Zelensky asema amefanya mazungumzo yenye tija na Trump kabla ya siku ya ukomo kwa Urusi kusitisha vita

Radio Fortune Africa -Na Cantona Joseph

https://zeno.fm/radio/radio-fortune-africa

.

Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine amesema yeye na Donald Trump wamefanya majadiliano yenye tija kuhusu vikwazo dhidi ya Urusi, ushirikiano wa kiulinzi na utengenezaji wa ndege zisizo na rubani kabla ya ziara ya mjumbe wa Marekani Steve Witkoff huko mjini Moscow.

Akimshukuru Trump kwa mazungumzo “yenye tija” siku ya Jumanne, Zelensky alidai kuwa Moscow ilikuwa suala “nyeti” haswa kabla ya siku ya ukomo ya Urusi kusitisha vita iliyowekwa na Rais Donald Trump.

Trump aliwahi kusema kuwa ikiwa Urusi itashindwa kusitisha mapigano na Ukraine ifikapo Ijumaa hii, itakabiliwa na vikwazo vikali au kushuhudiwa kwa vikwazo vingine dhidi ya wale wote wanaofanya biashara nayo.

Aidha, siku ya Jumatatu Rais Volodymyr Zelensky alisema kwamba wanajeshi wa Ukraine kaskazini-mashariki mwa Ukraine walikuwa wakipambana na “mamluki” wa kigeni kutoka nchi mbalimbali zikiwemo China, Pakistan na sehemu za Afrika, na kuapa kulipiza kisasi.

Zelensky aliwahi kuishutumu Moscow kwa kusajili wapiganaji wa China kwa ajili ya juhudi zake za vita dhidi ya Ukraine, mashtaka ambayo Beijing ilikanusha, wakati Korea Kaskazini pia imetoa maelfu ya wanajeshi wake kupigana katika eneo la Kursk nchini Urusi.

Witkoff atakuwa mjini Moscow siku ya Jumatano na anatarajiwa kukutana na Vladimir Putin.

Mwanafunzi wa Uganda ‘aliyetekwa nyara’ afungwa jela kwa video ya TikTok dhidi ya Museveni

.

Mwanafunzi wa chuo kikuu nchini Uganda ambaye alipotea ghafla miezi miwili iliyopita baada ya kuweka video kwenye mtandao wa TikTok ambayo ilikosoa vikali uongozi wa Rais Yoweri Museveni amefungwa jela.

Elson Tumwine alitoweka tarehe 8 Juni – na kuzua shutuma kutoka kwa upinzani na wanaharakati kwamba alitekwa nyara na kuzuiliwa kinyume cha sheria na maafisa wa kijeshi.

Kufuatia malalamiko ya kutoweka kwake, aliripotiwa kuachwa katika kituo cha polisi huko Entebbe katikati ya Julai na baadaye kushtakiwa kwa mawasiliano mabaya na matumizi mabaya ya kompyuta.

Mwanafunzi huyo alikiri kuwa na hatia na kuomba msamaha.

Mahakama ya hakimu mjini Entebbe ilimhukumu kifungo cha miezi miwili jela siku ya Jumatatu, ikibainisha maombi yake ya kuhurumiwa.

UN yashtushwa na ripoti juu ya uwezekano wa upanuzi wa operesheni ya Israeli huko Gaza

.

Umoja wa Mataifa Jumanne uliita taarifa kuhusu uwezekano wa uamuzi wa kupanua operesheni za kijeshi za Israeli katika Ukanda wa Gaza kuwa “za kutisha” ikiwa ni kweli.

Msaidizi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Miroslav Jenca aliuambia mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Gaza kwamba hatua hiyo “itakuwa na athari mbaya… na inaweza kuhatarisha zaidi maisha ya mateka waliosalia huko Gaza.

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limejadili mzozo wa eneo la Gaza baada ya Israeli kuitisha kikao cha dharura kujadili mateso ya mateka wanaoshikiliwa kwenye Ukanda huo.

“Sheria ya kimataifa iko wazi katika suala hilo; Gaza ni na lazima ibaki kuwa sehemu muhimu ya taifa la Palestina la siku zijazo,” UN ilisema.

Hali hii inafuatia kutolewa kwa video za hivi karibuni za Hamas na wanamgambo wengine wa Palestina wakionyesha mateka waliokonda kupita kiasi, ambao Katibu Mkuu wa UN aliita “ukiukaji usiokubalika wa hadhi ya mwanadamu.”

Hilo limepelekea Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kutarajiwa kupendekeza kukalia tena kikamilifu Ukanda wa Gaza atakapokutana na baraza lake la mawaziri la usalama, vyombo vya habari vya Israeli vinasema.

“Mkondo huu umeanza na hauwezi kusitishwa wala kubadilishwa. Tunaenda kuuteka kikamilifu Ukanda wa Gaza – na kuwashinda Hamas,” waandishi wa habari wa eneo hilo wamemnukuu afisa mwandamizi wa Israeli akisema.

Akijibu ripoti kwamba mkuu wa jeshi na viongozi wengine wa kijeshi wanapinga mpango huo, afisa huyo ambaye hakutajwa jina alisema: “Ikiwa hiyo sio sawa kwa mkuu wa majeshi, basi anapaswa kujiuzulu.”

Familia za mateka zinahofia mipango kama hiyo inaweza kuhatarisha wapendwa wao, huku 20 kati ya 50 wakiaminika kuwa hai huko Gaza, wakati kura za maoni zinaonyesha Waisraeli watatu kati ya wanne badala yake wanapendelea makubaliano ya kusitisha mapigano ili mateka warudi nyumbani.

Washirika wengi wa karibu wa Israel pia wameshutumu hatua hiyo huku wakishinikiza kusitishwa kwa vita na hatua za kupunguza mzozo wa kibinadamu.

Ndani ya Israeli, mamia ya maafisa wa usalama waliostaafu wa Israel, wakiwemo wakuu wa zamani wa mashirika ya kijasusi, walitoa barua ya pamoja kwa Rais wa Marekani Donald Trump siku ya Jumatatu, wakimtaka amshinikize Netanyahu ili amalize vita.

Wiki iliyopita, Uingereza na Canada ziliungana na Ufaransa katika kutangaza mipango yenye masharti ya kulitambua taifa la Palestina.

Waziri Mkuu wa Israeli sasa anatarajiwa kukutana na mawaziri wakuu na viongozi wa kijeshi ili kuamua hatua zinazofuata huko Gaza.

Redio ya jeshi la Israeli ilisema wanatazamiwa kujadili mipango ya awali ya jeshi kuzingira kambi kuu za wakimbizi na kufanya mashambulizi ya anga na ya ardhini.

Netanyahu alisema ataitisha mkutano wa baraza la mawaziri la usalama wiki hii.

Marekani kupitia upya hadhi ya Kenya ya mshirika mkuu asiye mwanachama wa NATO

.

Utawala wa Rais wa Marekani, Donald Trump, umependekeza kuhakiki upya hadhi ya Kenya ya mshirika mkuu asiye mwanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO), miezi michache tu baada ya Kenya kuwa nchi ya kwanza ya Kusini nwa Afrika mwa Jangwa la Sahara kupokea hadhi hiyo ya kifahari.

Kenya ilipata hadhi hiyo wakati wa ziara ya Kiserikali ya Rais William Ruto nchini Marekani mnamo mwezi Mei 2024.

Hadhi hiyo ambayo Kenya ilipewa mnamo mwezi Juni 24, 2024, iliimarisha Kenya kama mshirika mkuu wa Marekani barani Afrika na uhusiano kati ya nchi hizo mbili katika ulinzi, usalama na maeneo ya kiuchumi.

Kenya kama mshirika mkuu asiyekuwa mwanachama wa NATO sasa ipo mashakani baada ya Seneta wa Marekani James Risch kupendekeza marekebisho ya Sheria ya Uidhinishaji wa Kitaifa wa Ulinzi kwa Mwaka wa Fedha wa 2026, ambayo inalenga kupitia upya hadhi hiyo ya Kenya ndani ya siku 90.

Mapitio hayo yatatathmini sera za kigeni na za kidiplomasia za Kenya kama vile kujifungamanisha na Marekani na ushirikiano wake na China, Urusi na Iran.

Aidha, mapitio hayo pia yatajumuisha makubaliano yanayowezekana ya Kenya, uhusiano wa kisiasa au kifedha na wanamgambo wenye silaha kama vile al-Shabaab na Rapid Support Forces (RSF).

“Maelezo ya kina kuhusu uhusiano wa kijeshi na usalama wa Serikali ya Kenya na Jamhuri ya Watu wa China, Shirikisho la Urusi, na Iran, ikiwa ni pamoja na mazungumzo yoyote, makubaliano, au shughuli za pamoja tangu Juni 24, 2024,” ilisoma sehemu ya taarifa hiyo kwenye tovuti ya Bunge la Marekani.

Pia, mapitio hayo yatatathmini ikiwa serikali ya Rais Ruto inatumia usaidizi wa usalama na kijasusi wa Marekani kujihusisha na ukiukaji wa haki za binadamu kama vile utekaji nyara, watu kuteswa na ghasia dhidi ya raia.

Ikiidhinishwa, marekebisho hayo yatahitaji Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kupitia upya Kenya na kuwasilisha matokeo kwa Kamati husika ndani ya siku 180.

Hatua hiyo ya kisheria inaashiria mabadiliko makubwa katika mustakabali wa uhusiano wa Marekani na Kenya.

All Rights Reserved © The Cantona Group PLC||2025


Discover more from cantonadigital

Subscribe to get the latest posts sent to your email.

Leave a comment