Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Ikulu ya Marekani inasema itaanza kuwaachisha kazi wafanyikazi wengi wa serikali ndani ya siku mbili, huku wabunge wakilaumiwa kwa kusitisha shughuli za serikali kwa mara ya kwanza katika karibu miaka saba.
Shughuli za serikali zilianza kutatizika siku ya Jumatano baada ya Republican na Democrats bungeni kushindwa kukubaliana juu ya mpango mpya wa matumizi kabla ya tarehe ya mwisho ya usiku wa manane.
Kuna dalili ndogo kwamba pande zote mbili ziko tayari kuafikiana, na kura ya kumaliza kulemaa kwa shughuli hizo ilishindikana saa chache baada ya kuanza.
Tangu wakati huo, bunge la Seneti limeahirisha vikao vyake, na hivyo kuzua hofu kwamba hatua hiyo inaweza kuendelea na kutishia mamia ya maelfu ya kazi na vile vile hatari ya kugharimu uchumi wa Marekani kwa kupotea kwa mabilioni.
Wanaharakati wa Kenya Bob Njagi, Nicholas Oyoo watekwa nyara nchini Uganda

Wanaharakati wawili wa Kenya, Bob Njagi na Nicholas Oyoo, Jumatano alasiri walidaiwa kutekwa nyara na watu wanne waliokuwa na silaha wanaoaminika kuwa maafisa wa usalama.
Wawili hao, ambao walikuwa wamejiunga na kampeni za mgombea urais wa chama cha National Unity Platform, BObi Wine mnamo Jumanne , waliripotiwa kulazimishwa kuingia kwenye gari na simu zao kuzimwa.
Rafiki ambaye alinusurika masaibu hayo anadai kisa hicho kinahusishwa na kumuunga mkono Bobi Wine.
Video zilizorekodiwa wakati wa kampeni ya Bobi Wine katika Wilaya ya Kamuli, Mashariki mwa Uganda siku ya Jumanne zilimuonyesha Mwenyekiti wa Vuguvugu la Free Kenya, Bob Njagi akiwa jukwaani pamoja na kiongozi wa upinzani nchini Uganda Bobi Wine.
Kushambuliwa kwa mabasi ya Mwendokasi Tanzania: Watatu wakamatwa

Watu watatu wamekamatwa nchini Tanzania kufuatia vurugu zilizozuka baada ya watu wasiojulikana kushambulia mabasi yaendayo haraka maarufu kama mwendokasi.
Kulingana na Taarifa iliotumwa kwa vyombo vya habari, watatu hao wanaendelea kuhojiwa na polisi huku chanzo cha matukio hayo kikifuatiliwa na maafisa hao.
Aidha taarifa hiyo imesema kwamba watuhumiwa wengine waliohusika na tukio hilo wanatafutwa.
Picha za video zilizosambaa mitandaoni hapo awali zilionyesha baadhi ya vioo vya mabasi na vituo vikiwa vimevunjwa baada ya kushambuliwa kwa mawe usiku wa kuamkia leo Jijini Dar es Salaam.
Hivi karibuni njia hiyo ya usafiri inayotegemewa na maelfu ya wakaazi wa jiji hilo kubwa zaidi nchini Tanzania imekumbwa na malalamiko ya wananchi kutokana na uhaba wa mabasi ikilinganishwa na idadi ya abiria.
Hata hivyo jumatano asubuhi mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Albert Chalamila alifanya ziara ya kushtukiza katika kituo kikuu cha mabasi ya mwendo kasi na kuwaomba radhi watumiaji wa usafiri huo na kuwataka kuwa na subira wakati serikali ikiendelea na mipango ya kutatua adha wanazozipitia ikiwemo kuongeza idadi ya mabasi.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.