Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Mkuu huyo alishtakiwa mwezi uliopita, siku chache baada ya chapisho la Rais wa Marekani, Donald Trump kwenye mitandao ya kijamii akimshinikiza Mwanasheria Mkuu kuchukua hatua.
Na:Cantona Joseph|RFA

Aliyekuwa mkuu wa Shirika la Ujasusi wa ndani Marekani, FBI, James Comey amefikishwa katika mahakama ya shirikisho leo huko Virginia kwa mara ya kwanza tangu afunguliwe mashtaka.
Comey alishtakiwa mwezi uliopita, siku chache baada ya chapisho la Rais wa Marekani, Donald Trump kwenye mitandao ya kijamii akimshinikiza Mwanasheria Mkuu wa serikali Pam Bondi kuchukua hatua.
Chama cha Democratics na baadhi ya wataalamu wa sheria wanamtuhumu Trump kwa kutumia Idara ya Sheria kutafuta kulipiza kisasi dhidi ya maadui zake.
Trump alimfuta kazi Comey wakati wa muhula wake wa kwanza wa urais, na wawili hao wametupiana maneno mara kwa mara tangu wakati huo
Anakabiliwa na mashitaka mawili, lakiniComey anasema hana hatia na haogopi kukabiliwa na kesi.
Shitaka la kwanza, anatuhumiwa kutoa taarifa za uongo ndani ya Seneti ya Marekani alipotoa ushahidi wakati wa kikao cha Kamati ya Mahakama ya Seneti tarehe 30 Septemba 2020.
Taarifa hiyo inayodaiwa kuwa ya uwongo inahusiana na kumwambia Seneta katika kamati hiyo kwamba “hakumuidhinisha mtu katika FBI kuwa chanzo kisichojulikana katika ripoti ya vyombo vya habari” kuhusu uchunguzi wa FBI, wa kuchunguza iwapo Urusi iliingilia uchaguzi wa Marekani wa 2016.
Shitaka ya pili, kuzuia haki kutendeka, kwamba Comey “alijaribu kuzuia na kuhujumu uchunguzi mbele ya Kamati ya Mahakama ya Seneti kwa kutoa taarifa za uongo na za kupotosha” mbele ya kamati hiyo.
Baada ya kusomeshwa mashtaka hayo leo, amekana kufanya kosa lolote na kesi hiyo imepangwa kuanza kusikilizwa tarehe 5 Januari 2026.
Trump hjawahi kumsamehe James Comey kwa kuanzisha uchunguzi kuhusu uhusiano kati ya Urusi na timu ya kampeni ya urais ya Trump 2016 – ingawa hakuna njama ya uhalifu iliyowahi kufichuliwa.
Comey alikuwa mkuu wa FBI kutoka 2013 hadi 2017.
Hamas imekabidhi majina ya watu inaotaka waachiliwe katika mabadilishano na mateka

Siku ya Jumatano, Hamas imekabidhi orodha ya majina ya mateka na wafungwa wa Kipalestina ili kubadilishana na wateja wa Israel waliopo Gaza, na imesema ina matumaini juu ya mazungumzo ya kumaliza vita huko Gaza.
Mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja yanalenga kuweka njia za kusitisha mzozo huo, kuondolewa kwa vikosi vya Israelikutoka Gaza na makubaliano ya kubadilishana wafungwa na mateka.
Mojawapo ya hoja kuu katika mazungumzo hayo ni takwa la Israel la kutaka Hamas ipokenywe silaha, suala ambalo Hamas imekuwa haitaki kulijadili katika mazungumzo hayo yaliyoanza Jumatatu katika mji wa wa Misri wa Sharm el-Sheikh, chanzo kutoka Palestina ambacho kiko karibu na mazungumzo hayo kimeiambia Reuters.
Muda wa kutekelezwa kwa awamu ya kwanza ya mpango wa Trump bado haujakubaliwa, chanzo hicho kimesema.
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa mawaziri siku ya Alhamisi mjini Paris na mataifa ya Ulaya, Kiarabu na mataifa mengine kujadili mustakabali wa Gaza baada ya vita, vyanzo vitatu vya kidiplomasia vilisema Jumatano.
Mkutano huo ambao utafanyika sambamba na mazungumzo nchini Misri, unanuiwa kujadili jinsi ya kutekeleza mpango wa Trump na kutathmini ahadi za pamoja za nchi hizo.
Wakaazi wengi wa Gaza wamelazimika kuyahama makazi yao mara kwa mara huku wakikabiliwa na njaa na uhaba wa mafuta, maji na vifaa vya matibabu.
Waandamanaji vijana wakataa mwaliko wa rais wa Madagascar,

Vijana waandamanaji nchini Madagascar wamekataa mwaliko wa Rais Andry Rajoelina kujiunga na mazungumzo ya kitaifa, wakiishutumu serikali yake kwa “ukandamizaji” baada ya wiki kadhaa za maandamano katika taifa hilo la kisiwa.
“Hatutashiriki katika mazungumzo na serikali ambayo inakandamiza, kuwashambulia, na kuwadhalilisha vijana mitaani,” vijana hao walisema katika taarifa iliyochapishwa kwenye moja ya kurasa za Facebook zinazotumiwa kuhamasisha maandamano.
“Huwezi kuzungumza serikali ambayo inakandamiza wale wanaosimama na haki kila siku,” iliendelea taarifa hiyo, ikielezea pendekezo la rais la mazungumzo kama la udanganyifu.
“Serikali hii inazungumza juu ya mazungumzo, lakini inatawala kwa mabavu. Maadamu ukandamizaji unaendelea, maadamu sauti za watu zimenyamazishwa, hatutashiriki katika mazungumzo yoyote ya uwongo au ya maigizo,” waandamanaji waliongeza.
Rais Rajoelina anatarajiwa kuitisha mdahalo wa kitaifa leo mchana katika ikulu ya rais, na kuwaleta pamoja wanafunzi, wawakilishi wa vijana, na viongozi wa kiroho, sehemu ya kile anachoelezea kama kampeni mpya ya kusikiliza na “kuuelewa wasiwasi wa raia.”
Ameendelea kutoa mwaliko wa mazungumzo, kufanya mikutano na makundi mengine na kusisitiza nia yake ya kusikiliza katika jitihada za kutatua mgogoro unaoendelea nchini.
Siku ya Jumanne, waandamanaji walitoa makataa ya saa 48 kwa rais kutimiza matakwa yao la sivyo akabiliane na mgomo wa nchi nzima.
Mamia ya vituo vya afya DR Congo havina dawa,

Zaidi ya vituo 200 vya afya mashariki mwa Congo havina dawa kutokana na kuenea kwa uporaji na changamoto katika usambazaji kutokana na mapigano mwaka huu, imesema Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) siku ya Jumatano.
Taarifa hii imetolewa baada ya utafiti uliofanyika katika vituo mia mbili na arubaini vya afya katika mikoa ya Kivu ya Kusini na Kaskazini.
Huu ndio utafiti mkubwa zaidi kuwahi kufanywa na shirika la kimataifa la ICRC tangu waasi wa M23, kuanzisha mapigano makali dhidi ya wanajeshi wa serikali ya DRC, FRDC na washirika wao, na kisha kuyateka maeneo mengi ya Mashariki mwa Congo.
Utafiti huo umebainisha kuwa kila vituo tisa kati ya kumi havina dawa na vituo vingi vinakabiliwa na uhaba mkubwa wa madaktari, huku asilimia kumi na tatu ya vituo hivyo vimefungwa kabisa.
Ripoti zinasema kuwa uhaba wa dawa na madaktari ulianza punde tu kundi la M23 lilipouteka mji wa Goma mji ambao ndio mkubwa zaidi mashariki mwa DRC.
Rwanda imekanusha kuunga mkono kundi hilo la M23 na imerudi kusema kuwa shughuli zake katika eneo hilo ni za kujilinda kutokana na mashambulio yanayotekelezwa na waasi wa FDLR walioko nchini Congo. Lakini ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema Rwanda inadhibiti kundi hilo.
Mkurugenzi mkuu wa shirika la ICRC nchini DRC, Francois Moreillon, amesema janga la afya nchini DRC ni baya sana hasa kutokana na kuongezeka kwa mapigano na kupungua kwa ufadhili.
Shirika hilo limeonya kuwa maisha ya wakaazi wa mashariki mwa DRC yamo hatarini hasa kutokana na magonjwa ya Malaria, Ukimwi, kifua kikuu na magonjwa mengine ikiwa hayatatibiwa kwa wakati ufaao.
ICRC imetoa wito wa kuruhusiwa wahudumu wa afya katika maeneo yote yanaokumbwa na mapigano, ili kutoa huduma za afya na pia kujaza pengo zilizoachwa na madaktari waliokimbia mapigano.
Kundi la M23 na serikali ya DRC hawajasema lolote kuhusiana na ripoti hii.
Waziri anayetuhumiwa kughushi vyeti vya masomo ajiuzulu

Waziri wa Ubunifu, Sayansi na Teknolojia wa Nigeria, Uche Nnaji amejiuzulu siku chache baada ya kuibuka madai kuwa alighushi vyeti vyake vya masomo.
Kujiuzulu huko kunatokana na uchunguzi wa magazeti, uliodai Nnaji aliwasilisha vyeti vya uongo kwa Rais Bola Tinubu wakati wa uteuzi wake wa uwaziri mwaka 2023.
Msemaji wa Rais Bayo Onanuga amethibitisha kujiuzulu kwa Nnaji kupitia X siku ya Jumanne, akimnukuu waziri huyo akisema “amekuwa akilengwa na wapinzani wa kisiasa.”
Nnaji amekanusha tuhuma za kughushi na amesisitiza kuwa alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Nigeria, Nsukka (UNN) na shahada ya Microbiology/Biochemistry.
Madai hayo ya kughushi yamezua hasira miongoni mwa Wanigeria, kufuatia uchunguzi wa miaka miwili wa gazeti la Premium Times.
Wiki iliyopita, UNN iliripotiwa kuliambia gazeti hilo kwamba halina rekodi zinazothibitisha kwamba waziri huyo alihitimu Shahada ya Sayansi mwaka 1985, kama anavyodai.
Afisa mkuu wa chuo aliambia gazeti hilo kuwa Nnaji aliingia chuoni hapo mwaka 1981 lakini hakumaliza masomo yake wala kupokea cheti.
Kiongozi wa upinzani Atiku Abubakar ametaka uchunguzi huru na wa wazi kuhusu suala hilo, akisema Nnaji alipaswa “kufutwa kazi na kufunguliwa mashtaka kwa udanganyifu.”
Kusimamishwa au kuondolewa kwa waziri ni nadra nchini Nigeria – Nnaji ni wa pili kuondoka madarakani tangu Rais Tinubu aingie madarakani Mei 2023.
Januari iliyopita, aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kibinadamu na Kupunguza Umaskini, Betta Edu alisimamishwa kazi kufuatia ghadhabu ya umma kuhusu kashfa ya ufisadi. Dkt Edu, 37, alikanusha makosa yoyote.
Mtangulizi wa Tinubu, marehemu Muhammadu Buhari, aliwafuta kazi mawaziri wawili pekee katika kipindi chake cha miaka minane.
Israel yauzuia msafara mwingine wa boti za misaada unaoelekea Gaza

Msafara mpya wa misaada unaoelekea Ukanda wa Gaza ukiwa na chakula na vifaa vya matibabu umezuiliwa na wanajeshi wa Israel.
Msafara huo, unaoundwa na boti tisa na watu 150, ulisimamishwa katika maji ya kimataifa, kulingana na Muungano wa Freedom Flotilla na Thousand Madleens, ambao wanaendesha operesheni hiyo kwa pamoja.
“Jaribio lingine la kuvunja kizuizi cha kisheria cha majini na kuingia katika eneo la mapigano halijafanikiwa,” wizara ya mambo ya nje ya Israeli imesema.
Wiki iliyopita, jeshi la Israel lilisimamisha msafara wa boti 42 za misaada ukiwa na wanaharakati 479. Akiwemo mwanaharakati wa masuala ya mazingira wa Sweden, Greta Thunberg, walizuiliwa na baadaye kufukuzwa, lakini 138 wako kizuizini hadi sasa.
Waandalizi wa msafara huo mpya walisema boti zake tatu zilinaswa mapema asubuhi ya Jumatano, maili 120 kutoka pwani ya Gaza.
Ndani ya saa chache, taarifa zilionyesha boti zote tisa zilisimamishwa pia.
Serikali ya Israel imesema “boti na abiria wanapelekwa kwenye bandari ya Israel. Abiria wote wako salama na wana afya njema,” serikali ya Israel imesema.
Wanaharakati hao 150 wanatoka mataifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Uturuki ambayo wizara yake ya mambo ya nje iliita uingiliaji huo “ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa” na “kitendo cha uharamia.”
Israel imeunda mzingiro wa baharini kwenye pwani ya Gaza tangu 2007, wakati Hamas ilipochukua udhibiti wa Ukanda huo.
Serikali ya Burkina Faso yawashikilia wafanyakazi wa NGO kwa tuhuma za ‘ujasusi’

Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso imesema imewakamata wafanyakazi wanane wa shirika la kibinadamu lenye makao yake makuu nchini Uholanzi, ikiwatuhumu kwa “ujasusi na uhaini.”
Ni raia watatu kutoka Ulaya, Mmali, na Burkinabe wanne – miongoni mwao ni mkurugenzi na naibu wa NGO hiyo nchini Burkina Faso.
Waziri wa Usalama, Mahamadou Sana amesema shirika hilo lisilo la la serikali “lilikusanya na kusambaza taarifa nyeti za usalama ambazo zinaweza kuhatarisha usalama wa taifa na maslahi ya Burkina Faso, kwa mataifa ya kigeni.”
Shirika hilo la Kimataifa la Usalama wa NGO (INSO), ambalo hutoa taarifa za usalama kwa wafanyakazi wa misaada, limekanusha madai hayo.
Anthony Neal, mwakilishi wa shirika hilo lisilo la kiserikali ameiambia BBC kwamba mkurugenzi wake wa nchi ya Burkina Faso alizuiliwa tangu Julai wakati shirika hilo liliposimamishwa kazi. Wengine saba walikamatwa baadaye.
NGO hiyo ilisimamishwa Julai 31 kwa miezi mitatu na serikali kwa “kukusanya data nyeti bila idhini.” Imekuwa ikifanya kazi nchini tangu 2019.
Siku ya Jumanne, waziri wa usalama alisema licha ya kupigwa marufuku, wanachama wa shirika hilo waliendelea kukusanya taarifa kwa siri na kufanya mikutano.
Bw Neal amekanusha madai hayo, akisema shughuli zake za kukusanya taarifa zilikoma tarehe 31 Julai lakini wafanyakazi wake walibaki Burkina Faso kushughulikia marufuku hiyo na kutimiza ahadi za mkataba.
Taarifa ya shirika hilo imesisitiza kuwa taarifa inazokusanya si za siri na zilikusudiwa kwa ajili ya usalama wa wafanyakazi wa masuala ya kibinadamu.
Imeongeza kuwa serikali ya Burkinabé “wanafahamu kikamilifu” kazi yao na wamekuwa wakishirikiana na serkali.
Serikali ya kijeshi ya Burkina Faso inayoongozwa na Kapteni Ibrahim Traore ilichukua mamlaka katika mapinduzi miaka mitatu iliyopita, na imekuwa na uhusiano mbaya na mataifa ya Magharibi tangu wakati huo.
Katika kukabiliana na uasi unaozidi kuwa mbaya wa makundi ya Kiislamu yenye misimamo mikali, serikali ya kijeshi iliacha kufanya kazi na mkoloni wake wa zamani, Ufaransa, na badala yake ikageukia Urusi kwa usaidizi wa kijeshi.
Mashirika ya kutetea haki za binadamu tangu wakati huo yamelishutumu jeshi kwa kufanya dhuluma dhidi ya raia wakati wa kukabiliana na wanamgambo hao, na pia kukandamiza upinzani wa kisiasa na uhuru wa kujieleza.
Rais wa Madagascar kufanya mazungumzo ya kitaifa,

Rais wa Madagascar Andry Rajoelina amepanga kufanya “mazungumzo ya kitaifa” na makundi mbalimbali, ikiwa ni pamoja na wanafunzi, wawakilishi wa vijana, na viongozi wa kiroho katika ikulu yake baadaye mchana wa leo kwa saa za nchini humo.
Mazungumzo haya yanafuatia mfululizo wa mikutano aliyoifanya mwishoni mwa wiki ikiwa ni sehemu ya ahadi yake ya kuwasikiliza zaidi wananchi.
Jana usiku, aliteua mawaziri watatu wa baraza la mawaziri, wa Ulinzi, Usalama wa Umma, na Mjumbe wa Waziri anayesimamia polisi, kufuatia uteuzi wa awali wa Waziri Mkuu mpya.
Rais huyo anayekabiliwa na mzozo anaonekana kufanya kila kitu isipokuwa kutii matakwa ya waandamanaji vijana, ambao wamekuwa wakiandamana kwa zaidi ya wiki mbili.
Siku ya Jumanne, vijana waandamanaji walitoa makataa ya saa 48 kwa rais kutimiza matakwa yao la sivyo akabiliane na mgomo wa nchi nzima.
Lakini rais ameendelea kusisitiza umoja na haja ya kulinda nchi dhidi ya machafuko.
“Pamoja, lazima tuungane kupigana dhidi ya maovu haya na kujenga jamii mpya iliyosimikwa katika mshikamano na kuheshimiana,” aliandika Rajoelina jana kwenye ukurasa wa Facebook wa ofisi yake.
Baadhi ya raia wa Madagascar wameambia BBC kwamba ingawa wanaunga mkono malalamiko ya vijana hao, wana wasiwasi kwamba maandamano ya muda mrefu yanaweza kudhuru maisha yao.
“Ninamuunga mkono kikamilifu Gen Z, lakini sidhani kama maandamano ndiyo njia sahihi ya kushughulikia malalamiko yao. Watu wanapoandamana, siwezi kufanya biashara,” anasema Laza Brenda, ambaye anaendesha kioski cha kutengeneza simu za mkononi kando ya barabara.
Mjasiriamali Ulrichia Rabefitiavana anasema baadhi ya wateja wake wa kimataifa wameghairi kandarasi za mafunzo na hafla za semina ambazo kampuni yake ilikuwa ikisimamia kutokana na kutokuwa na uhakika uliosababishwa na maandamano.
Wakati Rajoelina akiendelea kupuuza wito wa kujiuzulu, na vyama vya upinzani vikishiriki zaidi katika maandamano yanayoongozwa na vijana, wengi wanahofia mzozo wa kisiasa unaoendelea utazidi kuwa mbaya katika siku zijazo.
Dada wa mwanamuziki Dolly Parton awaomba mashabiki wamuombee

Dada yake mwanamuziki Dolly Parton amewaomba mashabiki kumuombea mwimbaji huyo wa Marekani, kutokana na matatizo ya kiafya ambayo hayajabainishwa.
Gwiji huyo wa muziki wa Country mwenye umri wa miaka 79 aliahirisha matamasha ya Disemba, akiwaambia mashabiki anahitaji “taratibu za kitabibu” ili kukabiliana na “changamoto za kiafya” zinazoendelea.
“Jana usiku, nilikuwa nimekesha usiku kucha nikimuombea dada yangu, Dolly,” Freida Parton aliandika kwenye Facebook. “Wengi wenu mnajua hajisikii vizuri hivi karibuni.” “Kwa kweli ninaamini katika nguvu ya maombi, na nimeongozwa kuuomba ulimwengu wote unaompenda kuwa mashujaa wa maombi na kuomba pamoja nami.” Freida alimalizia ujumbe wake.
“Ana nguvu, anapendwa, na maombi yote yakiinuliwa kwa ajili yake, najua moyoni mwangu atakuwa sawa,” aliandika. “Godspeed, sissy yangu Dolly. Sote tunakupenda!”
Parton alikuwa ameratibiwa kufanya maonesho sita katika The Colosseum katika Caesars Palace mwezi Desemba.
Lakini aliahirisha maonesho hayo hadi Septemba mwaka ujao, akieleza kuwa hatakuwa na muda wa kutosha wa kuyafanyia mazoezi.
Parton hakufichua asili ya masuala ya afya yake, lakini hivi karibuni alilazimika kujiondoa kwenye hafla ya Dollywood baada ya kugunduliwa na jiwe la figo ambalo alisema lilikuwa linasababisha “matatizo mengi”.
Mapema mwaka huu, alipoteza mume wake mpendwa Carl Dean baada ya karibu miaka 60 ya ndoa.
Baadaye alitoa wimbo mpya, If You Had Been There, kwa kumbukumbu yake.
Mwanamuziki huyo anafahamika zaidi kwa vibao vingi vya country crossover vikiwemo Coat of Many Colours, I Will Always Love You, 9 To 5 na Jolene.
Somalia kuanzisha masomo ya lugha ya Kiswahili katika shule na vyuo vikuu

Somalia inatazamiwa kuanzisha lugha ya Kiswahili katika mtaala wa shule za kitaifa, Rais Hassan Sheikh Mohamud alitangaza jana wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiuchumi wa Afrika Mashariki (EACCON) mjini Mogadishu.
Katika mkutano huo unaohudhuriwa na mamia ya wajumbe, rais wa Somalia alitoa wito wa kuendelezwa kwa lugha ya Kiswahili.
“Vyuo vikuu vya nchi, hasa Chuo Kikuu cha Kitaifa cha Somalia, vinapaswa kuzingatia zaidi kukuza lugha ya Kiswahili, ambayo ni lugha ya Afrika Mashariki,” alisema rais wa Somalia.
Rais alisema hatua hii ni muhimu kwani hivi karibuni Somalia imekuwa sehemu ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
“Kukubali Kiswahili ni muhimu kwa ushirikiano wetu katika kanda,” alisema.
Waziri wa Elimu Farah Sheikh Abdulkadir pia alisema serikali inashirikiana na taasisi za kikanda kuandaa mfumo wa kukitambulisha Kiswahili nchi nzima.
“Tunajitahidi kuimarisha usomaji na utumiaji wa lugha ya Kiswahili nchini Somalia. Tunataka kuona Kiswahili kinakuwa lugha ya mawasiliano, biashara, na kujifunza, hata kuchukua nafasi ya Kiingereza wakati wa mkutano wetu ujao,” aliongeza.
Somalia ilijiunga rasmi na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) mwaka 2024, na kuwa nchi mshirika wa nane wa umoja huo pamoja na Kenya, Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Maelfu ya Wasomali wanazungumza Kiswahili, lugha ambayo Wasomali wamekuwa wakijifunza sana katika miongo ya hivi karibuni.
Shirika la Amnesty International lazitaka mamlaka za Tanzania kufichua alipo Polepole

Mamlaka za Tanzania hazina budi kufichua mara moja hatma na aliko aliyekuwa balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole, ambaye huenda alitoweka kwa nguvu.
Ni lazima pia wahakikishe usalama wake na kuwafikisha wale waliohusika na utekaji nyara wake na uwezekano wa kushambuliwa kwake mbele ya sheria kupitia michakato ya kisheria ya haki na ya uwazi, Amnesty International imesema katika taarifa iliyotolewa leo Oktoba 8, 2025.
Familia ya Humphrey Polepole ilisema ilitahadharishwa kuhusu uvamizi wa nyumba asubuhi ya tarehe 6 Oktoba 2025 katika makazi ya mwanadiplomasia huyo wa zamani na mkosoaji mkubwa wa serikali jijini Dar es Salaam.
Walipofika walikuta mlango umevunjwa, nyaya za umeme zikiwa zimekatwa na damu nyingi zikiwa kwenye eneo la tukio.
Video na picha zilizotolewa na familia zinaonekana kuthibitisha madai haya, zikionesha dalili za wazi za mapambano makali.
“Amnesty International ina wasiwasi mkubwa kwamba Humphrey Polepole anaweza kuwa alichukuliwa kwa nguvu na pengine kushambuliwa.
Serikali ya Tanzania lazima ifanye kila juhudi kumtafuta na kumrejesha kwenye usalama. Lazima wawajibishe watekaji,” Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika alisema.
Tukio hilo limekuja chini ya miezi mitatu baada ya Polepole kuripoti kuwa dada yake alitekwa nyara nyumbani kwake Bahari Beach, Dar es Salaam, Julai 17, 2025.
Alipigwa na baadaye kutupwa nyumbani kwake siku iliyofuata, usiku.
Kesi hii inaongeza katika orodha inayokua ya upotevu na mashambulizi dhidi ya wakosoaji wa serikali nchini Tanzania, na kuibua wasiwasi mkubwa kuhusu vitendo vya kimabavu nchini na kuongeza ukandamizaji wa kisiasa kabla ya uchaguzi mkuu wa Tanzania, unaotarajiwa kufanyika tarehe 29 Oktoba 2025.
Polepole aliyewahi kuwa kigogo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) alijiuzulu wadhifa wake wa kidiplomasia mapema mwaka 2025 baada ya kuikosoa serikali hadharani kwa kutozingatia haki, sheria na misingi ya katiba.
“Watu wengi sana wametoweka nchini Tanzania, katika miaka ya hivi karibuni bila uwajibikaji wowote. Mamlaka lazima zikomeshe hali hii ya kutokujali,” Tigere Chagutah alisema.
Familia ya Polepole iliripoti tukio hilo katika Kituo cha Polisi cha Mbezi tarehe 6 Oktoba, na wakili wake aliwasilisha ombi la ‘habeas corpus’ mahakamani tarehe 7 Oktoba 2025.
Wanafamilia waliiambia Amnesty International kwamba wakati wa uchunguzi wa polisi kuhusu kesi ya Polepole, askari walichukua vitu kadhaa kutoka nyumbani kwake, ikiwa ni pamoja na mashine yake ya na sefu.
Msemaji wa Polisi David Misime alisema Polepole alitakiwa kufika mbele ya Kurugenzi ya Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kutokana na tuhuma zilizotolewa kwenye mitandao ya kijamii lakini ameshindwa kutekeleza.
Mamlaka zinasema kuwa zinafanya kazi ili kuthibitisha uhalisi wa madai ya utekaji nyara.
Takriban watu 24 wameuawa baada ya parachuti kurusha mabomu kwenye tamasha Myanmar

Shambulio la kigaidi kwenye tamasha na maandamano katikati mwa Myanmar limeua takriban watu 24 na kuwajeruhi wengine 47, msemaji wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyo uhamishoni aliiambia BBC Burma.
Takribani watu 100 walikuwa wamekusanyika katika kitongoji cha Chaung U Jumatatu jioni kwa ajili ya tamasha la Thadingyut, sikukuu ya kitaifa yenye mizizi ya Wabudha ,wakati parachuti iliyokuwa na nguvu ya injini ilipodondosha mabomu mawili juu ya umati, afisa wa eneo hilo chini ya Kikosi cha Ulinzi cha Wananchi cha kupambana na junta alisema.
Tukio hilo pia lilikuwa mkesha wa mishumaa kupinga sera za junta.
Myanmar imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe tangu jeshi lake kunyakua mamlaka katika mapinduzi ya 2021.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa mzozo huo umeua zaidi ya raia 5,000.
Afisa huyo wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi aliiambia BBC Burma kwamba wakati wa mkusanyiko huo siku ya Jumatatu, walipata taarifa kuhusu uwezekano wa kutokea shambulio la angani na kujaribu kumaliza haraka maandamano yao, lakini waandamanaji walifika eneo la tukio mapema kuliko walivyotarajia.
“Walifika na kurusha bomu ndani ya dakika saba tu,” alisema.
“Bomu la kwanza lilipoanguka, nilianguka chini, lakini lilipiga sehemu ya chini ya goti langu.
Kulikuwa na watu waliouawa kando yangu.” Wenyeji waliambia BBC Burma kwamba uharibifu uliosababishwa na mabomu siku ya Jumatatu ulifanya iwe vigumu kutambua miili.
Mjumbe maalum wa Marekani, mkwe wa Trump kujiunga na mazungumzo ya amani ya Gaza

Mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff na mkwe wa Rais wa Marekani Donald Trump, Jared Kushner watajiunga na mazungumzo ya mpango wa amani wa Gaza kati ya wapatanishi wa Israel na Hamas nchini Misri siku ya Jumatano.
Kuwasili kwao kunakuja wakati siku ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja Jumanne ilimalizika bila matokeo yanayoonekana, afisa mkuu wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo aliiambia BBC.
Trump alitoa maoni siku ya Jumanne, wakati Israel ikiadhimisha kumbukumbu ya mwaka wa pili wa mashambulizi ya Oktoba 7 ya Hamas, akisema “kuna uwezekano kwamba tunaweza kuwa na amani Mashariki ya Kati”.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu hakuzungumzia hali ya mazungumzo hayo, lakini aliwaambia Waisraeli kuwa walikuwa katika “siku mbaya za uamuzi”.
Katika chapisho kwenye X, Netanyahu aliongeza kuwa Israel itaendelea kuchukua hatua ili kufikia malengo yake ya vita: “Kurejea kwa wote waliotekwa nyara, kuondolewa kwa utawala wa Hamas na ahadi kwamba Gaza haitakuwa tishio tena kwa Israel”.
Witkoff na Kushner walitarajiwa kuondoka Marekani Jumanne jioni na kuwasili Misri siku ya Jumatano, chanzo kinachofahamu kuhusu mazungumzo hayo kiliiambia BBC.
Bei ya dhahabu yapanda Marekani, wawekezaji watafuta mahali salama kuweka pesa zao

Bei ya dhahabu imefikia rekodi ya juu ya zaidi ya $4,000 (£2,985), huku wawekezaji wakitafuta maeneo salama ya kuweka pesa zao kutokana na wasiwasi kuhusu kutokuwa na uhakika wa kiuchumi na kisiasa kote ulimwenguni.
Gharama ya dhahabu imeshuhudia kupanda zaidi tangu miaka ya 1970, ikipanda kwa zaidi ya 25% tangu Aprili wakati Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza ushuru ambao umevuruga biashara ya kimataifa.
Wachambuzi wanasema suala jingine linalowatia wasiwasi wawekezaji ni kuchelewa kutolewa kwa data muhimu za kiuchumi kutokana na kufungwa kwa serikali ya Marekani, huku ikitarajiwa kuingia wiki yake ya pili.
Dhahabu inaonekana kama kinachojulikana kama uwekezaji wa mahali salama, ambao unatarajiwa kuhifadhi au kuongeza thamani yake wakati wa misukosuko ya soko au kuzorota kwa uchumi.
Bei ya dhahabu safi, kiasi unachopokea ukiuza madini hayo ya thamani kwenye kaunta, ilipanda zaidi ya $4,011 kwa ounce moja Jumatano asubuhi huko Asia.
Kufungwa kwa serikali ya Marekani, ambako kulichochewa na msukosuko wa mara kwa mara juu ya matumizi ya umma, ni “kinyume cha bei ya dhahabu”, alisema Christopher Wong wa OCBC, ambaye ni mtaalamu wa mikakati wa benki hiyo yenye makao yake makuu Singapore.
Wawekezaji wamegeukia mali salama kama dhahabu wakati wa kufungwa kwa serikali ya Marekani hapo awali.
Waisraeli waadhimisha kumbukumbu ya Oktoba 7 huku mazungumzo kuhusu mpango wa amani wa Gaza yakiendelea

Waisraeli wamekusanyika nchini kote kuadhimisha miaka miwili tangu shambulio lililoongozwa na Hamas tarehe 7 Oktoba 2023, huku mazungumzo yakiendelea nchini Misri kuhusu kumalizika kwa vita huko Gaza.
Shambulizi hilo lilishuhudia zaidi ya watu 1,200 wakiuawa na wengine 251 kurudishwa Gaza kama mateka. Ilikuwa siku moja mbaya zaidi kwa Wayahudi tangu mauaji ya Holocaust.
Israel ilijibu kwa kuanzisha mashambulizi ya kijeshi huko Gaza ambayo yameua zaidi ya watu 67,000, kulingana na wizara ya afya ya eneo hilo inayoendeshwa na Hamas.
Takwimu zake zinaonekana kuwa za kuaminika na UN na mashirika mengine ya kimataifa.
Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu alisema katika taarifa yake kwamba pamoja na “maumivu makubwa”, Israel imeonesha “ustahimilivu wa kimiujiza”.
Wakati huo huo, timu za mazungumzo za Israel na Hamas zilikutana katika eneo la mapumziko la Bahari ya Shamu la Misri la Sharm el-Sheikh kwa siku ya pili ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja kujadili masharti ya pendekezo hilo.
Afisa mkuu wa Palestina anayefahamu mazungumzo hayo aliiambia BBC kwamba kikao cha asubuhi kilimalizika bila matokeo yanayoonekana, huku kukiwa na kutoelewana kuhusu mapendekezo ya ramani ya Israel ya kujiondoa kutoka Gaza na juu ya dhamana ya Hamas inataka kuhakikisha Israel haianzishi tena mapigano baada ya awamu ya kwanza ya mpango huo.
Aliongeza kuwa mazungumzo hayo ni “magumu na bado hayajaleta mafanikio yoyote ya kweli,” lakini alibainisha kuwa wapatanishi wanafanya kazi kwa bidii ili kupunguza mapengo kati ya pande hizo mbili.
Hapo awali, afisa wa Palestina alisema mazungumzo hayo yalilenga katika masuala matano muhimu: usitishaji vita wa kudumu; kubadilishana mateka ambao bado wanashikiliwa na Hamas kwa wafungwa wa Kipalestina na wafungwa kutoka Gaza; kuondolewa kwa majeshi ya Israel kutoka Gaza; mipango ya utoaji wa misaada ya kibinadamu; na utawala wa baada ya vita wa eneo hilo.
Afisa wa soka wa Japan ahukumiwa kwa kutazama picha za unyanyasaji wa watoto

Afisa mkuu wa Shirikisho la Soka la Japan (JFA) amehukumiwa kifungo cha miezi 18 jela nchini Ufaransa baada ya kunaswa akitazama picha zinazoonesha unyanyasaji wa kingono kwa watoto akiwa ndani ya ndege, shirika hilo lilisema Jumanne.
Mkurugenzi wa kiufundi Masanaga Kageyama alizuiliwa wiki iliyopita wakati akiwa katika uwanja wa ndege wa Charles de Gaulle mjini Paris, gazeti la Ufaransa Le Parisien liliripoti, na kuongeza kwamba baadaye alikiri kuzitazama picha hizo, akisema hakujua kuwa ni kinyume cha sheria nchini Ufaransa.
Inaaminika kuwa alikuwa akielekea kwenye Kombe la Dunia la Vijana chini ya miaka 20 nchini Chile.
JFA ilisema mkataba wake utasitishwa mara moja, na kuongeza kuwa tukio hilo “halikubaliki kwenye ulimwengu wa soka”.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa mahakama iliiambia shirika la habari la AFP kwamba wafanyakazi wa ndege hiyo walitoa tahadhari baada ya kumuona Kageyama akitazama picha za ngono kwenye ndege.
Alikuwa akitumia kompyuta yake ya mkononi kwenye daraja la biashara la ndege ya Air France, na alipokabiliwa alidai kuwa picha hizo zilikuwa za “sanaa” na zilitengenezwa na AI, Le Parisien iliripoti.
Siku ya Jumatatu, mahakama ilimhukumu mwanaume huyo mwenye umri wa miaka 58 kifungo cha jela na faini ya euro 5,000 ($5,800) pamoja na marufuku ya miaka 10 ya kufanya kazi na watoto au kurejea Ufaransa, AFP iliripoti.
Katika taarifa ya Jumanne, JFA iliomba radhi kwa “matatizo” yaliyosababishwa na tukio hilo.
Ronaldo atajwa kuwa mwanasoka wa kwanza bilionea

Cristiano Ronaldo ametajwa kuwa mchezaji bilionea wa kwanza katika soka, kwa mujibu wa chombo cha habari cha masuala ya fedha, Bloomberg.
Ripoti juu ya mabilionea ya Bloomberg, ambayo inawafuatilia watu matajiri zaidi duniani kulingana na thamani yao halisi, imepima utajiri wa mshambuliaji huyo wa Ureno mwenye umri wa miaka 40 na Al-Nassr kwa mara ya kwanza.
Tathmini hiyo inazingatia mapato ya kazi, uwekezaji na matangazo na inasema thamani halisi ya Ronaldo ni dola bilioni 1.4 (£1.04bn).
Inasema alipata zaidi ya dola milioni 550 (£410m) kama mshahara kati ya 2002 na 2023, na mapato yake yaliyoripotiwa kupitia mikataba na ufadhili, ikiwa ni pamoja na mkataba wa muongo mmoja na Nike wenye thamani ya karibu dola milioni 18 (£13.4m) kwa mwaka.
Ronaldo alipojiunga na Al-Nassr kwenye Ligi ya Saudia mwaka 2022 aliripotiwa kuwa mchezaji anayelipwa vizuri zaidi katika historia ya soka na mshahara wa mwaka wa pauni milioni 177.
Mkataba wake ulipaswa kumalizika Juni 2025 lakini alitia saini mkataba mpya wa miaka miwili – unaoripotiwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola milioni 400m (£298m) – ambao utamweka katika klabu hiyo hadi atakapo timiza miaka 42.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.