Trump asema hakufahamishwa na Netanyahu kabla ya Israel kushambulia Qatar

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema siku ya Jumatatu kuwa hakujulishwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu mapema kuhusu shambulizi la Israel nchini Qatar wiki iliyopita.

Maoni ya Trump yanatolewa baada ya ripoti ya Axios kusema kuwa Netanyahu alimfahamisha rais wa Marekani kuhusu shambulizi hilo muda mfupi kabla ya kutokea.

Utawala wa Trump umesema uliarifiwa tu baada ya makombora kurushwa angani, na hivyo kumnyima Trump fursa ya kupinga shambulizi hilo.

Axios iliripoti, ikiwanukuu maafisa wa Israeli, kwamba Ikulu ya Marekani ilijua mapema, hata ikiwa muda wa kusitisha shambulizi hilo ulikuwa kidogo.

Israel ilifanya shambulizi la kujaribu kuwaua viongozi wa kisiasa wa Hamas kwa shambulizi la anga nchini Qatar siku ya Jumanne, na kuzidisha hatua yake ya kijeshi Mashariki ya Kati.

Shambulizi hilo lilishutumiwa pakubwa Mashariki ya Kati na kwingineko kama kitendo ambacho kinaweza kuzidisha hali ya wasiwasi katika eneo ambalo tayari linakumbana na changamoto zake.

Awali, Trump alisema hakuhusika katika uamuzi wa Israel kuivamia Qatar.

Alipoulizwa siku ya Jumatatu ikiwa Netanyahu alizungumza naye moja kwa moja kumtahadharisha kuwa Israel itavamia viongozi wa Hamas nchini Qatar, “Hapana, hapana, hawakunijulisha,” Trump alisema.

Ofisi ya Netanyahu ilisisitiza baada ya Axios kuripoti kwamba shambulizi hilo lilikuwa operesheni “huru kabisa” ya Israeli.

Marekani yaharibu meli inayodaiwa kuwa ya dawa za kulevya ya Venezuela

.

Rais wa Marekani Donald Trump amesema jeshi la Marekani limeharibu meli inayodaiwa kuwa ya mihadarati ya Venezuela iliyokuwa ikisafiri katika bahari ya kimataifa ikielekea Marekani.

Trump alisema siku ya Jumatatu kwamba wanaume watatu waliuawa katika shambulizi dhidi ya “makundi ya ulanguzi wa dawa za kulevya”. Hakutoa ushahidi wowote kuwa meli hiyo ilikuwa imebeba dawa za kulevya.

Muda mfupi kabla, mwenzake wa Venezuela Nicolás Maduro alisema Caracas itajilinda dhidi ya “uchokozi” wa Marekani, akimtaja mwanadiplomasia mkuu wa Marekani Marco Rubio “mbabe wa vifo na vita”.

Mvutano kati ya nchi hizo mbili uliongezeka baada ya Marekani kupeleka meli za kivita kusini mwa Caribbean kwa kile maafisa walisema ni operesheni za kukabiliana na mihadarati, na kufanya shambulizi lililosababisha vifo vya watu 11.

Uchaguzi wa Malawi 2025: Raia wanapiga kura kuchagua viongozi wao

.

Malawi inaelekea kwenye uchaguzi leo Jumanne utakaowakutanisha Rais Lazarus Chakwera na mtangulizi wake Peter Mutharika, huku nchi hiyo ikiendelea kukabiliwa na mfumuko wa bei uliokithiri na uhaba wa mafuta.

Wagombea wengine 15 akiwemo rais wa zamani Joyce Banda pia wanawania kiti cha urais, lakini wachambuzi wanatarajia kinyang’anyiro hicho kuwa kati ya wawili Chakwera, 70, na Mutharika, 85. Ikiwa hakuna atakayepata zaidi ya 50% ya kura, kutakuwa na duru ya pili.

Malawi imekabiliwa na mdororo wa kiuchumi tangu Chakwera kuchaguliwa mwaka 2020, huku kukiwa na kimbunga kikali na ukame uliofanya hali kuwa mbaya zaidi.

Kashfa za ufisadi zimechangia kukatishwa tamaa na pande zote mbili. Chakwera aliingia afisini akishutumu serikali ya zamani ya Mutharika kwa ufisadi uliokithiri, lakini usimamizi wake wa kesi umekosolewa kuwa wa kibaguzi na wa polepole.

Nchi yenye takriban watu milioni 22 pia itawapigia kura wabunge na madiwani wa mitaa leo siku ya Jumanne.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment