Malumbano ya kukosa heshima bado yanaendelea juu ya mwili wa rais wa zamani wa Zambia

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

.

“Unarudi nyumbani!” – msemo unaohusishwa na mashabiki wa soka wa Uingereza – sasa umepata umaarufu miongoni mwa baadhi ya Wazambia katika vita ya nini cha kufanya na mwili wa Rais wa zamani Edgar Lungu.

Lungu mwenye umri wa miaka 68 alifariki miezi miwili iliyopita nchini Afrika Kusini ambako alikuwa akitibiwa.

Katika tukio la hivi karibuni, mahakama ya Pretoria ilitoa uamuzi unaopendelea serikali ya Zambia, ikisema kwamba kwa maslahi ya umma, mwili wa Lungu unaweza kurejeshwa na kufanyiwa mazishi ya serikali, jambo ambalo ni kinyume na matakwa ya familia.

Uamuzi huo uliibua shangwe miongoni mwa baadhi ya wafuasi wa chama tawala, ambao walichapisha ujumbe wao kwenye mtandao wa Facebook kwa maneno: “Unarudi nyumbani,” kana kwamba Zambia ilikuwa imeshinda kombe.

Jibu lisilo na heshima, pengine, lakini limejitokeza kuashiria jinsi suala hili limeleta mgawanyiko.

Kwa wengine ambao wamechoshwa na mzozo huo huzuni iliyosababishwa na kifo cha Lungu imefifia na kuwa hisia ya uchovu.

Na licha ya matatizo mengi zaidi ya kiuchumi, mijadala ya umma inaendelea kutawaliwa juu ya kifo cha rais huyo wa zamani, ambaye aliongoza nchi hiyo kwa miaka sita kuanzia 2015.

Kiini cha mzozo wa ni wapi atakapozikwa umesababishwa na tofauti iliyokuwepo kati ya Lungu na mrithi wake – ambaye alimshinda katika uchaguzi wa 2021 – Hakainde Hichilema.

Jaji wa Afrika Kusini alipotoa uamuzi wake wiki iliyopita, hasira ya dada mkubwa wa Lungu ilijitokeza wazi.

Bertha Lungu alipandwa na hasira, akilia bila kujizuia huku akimrushia maneno yasiyopendeza Mwanasheria Mkuu wa Zambia, Mulilo Kabesha, ambaye pia alikuwepo mahakamani.

“Kabesha, Lungu si mtoto wa baba yako… si mtoto wa Hakainde… Hii ni uchungu sana. Sitaki kwenda Zambia,” alilia huku watu akiwemo mpwa wake, Tasila Lungu wakihangaika kumliwaza na kumziba mdomo.

Mwili bado haujarejeshwa Zambia kwa sababu familia ya Lungu inakata rufaa dhidi ya uamuzi wa jaji wa Afrika Kusini – kesi ambayo inatazamiwa kusikilizwa Jumatatu.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a Reply