Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wanasema wamekubaliana mpango mpya wa amani wa Gaza, na kuionya Hamas kuukubali.
Mpango huo unapendekeza kusitishwa mara moja kwa operesheni za kijeshi na Hamas kuwaachilia huru mateka 20 wa Israel na wengine zaidi ya 20 ambao wanaaminika kufariki dunia ndani ya saa 72, ili kubadilishana na mamia ya raia wa Gaza wanaozuiliwa.
Chanzo cha Palestina kinachofahamu mazungumzo ya kusitisha mapigano kiliambia BBC kwamba maafisa wa Hamas wamepewa pendekezo lenye kugusia vipendele 20 la Ikulu ya Marekani.
Moja wapo ya mapendekezo ni kwamba Hamas haitakuwa na jukumu lolote katika kutawala Gaza, na kufungua mlango kwa upatikanaji kamili wa taifa la Palestina.
Akizungumza katika mkutano na wanahabari kufuatia mazungumzo katika Ikulu ya White House, Trump aliutaja mpango huo kuwa “siku ya kihistoria kwa amani”.
Lakini alisema kuwa Netanyahu ataungwa mkono na Marekani “kumaliza kazi ya kuharibu tishio la Hamas” ikiwa Hamas haitakubali mpango huo.
Netanyahu kisha akasema Israel “itamaliza kazi” ikiwa Hamas itakataa mpango huo au haitaufuata.
Israel ‘haitajiondoa’ Gaza asema Netanyahu

Waziri mkuu wa Israel anawalenga wapinzani wanaojaribu kumshinikiza aondoe Wanajeshi wa Ulinzi wa Israel (IDF) kutoka Gaza , akisema hilo “halifanyiki”.
“Wanaendelea kusema, ‘Lazima ukubali masharti ya Hamas’. Watoe wote nje. IDF inahitaji kutoka na Hamas wanaweza kupata nafuu na wanaweza hata kukarabati Ukanda huo,” anasema. “Halifanyiki.”
Netanyahu anaongeza kuwa Rais Trump aliahidi uungaji mkono wake kamili kwa Israel iwapo Hamas itakataa mpango wake wenye vipengee 20 wa amani huko Gaza.
“Kumaliza operesheni ya kijeshi ya kuwaondoa Hamas. Na kwa hivyo nadhani kutoka kila upande ilikuwa ziara nzuri,” Netanyahu anasema.
Chapisho tofauti na Netanyahu kwenye mtandao wa kijamii asubuhi ya leo linaonesha video ya White House ya video zake na Rais Trump jana.
Mwanzoni mwa video hiyo, waziri mkuu wa Israel anaonekana akiandika barua katika kitabu inayosomeka: “Kwa Rais Donald Trump, [Bila shaka] rafiki mkubwa zaidi Israel amekuwa naye katika Ikulu ya White House.
Mpango wa amani wa Trump wa Gaza ni upi?

Baadhi ya vipengele vya mpango wa Trump ni;
Kusimamishwa mara moja kwa shughuli za kijeshi.
Kuachiliwa huru ndani ya saa 72 kwa mateka 20 wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas na mabaki ya zaidi ya dazeni mbili wanaoaminika kuwa wamekufa.
Mamia ya Wapalestina waliozuiliwa, na mabaki ya Wagaza wengine, kuachiliwa na Israel.
Hamas kuweka chini silaha zake na kutokuwa na jukumu lolote katika kuitawala Gaza.
Pindi pande zote zitakapokubaliana na pendekezo hilo, “msaada kamilikutumwa mara moja katika Ukanda wa Gaza”.
Mpango huo unaacha mlango wazi kwa taifa la Palestina la siku za usoni, ingawa Netanyahu alikataa tena hilo siku ya Jumatatu.
Majibu ya Hamas kuhusu mpango wa amani yanatarajiwa kuchukua siku kadhaa

Viongozi wa Hamas wanatarajiwa kuchukua siku kadhaa kutoa majibu yao kuhusu mpango huo wenye vipengele 20.
Inatoa wito wa kusitishwa kwa mapigano, kuachiliwa kwa mateka na Hamas ndani ya saa 72 baada ya makubaliano, na kuondoka taratibu kwa wanajeshi wa Israel kutoka Gaza.
Pia unadai kwamba Hamas iweke silaha chini jambo ambalo limekataliwa hapo awali isipokuwa kuwe na taifa huru la Palestina.
Video ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu iliyorekodiwa mara tu baada ya mkutano wake na waandishi wa habari katika Ikulu ya White House, huenda ikaongeza hali kutoridhishwa kwa Hamas.
Anasisitiza kuwa wanajeshi wa Israel watakaa katika sehemu kubwa ya Gaza.
Akisisitiza changamoto kwa kiongozi huyo wa Israel, waziri mkuu wa mrengo mkali wa kulia Bezalel Smotrich, amekosoa mpango huo na kuutaja kuwa ni “kufeli kidiplomasia”.
Qatar kuendelea na upatanishi baada ya Israel kueleza masikitiko kuhusu shambulizi dhidi ya Hamas

Waziri Mkuu wa Qatar amesema kuwa yuko tayari kuendeleza juhudi zake za kumaliza vita huko Gaza, baada ya mwenzake wa Israel kueleza masikitiko yake kuhusu shambulio la anga lililowalenga viongozi wa Hamas mjini Doha mapema mwezi huu.
Katika mazungumzo ya pande tatu na Rais wa Marekani Donald Trump, Benjamin Netanyahu alimwambia Sheikh Mohammed bin Abdul Rahman Al Thani kwamba anasikitishwa na mauaji ya afisa wa usalama wa Qatar katika shambulio la Septemba 9 na kukiuka mamlaka ya Qatar, kwa mujibu wa Ikulu ya White House.
Pia alithibitisha kuwa Israel haitafanya shambulio kama hilo tena katika siku zijazo, alisema.
Hamas ilisema viongozi wake walinusurika katika shambulio hilo lakini wanachama watano wa ngazi ya chini waliuawa pamoja na afisa huyo wa Qatar.
Mazungumzo kati ya viongozi wa Israel na Qatar yalifanyika siku ya Jumatatu, muda mfupi kabla ya Trump kutangaza mpango mpya wenye vipengele 20 wa kumaliza mzozo wa Gaza.
Trump ameitaka Hamas kukubali masharti hayo.
Netanyahu alielezea kuunga mkono mpango huo, sawa na mataifa manane ya Kiarabu na Kiislamu ikiwa ni pamoja na Qatar, ambayo imekabidhi nakala kwa maafisa wa Hamas huko Doha.
Putin asema Urusi inashinda ‘vita vya haki’ nchini Ukraine

Rais wa Urusi Vladimir Putin amesema Jumatatu kwamba vikosi vya Urusi vinashinda katika kile alichosema kuwa “vita vya haki” nchini Ukraine.
“Wapiganaji wetu na makamanda wanaendelea na mashambulizi, na nchi nzima, Urusi yote, inapigana vita hivi vya haki na kufanya kazi kwa bidii,” Putin alisema katika video iliyochapishwa kwenye tovuti ya Urusi.
“Kwa pamoja tunatetea upendo kwa Nchi yetu na umoja wa hatima yetu ya kihistoria, tunapigana na tunashinda.”
Urusi ilianzisha uvamizi dhidi ya Ukraine mnamo Februari 24, 2022, na kuiita “operesheni maalum ya kijeshi”. Kyiv na washirika wake wanasema uvamizi huo ni jaribio la kibeberu la unyakuzi wa ardhi.
Vita hivyo bado havijapata ufumbuzi licha ya juhudi za kidiplomasia za Rais wa Marekani Donald Trump kumaliza mzozo huo, ikiwa ni pamoja na mikutano tofauti na Putin, Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy na viongozi wengine wa Ulaya.
Marekani yawarudisha Wairani nyumbani baada ya makubaliano na Tehran

Utawala wa Trump unarudisha Wairani 100 nchini kwao kutoka Marekani, gazeti la New York Times liliripoti Jumanne, likiwanukuu maafisa wawili wakuu wa Iran waliohusika katika mazungumzo na afisa wa Marekani anayejua mipango hiyo.
Maafisa wa Iran walisema kwamba ndege ya kukodishwa na Marekani, iliondoka Louisiana Jumatatu usiku na ilipangwa kuwasili Iran kupitia Qatar siku ya Jumanne, ripoti hiyo iliongeza.
Safari za ndege nchini Afghanistan zasitishwa baada ya mtandao kuzimwa

Uwanja wa ndege mkuu wa Afghanistan umesimamisha huduma zake huku nchi hiyo ikikabiliana na hitilafu ya kukatika kwa mtandao wa intaneti kote uliowekwa na serikali ya Taliban.
Taliban bado haijatoa sababu rasmi ya uamuzi huo, ambao ulianza kutekelezwa siku ya Jumatatu, lakini walisema utadumu hadi ilani nyingine.
Mawasiliano nchini Afghanistan, na kwa ulimwengu mzima, yameathiriwa sana, kama vile huduma muhimu, ikiwa ni pamoja na benki, malipo na upatikanaji wa elimu ya mtandao, msaada mkubwa kwa wanawake na wasichana wengi.
Uwanja wa ndege katika mji mkuu Kabul, wakati huo huo, “ulikaribia kutelekezwa”, kulingana na mkazi mmoja, bila ushahidi wa ndege kuwasili au kuondoka.
Huduma ya ufuatiliaji wa safari za ndege Flightradar24 ilionesha kuwa safari chache za ndege zinazoingia na kutoka Jumanne ziliahirishwa.
Nyingi zaidi zilikuwa na alama ya “kutojulikana”. Abiria mmoja ambaye alipanga kuruka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kabul mnamo Jumanne aliambiwa hakutakuwa na safari za ndege hadi Alhamisi.
Mtu mwingine alisema safari zote za ndege kutoka uwanja wa ndege wa Kabul zimekatishwa tangu Jumatatu jioni. Aliongeza kuwa maisha ya Kabul “yanaonekana kuwa ya kawaida”, lakini akaongeza kuwa “hakuna mawasiliano kabisa” kote nchini.
Serikali ya Taliban yazima mfumo wa mawasiliano

Serikali ya Taliban nchini Afghanistan imezima mfumo wa mawasiliano nchi nzima, wiki kadhaa baada ya kuanza kukatika kwa miunganisho ya intaneti.
Nchi kwa sasa inakabiliwa na “kukatika kabisa kwa mtandao”, shirika la uangalizi wa mtandao la Netblocks linaripoti.
Mashirika ya habari ya kimataifa yanasema yamepoteza mawasiliano na ofisi zao katika mji mkuu Kabul. Mtandao wa rununu na TV za satelaiti pia zimetatizwa sana kote nchini Afghanistan.
Taliban bado haijatoa sababu rasmi ya kuzima intaneti lakini tangu kutwaa madaraka mwaka wa 2021, Taliban wameweka vikwazo vingi kwa mujibu wa tafsiri yao ya sheria ya Kiislamu.
Uokoaji unaendelea huku wanafunzi watatu wakifariki na wengine wakinaswa chini ya jengo Indonesia

Takriban watu 38, wengi wao wakiwa wavulana matineja, wanaaminika kuwa wamenaswa chini ya Shule ya Bweni ya Kiislamu ya Al Khoziny katika mji wa Sidoarjo Mashariki mwa Java.
Walikuwa wamekusanyika kwa ajili ya maombi wakati jengo lilipoporomoka.
Jengo hilo la gorofa mbili lilikuwa na msingi usio imara na halikuweza kuhimili uzito wa ujenzi wa ziada wa orofa mbili zaidi, shirika la kukabiliana na majanga lilisema Jumanne.
Wasichana walikuwa wakisali katika sehemu nyingine ya jengo hilo na walifanikiwa kutoroka, kwa mujibu wa Associated Press.
Hadi kufikia sasa wanafunzi watatu wamefariki na wengine kadhaa bado hawajapatikana.
Wanafunzi katika shule hiyo ni kati ya umri wa miaka 12 na 17.
Mamia ya maelfu ya ajira zayumba huku mkataba wa Agoa ukifia ukomo wake

Mamia ya maelfu ya ajira Afrika zinayumba huku Mkataba wa Ukuaji na Fursa ya Afŕika (Agoa) ukifikia ukomo wake hii leo.
Mpango wa biashara wa miaka 25 umeruhusu zaidi ya nchi 30 za Afrika kusafirisha bidhaa bila kutozwa ushuru hadi Marekani.
Mkataba huo umefika ukomo wake na hakuna kilichosemwa juu ya kuuongeza, wafanyakazi waliokuwa wakipata riziki katika kampuni hizo wakiwa hawana uhakika wa jinsi hali itakavyokuwa ama viwandani au masoko.
Wajumbe kutoka nchi za Afrika wamekuwa wakitaka mkataba huo uongezwe, lakini hadi kufikia sasa Marekani haijatoa ishara za wazi za kutaka utekelezaji wa hilo. Kwa miongo kadhaa, mpango huo umeonekana kama msingi wa uhusiano wa kiuchumi wa Marekani na Afrika.
Mkataba huo ulikusudiwa kukuza bara Afrika, kuunda ajira na biashara kuwa mbadala wa misaada.
Viongozi wa Kiafrika walisisitiza suala hilo katika Mkutano Mkuu wa UN wa wiki iliyopita lakini serikali zimekuwa zikifuatilia chaguzi zingine kulinda viwanda vyao.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.