Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Chama cha Wafanyakazi wa Usafiri wa Anga nchini Kenya (KAWU), leo kimetoa notisi ya siku saba kabla ya kufanya mgomo, na kutaka bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege ya Kenya (KAA) ijiuzulu kutokana na matatizo ya wafanyakazi na kushindwa kwa mkataba uliositishwa wa kukodisha uwanja huo.
Mgomo huo unaweza kutatiza shughuli katika uwanja mkuu wa ndege wa kimataifa wa Kenya, mojawapo ya vituo vya usafiri wa anga vilivyo na shughuli nyingi zaidi barani Afrika.
Katibu Mkuu wa KAWU, Moses Ndiema amekataa kusema ni lini mgomo huo utaanza, akisema unaweza kuanza wakati wowote baada ya muda wa notisi kumalizika.
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege vya Kenya bado haijatoa kauli yoyote.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wafanyakazi katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta walifanya mgomo wa siku moja mwaka mmoja uliopita kutokana na wasiwasi kuhusu mpango wa kukodisha uwanja huo kwa kampuni ya Adani Group, inayoongozwa na mmoja wa watu tajiri zaidi barani Asia, bilionea wa India, Gautam Adani.
Hatimaye Kenya ilitupilia mbali mpango huo uliopendekezwa baada ya Marekani kumfungulia mashtaka Adani na watu wengine saba kwa kuripotiwa kulipa takriban dola milioni 265 kama hongo kwa maafisa wa serikali ya India, madai ambayo Adani Group imekanusha.
Katibu Mkuu wa KAWU Moses Ndiema, katika barua yake ya Septemba 23 ambayo imeonekana na Reuters, anaihutumu KAA kwa kutokuwa na uwezo na kushindwa kuchukua hatua kwa maslahi ya Kenya.
Maelfu wahamishwa huku China ikijiandaa na kimbunga kikali

China imewahamisha maelfu ya watu na kuamuru takriban miji 10 kufunga shule na baadhi ya biashara huku kimbunga kikali zaidi kwa mwaka kikitarajiwa katika pwani yake ya kusini.
Kimbunga hicho kinatarajiwa kupiga katika mkoa wa Guangdong nchini China siku ya Jumatano, ambapo takriban watu 370,000 wamehamishwa hadi sasa, huku mamlaka ikionya hali itakuwa mbaya.
Kimbunga Ragasa kimepewa jina la “Mfalme wa Vimbunga” na shirika la hali ya hewa la China na kinatarajiwa kuelekea kaskazini mwa Vietnam katika siku zijazo, na kinaweza kuathiri mamilioni ya watu.
Siku ya Jumanne, rafu za maduka makubwa huko Hong Kong zilikuwa tupu watu wakinunua mkate, mboga mboga, nyama na tambi za papo hapo huku wakazi wakijiandaa.
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Hong Kong ulisema unatarajia “idadi kubwa ya safariza ndege” kuanzia siku ya Jumanne hadi siku inayofuata.
Katika miji ya kusini mwa China, wamiliki wa maduka walirundika mifuko ya mchanga mbele ya maduka yao ili kujiandaa na kuwasili kwa kimbunga, huku wakaazi katika maeneo ya mabondeni karibu na mbele ya bahari wakiwa na wasiwasi haswa juu ya mawimbi ya maji.
Wengi pia wamefunga madirisha ya nyumba na biashara zao, wakitumaini kuzuia uharibifu kutokana na upepo.
Bado haijabainika ni kwa kiasi gani mabadiliko ya tabia nchi yamechangia kimbunga cha Ragasa. Lakini joto linaloongezeka duniani linatarajiwa kuongeza dhoruba na vimbunga kuwa vikali zaidi, kulingana na wanasayansi wa Umoja wa Mataifa.
Hiyo uwepo wa upepo mkali, mvua kubwa na hatari ya mafuriko katika maeneo ya pwani.
Kimbunga Ragasa kilipita katika kisiwa cha Taiwan usiku wa jana, takriban watu sita walijeruhiwa na zaidi ya safari 100 za ndege za kimataifa kufutwa.
Ragasa kilipita katika kisiwa cha mbali kaskazini mwa Ufilipino siku ya Jumatatu, na kuua mtu mmoja huku maelfu ya familia zikihamishwa kabla ya kimbunga hicho kuanguka.
Shule na ofisi za serikali zilifungwa, ikiwa ni pamoja na katika mji mkuu wa Manila.
Kimbunga Ragasa kinavuma kwa upepo mkali wa hadi kilomita 285 kwa saa (177mph) katika kiwango chake cha juu siku ya Jumatatu, na kimesababisha mafuriko, mawimbi ya dhoruba na maporomoko ya ardhi katika nchi hiyo.
Kimbunga kikuu cha Mangkhut cha 2018 – ambacho ndio kikubwa kikali zaidi kupiga eneo Hink Kong – kilijeruhi watu 200, kuzamisha meli na miundombinu kuharibika, na kuacha hasira ya HK $ 4.6bn ($592m: £438m).
Mnamo mwaka wa 2017, kimbunga Hato kilisababisha mafuriko makubwa na kujeruhi zaidi ya watu 100 katika jiji hilo.
Mwanamke apatikana na hatia ya kuwaua watoto wake wawili

Mama mmoja nchini New Zealand amepatikana na hatia ya kuwaua watoto wake wawili na kuificha miili yao kwenye mabegi.
Hakyung Lee, 44, alipatikana na hatia ya mauaji katika Mahakama Kuu ya Auckland Jumanne, baada ya kesi iliyochukua takriban wiki mbili. Awali alikana kuwauawa.
Mawakili wa Lee walidai alikuwa hajitambui wakati wa mauaji hayo, ambayo yalitokea miezi kadhaa baada ya mumewe kufariki kutokana na saratani. Lakini waendesha mashitaka walisema alifanya akiwa akiwa anajitambua.
Mabaki ya watoto wake yaligunduliwa mwaka 2022 na familia ambayo ilikuwa imenunua vifaa kutoka katika ghala lililotelekezwa kwenye mnada huko Auckland.
Miili hiyo inaaminika kuhifadhiwa hapo kwa miaka kadhaa.
Lee alikamatwa Ulsan, Korea Kusini, Septemba 2022 na kurejeshwa New Zealand baadaye mwaka huo.
Wakati wa kusikilizwa kwa kesi hiyo, mahakama ilielezwa kuwa miili ya watoto hao haikuwa na dalili zozote za kiwewe, ingawa ilikuwa wazi kuwa waliuawa na mtu.
Mchunguzi wa maiti aligundua walikufa kwa mauaji, ikiwemo matumizi ya Nortriptyline, dawa ya kutuliza mfadhaiko, mwendesha mashtaka alisema.
Mahakama ilielezwa kwamba Lee alinunua dawa hiyo kutoka katika duka la dawa Agosti 2017 – miezi mitano baada ya mumewe, Ian Jo, kugunduliwa na saratani.
Upande wa utetezi ulidai afya ya akili ya Lee ilizorota baada ya kifo cha mumewe na aliamini kuwa ni bora wafe wote pamoja.
Hii ilimfanya ajaribu kujiua yeye na watoto wake kwa dawa ya hiyo ya kutuliza mfadhaiko. Baada ya kula dawa hiyo yeye alizinduka, lakini akakuta watoto wake wamekufa.
Lee alificha miili ya watoto, kubadilisha jina lake na kurudi Korea Kusini, mwendesha mashtaka alisema.
Mauaji hayo yalikuwa ni “kitendo cha ubinafsi ili kuondokana na mzigo wa uzazi wa peke yake,” mwendesha mashtaka alisema.
Siku ya Jumanne, Lee aliinamisha kichwa chini na hakutoa maoni yoyote wakati mahakama ilipotoa uamuzi huo, ambao ulikuja baada ya takriban saa tatu za kesi.
Lee anatazamiwa kuhukumiwa mwezi Novemba. Anakabiliwa na kifungo cha hadi maisha jela, AFP iliripoti.
Mvulana wa miaka 13 ajificha kwenye magurudumu ya ndege kutoka Kabul hadi Delhi

Mvulana wa Afghanistan mwenye umri wa miaka 13 alifanya safari ya hatari kutoka Kabul hadi Delhi, akijificha kwenye sehemu ya magurudumu ya ndege ya abiria ya Kam Air.
Maafisa wanasema kijana huyo, ambaye anatoka katika mji wa Kunduz kaskazini mwa Afghanistan, alipatikana akirandaranda kwenye barabara ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Delhi baada ya ndege hiyo kutua siku ya Jumatatu.
Alizuiliwa na maafisa wa usalama wa India na kuhojiwa kwa saa kadhaa kabla ya kurejeshwa Kabul kwa ndege hiyo hiyo.
Inasemekana kijana huyo aliwaambia maafisa kwamba alifanya hivyo kwa hamu tu ya kutaka kujua.
Msemaji wa Kikosi cha Usalama cha India (CISF) alisema mvulana huyo alifanikiwa kusafiri bila kutambuliwa katika ndege ya Kam Airlines RQ-4401, ambayo ilitua Delhi siku ya Jumapili.
Polisi walimkuta akirandaranda peke yake na kumpeleka kando kwa mahojiano.
Inasemekana kijana huyo aliwaambia maafisa kwamba alijificha kwenye sehemu ya magurudumu ya nyuma ya ndege hiyo.
Gazeti la Indian Express liliripoti kwamba kijana huyo alitaka kusafiri hadi Iran na hakujua kwamba ndege aliyoingia ilikuwa ikielekea Delhi, na si Tehran.
Kulingana na gazeti hilo, mvulana huyo aliingia kinyemela kwenye uwanja wa ndege wa Kabul, akalifuata kundi la abiria, na kujibanza kwenye gurudumu la nyuma la ndege hiyo – na kuingia ndani kwenye eneo ambalo huhifadhi magurudumu. Alikuwa amebeba tu spika ya rangi nyekundu pamoja naye.
Kumekuwa na matukio ya watorokaji kujificha kwenye ndege kuelekea Marekani au Ulaya, wakitoroka nchi zao. Lakini ni wachache sana kati yao wanaofika wakiwa hai.
Wataalamu wanasema watoro wengi katika safari hizo za ndege mara nyingi huwa hawana fahamu wakati wa ndege kushuka, jambo linalowaweka katika hatari ya kuangukia na kufa pale magurudumu yanaposhushwa.
Mwaka 2022, mwanamume Mkenya mwenye umri wa miaka 22 alipatikana akiwa hai kwenye eneo la gurudumu la ndege ya mizigo huko Amsterdam.
Rais wa zamani wa Malawi anaongoza katika kura za Urais

Rais wa zamani wa Malawi Peter Mutharika anaongoza katika kinyang’anyiro cha urais nchini humo, huku thuluthi mbili ya wilaya zikiwa tayari zimeshatoa matokeo.
Mzee huyo mwenye umri wa miaka 85 amepata takriban 66% ya kura halali zilizohesabiwa hadi sasa, huku mpinzani wake wa karibu, rais aliyemaliza muda wake Lazarus Chakwera, 70, akipata karibu 24% ya kura.
Matokeo yaliyotangazwa hadi sasa yanaonyesha kuwa Mutharika ameshinda katika maeneo yanayojulikana kuwa ngome za Chakwera, ikiwa ni pamoja na mji mkuu, Lilongwe, na Nkhotakota.
Lakini kambi ya Chakwera ina matumaini kuwa mara tu matokeo yatakapotangazwa kutoka maeneo mengine, kura zake zitaongezeka, na hivyo kulazimisha duru ya pili.
Mgombea wa urais anahitaji zaidi ya 50% ya kura ili kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa wiki iliyopita.
Tume ya Uchaguzi ya Malawi ina hadi mwisho wa Jumatano kutangaza matokeo ya mwisho.
Takribani wilaya mbili kati ya 12 ambazo bado hazijatangaza matokeo – zina idadi kubwa ya wapiga kura waliojiandikisha, na kambi ya Chakwera inaamini atafanya vizuri katika wilaya hizo na maeneo ya vijijini karibu na Lilongwe na Dedza.
Wilaya nyingine mbili, ambako Mutharika anatarajiwa kufanya vyema, matokeo yake yamezuiliwa na tume ya uchaguzi huku ikihakiki iwapo ni sahihi.
Tume hiyo ilisema imejitolea kuendesha zoezi hilo kwa uwazi, usahihi na uaminifu.
Imesema inachunguza kwa makini kila karatasi ya kuhesabu kura, baada ya mahakama ya kikatiba kubatilisha ushindi wa Mutharika mwaka 2019 kwa sababu ya kasoro.
Chakwera alishinda uchaguzi wa marudio kwa tofauti kubwa, lakini wakati wa urais wake mgogoro wa kiuchumi wa Malawi umeongezeka, na mfumuko mkubwa wa bei, uhaba wa chakula na mafuta na kukatika kwa umeme mara kwa mara.
Museveni aidhinishwa rasmi kugombea urais katika uchaguzi mkuu ujao wa Uganda

Rais wa Uganda Yoweri Museveni mwenye umri wa miaka 81 ameidhinishwa na tume ya uchaguzi ya nchi hiyo kugombea urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka ujao.
Akiwa amevalia rangi za manjano za cha chama tawala cha National Resistance Movement, Museveni aliwasili katika ofisi za Tume ya Uchaguzi akiambatana na Janet Museveni mke wa rais, Anita Among spika wa Bunge na maafisa wengine wakuu wa chama.
Katika Hotuba yake ya uteuzi, Museveni ameishukuru Tume kwa kuidhinisha ugombea wake. Pia aliipongeza sehemu yake tawala ya NRM kwa kumwamini na kumchagua kama bendera ya urais katika uchaguzi ujao.
“Tuna misukumo miwili mikuu, msukumo namba moja ni kwa tabaka la kati na wawekezaji kutoka nje kubadilisha kabisa Uganda kutoka nchi ya kipato cha chini hadi nchi ya kipato cha kati kuelekea nchi ya kwanza ya ulimwengu.” Alisema.
Bw. Museveni, ambaye ametawala nchi hiyo ya Afrika mashariki kwa karibu miongo minne, anatafuta muhula wa saba wa kuchaguliwa. Baada ya kurasimisha ugombea wake, Museveni anatarajiwa kuzungumza na wafuasi wake katika mkutano wa hadhara katika uwanja wa uhuru nje kidogo ya mji mkuu Kampala.
Mpinzani wake mkuu katika uchaguzi wa urais wa 2021 mwanamuziki aliyegeuka kuwa mwanasiasa Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine atateuliwa kesho.
Vyama vinne vya kisiasa tayari vimejiondoa katika kinyang’anyiro cha urais, ikiwa ni pamoja na Democratic Party, chama kongwe zaidi cha kisiasa nchini Uganda na Political Front for Freedom [PFF] kilichoanzishwa na Dk. Kizza Besigye, mkosoaji mkubwa wa Museveni.
Kwa mara ya pili mfululizo nchi hiyo itafanya uchaguzi bila mgombea urais mara nne, Dk. Besigye kuonekana kwenye karatasi ya kura. Alikamatwa mwaka jana akiwa Kenya, bado yuko kizuizini kwa mashtaka ya uhaini. Anakanusha makosa yoyote.
Hata hivyo, wakosoaji wanasema Museveni ametawala Uganda kwa mkono wa chuma tangu achukue madaraka kama kiongozi wa waasi mwaka 1986 na ameshinda kila uchaguzi tangu wakati huo.
Wakati wa uchaguzi uliopita wa 2021, alishinda kwa 58% wakati mpinzani wake wa karibu, Bobi Wine alishika nafasi ya pili kwa 34%. Nchi hiyo itafanya uchaguzi mkuu ujao Januari 12 mwaka ujao.
Mashambulizi ya Israel yaendelea huku mataifa kadhaa yakilitambua taifa la Palestina

Nchi kadhaa zimeutambua rasmi uraia wa Palestina katika muda wa siku mbili zilizopita huku Israel ikiendelea na mashambulizi yake katika mji wa Gaza.
Vifaru na magari ya kivita yameonekana katika mji huo ambao zamani ulikuwa makazi ya mamia ya maelfu ya watu ambapo jeshi la Israeli limeharibu vitalu vikubwa vya makazi na kuwalazimu wakaazi kuacha nyumba zao.
Mashambulizi hayo yanaendelea huku Rais wa Marekani Donald Trump akijiandaa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York baadaye leo, ambapo viongozi wa dunia wamekusanyika kwa ajili ya mkutano wa 80 wa kila mwaka wa shirika hilo.
Trump hakuhudhuria kongamano la kabla ya mkutano kuhusu suluhu la mataifa mawili katika mzozo wa Israel na Gaza. Ufaransa, ambayo iliandaa hafla hiyo pamoja na Saudi Arabia, ililitambua rasmi taifa la Palestina katika hafla hiyo, kufuatia matangazo sawa na hayo kutoka Uingereza, Canada na Australia siku ya Jumapili.
Marekani imeshutumu hatua hiyo kuwa haisaidii kumaliza mzozo huo, na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema “hakutakuwa na taifa la Palestina”.
Trump anatarajiwa kukutana na viongozi kutoka Mashariki ya Kati katika mkutano tofauti katika Umoja wa Mataifa baada ya hotuba yake.
Spika wa DRC Vital Kamerhe ajiuzulu

Vital Kamerhe, Spika wa Baraza la Chini la Bunge katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, amewasilisha jana waraka wa kujiuzulu Jumanne baada ya kukabiliwa na shinikizo kutoka kwa ombi linaloungwa mkono na zaidi ya wengi katika bunge la taifa.
Wakati wabunge wakijiandaa kupiga kura ikiwa watamwondoa au kumruhusu aendelee, Kamerhe alichagua kujiuzulu kabla ya mjadala au kura kufanyika. Ombi hilo pia lililenga wanachama wengine wanne wa ofisi yake.
Mvutano umekuwa ukiongezeka kati ya Rais Félix Tshisekedi na Kamerhe, ambao wamekuwa washirika wa karibu.
Makubaliano yao ya kusaidiana yanayolenga kusaidiana kupanda urais yamevunjika, na kujiuzulu kwa leo kunaweza kuashiria talaka ya kisiasa.
Hii sio mara ya kwanza kwa Kamerhe kujiuzulu kama Spika. Mnamo 2009, alijiuzulu baada ya kumkosoa Rais wa wakati huo Joseph Kabila kwa kuruhusu wanajeshi wa Rwanda kuingia nchini bila idhini ya bunge.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.