Merz abeba jukumu la kurekebisha mgogoro wa serikali

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Serikali ya Ujerumani inajichimbia kwa siku mbili za kujenga mshikamano

Serikali ya Kansela Friedrich Merz inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa ndani baada ya miezi minne tu madarakani. Migawanyiko kuhusu bajeti, kodi, pensheni na uhamiaji inatia wasiwasi, lakini pia inaleta fursa ya muafaka.

Ni miezi minne tu tangu kuingia madarakani, lakini serikali ya Kansela Friedrich Merz inakabiliwa na mgogoro mkubwa wa uongozi. Hali ya kutoridhika miongoni mwa wananchi imepanda, huku kura za maoni zikionesha ni asilimia 22 pekee ya wapiga kura wanaoridhishwa na kazi ya serikali. Katika mazingira haya, Merz na mawaziri wake wanajifungia kwa siku mbili mjini Berlin kutafuta dawa ya migawanyiko yao ya kisiasa.

Suala la fedha za taifa limeibua mivutano mikubwa. Merz aliahidi kulinda “kikomo cha deni” lakini alilegeza msimamo huo na kuruhusu mikopo mikubwa kwa ajili ya miundombinu na ulinzi. Hata hivyo, hatua hii imeigharimu serikali imani ya wapiga kura, huku chama chake muungano wa CDU/CSU kikisukuma sera za kubana matumizi na washirika wao SPD wakisisitiza ongezeko la kodi.

Tofauti za kimsingi zinaonekana wazi: SPD inataka ongezeko la kodi kwa matajiri, mapato makubwa na urithi ili kuimarisha usawa wa kijamii, wakati muungano wa CDU/CSU unapinga hatua hiyo ukisema ni mzigo kwa uchumi. Baadhi ya wahafidhina wameonesha utayari wa makubaliano juu ya kodi ya urithi, ishara ya uwezekano wa muafaka mdogo.

Wakuu wa vyama vinavyounda serikali ya mseto, Markus Söder, Waziri Mkuu wa Bavaria, Friedrich Merz (CDU), Kansela wa Shirikisho, Bärbel Bas (SPD), Waziri wa Shirikisho wa Kazi na Masuala ya Kijamii, na Lars Klingbeil, Waziri wa Shirikisho wa Fedha.

Viongozi wa CDU/CSU wamekosoa jina la “Mapato ya Raia” lililoanzishwa na serikali ya awali, wakisema linapotosha kwa kupendekeza kila mtu ana haki ya msaada wa kijamii. Kwa sasa, zaidi ya watu milioni 5.4 wanapokea malipo hayo, wakiwemo wakimbizi wa vita kutoka Ukraine. SPD inakanusha madai ya udanganyifu mkubwa, ingawa pande zote mbili zimekubaliana kulinda mfumo huo dhidi ya ulaghai wa kitaasisi.

Mfumo wa pensheni unakabiliwa na shinikizo kutokana na idadi kubwa ya wastaafu. CDU/CSU wanataka mageuzi zaidi, ikiwemo kuongeza umri wa kustaafu, huku SPD ikilenga kulinda pensheni bora. Wakati huo huo, CSU inataka ongezeko maalum kwa akina mama waliozaa kabla ya 1992, jambo litakaloongeza mzigo wa kifedha kwa serikali.

Migawanyiko kuhusu wahamiaji na ajira ya kijeshi

Serikali imechukua msimamo mkali zaidi katika udhibiti wa mipaka, hatua iliyosifiwa na baadhi ya mawaziri wa CSU. Hata hivyo, mapendekezo ya kupunguza marupurupu kwa wakimbizi wa Ukraine yamepingwa vikali na SPD. Tofauti hizi zinajitokeza katika wakati ambapo chama cha siasa kali za mrengo wa kulia AfD kinapata nguvu kwa ajenda ya kupinga wahamiaji.

Swali la kurudisha utumishi wa kijeshi pia limeibua mgawanyiko. Muswada mpya unapendekeza mfumo wa hiari kwa vijana, lakini Waziri wa Ulinzi Boris Pistorius kutoka chama mshirika cha SPD amesema iwapo haitatosha, basi kutakuwa na utumishi wa lazima. Hata hivyo, msimamo huu unapingwa ndani ya SPD yenyewe, ambayo iliidhinisha azimio dhidi ya ajira ya lazima.

Uhusiano wa washirika wa serikali ulitikisika zaidi baada ya kushindwa kwa kura ya kumchagua jaji wa Mahakama ya Katiba mwezi Julai. Tukio hilo lilifufua kumbukumbu za Mei, pale Merz mwenyewe alipohitaji duru ya pili ya kura ili kuwa kansela kwa sababu ya upinzani kutoka ndani ya muungano wake. Hali hii imeacha kivuli cha kutoaminiana.

Kwa siku mbili zijazo, mawaziri wa serikali watajaribu kurekebisha nyufa na kuimarisha mshikamano katika mkutano wa Villa Borsig. Hii ni nafasi kwa Merz kuonesha uongozi wake na kujenga imani mpya, huku changamoto za bajeti, pensheni, uhamiaji na ulinzi zikibaki kama mawe ya kujaribu uimara wa muungano wake mchanga.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment