Serikali ya Marekani yamfuta kazi Mkurugenzi wa kudhibiti na kuzuia magonjwa

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

Susan Monarez aliidhinishwa kuongoza shirika la afya ya umma la Marekani na Seneti mwezi Julai
Maelezo ya picha,Susan Monarez aliidhinishwa kuongoza shirika la afya ya umma la Marekani na Seneti mwezi Julai

Ikulu ya Marekani imemfuta kazi Mkurugenzi wa Vituo vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), Dkt. Susan Monarez, baada ya kukataa kujiuzulu siku ya Jumatano.

Kupitia taarifa rasmi, Ikulu ilieleza kuwa Dkt. Monarez “hailingani na ajenda ya rais,” na kwa sababu hiyo akaondolewa rasmi katika nafasi yake katika taasisi hiyo ya afya ya umma.

Hapo awali, Idara ya Afya ya Marekani ilikuwa imetangaza kuondoka kwake, hali iliyosababisha majibu kutoka kwa mawakili wa Dkt. Monarez waliodai kuwa hakujulishwa kuhusu hatua hiyo na kwamba hakuwa na nia ya kujiuzulu.

Mawakili wake walidai kuwa mteja wao alikuwa akilengwa kwa sababu ya kukataa “kupitisha maagizo yasiyo ya kisayansi na ya hatari, na kufukuza wataalamu wa afya waliobobea,” huku wakimtuhumu Waziri wa Afya, Robert F. Kennedy Jr., kwa “kutumia afya ya umma kama silaha ya kisiasa.”

“Kama ilivyoelezwa wazi katika tamko la mawakili wake, Susan Monarez hailingani na ajenda ya rais,” Ikulu ilisisitiza baadaye Jumatano, ikiongeza kuwa amefutwa kazi rasmi kama mkurugenzi wa CDC.

Dkt. Monarez, mwanasayansi mwenye uzoefu wa muda mrefu katika serikali ya shirikisho, aliteuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump kuongoza CDC, na uteuzi wake ulithibitishwa na Seneti kwa kura zilizogawanyika kisiasa mnamo Julai.

Uteuzi wake ulifuatia hatua ya Trump ya kuondoa uteuzi wa awali wa aliyekuwa Mbunge wa Republican, Dave Weldon, ambaye alikumbwa na upinzani kutokana na misimamo yake kuhusu chanjo na uhusiano wake na ugonjwa wa usonji (autism).

Kuondolewa kwa Dkt. Monarez kunajiri takriban wiki moja baada ya chama cha wafanyakazi wa CDC kutangaza kuwa wafanyakazi wapatao 600 walifutwa kazi.

Mabadiliko hayo makubwa yamewaathiri wafanyakazi waliokuwa wakihusika na agenda ya serikali dhidi ya magonjwa ya kuambukiza kama mafua ya ndege, pamoja na watafiti wa hatari za kimazingira na wale waliokuwa wakishughulikia maombi ya taarifa za umm

Urusi yachagua mashambulizi badala ya meza ya mazungumzo – Zelensky

Picha ya Rais wa Ukraine Zelensky
Maelezo ya picha,Picha ya Rais wa Ukraine Zelensky

Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, amesema kuwa watu wanane, akiwemo mtoto mmoja, wameuawa katika mashambulizi ya usiku dhidi ya mji mkuu, Kyiv.

Akielezea mashambulizi hayo kama “shambulio kubwa dhidi ya miji na jamii zetu,” Zelensky amesema kuwa makumi ya watu wamejeruhiwa, na wahudumu wa dharura wanaendelea kuwaokoa waliokwama chini ya kifusi.

Katika taarifa yake, Zelensky amesema: “Mashambulizi haya ni jibu la wazi kwa kila mtu duniani ambaye, kwa wiki na miezi kadhaa, amekuwa akitoa wito wa kusitisha mapigano na kwa diplomasia ya kweli.”

Akaongeza: “Urusi inachagua makombora badala ya meza ya mazungumzo. Inachagua kuendelea kuua badala ya kumaliza vita. Na hili linamaanisha kuwa Urusi bado haiogopi athari za matendo yake.

“Tunatarajia majibu kutoka kwa kila mtu duniani ambaye amewahi kutoa wito wa amani lakini sasa anakaa kimya badala ya kuchukua msimamo wa kimaadili. Na kwa hakika, huu ni wakati wa kuweka vikwazo vipya na vikali dhidi ya Urusi kwa yote inayoendelea kufanya.”

Kwa mujibu wa jeshi la anga la Ukraine, mashambulizi ya anga ya usiku kutoka Urusi yalihusisha ndege zisizo na rubani 598, makombora 11 ya mwendo wa risasi na makombora 20 ya masafa marefu, yaliyolenga maeneo mbalimbali nchini humo.

Kati ya hayo, droni 563, makombora 8 ya mwendo wa risasi, na makombora 18 ya masafa marefu yaliangushwa kabla ya kufikia malengo yao.

Haijafahamika bado ni mashambulizi mangapi yaliyolenga moja kwa moja Kyiv.

Hili limekuwa shambulio kubwa zaidi dhidi ya mji mkuu tangu tarehe 31 Julai, ambapo zaidi ya watu 30 waliuawa.

Kabla ya hapo, tarehe 21 Agosti, Urusi ilifanya shambulio kubwa la anga lililohusisha droni 574 na makombora 40, likilenga zaidi maeneo ya magharibi mwa Ukraine, na kusababisha kifo cha mtu mmoja na kujeruhi zaidi ya watu 20.

Trump aongoza kikao kuhusu mustakabali wa Gaza baada ya vita

Picha ya Rais wa Marekani Donald Trump mnamo Agosti 26, 2025.
Maelezo ya picha,Picha ya Rais wa Marekani Donald Trump mnamo Agosti 26, 2025.

Rais wa Marekani, Donald Trump, aliongoza kikao maalum siku ya Jumatano kujadili hali ya Ukanda wa Gaza mara baada ya kumalizika kwa vita vinavyoendelea, kwa mujibu wa afisa mwandamizi wa Ikulu ya White House.

Kikao hicho kilihudhuriwa na aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Tony Blair, pamoja na Jared Kushner, mjumbe wa zamani wa Trump kwa masuala ya Mashariki ya Kati.

Pia walikuwepo maafisa waandamizi wa serikali ya Marekani.

Kwa mujibu wa chanzo hicho kilichozungumza na shirika la habari la Reuters, mazungumzo yalihusu masuala yote muhimu yanayohusiana na Gaza, yakiwemo kuongeza kiwango cha misaada ya chakula, mzozo wa mateka unaoendelea, na mikakati ya kisera kwa kipindi cha baada ya vita.

Afisa huyo aliweka wazi kuwa kikao hicho kilikuwa cha kisiasa tu, na ni sehemu ya mikutano ya mara kwa mara inayofanywa na Trump na washauri wake wa karibu.

Hata hivyo, Hamas ililaani kikao hicho hata kabla ya kufanyika, ikilituhumu vikali utawala wa Marekani kwa kuonyesha upendeleo kwa Israel.

Kupitia taarifa rasmi, kiongozi wa Hamas, Izzat al-Rishq, alielezea mshangao wa wanamgambo wa Hamas kufuatia matamshi ya hivi karibuni ya mshauri wa Marekani, Witkoff, ambaye alilaumu Hamas kwa kuvuruga mazungumzo ya usitishaji wa mapigano.

Katika tukio jingine lililojiri sambamba, Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo, alitoa wito mzito kwa jumuiya ya kimataifa kusitisha vita vilivyozidi miaka miwili kati ya Israel na Hamas.

“Kwa mara nyingine tena ninatoa ombi… la kukomesha mzozo katika ardhi takatifu, ambao umesababisha hofu kubwa, uharibifu na vifo,” Papa alisema katika hadhira yake kuu ya kila wiki huko Vatican.

Aliendelea, “Ninatoa wito wa kuachiliwa kwa mateka wote, usitishaji wa kudumu wa mapigano, kuwezesha upatikanaji salama wa kibinadamu, na heshima kamili kwa sheria ya kimataifa ya kibinadamu.”

Hata hivyo, Papa hakutaja Israeli au Hamas kwa jina, lakini alisema kuwa sheria za kimataifa zinahitaji “ulinzi wa raia, kukataza adhabu ya pamoja, matumizi ya nguvu kiholela, na kulazimishwa kuhama watu.”

Kim Jong Un kuungana na Putin na viongozi wengine katika gwaride la kijeshi nchini China

Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim (kushoto) atakutana na kiongozi wa China Xi (Kulia) mwezi Septemba
Maelezo ya picha,Kiongozi wa Korea Kaskazini Kim (kushoto) atakutana na kiongozi wa China Xi (Kulia) mwezi Septemba

Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un, anatarajiwa kuhudhuria gwaride la kijeshi litakalofanyika jijini Beijing wiki ijayo, kwa mujibu wa taarifa kutoka Wizara ya Mambo ya Nje ya China.

Hii inaelezwa kuwa ndiyo mara yake ya kwanza kushiriki katika mkutano wa kimataifa wa viongozi wa juu.

Gwaride hilo, linalojulikana kama Siku ya Ushindi, litaadhimisha miaka 80 tangu China ilipoingia vitani dhidi ya Japan na kuhitimisha Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Rais wa Urusi, Vladimir Putin, pia atahudhuria tukio hilo akiwa miongoni mwa wakuu wa nchi 26 wanaotarajiwa kushiriki.

Tukio hili linakuja siku chache baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kueleza nia ya kukutana na Kim Jong Un.

China inatarajiwa kuonesha kikosi chake cha kijeshi na teknolojia ya kisasa, ikiwemo ndege za kivita kwa mamia, vifaru, na mifumo ya kisasa ya kukabiliana na ndege zisizo na rubani.

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa muundo mpya wa jeshi la China kuoneshwa kikamilifu katika gwaride la hadhara.

Gwaride hilo lililopangiliwa kwa umahiri mkubwa litafanyika katika Uwanja wa Tiananmen, likihusisha zaidi ya wanajeshi elfu kumi, wakiwemo askari kutoka vitengo 45 vya jeshi la China na askari waliostaafu wa vita.

Tukio hilo la dakika 70 litasimamiwa na Rais wa China, Xi Jinping, na linatarajiwa kufuatiliwa kwa karibu na wachambuzi wa masuala ya kijeshi na mataifa ya Magharibi.

Kuhudhuria kwa Kim kunaashiria hatua kubwa ya kidiplomasia, ikilinganishwa na gwaride la mwaka 2015 ambapo Korea Kaskazini iliwakilishwa na afisa wa ngazi ya juu, Choe Ryong-hae.

Uwepo wa Kim katikati ya Beijing, akisimama pamoja na Putin wa Urusi na Xi wa China, utakuwa tukio la kuvutia kisiasa na picha ya ujumbe wa nguvu wa ushirikiano wa mataifa hayo.

Aidha, ni mafanikio muhimu ya kidiplomasia kwa Rais Xi Jinping, hasa katika kuonesha ushawishi wake wa kikanda na kimataifa.

Mwanaharakati Boniface Mwangi, autaka urais Kenya

Mwangi

Mwanaharakati wa haki za binadamu nchini Kenya, Boniface Mwangi, ambaye amejipatia umaarufu kutokana na kushiriki kwa kiasi kikubwa maandamano ya kupinga serikali, ametangaza Jumatano kwamba atagombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2027.

Uamuzi wake utaonyesha iwapo uungwaji mkono mkubwa wa maandamano, hasa kutoka kwa vijana wa Kenya katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, unaweza kutafsiriwa kuwa nguvu ya kisiasa kupitia kura.

Mwangi aliwahi kugombea ubunge mwaka 2017 kwa ajenda ya kupinga ufisadi, lakini hakufanikiwa. Kwa miaka mingi amejijengea sifa ya kuwa msemaji jasiri dhidi ya ukiukwaji wa haki za binadamu ndani na nje ya Kenya. “Uongozi wetu umetufeli kwa njia nyingi.

Unalipa kodi ukitarajia huduma, kinyume chake unalazimika kutoa rushwa ili kupata huduma hizo hizo,” alisema wakati wa uzinduzi wa azma yake ya kugombea urais.

“Kwa hivyo tunaposimama hapa, ni lazima turudishe nchi mikononi mwetu.”

Mnamo Mei mwaka huu, Mwangi alifukuzwa nchini Tanzania baada ya kusafiri huko kushuhudia kesi ya uhaini inayomkabili kiongozi wa upinzani, Tundu Lissu. Aidha, mnamo Julai, mahakama ya Kenya ilimfungulia mashtaka ya kumiliki mabomu ya machozi na risasi moja iliyopatikana nyumbani kwake.

Alikana mashtaka hayo, akisema mamlaka hayana ushahidi na akaitaja kesi hiyo kama “aibu kubwa.”

Manchester United yaibishwa na vibonde Grimsby, yaondoshwa Carabao Cup

x

Manchester United wamepata aibu kubwa baada ya kuondolewa kwenye Carabao Cup na vibonde Grimsby ya League Two, wakipoteza kwenye mikwaju ya penalti 12-11 uwanjani Blundell Park.

United walijikuta nyuma kwa mabao mawili mapema kipindi cha kwanza, huku kipa aliyerejea langoni Andre Onana akihusika na bao la pili la Grimsby. Charles Vernam na Tyrell Warren walifunga mabao ya wenyeji kabla ya Bryan Mbeumo na Harry Maguire kusawazisha dakika ya mwisho.

Katika mikwaju ya penalti, Matheus Cunha alikosa penalti ya tano ya United, kisha Mbeumo pia akagonga mwamba, na hivyo kuipa Grimsby ushindi wa kihistoria. Mashabiki wenye furaha walivamia uwanja kuadhimisha ushindi huo.

Kocha Ruben Amorim alionekana kupoteza mwelekeo benchi la ufundi huku timu yake ikipoteza nafasi nyingine ya kushiriki kwenye fursa ya mataji msimu huu. Kocha huyo amekuwa na rekodi zisizoridhisha tangu amejiunga na timu hiyo msimu uliopita, huenda akaingia kwneye mjadala wa mabosi kuhusu hatma yake.

Nyimbo za kejeli kutoka kwa mashabiki wa Grimsby zilisikika mara kwa mara kipindi cha kwanza na zaidi baada ya mchezo.

Kwa ujumla, United walionyesha jitihada za kutaka kushinda mchezo kupitia mabadiliko ya wachezaji kadhaa, lakini makosa ya kipa na kushindwa kwenye mikwaju ya penati yaligharimu timu hiyo, ikiacha historia ya Grimsby kuwa mojawapo ya usiku wa kipekee klabuni humo.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment