Trump awataka wapatanishi ‘kufanya haraka’ huku mazungumzo muhimu ya amani ya Gaza yakianza

Radio Fortune Africa -Ukweli na Burudani

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Rais wa Marekani Donald Trump amewataka wote wanaohusika katika juhudi za kumaliza vita vya Gaza “kufanya haraka” huku wapatanishi wakipanga kukutana nchini Misri siku ya Jumatatu.

Trump

Na:Cantona Joseph|RFA

Rais wa Marekani Donald Trump amewataka wote wanaohusika katika juhudi za kumaliza vita vya Gaza “kufanya haraka” huku wapatanishi wakipanga kukutana nchini Misri siku ya Jumatatu kwa mazungumzo ya amani yasiyo ya moja kwa moja kati ya Hamas na Israel.

Mazungumzo hayo yanakuja baada ya Hamas kukubaliana na baadhi ya sehemu za mpango wa amani wa Marekani wenye vipengele 20, ikiwa ni pamoja na kuwaachia huru mateka na kukabidhi utawala wa Gaza, lakini wanatafuta mazungumzo kuhusu masuala mengine.

Majibu ya kundi hilo hayakutaja matakwa muhimu ya kuweka silaha chini na kutokuwa na jukumu la baadaye katika utawala wa Gaza.

Akiandika kwenye mitandao ya kijamii kwamba mazungumzo yalikuwa “yamefanikiwa sana”, Trump alisema: “Nimeambiwa awamu ya kwanza inapaswa kukamilika wiki hii, na ninaomba kila mtu afanye haraka.”

Mpango huo wenye vipengele 20 unapendekeza kusitishwa mara moja kwa mapigano na kuachiliwa kwa mateka 48, 20 pekee kati yao wanaodhaniwa kuwa hai, badala ya mamia ya Wagaza wanaozuiliwa.

Netanyahu alisema katika hotuba ya runinga siku ya Jumamosi kwamba anatumai kutangaza kuachiliwa kwa mateka “katika siku zijazo”.

Shughuli za uokoaji zaendelea baada ya mamia kukwama mlima Everest

Everest ndio kilele cha juu zaidi ulimwenguni cha zaidi ya 8,849m.

Shughuli za uokoaji zaendelea baada ya mamia kukwama mlima Everest.

Zaidi ya wasafiri 200 walikwama kwenye theluji kwenye miteremko ya Tibet ya Mlima Everest , huku vyombo vya habari vya serikali ya China vikisema kuwa wote wamewasiliana na mamlaka.

Takribani wasafiri 350 wamehamishiwa hadi sehemu salama katika kitongoji cha eneo hilo.

Haya yanajiri huku kukiwa na hali mbaya ya hewa katika eneo hilo. Katika nchi jirani ya Nepal, takriban watu 47 wamekufa tangu Ijumaa baada ya mvua kubwa kusababisha maporomoko ya ardhi na mafuriko.

Everest ndio kilele cha juu zaidi ulimwenguni cha zaidi ya 8,849m. Ingawa watu wengi hujaribu kupanda kilele kila mwaka, inachukuliwa kuwa safari hatari sana.

Polisi Tanzania yaonya usambazaji maudhui ya ‘uhalifu na uchochezi’

Jeshi la Tanzania, limetoa tamko la onyo dhidi ya majaribio ya kulihusisha jeshi hilo katika siasa.

Jeshi la Polisi nchini Tanzania limetoa onyo dhidi ya kile wanachodai matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kueneza maudhui yanayodhaniwa kuwa ya uhalifu na uchochezi, kufuatia kusambaa kwa video inayomuonesha mtu anayejitambulisha kwa jina la ‘Kapteni Tesha’ ambaye ni afisa wa Jeshi la Tanzania (JWTZ).

Katika video hiyo, mwanaume ambaye hadhi yake ya kijeshi haijathibitishwa anaonesha ukosoaji mkali kwa serikali, akidai ufisadi, uingiliaji wa kisiasa katika jeshi na ukiukaji wa haki za binadamu.

Katika video hiyo ya saa 1 na dakika 20, ‘Kapteni Tesha’ anaonekana akimtaka Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Jacob Mkunda kuchukua jukumu hilo na kuhakikisha nchi inaungana na kuzingatia haki za raia wake.

Taarifa iliyotolewa na polisi Jumapili, ilionya kuwa kumekuwa na mtindo wa watu kushiriki maudhui kwenye mitandao ya kijamii ambayo si tu kwamba ni kinyume cha sheria kwa mujibu wa sheria za nchi bali pia yanatishia utulivu wa umma na kudhoofisha maadili ya Kitanzania.

“Tabia hizi lazima zilaaniwe na kupigwa vita na mtu yeyote anayeelewa umuhimu wa amani kwao na kwa familia zao,” ilisema taarifa hiyo.

Mapema jeshi la Tanzania, TPDF ilitoa tamko la onyo dhidi ya majaribio ya kulihusisha jeshi hilo katika siasa.

Taarifa hiyo ilieleza wasiwasi wake juu ya kile ilichoeleza kuwa ni mwenendo unaokua wa watu wanaojaribu kuhusisha jeshi na ajenda ya kisiasa kupitia mitandao ya kijamii.

Kaimu Mkurugenzi wa Habari na Uhusiano wa Jeshi hilo Kanali Bernard Masala Mlunga alieleza kuwa baadhi ya watu hao wanadai kuwa wanajiunga na jeshi hilo kwa uongo au ni waliokuwa wanachama waliofukuzwa kazi kwa utovu wa nidhamu au harakati za kisiasa.

“Jeshi linaendelea kutekeleza majukumu yake ya kikatiba kwa uadilifu, uaminifu na weledi kwa mujibu wa sheria za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,” alisema Kanali Mlunga.

BBC iliwasiliana na maafisa wa kijeshi ili kutoa maoni na kuthibitisha utambulisho wake lakini haikupata majibu.

Wanaharakati wa Tanzania wamesambaza video hiyo inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii wakidai kuwa jeshi linaunga mkono raia wake.

Haya yanajiri huku Tanzania ikijiandaa kufanya uchaguzi mkuu ndani ya wiki tatu. Chama kikuu cha upinzani Chadema kimepigwa marufuku kushiriki uchaguzi na kiongozi wake Tundu Lissu ambaye yuko rumande anakabiliwa na kesi ya uhaini.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment