Mwanamitindo maarufu wa Italia Giorgio Armani afariki dunia

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Armani anajulikana kwa kubuni chapa ya suti za wanaume na wanawake kwa mtindo wa kisasa
Maelezo ya picha,Armani anajulikana kwa kubuni chapa ya suti za wanaume na wanawake kwa mtindo wa kisasa

Wapenzi wa fasheni hasa mavazi umewahi kukutana na nguo ina chapa ya Armani inayoundwa nchini Italia.

Mbunifu wa mitindo wa Italia na mmiliki wa chapa hiyo bilionea Giorgio Armani amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 91.

Armani alitambulika kama nembo ya mtindo wa Kiitaliano, akijulikana kwa kubuni mavazi yenye mvuto na ustadi wa hali ya juu.

Alibadilisha taswira ya suti za wanaume na wanawake, akizipa muonekano wa kisasa unaoendana na mahitaji ya dunia ya leo.

Chapa yake (Armani) ilianza kama kampuni ya mavazi lakini baadaye ilitanuka hadi sekta nyingine kama muziki, michezo na hoteli za kifahari, na hivyo kuwa alama ya maisha ya ustaarabu.

Mbali na ubunifu wake, Armani alikuwa pia mfanyabiashara hodari.

Kampuni yake ilikuwa ikipata mapato ya zaidi ya pauni bilioni 2 kila mwaka, na ikabaki kuwa kati ya chapa zenye ushawishi mkubwa duniani.

Katika taarifa rasmi iliyotolewa kupitia ukurasa wa Instagram wa chapa hiyo, ilielezwa kuwa: “Giorgio Armani aliendelea kufanya kazi hadi siku zake za mwisho, akiwa ameweka maisha yake kwa kampuni, makusanyo ya mitindo, na miradi mingi ya baadaye iliyokuwa inaendelea.”

Taarifa hiyo iliendelea kusisitiza kuwa alikuwa: “Mwenye bidii isiyochoka hadi mwisho wa maisha yake.”

DRC, Rwanda na kamati ya usimamizi wakiri mkataba wa amani unachelewa kutekelezwa kikamilifu

Rais Trump (katikati), Mwezi Julai aliwakaribisha ofisini kwake Olivier Nduhungirehe wa Rwanda na Thérèse Kayikwamba wa DRC baada ya kutia saini makubaliano ya amani.
Maelezo ya picha,Rais Trump (katikati), Mwezi Julai aliwakaribisha ofisini kwake Olivier Nduhungirehe wa Rwanda na Thérèse Kayikwamba wa DRC baada ya kutia saini makubaliano ya amani.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda na wanachama wengine wa Kamati ya Pamoja ya Usimamizi wametambua kuwa utekelezaji wa baadhi ya vipengele vya mkataba wa amani uliotiwa saini mwezi Juni kwa msaada wa Marekani umechelewa zaidi ya ilivyotarajiwa.

Taarifa hiyo ilitolewa kupitia tamko la pamoja lililotangazwa Jumatano, kufuatia kikao cha pili cha kamati hiyo kilichofanyika mjini Washington, Marekani.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ghasia zinazoendelea mashariki mwa DRC licha ya kusainiwa kwa mkataba wa amani zimeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika utekelezaji wa makubaliano hayo.

Hata hivyo, wanakamati hao walisisitiza dhamira yao ya pamoja ya kuhakikisha utekelezaji kamili na kwa wakati wa makubaliano hayo, ili kufanikisha amani, uthabiti na maendeleo katika eneo la mashariki mwa DRC na ukanda mzima wa Maziwa Makuu.

Mbali na juhudi zinazoongozwa na Marekani, kuna pia mchakato mwingine wa amani unaoendelea chini ya usimamizi wa serikali ya Qatar, ambao unahusisha mazungumzo ya moja kwa moja kati ya serikali ya DRC na waasi wa M23/AFC.

Licha ya kutiwa saini kwa tamko la misingi mjini Doha mwezi Julai, serikali ya DRC na waasi wa M23 walishindwa kuheshimu tarehe ya mwisho ya Agosti 18 ya kusaini mkataba kamili wa amani.

M23 ilisitisha ushiriki wake katika mazungumzo hayo, ikilaumu serikali kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Hata hivyo, mapema wiki hii, kundi hilo lilithibitisha tena kujitolea kwake kuendelea kushiriki mchakato wa Doha.

Taasisi ya Rais wa zamani wa Afrika Kusini, Thabo Mbeki Foundation, imeandaa kongamano la siku nne kuhusu amani na usalama linalofanyika Gauteng, Afrika Kusini.

Kongamano hilo linakusudia kutafuta suluhu kwa changamoto kuu za kiusalama barani Afrika, likiwemo suala la migogoro mashariki mwa DRC.

Hata hivyo, serikali ya DRC imekataa kushiriki kongamano hilo, ikitilia shaka uadilifu na usawa wa uongozi wa Mbeki katika mchakato huo.

Mwanasiasa wa upinzani, Martin Fayulu, alisifu juhudi za taasisi hiyo lakini akakosoa baadhi ya mapungufu ya kiutaratibu katika maandalizi ya kongamano hilo.

Katika taarifa yake, Fayulu alitoa wito wa kuungwa mkono kwa mchakato mbadala unaoongozwa na viongozi wa dini nchini DRC, akisema:

“Natumaini kuwa Taasisi ya Thabo Mbeki itatoa kipaumbele kwa mchakato unaoongozwa na Kinshasa kwa kuhakikisha ushiriki wa wadau wote wa kitaifa bila ubaguzi.”

Pia alisisitiza kuwa kuunga mkono juhudi za ndani za kitaifa kutasaidia kujenga amani ya kudumu.

Pande zote mbili serikali ya DRC na kundi la M23 zimeendelea kushutumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano.

Mahakama ya Marekani yabatilisha uamuzi wa utawala wa Trump wa kusitisha ufadhili kwa Chuo Kikuu cha Harvard

gg

Mahakama nchini Marekani imebatilisha uamuzi wa serikali ya Rais Donald Trump wa kusitisha mabilioni ya dola za ufadhili wa tafiti kwa Chuo Kikuu cha Harvard, ikisema kuwa hatua hiyo ilikiuka haki za kikatiba za taasisi hiyo.

Katika uamuzi uliotolewa na Jaji Allison Burroughs, aliyeko Boston, mahakama ilibaini kuwa serikali ilivunja haki ya Harvard ya uhuru wa kujieleza kwa kufuta karibu dola bilioni 2 za ruzuku ya tafiti.

“Mahakama inabatilisha maagizo ya kusitisha ufadhili na barua za kukatiza mikataba, kwa kuwa yalikiuka Marekebisho ya Kwanza ya Katiba ya Marekani,” aliandika Jaji Burroughs.

Uamuzi huu umeelezewa kama ushindi wa kihistoria kwa Harvard, lakini Ikulu ya Marekani imeahidi kukata rufaa.

Serikali ya Trump ilitoa tuhuma dhidi ya chuo hicho ikidai kuwa kinashabikia chuki dhidi ya Wayahudi, kueneza itikadi za mrengo mkali wa kushoto, na kuonyesha upendeleo wa kikabila.

Tofauti na Harvard, vyuo vingine vitatu vya ligi ya Ivy Columbia, Pennsylvania (Penn), na Brown vilichagua kufikia makubaliano na utawala wa Trump ili kuzuia kusitishwa kwa ufadhili wao, badala ya kuchukua hatua za kisheria.

Katika taarifa iliyotolewa wakati wa kufunguliwa kwa kesi mwezi Aprili, uongozi wa Harvard uliapa kupambana na chuki ya kidini na kikabila, lakini pia ukasisitiza dhamira ya taasisi hiyo kulinda uhuru wa taaluma na utafiti.

Rais wa chuo hicho alieleza kuwa: “Hakuna serikali inapaswa kuamuru ni nini kinachopaswa kufundishwa na vyuo vikuu binafsi, nani wa kuandikishwa au kuajiriwa, au maeneo gani ya utafiti yanayopaswa kuendelezwa.”

Utawala wa Trump pia ulitishia kufuta hadhi ya chuo hicho ya kutolipa kodi (tax-exempt status), pamoja na kuchukua umiliki wa hataza zilizotokana na tafiti zilizofadhiliwa na serikali.

Harakati hizi zilikuja wakati ambapo serikali ilikuwa ikiendeleza mashinikizo kwa taasisi za elimu ya juu, hasa zile zinazotuhumiwa kupinga sera za serikali au kushabikia misimamo ya upande wa kushoto wa kisiasa.

Kwa sasa, mazungumzo yanaendelea kati ya Harvard na maafisa wa serikali juu ya uwezekano wa kufikia makubaliano ya kurudisha ufadhili huo.

Trump ametangaza kuwa anataka chuo hicho kilipie angalau dola milioni 500 kama sehemu ya suluhu ya mzozo huo.

Israel yakataa pendekezo la Hamas la ”makubaliano ya jumla”

gg

Israel imekataa pendekezo jipya la kundi la Hamas la kufikia “makubaliano ya jumla” ya kumaliza vita vinavyoendelea katika Ukanda wa Gaza na kuwaachilia wafungwa wote wa Israel walioko mikononi mwa Hamas.

Katika taarifa rasmi, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israel ilielezea pendekezo hilo kuwa ni “propaganda isiyo na jipya.”

Kwa upande wao, wanamgambo wa Hamas lwalitangaza jana kwamba wako tayari kufikia makubaliano hayo, ambayo yangejumuisha kuachiliwa kwa mateka wanaowashikilia kwa kubadilishana na idadi maalum ya wafungwa wa Kipalestina, kama sehemu ya makubaliano mapana ya kusitisha vita.

Hamas iliongeza kuwa: “Tunaunga mkono kuundwa kwa serikali huru ya kitaifa ya wataalamu, ambayo itasimamia masuala yote ya Ukanda wa Gaza na kuanza kazi mara moja katika sekta zote.”

Taarifa hiyo ya Hamas ilitolewa baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kutoa wito kwa Hamas kuwaachilia “mateka 20 waliobaki wakiwa hai.”

Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli, Benjamin Netanyahu, ilijibu kwa kusema:

“Kwa bahati mbaya, huu ni ujanja mwingine wa Hamas usio na chochote kipya.” Iliongeza kuwa: “Vita vya Gaza havitakoma hadi mateka wote waachiliwe, Hamas ivuliwe silaha, Ukanda wa Gaza upokonywe silaha kikamilifu, Israel iweke udhibiti wa kiusalama, na kuanzishwe utawala mbadala wa kiraia.”

Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Gaza imeripoti vifo 84 na majeruhi 338 katika saa 24 zilizopita.

Aidha, baadhi ya waathiriwa bado wako chini ya vifusi na hawawezi kufikiwa na vikosi vya uokoaji.

Tangu kuzuka kwa vita hivyo mwaka 2023, jumla ya watu 64,231 wameuawa na wengine 161,583 wamejeruhiwa, kwa mujibu wa takwimu za karibuni zilizotolewa na wizara hiyo Alhamisi.

Afisa mwandamizi wa Kitengo cha Kuratibu Shughuli za Serikali katika Maeneo (COGAT) alisema kuwa Israeli inatarajia takriban watu milioni moja kuhama kutoka Jiji la Gaza kuelekea kusini.

Hadi sasa, takriban Wapalestina 70,000 wamehama kutoka kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Afisa huyo wa Wizara ya Ulinzi, ambaye hakutaka kutajwa jina, alisema kuwa Israeli inakusudia kuanzisha eneo la kibinadamu, ambalo litatangazwa rasmi katika siku chache zijazo.

Eneo hilo linapangwa kuanzia kambi za wakimbizi katikati mwa Gaza hadi katika ukanda wa pwani wa Al-Mawasi kusini, na pia kupanuliwa kuelekea mashariki.

Hata hivyo, Shirika la Utangazaji la Israeli limeripoti kuwa Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron, aliomba kufanya ziara rasmi nchini Israeli, lakini Waziri Mkuu Netanyahu alikataa ombi hilo.

Alishikilia kuwa Ufaransa inapaswa kwanza kubadili msimamo wake wa kuitambua Palestina kama taifa huru.

Ufaransa inaongoza juhudi za kidiplomasia katika Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwezi huu, zinazolenga kulitambua taifa la Palestina.

Nchi nyingine kama Ubelgiji, Australia, Kanada, na Ufaransa tayari zimeonesha nia ya kulitambua taifa hilo, hatua iliyokosolewa vikali na viongozi wa Israeli wakiongozwa na Netanyahu.

Makumi ya watu wafariki baada ya boti kugonga kisiki nchini Nigeria

.

Makumi ya watu wamefariki katika jimbo la kaskazini la Niger nchini Nigeria baada ya boti iliyokuwa imebeba takriban watu 100 kuzama kwenye mto.

Boti hiyo iliyoripotiwa kuwa na abiria wengi miongoni mwao watoto, ilipinduka ilipogonga kisiki cha mti kilichokuwa chini ya maji karibu na jamii ya Gausawa katika eneo la Serikali ya Mtaa ya Borgu, maafisa walisema.

Shirika la dharura la serikali limesema watu 29 wamefariki na wengine zaidi ya 50 kuokolewa, huku shughuli za kuwatafuta zikiendelea.

Afisa mmoja wa eneo hilo ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba idadi ya waliofariki imeongezeka hadi 60

Tukio hilo limeripotiwa kutokea majira ya saa 11:30 Jumanne asubuhi kwenye Mto Malale, baada ya boti hiyo kuanza safari Tungan Sule wilayani Malale.

Picha za setilaiti zinaonyesha kiwango cha maporomoko ya ardhi ya Sudan

Picha ya Setilaiti

Tumepokea picha za ubora wa juu za setilaiti zinazoonyesha eneo lililoathiriwa na maporomoko ya ardhi yaliyosababisha maafa siku ya Jumapili katika eneo la Darfur magharibi mwa Sudan.

Picha kutoka kwa kampuni maalum ya setilaiti Maxar zilituwezesha kutathmini ukubwa wa maporomoko hayo.

Tumelinganisha picha za setilaiti na video na picha za matokeo ambayo tulithibitisha hapo awali kuwa zilipigwa katika eneo la kusini mwa kijiji cha Tarseen katika milima ya Marra.

Kulingana na uchanganuzi wa Maxar wa picha hizo “mtiririko wa udongo uliotokana na maporomoko ya ardhi inakuonekana kuelekea katikati ya jiji lolote karibu na eneo hilo.

Hii inalingana na kile BBC Verify imekuwa ikiona katika video za baadaye zilizowekwa kwenye mitandao ya kijamii.

Pi inazua maswali kuhusu ni watu wangapi waliofariki, ikizingatiwa kundi la watu wenye silaha linalodhibiti eneo hilo limesisitiza kuwa zaidi ya watu 1,000 walifariki.

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanakadiria kwa uchache watu 370 walifariki lakini wamesema ni vigumu kutathmini ukubwa wa tukio hilo au idadi kamili ya vifo kutokana na ugumu wa kufikia eneo hilo.

Wafanyakazi wa kutoa misaada kutoka mashirika kadhaa wanatarajiwa kufika eneo lililoathiriwa leo Alhamisi.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment