Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa


Shirika la Msalaba Mwekundu lilichukua mabaki hayo kwenye majeneza na kuyakabidhi kwa wanajeshi wa Israel usiku wa Jumanne.
Na:Cantona Joseph|RFA
China yashikilia ramani 60,000 kwa ‘kuichora vibaya’ Taiwan

Maafisa wa forodha wa China katika mkoa wa Shandong mashariki wamekamata ramani 60,000 ambazo “zimekichora vibaya” kisiwa kinachojitawala cha Taiwan, ambacho Beijing inadai kuwa sehemu ya ardhi yake.
Ramani hizo, serikali inasema, “zimeacha visiwa muhimu” katika Bahari ya China Kusini, ambapo madai ya umiliki ya Beijing yanaingiliana na yale ya majirani zake, ikiwa ni pamoja na Ufilipino na Vietnam.
Ramani ” zenye matatizo,” zinazokusudiwa kuuzwa nje ya nchi, haziwezi kuuzwa kwa sababu “zinahatarisha umoja wa kitaifa, mamlaka na uadilifu wa eneo” la China, mamlaka imesema.
China ilisema kuwa ramani hizo pia hazikuwa na mipaka ya dashi tisa, ambayo inaweka mipaka ya madai ya Beijing karibu na Bahari ya Kusini ya China.
Ramani zilizokamatwa pia hazioneshi mpaka wa baharini kati ya China na Japan, mamlaka ilisema. Serikali imesema ramani zimeuandika vibaya “mkoa wa Taiwan,” bila kubainisha ni nini hasa kilichoandikwa vibaya.
China inaiona Taiwan inayojitawala yenyewe kuwa eneo lake. Lakini Taiwan inajiona kuwa tofauti na bara la China, ikiwa na katiba yake na viongozi waliochaguliwa kidemokrasia.
ChatGPT kuanza kuruhusu maudhui ya ngono

Kampuni ya OpenAI inapanga kuruhusu maudhui ya ngono kwenye ChatGPT yake kwa watu wazima waliothibitishwa, amesema bosi wa kampuni hiyo Sam Altman.
Katika chapisho kwenye X siku ya Jumanne, Bw Altman amesema matoleo yajayo ya ChatGPT ndio yatakuwa na huduma hiyo kwa anayetaka.
Hatua hii, inafanana na ile ya Elon Musk kupitia xAI ambapo alizindua hivi karibuni maudhui ya ngono kupitia Grok.
OpenAI haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni kufuatia chapisho la Altman.
Mabadiliko yaliyotangazwa na kampuni hiyo yanakuja baada ya kushtakiwa mapema mwaka huu na wazazi wa kijana wa Marekani ambaye alijiua.
Kesi iliyowasilishwa na Matt na Maria Raine, ambao ni wazazi wa Adam Raine mwenye umri wa miaka 16, ilikuwa ni hatua ya kwanza ya kisheria kuishutumu OpenAI kwa kifo cha mtoto huyo.
Wanandoa hao wa California wameikosoa kampuni hiyo – kwa kutofanya vya kutosha kulinda matumizi bora ya chatbot yake.
Familia hiyo ilielezea mazungumzo kati ya Adam, ambaye alikufa Aprili, na ChatGPT ambayo yanaonesha akielezea kuwa ana mawazo ya kujiua.
Wakosoaji wanasema uamuzi wa OpenAI wa kuruhusu ngono kwenye jukwaa hilo unaonyesha hitaji la udhibiti zaidi katika ngazi za shirikisho na serikali.
“Watahakikishaje kuwa watoto hawawezi kufikia sehemu za ChatGPT ambazo ni za watu wazima pekee?” Amehoji Jenny Kim, kutoka kampuni ya uwakili ya Boies Schiller Flexner.
Utafiti uliochapishwa mwezi huu na Shirika la Kituo cha Demokrasia na Teknolojia (CDT) uligundua kuwa mwanafunzi mmoja kati ya watano aliripoti kwamba yeye au mtu anayemjua ana uhusiano wa kimapenzi na AI.
Profesa wa biashara wa Chuo Kikuu cha Tulane Rob Lalka, ambaye aliandika kitabu cha hivi majuzi The Venture Alchemists, anasema kampuni kubwa za za AI zinajikuta kwenye vita vya kupata soko.
Wahamiaji watahitajika kujua Kiingereza kwa kiwango cha A ili kufanya kazi Uingereza

Baadhi ya wahamiaji wanaokwenda Uingereza watahitajika kuzungumza Kiingereza kwa kiwango cha A chini ya sheria kali zitakazoanzishwa na serikali.
Mabadiliko hayo, ambayo yataanza kutekelezwa kuanzia tarehe 8 Januari 2026, yataathiri wanaotaka kusoma na wale wanaoomba viza za kazi.
Sheria mpya ni sehemu ya mipango mipana ya kupunguza viwango vya uhamiaji nchini Uingereza iliyoainishwa mwezi Mei.
Waziri wa Mambo ya Ndani Shabana Mahmood amesema: “Ikiwa utakuja katika nchi hii, lazima ujifunze lugha yetu.”
Wahamiaji watahitaji Kiingereza sanifu cha kiwango cha A ili kufanya kazi nchini Uingereza. Ni jambo lisilokubalika kwa wahamiaji kuja hapa bila kujifunza lugha yetu.”
Waombaji watafanyiwa mitihani ya kuzungumza, kusikiliza, kusoma na kuandika katika ofisi zilizoidhinishwa na Wizara hiyo, na matokeo yao yataangaliwa kama sehemu ya mchakato wa viza.
Ili kuwenda Uingereza kama mfanyakazi kupitia viza hiyo, ni lazima mwajiriwa afanye kazi kwa mwajiri aliyeidhinishwa na serikali na awe analipwa angalau pauni £41,700 kwa mwaka.
Hatua zingine ni pamoja na kupunguza muda ambao wanafunzi wa kimataifa wanaweza kukaa Uingereza baada ya kozi yao kumalizika kutoka miaka miwili hadi miezi 18, ambayo itaanza kutumika Januari 2027.
Wanafunzi pia watalazimika kukidhi mahitaji ya kifedha, yaliyoongezwa hadi £1,171 kwa mwezi nje ya London, kutoka £1,136 kwa miezi tisa.
Makadirio ya Wizara ya Mambo ya Ndani yanaonyesha hatua hiyo inaweza kupunguza idadi ya watu wanaokwenda Uingereza hadi 100,000 kwa mwaka.
Marekani imeishambulia boti nyingine katika pwani ya Venezuela na kuua watu sita

Marekani imeishambulia boti nyingine kwenye pwani ya Venezuela siku ya Jumanne na kuua watu sita, Rais Donald Trump amesema.
Katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii, Trump amesema boti hiyo ni ya “magaidi” na ilikuwa “ikisafirisha mihadarati.”
Hili ni shambulio la tano la utawala wa Trump kwenye boti inayotuhumiwa kusafirisha dawa za kulevya kwenye maji ya kimataifa tangu Septemba.
Kwa jumla, watu 27 wameripotiwa kuuawa, lakini Marekani haijatoa ushahidi au maelezo kuhusu utambulisho wa boti hizo au wale waliokuwemo.
Baadhi ya mawakili wameishutumu Marekani kwa kukiuka sheria za kimataifa, na mataifa jirani kama Colombia na Venezuela yamelaani shambulio hilo.
Katika chapisho lake, Trump amesema “taarifa za kijasusi zimethibitisha kuwa boti hiyo ilikuwa ikisafirisha mihadarati, na inahusishwa na mitandao haramu ya wagaidi wa mihadarati, na ilikuwa ikipitia katika njia inayojulikana” kwa magendo.
Moto katika kiwanda cha nguo waua watu 16

Takriban watu 16 wamefariki dunia baada ya moto mkubwa kuzuka katika kiwanda cha nguo nchini Bangladesh, huku maafisa wakionya kuwa huenda idadi hiyo ikaongezeka.
Miili kumi na sita imepatikana lakini ilichomeka kiasi cha kutotambulika, shirika la zima moto limesema.
Jamaa waliofadhaika walikusanyika nje ya kiwanda cha ghorofa nne katika eneo la Mirpur huko Dhaka siku ya Jumanne kuwatafuta wapendwa wao ambao bado hawajapatikana.
Moto huo uliozuka katika kiwanda hicho mwendo wa saa sita mchana, ulizimwa baada ya saa tatu. Lakini ghala la kemikali lililo karibu liliendelea kuwaka, serikali imesema.
Mkurugenzi wa huduma ya zima moto Mohammad Tajul Islam Chowdhury aliviambia vyombo vya habari vya ndani kuwa waathiriwa walikufa “papo hapo” baada ya kuvuta “gesi yenye sumu kali.”
Polisi na maafisa wa kijeshi bado wanajaribu kuwatafuta wamiliki wa kiwanda na ghala hilo, Bw Chowdhury aliwaambia wanahabari.
Uchunguzi kuhusu iwapo ghala hilo lilikuwa likifanya kazi kihalali pia unaendelea, aliongeza.
Wanafamilia waliokuwa na machozi walisimama nje ya majengo yaliyokuwa yameungua, wengi wao wakiwa wameshikilia picha za jamaa zao waliopotea.
Miongoni mwao ni mwanaume anayemtafuta binti yake, Farzana Akhter.
“Niliposikia kuhusu moto, nilikuja mbio. Lakini bado sijampata….namtaka binti yangu,” aliliambia shirika la habari la Reuters.
Mwaka 2021, moto katika kiwanda cha chakula na vinywaji uliwaacha watu wasiopungua 52 wakiwa wamekufa na wengine 20 kujeruhiwa. Kiwanda hicho kilijengwa kinyume cha sheria na hakikuwa na mlango wa dharura, uchunguzi ulieleza.
Ajali mbaya zaidi ya viwanda nchini humo hadi sasa ilitokea mwaka 2013, wakati jengo la biashara la ghorofa nane liliporomoka na kuua zaidi ya watu 1,100.
Hamas yairejesha miili mingine minne ya mateka

Hamas imerejesha miili ya mateka wengine wanne waliofariki, Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) limesema.
Shirika la Msalaba Mwekundu lilichukua mabaki hayo kwenye majeneza na kuyakabidhi kwa wanajeshi wa Israel usiku wa Jumanne.
Kurejesha huko kumekuja baada ya Israel kuonya kuwa itazuia misaada kauingia Gaza hadi Hamas itakaporudisha miili ya mateka wote 28 waliofariki.
Kundi hilo la wapiganaji la Palestina limewarudisha mateka 20 waliokuwa hai na wanne waliokuwa wamekufa siku ya Jumatatu.
Miili ya Wapalestina 45 waliokuwa wanazuiliwa nchini Israel imerejeshwa Gaza siku ya Jumanne, Shirika la Msalaba Mwekundu lilisema katika taarifa yake.
Kwa mujibu wa mpango wa Rais wa Marekani Donald Trump wa kusitisha mapigano, ambao Israel na Hamas waliukubali, unaitaka Hmas kuwakabidhi mateka wote 48 ifikapo siku ya Jumatatu.
Wakati mateka wote walio hai wakirejeshwa, shinikizo linaongezeka kwa Hamas kutoka serikali ya Israel juu ya mabaki ya mateka ambao Hamas bado hawajawarejesha.
Wapalestina wanazidi kuwa na wasiwasi kwamba Hamas kuchelewesha kurejesha miili hiyo kunaweza kuleta sintofahamu katika mustakabali wa usitishaji mapigano.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.