Mwanajeshi wa Marekani ahukumiwa kwa kufanya ujasusi kwa ajili ya China

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Baharia wa Jeshi la Wanamaji la Marekani huko California amehukumiwa kwa kosa la ujasusi kwa kuuza siri za kikosi hicho kwa afisa wa China ambaye alimsajili kupitia mtandao ya kijamii.

Jinchao Wei, 25, alipatikana na hatia ya mashtaka sita, ikiwa ni pamoja na ujasusi, njama ya kufanya ujasusi, na usafirishaji haramu wa data za siri kuhusu meli za Jeshi la Wanamaji la Marekani.

“Vitendo vya mshtakiwa vinawakilisha usaliti mkubwa wa uaminifu aliopewa kama mwanajeshi wa Marekani,” Mwanasheria wa Marekani Adam Gordon alisema katika taarifa yake baada ya hukumu kusomwa.

“Kwa kufanya biashara ya siri za kijeshi kwa Jamhuri ya Watu wa China kwa ajili ya pesa taslimu, alihatarisha sio tu maisha ya wanamaji wenzake bali pia usalama wa taifa zima na washirika wetu.”

Wei, anayejulikana pia kama Patrick Wei, alikamatwa mnamo Agosti 2023 kwa mashtaka ya ujasusi alipokuwa akiwasili kufanya kazi kwenye meli ya mashambulizi ya amphibious, USS Essex.

Raia wa Marekani kwa kuandikishwa uraia, Wei alikuwa fundi mitambo na mwenye kibali cha usalama, na pia alipata taarifa nyeti kuhusu meli hiyo na nyingine zilizokuwa eneo la Pasifiki.

Wakati wa kesi yake ya wiki nzima, waendesha mashtaka waliwasilisha ushahidi ikiwa ni pamoja na mazungumzo ya simu, jumbe za kielektroniki, na jumbe za sauti ambazo Wei alibadilishana na mhudumu wake wa Kichina.

Wei alimwita mhudumu huyo wa Kichina “Big Brother Andy” na kuomba waweke uhusiano wao kuwa siri kwa kutumia programu nyingi zilizosimbwa kuwasiliana na kukubali malipo. Wei pia alitumia kompyuta mpya na simu ya mhudumu wake.

Israel yaidhinisha mradi wa makazi ya Ukingo wa Magharibi wenye utata

.

Israel imetoa idhinisho la mwisho kwa mradi wa makazi wenye utata ambao utaondoa kabisa Ukingo wa Magharibi unaokaliwa na Jerusalem Mashariki na kugawanya eneo hilo mara mbili.

Ujenzi katika eneo la E1 umesitishwa kwa miongo miwili huku kukiwa na upinzani mkali wa kimataifa. Wakosoaji wanaonya kuwa mpango huo utaondoa matumaini ya kuwepo kwa taifa la Palestina.

Siku ya Jumatano, kamati ya wizara ya ulinzi iliidhinisha mpango wa nyumba 3,400 katika eneo la E1. Waziri wa fedha wa mrengo wa kulia mwenye msimamo mkali Bezalel Smotrich, ambaye alizindua mpango huo wiki jana, alisema wazo la taifa la Palestina “linaondolewa”.

Mamlaka ya Palestina ililaani hatua hiyo ikisema kuwa ni kinyume cha sheria na itaharibu matarajio ya kupatikana kwa suluhisho la serikali hizo mbili.

Hatua hiyo inafuatia kuongezeka kwa idadi ya nchi zilizosema zitatambua taifa la Palestina, ambalo Israel imelaani.

Israel imejenga takriban makazi 160 ya Wayahudi 700,000 tangu ilipoikalia kwa mabavu Ukingo wa Magharibi na Jerusalem Mashariki – ardhi ambayo Wapalestina wanataka, pamoja na Gaza, kwa taifa linalotarajiwa – wakati wa vita vya Mashariki ya Kati vya 1967. Takriban Wapalestina milioni 3.3 wanaishi kando yao.

Makazi hayo ni kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa – msimamo ulioungwa mkono na maoni ya ushauri ya Mahakama ya Kimataifa ya Haki mwaka jana.

Serikali za Israel zilizofuatana zimeruhusu kuendelezwa kwa makazi. Hata hivyo, upanuzi umeongezeka kwa kasi tangu Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu aliporejea madarakani mwishoni mwa 2022 akiwa mkuu wa muungano wa mrengo wa kulia, unaounga mkono walowezi, pamoja na kuanza kwa vita vya Gaza vilivyochochewa na shambulizi la Hamas la tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya Israel.

Jeshi la Israel lasema hatua za kwanza za kushambulia mji wa Gaza zimeanza

.

Jeshi la Israel linasema limeanza “hatua za awali” za mashambulizi ya ardhini yaliyopangwa kuuteka na kukalia kwa mabavu mji wote wa Gaza na tayari wameshikilia viunga vyake.

Msemaji wa jeshi alisema kuwa wanajeshi tayari wanaendelea kupanga mikakati yao katika maeneo ya Zeitoun na Jabalia ili kuweka msingi wa mashambulizi hayo, ambayo Waziri wa Ulinzi Israel Katz aliidhinisha siku ya Jumanne na yatajadiliwa kwenye baraza la mawaziri la usalama baadaye wiki hii.

Takriban wanajeshi wa akiba 60,000 wameitwa kuanzia mwanzo wa Septemba ili kuwaachilia walio kazini kwa ajili ya operesheni hiyo.

Hamas imeishutumu Israel kwa kukwamisha makubaliano ya kusitisha mapigano kwa ajili ya kuendeleza “vita vya kikatili dhidi ya raia wasio na hatia”, shirika la habari la Reuters liliripoti.

Mamia kwa maelfu ya Wapalestina katika mji wa Gaza wanatarajiwa kuamriwa kuhama na kuelekea kwenye makazi kusini mwa Gaza huku matayarisho ya Israel yakiendelea.

Washirika wengi wa Israel wamelaani mpango huo, huku Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron akionya Jumatano kwamba “unaweza tu kusababisha maafa kwa wote wawili na hatari ya kulitumbukiza eneo lote katika mzunguko wa vita vya kudumu”.

Wakati huo huo, Kamati ya Kimataifa ya Msalaba Mwekundu (ICRC) ilisema kuhamisha watu zaidi na kuongezeka uhasama kuna “hatarisha kuzidisha hali ambayo tayari ni janga” kwa wakazi milioni 2.1 wa Gaza.

Serikali ya Israel ilitangaza nia yake ya kuliteka eneo lote la Ukanda wa Gaza baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas juu ya kusitisha mapigano na kuachiliwa huru kwa mateka kusambaratika mwezi uliopita.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment