Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Israel na Hamas wanatarajiwa kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Misri leo, yenye lengo la kutekeleza mpango wa amani wa Donald Trump wa Gaza.
Na:Cantona Joseph|RFA
Watu 21 wameuawa huko Gaza na wengine 96 kujeruhiwa katika saa 24 zilizopita, wizara ya afya inayoendeshwa na Hamas inasema katika taarifa yake ya hivi punde.
Kwa upande mwingine kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) imesema iko tayari kufanya kazi katika kubadilishana mateka wanaoshikiliwa Gaza na wafungwa nchini Israel.
NGO hiyo imesimamia kuachiliwa kwa mateka 148 na wafungwa 1,931 tangu Oktoba 2023, pamoja na kurejea kwa mabaki ya binadamu.
“Usitishaji mapigano wa kudumu ni muhimu katika kuokoa maisha na kuvunja mzingiro wa vifo na uharibifu,” rais wa ICRC Mirjana Spoljaric anasema.
“Pia tuko tayari kuleta misaada huko Gaza na kuisambaza kwa usalama kwa raia wanaohitaji sana.”
Israel na Hamas wanatarajiwa kuanza mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja nchini Misri leo, yenye lengo la kutekeleza mpango wa amani wa Donald Trump.
Hamas imekubali sehemu za mpango wa Trump wenye vipengele 20 – ikiwa ni pamoja na kuachiliwa kwa mateka wa Israel – lakini haijakubali masharti yote.
Ujumbe wa Hamas unaongozwa na Khalil al-Hayya, ambaye Israel ilijaribu kumuua nchini Qatar mwezi uliopita.
Idadi ya waliouawa tangu jeshi la Israel lianzishe mashambulizi kujibu shambulio lililoongozwa na Hamas kusini mwa Israel tarehe 7 Oktoba 2023 imeongezeka hadi 67,160, wizara hiyo inasema.
Wengi wa waliouawa na kujeruhiwa bado wako chini ya vifusi, na huduma za dharura kwa sasa haziwezi kuwafikia, wizara hiyo inasema.
Polisi Tanzania watuhumiwa kuwajeruhi wanachama 16 wa Chadema

Jeshi la polisi nchini Tanzania lanatuhumiwa kuwajeruhi wanachama 16 wa chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakati wa makabiliano nje ya mahakama jijini Dar es Salaam.
Kundi hilo lilikuwa limekusanyika kufuatilia mwenendo wa kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti wa chama chao, Tundu Lissu.
Chama hicho ambacho ni kikuu cha upinzani nchini Tanzania kimesema wanachama wake kadhaa walijeruhiwa wakati polisi wakiwaondoa kwa nguvu kutoka katika majengo ya mahakama.
Chadema imelaani tukio hilo na kueleza kuwa ni ukandamizaji wa kikatili dhidi ya wafuasi wa upinzani.
Imesema waliojeruhiwa wanapatiwa matibabu hospitalini.
Polisi bado hawajazungumza chochote kuhusu tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Chadema, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche amefika hospitali ya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaa, kuwajuulia hali majeruhi.
Kwa upande mwingine, mvutano umetokea kati ya baadhi ya mawakili wa Jamhuri na wale wa upande wa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu muda mfupi baada ya kesi ya uhaini inayomkabili mwenyekiti huyo kuahirishwa.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi, mvutano huo ulitokea leo Jumatatu, Oktoba 6, 2025, katika ukumbi wa Mahakama Kuu, Masjala Ndogo ya Dar es Salaam, ambapo mawakili waliokuwa wakimsaidia Lissu kisheria pamoja na makada wa Chadema waliokuwa mahakamani hapo kufuatilia kesi hiyo waligombea sehemu ya kukaa na baadhi ya mawakili wa Serikali.
Tukio hilo lilijiri muda mfupi baada ya mahakama kuahirisha kesi na Lissu kurejeshwa rumande, hali iliyosababisha mawakili na baadhi ya wafuasi kutupiana maneno kwa dakika chache kabla kutulizwa.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi kesho, wakati mahakama hiyo ikitarajiwa kujibu hoja zilizotolewa katika kikao cha Jumatatu.
Wakati wa shauri hilo, Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu, alihoji kwa nini tarehe ya hukumu imepangwa kabla ya kesi hiyo kuanza.
Lissu anakabiliwa na mashtaka ya uhaini. Ikiwa atapatikana na hatia, anaweza kukabiliwa na adhabu ya kifo.
Trump kuwapa kipaumbele wakimbizi Wazungu kutoka Afrika Kusini

Utawala wa Rais Donald Trump, Marekani unajiandaa kuweka kiwango cha kupokea wakimbizi kuwa watu 7,500 mwaka huu, na kuwapa kipaumbele Waafrika Kusini Wazungu, wamesema watu watatu wanaofahamu suala hilo.
Iwapo mpango huo utakamilika, kiwango kilichopangwa kitashuka kutoka watu 125,000 kilichowekwa mwaka jana chini ya Rais wa zamani Joe Biden.
Trump, kutoka chama cha Republican, alipunguza viwango vya kupokea wakimbizi wakati wa urais wake mwaka 2017-2021 kama sehemu ya kupunguza uhamiaji halali na haramu. Baada ya kurejea ofisini Januari 2025, alizuia kupokea wakimbizi.
Wiki kadhaa baadaye, Trump alitoa agizo kuwa wakimbizi kutoka Waafrika Kusini wenye asili ya Kizungu ambao ni wachache katika nchi hiyo, kuwa wanakabiliwa na ubaguzi wa rangi na ghasia.
Serikali ya Afrika Kusini imekanusha madai hayo.
Kundi la kwanza la Waafrika Kusini 59 waliwasili mwezi Mei, na kufikia 138 mwanzoni mwa Septemba, Reuters iliripoti.
Katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa wiki iliyopita, Trump alihimiza mataifa mengine kujiunga na kampeni ya kimataifa ya kurejesha ulinzi mkali wa mipaka, na kuunda mfumo mpya kuhusu wahamiaji.
Kesi yafunguliwa dhidi ya mtengeneza dawa za kikohozi zinazohusishwa na vifo vya watoto

Polisi nchini India wameanza kuchukua hatua dhidi ya mtengenezaji wa dawa ya kikohozi, ambayo ilipatikana na viwango hatari vya kemikali ya sumu, baada ya vifo vya watoto 14 wanaoaminika kutumia dawa hiyo.
India imekabiliwa na uchunguzi juu ya ubora wa dawa zake, huku dawa za kikohozi zikihusishwa na vifo vya watoto nchini Cameroon, Gambia na Uzbekistan katika miaka michache iliyopita.
Sampuli ya dawa ya, ‘Coldrif’, kati ya dawa 19 zilizochunguzwa baada ya vifo katika jimbo la Madhya Pradesh, zilikuwa na 46.28% ya kemikali ya diethylene glycol, ambayo inazidi kiwango kinachoruhusiwa cha 0.1%, maabara ya serikali ya dawa ilisema katika ripoti yake..
Polisi wamesajili kesi ya jinai siku ya Jumapili dhidi ya daktari na mtengenezaji.
Diethylene glycol, inayotumika katika bidhaa kama vipodozi na vilainishi, husababisha dalili ambazo Shirika la Afya Ulimwenguni linasema zinaweza kuwa ni kutapika na maumivu ya tumbo hadi kudhuru figo, na inaweza kusababisha kifo.
Kampuni ya Sresan Pharma inakabiliwa na shutuma za mauaji ya bila kukusudia, kubadilisha muundo wa dawa, na kutengeneza, kuuza au kusambaza dawa kinyume na Sheria ya Dawa na Vipodozi.
Hatua za udhibiti pia zimechukuliwa dhidi ya kampuni hiyo, wizara ya afya imesema, bila kutoa maelezo, na Shirika la Kudhibiti Dawa lilipendekeza kufutwa kwa leseni yake ya utengenezaji.
Kampuni ya Sresan Pharma haijatoa kauli yoyote hadi sasa.
Iwapo watapatikana na hatia, kampuni hiyo na maafisa wake wanaweza kukabiliwa na faini na kifungo cha maisha jela.
India inasambaza 40% ya zinazotumika Marekani, 25% ya dawa zote zinazotumika Uingereza, na zaidi ya 90% ya dawa zote katika mataifa mengi ya Afrika.
Mvua kubwa yasababisha vifo vya watu 47 Nepal

Mvua kubwa imesababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko yaliyofunga barabara, kusomba madaraja na kuua watu wasiopungua 47 tangu Ijumaa nchini Nepal, maafisa walisema siku ya Jumapili.
Watu 35 waliuawa katika maporomoko ya udongo katika wilaya ya Ilam mashariki inayopakana na India, alisema Kalidas Dhauboji, msemaji wa Jeshi la Polisi.
Watu tisa walitoweka baada ya kusombwa na mafuriko na wengine watatu waliuawa katika radi katika maeneo mengine nchini Nepal, aliongeza.
“Juhudi za uokoaji watu waliopotea zinaendelea,” alisema Shanti Mahat, msemaji wa Mamlaka ya Usimamizi wa Maafa nchini Nepal.
Katika mpaka katika eneo la mlima la Darjeeling mashariki mwa India huko West Bengal, takriban watu saba waliuawa kutokana na maporomoko ya ardhi kufuatia mvua kubwa, kulingana na ripoti za vyombo vya habari vya ndani.
“Miili saba tayari imepatikana kutoka kwenye vifusi. Tuna taarifa kuhusu watu wawili kufukiwa. Kazi inafanywa kuipata miili yao pia,” Abhishek Roy, afisa wa polisi wa wilaya ya Darjeeling alisema Jumapili, kulingana na chapisho la shirika la habari la India ANI kwenye mtandao wa kijamii X.
Barabara kuu kadhaa zimezibwa na maporomoko ya ardhi na kusombwa na mafuriko, na kusababisha mamia ya abiria kukwama, mamlaka imesema.
“Safari za ndege za ndani kwa kiasi kikubwa zimetatizika lakini safari za ndege za kimataifa zinafanya kazi kama kawaida,” alisema Rinji Sherpa, msemaji wa uwanja wa ndege wa Kathmandu.
Mamia ya watu hufa kila mwaka katika maporomoko ya ardhi na mafuriko ambayo ni ya kawaida Nepali, nchi yenye milima mingi wakati wa msimu wa mvua nyingi, ambayo kwa kawaida huanza katikati ya Juni na kuendelea hadi katikati ya Septemba.
Maafisa wa mamlaka ya hali ya hewa walisema mvua huenda ikanyesha hadi Jumatatu na wanachukua “tahadhari ya hali ya juu” kusaidia watu walioathiriwa na janga hilo.
Waziri Mkuu wa Ufaransa ajiuzulu chini ya mwezi mmoja madarakani

Waziri Mkuu wa Ufaransa Sébastien Lecornu amejiuzulu, chini ya siku moja baada ya baraza lake la mawaziri kutangazwa.
“Masharti hayakutimizwa ili mimi kuwa waziri mkuu,” Lecornu alisema Jumatatu asubuhi, na kukosoa ukosefu wa utayari kwa vyama vya siasa ili kufikia makubaliano.
Ikulu ya Elysée ilitoa tangazo hilo baada ya Lecornu kukutana na Rais Emmanuel Macron kwa saa moja Jumatatu asubuhi.
Hatua hiyo ya kushangaza inajiri siku 26 baada ya Lecornu kuteuliwa kuwa waziri mkuu kufuatia kusambaratika kwa serikali ya awali ya François Bayrou.
Vyama vyote katika Bunge la Kitaifa vilikosoa vikali muundo wa baraza la mawaziri la Lecornu, ambalo kwa kiasi kikubwa halijabadilishwa kutoka la Bayrou, na kutishia kupiga kura kulisambaratisha.
Vyama vingi sasa vinataka uchaguzi wa mapema, huku baadhi wakimtaka Macron ajiuzulu – ingawa amekuwa akisema hatajiuzulu kabla ya muhula wake kumalizika 2027.
“Jambo la busara la kufanya sasa ni kufanya uchaguzi,” amesema Marine Le Pen wa chama cha mrengo wa kulia, National Rally (RN).
Lecornu – waziri wa zamani wa majeshi na mtu wa karibukwa Macron – alikuwa waziri mkuu wa tano wa Ufaransa katika kipindi cha chini ya miaka miwili.
Siasa za Ufaransa zimekuwa na msukosuko mkubwa tangu Julai 2024, wakati uchaguzi wa bunge uliposababisha kokosekana chama chenye wingi wa viti.
Hii imefanya kuwa vigumu kwa waziri mkuu yeyote kupata uungwaji mkono unaohitajika kupitisha miswada yoyote.
Serikali ya Bayrou ilipigiwa kura ya kutokuwa na imani mwezi Septemba baada ya bunge la Ufaransa kukataa kuunga mkono bajeti yake ya kubana matumizi, ambayo ililenga kupunguza matumizi ya serikali kwa €44bn ($51bn; £38bn).
Wagonjwa sita wafariki dunia kwa ajali ya moto wakiwa ICU huko India

Wagonjwa sita waliokuwa mahututi wamefariki dunia katika ajali ya moto iliyozuka katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) cha hospitali iliyoko katika mji wa Jaipur, magharibi mwa India.
Moto huo, unaoshukiwa kusababishwa na shoti ya umeme, ulianza Jumapili usiku katika eneo la wagonjwa wanaohitaji uangalizi wa karibu ICU la Hospitali ya Sawai Man Singh.
Wagonjwa 11 walikuwa ICU wakati huo.
Waathiriwa ni pamoja na wanawake wawili na wanaume wanne.
Jamaa za waathiriwa wameshutumu wafanyakazi kwa uzembe, jambo ambalo viongozi wa hospitali wamekanusha.
Serikali ya jimbo la Rajasthan, ambalo mji mkuu wake ni Jaipur, imetangaza uchunguzi kuhusu tukio hilo.
“Kila hatua inayowezekana inachukuliwa ili kuhakikisha usalama wa mgonjwa, matibabu, na utunzaji kwa wale walioathiriwa, na hali hiyo inafuatiliwa kila wakati,” Waziri Mkuu wa jimbo hilo Bhajanlal Sharma alisema Jumapili.
Hospitali ya Sawai Man Singh, inayoendeshwa na serikali ya jimbo, ni mojawapo ya hospitali kubwa zaidi mjini Rajasthan na inatibu maelfu ya wagonjwa kila siku.
Moto huo ulizuka kabla ya saa sita usiku katika kituo cha majeruhi cha hospitali hiyo na punde ukasambaa ndani ya jengo hilo.
Wagonjwa 14 walihamishwa kutoka wadi ya karibu ya ICU huku moshi mwingi ukitawala chumba hicho.
Zimamoto walivunja madirisha na kukabiliana na moto huo kwa karibu saa mbili kabla ya kuudhibiti, shirika la habari la PTI liliripoti.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.