kazi kama rafiki na ndugu.”

Kupitia taarifa aliyetuma kwa vyombo vya habari kiongozi huyo wa Afrika Kusini amemsifia Raila kuwa alihakikisha bara la Afrika lina usalama kutokan na nyadhifa alizokuwa nazo.

“Raila Odinga alijitolea kuendeleza taifa lake na pia ustawi na kunyamazisha bunduki katika bara letu, kama inavyothibitishwa na uteuzi wake na Muungano wa Afrika kuendeleza amani nchini Côte d’Ivoire mwaka wa 2010.”

Aidha Ramaphosa amemtaja Raila kama kiongozi aliyejitolea na kuweka masilahi ya nchi na bara lake kwanza.

Waombolezaji wamiminika nyumbani kwao Bondo

Waombolezaji wa eneo la Kisumu wamemiminika katika eneo la makazi la aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga kuuungana na familia wakati huu wa kuomboleza.

Kupitia vyombo habari vya eneo, waombolezaji wanabubujikwa na machozi huku wakiwa wameshika matawi kama ishara ya kuomboleza na familia ya Odinga.

Waombolezaji wengine wameshuhudiwa katika barabara za eneo la Kisumu wakipiga mayowe, kama namna ya kutoa risala zao.

Hili ni eneo ambalo Raila Odinga amekuwa na wafuasi wengi.

Rais Samia atuma salamu za rambirambi

Hj

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametuma salamu za rambi rambi baada ya kifo cha mwanasiasa wa upinzani nchini Kenya, bwana Raila Odinga.

Kupitia ukurasa wake wa Instgram Samia amesema, “imepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Mheshimiwa Raila Amolo Odinga. Tumempoteza kiongozi mahiri, Mwanamajumui wa Afrika, mpenda amani na mtafuta suluhu, ambaye ushawishi na upendo wake haukuwa tu ndani ya Kenya, bali Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla. Msiba huu si wa Kenya pekee, bali wetu sote.”

Tunaungana kuwaombea kwa Mwenyezi Mungu awajalie subra, faraja na imani katika kipindi hiki, na ailaze roho ya mpendwa wetu, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, mahali pema peponi.

Raila Odinga aaga Dunia: Ruto akutana na Baraza la Usalama huku kikao cha Bunge kikiahirishwa

.

Rais William Ruto amekuwa na kikao kisicho cha kawaida cha Baraza la Usalama la Kitaifa, na baadaye ataongoza kikao maalum cha Baraza la Mawaziri saa nane na nusu mchana.

Wakati huo huo, Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetangula ameahirisha kikao cha Jumatano asubuhi katika Bunge la Kitaifa.

Ruto anatarajiwa kuhutubia taifa kufuatia kifo cha Raila Odinga ambaye amefariki wakati akifanyiwa matibabu katika hospitali moja nchini India.

Wasifu wa Raila Odinga, kiongozi wa upinzani Kenya

Bw Odinga

Raila Amolo Odinga alizaliwa Januari tarehe 7 mwaka 1945 Magharibi mwa Kenya katika mkoa wa Nyanza.

Bw Odinga, anayejulikana kwa wafuasi wake kama “Agwambo” kumaanisha mwenyekiti au mtu wa kushangaza kwa lugha yake asili ya Dholuo, ni kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM). Ni kawaida kuwasikia wafuasi wake pia wakimuita ‘Baba’.

Aliwahi kuhudumu kama waziri mkuu wa kwanza wa Kenya, wadhifa ulioundwa kufuatia Mkataba wa Kitaifa ulioafikiwa kumaliza ghasia za baada ya uchaguzi mwaka 2007-2008, ambapo aligawana mamlaka na Rais Mwai Kibaki.

Bw Odinga, mwenye umri wa miaka 72 kwa sasa amekuwa miongoni mwa viongozi watano wanaojiita Pentagon ambao wanaongoza muungano wa umoja wa vyama vya upinzani, National Super Alliance (NASA).

Kwenye muungano huo, alishirikiana na Bw Kalonzo Musyoka (makamu wa rais wa zamani na kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement -WDM), Bw Musalia Mudavadi (makamu wa rais wa zamani na kiongozi wa chama cha Amani National Congress – ANC), Bw Moses Wetangula (kiongozi wa chama cha Forum for Restoration of Democracy Kenya – Ford Kenya) na Bw Isaac Ruto (kiongozi wa Chama cha Mashinani – CCM).

Kama hayati babake, Jaramogi Oginga Odinga, Raila aliishi kukamatwa na kuachiliwa mara kwa mara tangu mwaka 1982 hadi 1991 kwa harakati zake za kupigania mageuzi wakati wa muhula wa pili wa utawala wa rais Daniel arap Moi.

Kufuatia kuidhinishwa kwa katiba mpya, mwezi Agosti, mwaka 2010, amekuwa akisema kwenye kampeni zake kuwa nia yake ni kuleta mageuzi ya kisiasa na pia kumaliza ufisadi.

Bw Odinga ni mwanasiasa anayesifika sana kwa ushawishi wake kisiasa na amekuwa katika msitari wa mbele kuunda vyama vya miungano na wanasiasa ambao ni mahasimu wake.

Baada ya uchaguzi wa mwaka 1997 ambapo Raila alishikilia nafasi ya tatu, kufuatia kuundwa kwa muungano wa chama chake (NDP) na chama cha rais wa zamani Daniel moi (KANU), aliteuliwa kama waziri wa kawi katika serikali ya muhula wa mwisho wa Moi.

Bw Musyoka, Bw Odinga na Bw Wetangula
Maelezo ya picha,Bw Odinga amekuwa aliikosoa serikali ya Rais Kenyatta akiwa na Bw Musyoka (Kushoto) na Bw Wetangula

Mwaka 2002, baada ya Moi kumuunga mkono uhuru Kenyatta, kama mrithi wake, Raila na maafisa wengine wa KANU ikiwemo Kalonzo Musyoka na wafuasi wengine, walipinga ungwaji mkono wa Kenyatta kugombea Urais.

Waliungana na kiongozi wa upinzani Mwai Kibaki na na kuunda muungano wa National Rainbow Coalition (Narc) ambao baadaye ulishinda uchaguzi wa mwaka 2002.

Raila aliungana na Rais Mwai Kibaki kuunda serikali ya Muungano ya NARC baada ya kumuondoa mamlakani rais mstaafu Daniel Moi.

Mwaka 2005 aliungana na Uhuru Kenyatta aliyekuwa kama kiongozi rasmi wa upinzani, ili kushinda kura ya maoni kuhusu rasimu ya katiba chini ya serikali ya Rais Kibaki .

Wakati Kibaki alipomfuta kazi na washirika wake, aliunda chama cha ODM ambacho kilipiga kura ya ‘La’ dhidi ya rasimu ya katiba mpya ambayo ilishindwa mwaka 2005.

Aliongoza kampeni mwaka 2007 na kwa shingo upande kukubali ushindi wa rais Kibaki Katika uchaguzi uliokumbwa na utata, ghasia na mauaji.

Bw Odinga
Maelezo ya picha,Bw Odinga alifungwa jela miaka ya 1980

Lakini hatimaye alilazimika kujiunga na Kibaki katika serikali ya Muungano.

Desemba mwaka 2012, Raila alilazimika kupiga moyo konde na kurudiana na Kalonzo Musyoka chini ya muungano wa CORD, kwani daima husema katika siasa, hakuna maadui wa kudumu.

Raila anaamini kuwa Wakenya wanastahili kuhudumiwa vyema zaidi kuliko ahadi wanazopewa na kwamba chini ya utawala wake.

Raila anaahidi kuleta mageuzi na kuhakikisha uongozi bora.

Amekuwa akiahidi kuwa serikali yake itawekeza katika viwanda vya kisasa, mabohari pamoja na vituo vya teknolojia ya mawasiliano katika maeneo ya kuvulia, ushirikiano na sekta ya kibinafsi ili kuimarisha kilimo.

Kwa miaka miwili, pamoja na wanasiasa wengine akiwemo Bw Musyoka na Bw Wetangula, walikuwa wanaishinikiza serikali kufanya mazungumzo na upinzani kuhusu mwelekeo wa nchi.

Baadaye, watatu hao walianzisha kampeni ya kisiasa iliyofahamika kama Okoa Kenya Movement ambapo waliandaa mikutano na maandamano ya kuipinga serikali.

Aidha, walitumia kampeni hiyo kushinikiza mageuzi katika Tume Huru ya Uchaguzi (IEBC), hatua iliyopelekea kuondolewa kwa aliyekuwa mwenyekiti Ahmed Isaack Hassan.

Agosti 2017, uchaguzi ulipofanyika, tume ya uchaguzi ilitangazwa kwamba alikuwa ameshindwa na Rais Kenyatta.

Alipinga matokeo hayo Mahakama ya Juu na uchaguzi huo ukafutiliwa mbali na uchaguzi mpya kuandaliwa tarehe 26 Oktoba.

Lakini Bw Odinga alisusia uchaguzi huo akisisitiza wkamba mageuzi yalihitajika katika tume ya uchaguzi kabla ya uchaguzi huru na wa haki kufanyika.

Mahakama ya Juu ilipoidhinisha kuchaguliwa kwa Bw Kenyatta na baadaye akaapishwa tarehe 28 Novemba, Bw Odinga alisema kamwe kwamba hatamtambua kama kiongozi aliyechaguliwa na wananchi Kenya.

Miili ya mateka watatu iliorejeshwa kutoka Gaza yatambuliwa

Uii

Miili ya mateka watatu waliokabidhiwa kwa Israel na Hamas usiku wa jana imetajwa kuwa ni Tamir Nimrodi, Etian Levy na Uriel Baruch, kwa mujibu wa Familia za Mateka na waliopotea

Mwili wa nne uliopelekwa Israel bado haujatambuliwa.

Taarifa hizi zinakuja baada ya Israel kuonya kuwa itazuia misaada kuingia Gaza na kuchelewesha kufungua tena kivuko cha Rafah hadi Hamas irejeshe miili ya mateka wote 28 waliofariki.

Kurudi polepole kwa mateka waliokufa kumechochea hasira nchini Israel, na Wapalestina wanazidi kuwa na wasiwasi kwamba ucheleweshaji huo unaweza kuleta sintofahamu kwa mustakabali wa usitishaji mapigano.

Miili ya Wapalestina 45 waliokuwa wamezuiliwa nchini Israel imerejeshwa Gaza siku ya Jumanne, Shirika la Msalaba Mwekundu linasema.

Huko Gaza, mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa yanasema changamoto za kuleta vifaa na kuanza ujenzi ni kubwa

Wakati huo huo, Donald Trump anasema ikiwa Hamas hawataweka silaha chini kwa hiari, tutawapokonya kwa nguvu.

China yashikilia ramani 60,000 kwa ‘kuichora vibaya’ Taiwan

Hy
Maelezo ya picha,Maafisa wa forodha wameshikilia ramani hizo zilizokuwa zikisafirishwa kwenda nje ya nchi

Maafisa wa forodha wa China katika mkoa wa Shandong mashariki wamekamata ramani 60,000 ambazo “zimekichora vibaya” kisiwa kinachojitawala cha Taiwan, ambacho Beijing inadai kuwa sehemu ya ardhi yake.

Ramani hizo, serikali inasema, “zimeacha visiwa muhimu” katika Bahari ya China Kusini, ambapo madai ya umiliki ya Beijing yanaingiliana na yale ya majirani zake, ikiwa ni pamoja na Ufilipino na Vietnam.

Ramani ” zenye matatizo,” zinazokusudiwa kuuzwa nje ya nchi, haziwezi kuuzwa kwa sababu “zinahatarisha umoja wa kitaifa, mamlaka na uadilifu wa eneo” la China, mamlaka imesema.

China ilisema kuwa ramani hizo pia hazikuwa na mipaka ya dashi tisa, ambayo inaweka mipaka ya madai ya Beijing karibu na Bahari ya Kusini ya China.

Ramani zilizokamatwa pia hazioneshi mpaka wa baharini kati ya China na Japan, mamlaka ilisema. Serikali imesema ramani zimeuandika vibaya “mkoa wa Taiwan,” bila kubainisha ni nini hasa kilichoandikwa vibaya.

China inaiona Taiwan inayojitawala yenyewe kuwa eneo lake. Lakini Taiwan inajiona kuwa tofauti na bara la China, ikiwa na katiba yake na viongozi waliochaguliwa kidemokrasia.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment