Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph
https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa
Rais wa Marekani amekubali vita vya Ukraine “ilikuwa vigumu kutatua” baada ya siku kadhaa za mazungumzo ya kiwango cha juu.

Ikulu ya Urusi imepuuzilia mbali mazungumzo kuhusu mkutano kati ya Rais wa Urusi Vladimir Putin na Volodymyr Zelensky wa Ukraine, huku Donald Trump akitoa wito kwa viongozi hao wawili kukutana ili kujadili kumaliza vita nchini Ukraine.
Shinikizo la kufanyika kwa mkutano baina ya nchi hizo mbili linakuja baada ya rais wa Marekani kukutana na Putin mjini Alaska wiki iliyopita, na kuwakaribisha viongozi saba wa Ulaya na Zelensky katika Ikulu ya White House siku ya Jumatatu.
Trump alikiri mzozo huo ulikuwa “vigumu” kusuluhisha na akakubali kuwa inawezekana rais wa Urusi hakutaka kumaliza uhasama.
“Tutajua kuhusu Rais Putin katika wiki kadhaa zijazo,” alisema Jumanne. “Inawezekana kwamba hataki kufanya makubaliano.”
Putin alikabiliwa na “wakati mgumu” ikiwa ndivyo ilivyokuwa, Trump aliongeza, bila kutoa maelezo yoyote.
Rais wa Urusi siku ya Jumatatu alimwambia Trump kuwa yuko “sawa” na wazo la mazungumzo ya moja kwa moja na Ukraine, lakini siku iliyofuata Waziri wa Mambo ya Nje Sergei Lavrov alipuuzilia mbali ahadi hiyo hatua ambayo tayari haijaeleweka.
Mkutano wowote ungepaswa kutayarishwa “hatua kwa hatua… kuanzia ngazi ya wataalam na baada ya hapo kupitia hatua zote zinazohitajika”, alisema, akirudia maneno ya mara kwa mara ya Urusi.
Dmitry Polyanskiy, naibu mwakilishi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa, aliiambia BBC “hakuna mtu [aliyekataa]” fursa ya mazungumzo ya moja kwa moja, “lakini haipaswi kuwa mkutano kwa ajili tu ya mkutano uwe umefanyika”.
Siku ya Jumanne, iliripotiwa kwamba Putin alikuwa amependekeza kwa Trump kwamba Zelensky anaweza kusafiri hadi Moscow kwa mazungumzo, jambo ambalo Ukraine haikuweza kukubali kamwe.
Pendekezo hilo linaweza kuwa ni njia ya Urusi ya kuweka chaguo lisilowezekana ambalo Ukraine haiwezi kukubaliana nalo.
Israel inadai kuachiliwa kwa mateka wote wa Gaza huku ikitiliwa shaka iwapo itakubali pendekezo la kusitisha mapigano

Israel inataka kuachiliwa huru kwa mateka wote 50 wanaoshikiliwa huko Gaza, afisa mmoja wa Israel amesema, na kusababisha wasiwasi iwapo itakubali pendekezo jipya la kusitishwa kwa mapigano kwa siku 60 ambalo Hamas ilikubali Jumatatu.
Pendekezo hilo, lililotolewa na Qatar na Misri, litashuhudia kuachiliwa kwa karibu nusu ya mateka na “inakaribiana” na pendekezo la Marekani ambalo Israel ilikuwa imekubali hapo awali, kulingana na Qatar.
Israel haijaikataa waziwazi – lakini msemaji wa serikali ya Israel David Mencer aliiambia BBC kwamba haipendezwi na “mkataba wa nusu nusu”.
“Mambo yamebadilika sasa. Waziri mkuu ameweka mpango wa mustakabali wa Gaza,” Mencer alisema.
Duru za Palestina zilisema pendekezo hilo litashuhudia mateka 10 walio hai na 18 waliokufa wakikabidhiwa Israel huku pande zote zikijadiliana usitishaji wa kudumu wa mapigano na kurejea kwa mateka wengine.
Israel inaamini kuwa ni mateka 20 tu kati ya 50 ambao bado wako hai baada ya miezi 22 ya vita.
Baadaye wiki hii, baraza la mawaziri la Israel linatazamiwa kuidhinisha mpango wa jeshi kuukalia kwa mabavu mji wa Gaza, ambapo mashambulizi makali ya Israel tayari yamewafanya maelfu ya watu kukimbia makazi yao.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alitangaza nia ya Israel ya kuteka Gaza yote – ikiwa ni pamoja na maeneo ambayo wakazi wake wengi wa Wapalestina milioni 2.1 wametafuta hifadhi – baada ya mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja na Hamas kuhusu makubaliano ya kusitisha mapigano kusambaratika mwezi uliopita.
Vichwa sita vilivyokatwa vyapatikana barabarani nchini Mexico

Vichwa sita vilivyokatwa vimepatikana kwenye barabara katikati mwa Mexico, katika eneo ambalo kwa kawaida halihusishwi na vurugu za magenge ya wahalifu.
Mamlaka za eneo hilo ziligundua tukio hilo la kutisha mapema Jumanne asubuhi kwenye njia inayounganisha majimbo yenye amani ya Puebla na Tlaxcala.
Polisi hawajatoa sababu za mauaji hayo au kusema ni kundi gani kati ya wahalifu wanaofanya kazi nchini Mexico ambalo huenda lilitekeleza mauaji hayo.
Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa blanketi iliachwa kwenye eneo la tukio na ujumbe ukitoa onyo kwa magenge yanayopingana na ambayo inaonekana ilitiwa saini na kikundi kiitwacho “La Barredora”, ikimaanisha kufagia.
Ni jina sawa na kundi la wahalifu lisilojulikana sana linaloendesha shughuli zake katika jimbo la magharibi la Guerrero lakini haijabainika iwapo walihusika na shambulio hilo au kwa nini.
Ofisi ya mwendesha mashtaka wa eneo hilo ilisema vichwa vilivyopatikana Tlaxcala ni vya wanaume na imeanzisha uchunguzi kuhusu mauaji hayo, kulingana na shirika la habari la AFP.
Pamoja na biashara haramu ya madawa ya kulevya, kuna suala la mafuta ya magendo katika eneo hilo ambayo inazalisha mabilioni ya dola kwa mwaka kwa makundi yanayoendesha shughuli hiyo haramu.
Mnamo mwezi Juni, miili ya watu 20 – wanne kati yao waliokatwa vichwa – ilipatikana huko Sinaloa, jimbo lililokumbwa na ghasia za magenge.
Vijana saba wa Mexico pia waliuawa kwa kupigwa risasi kwenye sherehe za Kanisa Katoliki katika jimbo la kati la Guanajuato mnamo mwezi Mei.
Vurugu kati ya makundi ya wapiganaji zimeongezeka katika miaka ya hivi karibuni, huku mamia kwa maelfu ya watu wakiuawa na makumi ya maelfu kupotea tangu serikali ilipoanza kutumia jeshi la Mexico dhidi ya magenge mnamo mwaka 2006.
Makumi ya wahamiaji wa Afghanistan kutoka Iran wafariki katika ajali ya basi

Ajali ya trafiki magharibi mwa Afghanistan imeua watu 73, wakiwemo watoto 17, wengi wao wakiwa kwenye basi lililokuwa limewabeba wahamiaji wa Afghanistan waliofukuzwa kutoka Iran, afisa wa Taliban alithibitisha kwa BBC Pashto.
Basi hilo lililokuwa likielekea Kabul lilishika moto Jumanne usiku baada ya kugongana na lori na pikipiki katika mkoa wa Herat, alisema Ahmadullah Mottaqi, mkurugenzi wa habari na utamaduni wa Taliban huko Herat.
Kila mtu ndani ya basi aliuawa, pamoja na watu wawili kutoka kwa magari mengine, alisema.
Katika miezi ya hivi karibuni Iran imeongeza kasi ya kuwafukuza wahamiaji wa Afghanistan wasio na vibali ambao wamekimbia migogoro katika nchi yao.
“Abiria wote walikuwa wahamiaji ambao walikuwa wamepanda gari huko Islam Qala,” msemaji wa gavana wa mkoa Mohammad Yousuf Saeedi aliiambia AFP, akimaanisha mji karibu na mpaka wa Afghanistan na Iran.
Polisi wa Herat walisema ajali hiyo ilitokea kwa sababu ya “kasi na uzembe” wa dereva wa basi hilo, AFP iliripoti.
Ajali za trafiki ni za kawaida nchini Afghanistan, ambapo barabara zimeharibiwa na miongo kadhaa ya migogoro na kanuni za kuendesha gari hazitekelezwi inavyostahili.
Tangu miaka ya 1970, mamilioni ya Waafghanistan wamekimbilia Iran na Pakistan, na mawimbi makubwa wakati wa uvamizi wa Soviet nchini Afghanistan mnamo 1979 na kufuatia kurejea kwa Taliban madarakani mnamo 2021.
Hii imechangia kuongezeka kwa hisia za chuki dhidi ya Afghanistan nchini Iran, huku wakimbizi wakikabiliwa na ubaguzi wa kimfumo.
Iran hapo awali ilikuwa imetoa makataa ya Julai kwa Waafghanistan wasio na vibali kuondoka kwa hiari.
Salah na Rogers washinda Tuzo za Chama cha Wanasoka wa Kulipwa

Winga wa Liverpool, Mohamed Salah ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Chama cha Wanasoka wa Kulipwa, huku kiungo wa Aston Villa, Morgan Rogers akichaguliwa kuwa mchezaji bora chipukizi wa mwaka.
Meneja wa zamani wa England Sir Gareth Southgate ndiye mpokeaji wa tuzo ya sifa ya PFA 2025 kwa mchango wake katika soka na mafanikio akiwa na timu ya taifa.
Salah, 33, ndiye mchezaji wa kwanza kushinda tuzo hiyo mara tatu baada ya kuwa na mchango mkubwa katika mafanikio ya Liverpool msimu uliopita.
Alipoulizwa kama alikuwa na matamanio ya kushinda tuzo wakati akikulia Misri, alisema: “Ni kweli nilitaka kuwa mchezaji wa mpira wa soka na nilitaka kuwa maarufu na kutunza familia yangu, lakini hufikirii mambo makubwa wakati bado uko Misri.
“Unapokua, unaanza kuona mambo kwa njia tofauti, kuwa na tamaa na unaanza kuwa na mtazamo mpana.”
Mchezaji huyo wa kimataifa wa Misri alikuwa mfungaji bora wa Ligi ya Primia msimu wa 2024-25.
Mchezaji mwenzake wa Reds Alexis Mac Allister, nahodha wa Manchester United Bruno Fernandes, mshambuliaji wa Newcastle Alexander Isak, mshambuliaji wa Chelsea Cole Palmer na kiungo wa kati wa Arsenal Declan Rice pia walikuwa kwenye orodha ya walioteuliwa.
All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025
Discover more from cantonadigital
Subscribe to get the latest posts sent to your email.