Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Kwa mujibu wa Tume huru ya taifa ya uchaguzi (INEC), uteuzi wa wagombea utafanyika kati ya saa 1.30 mpaka saa 10:00 alasiri.

Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) inatarajiwa leo, Jumatano Agosti 27, 2025, kufanya zoezi la uteuzi wa wagombea wa nafasi ya Rais na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na wagombea wa Ubunge na Udiwani kote nchini.
Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi na masharti ya Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya Mwaka 2024, uteuzi huo utaanza saa 1:30 asubuhi na kukamilika saa 10:00 jioni.
Zoezi la uteuzi wa wagombea wa urais litafanyika katika ofisi za INEC, Njedengwa jijini Dodoma, wakati wagombea wa ubunge watawasilisha fomu kwa wasimamizi wa uchaguzi katika ngazi ya majimbo na wagombea udiwani kwa wasimamizi wasaidizi katika ngazi ya kata.
Mara baada ya kukamilika kwa zoezi la uteuzi, INEC imesema majina ya wagombea wote yatabandikwa kwenye mbao za matangazo katika maeneo husika kwa ajili ya ukaguzi wa umma.
Tume imewataka vyama vya siasa na wagombea kuhakikisha wanazingatia muda uliopangwa na maelekezo waliyopatiwa, ili kuepuka changamoto katika zoezi hilo muhimu.
Trump kuongoza mkutano kuhusu hali ya Gaza siku moja baada ya vita kumalizika

Rais wa Marekani Donald Trump ataongoza mazungumzo kuhusu Gaza katika Ikulu ya White House siku ya Jumatano, kwa mujibu wa Mjumbe Maalum wa Marekani Steve Witkoff, akiongeza kuwa Washington inatarajia azimio la vita vya Israel huko Gaza ifikapo mwisho wa mwaka.
Trump alikuwa ameahidi kumalizika kwa haraka kwa vita huko Gaza wakati wa kampeni yake ya uchaguzi wa 2024, lakini baada ya kuchukua madaraka mnamo Januari, lengo hilo linaonekana kutoweza kufikiwa.
Mkutano huu mpana, unaoongozwa na Trump, unaenda sambamba na mkutano kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio na mwenzake wa Israel, Gideon Sa’ar, mjini Washington siku ya Jumatano, kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani.
Alipoulizwa katika mahojiano na Fox News kama kulikuwa na mpango wa awamu ya baada ya vita huko Gaza, Witkoff alisema, “Ndiyo, tuna mkutano katika Ikulu ya White House (Jumatano) ambao utaongozwa na rais, na kuna mpango wa kina ambao tunatayarisha kuhusu siku inayofuata.”
Alipoulizwa, “Je, Israeli inapaswa kuchukua hatua yoyote tofauti kumaliza vita na kuwarudisha mateka nyumbani?” Witkoff alijibu, “Tunaamini tutasuluhisha hili kwa njia moja au nyingine, bila shaka kabla ya mwisho wa mwaka huu.”
Witkov alithibitisha kuwa Israel iko tayari kuendelea na mazungumzo na Hamas. Pia alieleza kuwa vuguvugu hilo limeonesha nia yake ya kufikia suluhu.
UN yataka haki itendeke kutokana na mashambulizi ya Israel dhidi ya hospitali ya Gaza

Umoja wa Mataifa umesema “kuna haja ya kupatikana kwa haki” kufuatia mashambulizi ya Israel dhidi ya hospitali ya Gaza na kusababisha vifo vya takribani watu 20, huku uchunguzi wa awali wa jeshi la Israel ukisema kuwa mashambulizi hayo yalilenga “kamera iliyokuwa iliyowekwa na Hamas”.
Lawama kuhusu shambulio hilo, ambalo waathiriwa wake ni pamoja na waandishi wa habari watano na wafanyakazi wanne wa afya, zimekuwa zikiongezeka, huku Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer akikielezea kuwa “haiwezi kutetewa kabisa”.
Baadaye Jumanne Jeshi la Ulinzi la Israel (IDF) lilitoa matokeao ya uchunguzi wake wa awali, ambao ulibaini “dosari” kadhaa kwa uchunguzi zaidi.
Hatua hiyo ilikuja wakati Waisraeli wakizindua siku ya maandamano ya nchi nzima kuitaka serikali yao kukubali makubaliano ya kuwaachilia mateka.
Urusi kujenga kituo cha nyuklia cha aina yake Niger

Urusi imeahidi kujenga kituo cha umeme wa nyuklia nchini Niger, taifa lenye utajiri wa urani lakini linaloagiza umeme wake mwingi.
Ingawa huenda mpango huo usitekelezwe, ni hatua inayoongeza ushawishi wa Moscow barani Afrika wakati Niger ikizidisha mgongano na Ufaransa, aliyekuwa mtawala wa kikoloni.
Mwezi Juni, serikali ya kijeshi ya Niger ilitaifisha mgodi wa urani uliokuwa chini ya kampuni ya Kifaransa Orano, hatua iliyofungua mlango kwa Urusi kujitokeza kama mshirika mpya.
Kampuni ya serikali ya Urusi, Rosatom, tayari imesaini makubaliano ya kushirikiana katika uzalishaji wa nishati na matumizi ya kitabibu pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalamu wa ndani.
Iwapo mradi huu utatekelezwa, utakuwa wa kwanza wa aina yake Afrika Magharibi.
Wakati Ufaransa ilichukua urani ya Niger kwa miongo kadhaa kuendesha mitambo yake ya nyuklia, taifa hilo la Afrika lilibaki likitegemea makaa na umeme wa kuagiza kutoka Nigeria.
Waziri wa Nishati wa Urusi Sergei Tsivilev alisema mjini Niamey Julai 28 kuwa lengo la Moscow si uchimbaji pekee wa urani, bali kujenga mfumo mzima wa nishati ya atomiki kwa matumizi ya amani nchini Niger.
Urusi yaingia mkoa wa Dnipropetrovsk, Ukraine yathibitisha

Jeshi la Ukraine limekiri kuwa majeshi ya Urusi yamevuka na kuingia katika mkoa wa viwanda wa Dnipropetrovsk, mashariki mwa nchi hiyo, na kujaribu kujikita katika eneo hilo.
Afisa wa kundi la kijeshi la Dnipro, Viktor Trehubov, ameiambia BBC kuwa huu ndio mashambulizi ya kwanza ya kiwango kikubwa katika mkoa huo, ingawa alisisitiza kuwa jeshi la Ukraine limefanikiwa kusimamisha kasi ya adui.
Tangu mapema kiangazi, Urusi imekuwa ikidai mara kwa mara kuwa majeshi yake yameingia Dnipropetrovsk kupitia Donetsk, ambapo mapigano makali yamekuwa yakiendelea.
Mwezi Juni, viongozi wa Urusi walitangaza kuanza kwa operesheni katika eneo hilo, lakini ripoti za hivi karibuni kutoka Ukraine zinaonesha kuwa wapiganaji wa Urusi wamepenya kidogo tu katika mpaka wa mkoa huo.
Mkoa wa Dnipropetrovsk, ambao kabla ya vita ulikuwa na wakazi zaidi ya milioni tatu, ni kituo kikubwa cha pili cha viwanda nchini Ukraine baada ya Donbas (inayojumuisha Donetsk na Luhansk).
Ingawa Urusi haijatangaza rasmi kudai Dnipropetrovsk kama ilivyofanya kwa baadhi ya mikoa ya mashariki, imekuwa ikishambulia miji yake mikuu ikiwemo mji wa Dnipro.
Hali hii inakuja wakati Marekani ikiendelea kuongoza juhudi za kidiplomasia kumaliza vita, licha ya mazungumzo kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na Rais wa Urusi Vladimir Putin yaliyofanyika Alaska kutoonesha mafanikio makubwa.
Ripoti zinaeleza kuwa Putin alimweleza Trump yuko tayari kusitisha vita endapo Ukraine itakubali kukabidhi maeneo ya Donetsk yanayodhibitiwa na Kyiv, ingawa wananchi wengi wa Ukraine wanaamini Urusi ina ajenda pana zaidi.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.