Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Rais wa Urusi Vladimir Putin anasema alifikia “maelewano” na Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mpamgo wa kumaliza vita vya Ukraine, katika mkutano wao huko Alaska mwezi uliopita.
Lakini hakusema kama atakubali mazungumzo ya amani na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky yaliyosimamiwa na Trump, ambaye inaonekana alitoa Jumatatu kama tarehe ya mwisho ya jibu la Putin.
Akizungumza wakati wa mkutano wa kilele nchini China, Putin aliendelea kutetea uamuzi wake wa kuivamia Ukraine, kwa mara nyingine tena akilaumu vita dhidi ya nchi za Magharibi.
Kufuatia mkutano wa Alaska, mjumbe maalum wa Marekani Steve Witkoff alisema Putin amekubali kudhaminiwa usalama wa Ukraine kama sehemu ya uwezekano wa makubaliano ya amani ya siku zijazo, ingawa Moscow bado haijathibitisha hilo.
Putin alikuwa akizungumza mjini Tianjin katika mkutano wa kilele wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai, ambapo alikutana na Xi Jinping na Narendra Modi.
Aliwashukuru viongozi wa China na India kwa msaada wao na juhudi zao za “kuwezesha utatuzi wa mgogoro wa Ukraine”.
China na India ndio wanunuzi wakubwa wa mafuta ghafi ya Urusi, na yamekuwa yakikosolewa na mataifa ya Magharibi kwa kuunga mkono uchumi wa Urusi ambao umeathiriwa na juhudi za vita.
Katika hotuba yake, Putin pia alisema kwamba “maelewano yaliyofikiwa” katika mkutano wake na Trump huko Alaska ni “Hatua, kuelekea njia ya amani nchini Ukraine”.
Rais wa China azungumzia ‘tabia ya uonevu’ katika utaratibu wa dunia

Rais wa China Xi Jinping amepinga kile alichokiita ‘tabia ya uonevu’ katika utaratibu wa ulimwengu wakati akitoa hotuba katika mkutano muhimu wa usalama na kiuchumi kaskazini mwa China wa Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO).
Katika kile kinachoonekana kama ukosoaji wa Marekani, Bwana Xi alitoa wito kwa viongozi zaidi ya ishirini wa dunia waliohudhuria mkutano huo kupinga kile alichokiita ‘fikra za Vita Baridi’.
China na Urusi ziliwahi kusema Shirika la Ushirikiano la Shanghai (SCO) ni njia mbadala ya Ushirikiano wa Jeshi la NATO.
“Hali ya sasa ya kimataifa inakuwa ya machafuko,” Xi aliwaambia viongozi.
“Majukumu ya usalama na maendeleo yenye kukabili nchi wanachama yamekuwa magumu zaidi,” aliongeza.
“Ukitazama siku zijazo, huku ulimwengu ukiwa unapitia msukomsuko na mabadiliko, lazima tuendelee kufuata ari ya SCO, kuwa makini, kufikiria mbele na kufanya maamuzi mazuri, na kushirikiana vizuri kama shirika,” Rais wa Xi Jinping alisema.
Marufuku ya kutotoka nje yawekwa katika maeneo yenye ghasia za kikabila Kenya

Mamlaka nchini Kenya imeweka marufuku ya kutotoka nje kwa siku saba kuanzia jioni hadi alfajiri katika baadhi ya sehemu za kaunti ya Nakuru baada ya kuanza kwa ghasia za kikabila.
Takriban mtu mmoja ameuawa na wengine wanane kujeruhiwa huku nyumba takriban 12 zikichomwa moto kufuatia mapigano ya kikabila huko Tipis na maeneo ya Mwisho wa Lami.
Vurugu hizo, ambazo ziliibuka Jumamosi katika mpaka wa Nakuru -Narok, zilisababisha familia kadhaa kuhama makazi yao baada ya washambuliaji kuchoma moto nyumba na mali.
Kufikia jana Jumapili 31/08/2025, hali ya wasiwasi bado ilikuwa juu wakaazi walipofunga sehemu za Barabara ya Nakuru -Narok huko Mwisho Wa Lami, wakipinga mauaji hayo na kudai serikali iingilie kati.
Kufuatia ghasia hizo, serikali imepeleka maafisa wa usalama eneo hilo kurejesha utulivu.
Waasi wa Houthi wavamia majengo ya UN nchini Yemen

Waasi wa Yemen wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran walivamia ofisi za Umoja wa Mataifa katika mji mkuu wa Yemen Sanaa siku ya Jumapili na kuwaweka kizuizini takriban wafanyakazi 11 wa Umoja huo, shirika hilo lilisema.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alisema Wahouthi waliingia kwa nguvu katika majengo ya Mpango wa Chakula Duniani (WFP), wakachukua mali ya Umoja wa Mataifa na kujaribu kuingia katika ofisi nyingine za Umoja huo katika mji mkuu.
Mjumbe Maalumu wa Umoja wa Mataifa kwa Yemen Hans Grundberg alisema katika taarifa tofauti kwamba wafanyakazi11 wanazuiliwa huko Sanaa na mji wa bandari wa Hodeidah.
Grundberg alisema kuzuiliwa kwao ni pamoja na wafanyikazi wengine 23 wa UN waliowekwa kizuizini hapo awali, wengine tangu 2021, na mmoja ambaye alikufa kizuizini mwaka huu.
Kocha wa zamani wa Man Utd Ten Hag atimuliwa Leverkusen

Kocha wa zamani wa Manchester United Erik ten Hag amefutwa kazi na klabu ya Ujerumani Bayer Leverkusen baada ya mechi mbili pekee za ligi kuu.
Ten Hag, 55, alisajiliwa na klabu hiyo ya Ujerumani msimu wa kiangazi baada ya kutimuliwa na United mwezi Oktoba.
“Hakuna aliyetaka kuchukua hatua hii,” mkurugenzi mkuu wa Leverkusen Simon Rolfes aliambia tovuti ya klabu ”lakini, wiki chache zilizopita zimeonyesha ni vigumu kuunda timu mpya itakayofikia mafanikio tunayotarajia.”
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.